Friday 29 December 2023

ADC YAJIWEKA MGUU SAWA UCHAGUZI WA 2024/2025


Na Oscar Assenga,TANGA

CHAMA cha Alliance For Democratic Change (ADC-Dira ya Mabadiliko ) kimeanza kujiweka sawa kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na ule Mkuu mwaka 2025 baada ya kutangaza kufanyika kwa uchaguzi wa ndani wa chama hicho kwa mwaka 2024.

Akizungumza leo Katibu Mkuu wa ADC Taifa Doyo Hassan Doyo (Pichani kulia) alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho toleo la tatu la mwaka 2019,Uchaguzi wa viongozi ndani ya chama hufanyika kila baada ya miakaa mitano.

Alisema kwamba tamko hilo linaonyeshwa katika katiba yao kwenye sura ya nane ibara ya 53(i) “Ukomo wa uongozi ni miaka mitano” na sasa ni wakati wa kufanyika chaguzi ambazo zitawapa fursa ya kupatikana viongozi wapya katika ngazi mbalimbali.

Katibu huyo alisema kutokana na chama kufanya uchaguzi ndani ya chama mnamo mwaka 2019 ambapo ulifanyika Mkutano mkuu mwezi Aprili katika ukumbi wa Hotel ya Madinat Bahri iliyopo Zanzibar.

Aidha alisema kwamba mwaka 2024 viongozi waliopo madarakani wanatimiza miaka mitano tangu kufanyika uchaguzi na mkutano mkuu husika kwa madhumuni ya kuchagua viongozi ambao wako madarakani hadi muda huu.

“Kwa kuzingatia utekelezaji wa miongozo kutoka katika katiba yetu Ofisi ya chama makao makuu inatoa ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama hicho kwa mwaka 2024”Alisema Katibu huyo.

Katibu huyo alisema kwamba uchaguzi huo ngazi ya Tawi utaanza Januari Mosi hadi Januari 31 mwakani wakati ule wa kata utafanyika kati ya Februari Mosi hadi February 29 mwaka 2024 utakaokwenda sambamba na ule wa majimbo.

Alisema baada ya hapo kutafanyika chaguzi ngazi ya wilaya utaanza Machi 1 mpaka Machi 31 mwakani utakaoambatana na ule ngazi ya Kanda huku akiwataka wanachama kuchangamkoa fursa za kuwania nafasi mbalimbali.

Katibu huyo alisema baada ya hapo kutafanyika uchaguzi Mkuu wa chama chicho ambao unatarajiwa kwisha mwezi Mei mwakani na hatimaye kuweza kupata safu mpya za uongozi.

Hata hivyo Katibu huyo alitoa agizo kwa viongozi wote wa chama hicho nchi nzima kusimamia zoezi hilo kwa ufanisi na kushirikisha wanachama wote wa ADC ili kukamilisha chaguzi hizo kwa mafanikio.
Share:

WASHINDI WA TCAA FUN RUN WAAGWA UWANJA WA NDEGE WA JNIA WAKIELEKEA DUBAI


Mamlaka ya USafiri wa Anga nchini imeratibu zoezi la kuwaaga washindi watano wa mbio za kujifurahisha (FUN RUN) zilizofanyika Oktoba 29 jijini Dar es salaam zikiwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 tangu kuundwa kwa TCAA.

Washindi hao walipata zawadi za tikteki kutoka kwa wadau wa Usafiri wa Anga ambao ni mashirika ya ndege ya Ethiopian Airlines, Kenya Airways na Fly Dubai ambapo wataelekea Dubai kwa mapumziko ya siku tano.

Akizungumza wakati wa kuwaaga, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya miaka 20 ya TCAA ambaye pia ni Meneja Mipango wa Mamlaka hiyo Bi. Mellania Kasese aliwapongeza washindi hao na kuyashukuru Mashirika yaliyotoa tiketi hizo kwa kutimiza ahadi hiyo na kuishukuru TCAA kwa kugharamia fedha za kujikimu kwa washindi hao wawapo katika mapumziko hayo.


"Ni siku ya sote kufurahia utimilifu wa zoezi hili kwa washindi wetu hawa watano ambao walipatikana miongoni mwa zaidi ya washiriki 300. Nawatakia safari njema na hii iendelee kuwa chachu ya kujali afya zenu lakini ikawe hamasa kwa wengine ili wajikite katika kuimarisha afya zao kwa mazoezi," amesema Mellania.


Meneja wa Shirika la Ndege la Ethiopia Bi. Seble Woldemariam amewapongeza washindi na kuwataka kutumia fursa hii kufanya utalii na kujifunza mengi mema na mazuri watakayojionea huko waendako.
Meneja Mipango TCAA Melania Kasese akizungumza na wanahabari wakati wa tukio la kuwaaga washindi wa TCAA FUN RUN waliojishindia tiketi za kuelekea Dubai ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)
Bw. Samuel Makalla mtumishi wa TCAA akielezea maandalizi aliyofanya kuelekea safari ya Dubai mara baada kuibuka mshindi wa TCAA FUN RUN kwenye Maadhimisho ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)
Mtumishi wa TCAA Bw. Aidan Adrian ambaye ni miongoni mwa washindi akitoa shukrani kwa wote waliofanikisha zoezi hilo wakati TCAA FUN RUN iliyofanyika katika maadhimisho ya Miaka 20 ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) iliyopelekea kutangazwa mshindi wa mashindano hayo.
Mtumishi wa LATRA Bw. Lugano Mwasomola ambaye ni miongoni mwa washindi akitoa shukrani kwa wote waliofanikisha zoezi hilo pamoja nasafari hiyo ya kwenda Dubai wakati wa hafla ya kuondoka hapa nchini kuelekea Dubai.




Meneja wa Shirika la Ndege la Ethiopia Bi. Seble Woldemariam (katikati) akizungumza wakati wa kuwaaga washindi wa tiketi ya kuelekea Dubai ambapo Shirika hilo ni miongoni mwa wadau waliotoa tiketi moja wapo kwa mshindi.


Meneja Mipango kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Melania Kasese akiwa kwenye picha ya pamoja na washindi wa tiketi ya kuelekea Dubai pamoja na viongozi wa Shirika la Ndege la Ethiopia pamoja na Emirate wakati wa kuondoka nchini kwa ajili ya kwenda kutembea Dubai.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA DESEMBA 29,2023

Share:

Thursday 28 December 2023

SERIKALI KUWANYANYUA VIJANA KIUCHUMI NA KIMITAJI - KATAMBI




Na: Mwandishi wetu - Mwanza

SERIKALI imeendelea kubuni Mikakati ya kuhakikisha Vijana wanapata ujuzi na fursa za kuwainua kiuchumi ili waweze kujiajiri na kuajiri wenzao.


Hayo yamebainishwa Desemba 27, 2023 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 15 la Umoja wa Vijana Wakatoliki wa Vyuo vya kati na Vyuo Vikuu Tanzania (TMCS) Taifa, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.

Aidha, Mhe. Katambi amesema kuwa Serikali kwa kutambua mchango wa vijana katika ujenzi wa taifa vijana nchini wameendelea kunufaika kwa kupatiwa mafunzo ya kuendeleza ujuzi wao, kuboresha Mwongozo wa Utoaji Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF) na kutenga maeneo katika Halmashauri kwa ajili ya shughuli za vijana.

Mhe. Katambi pia amewataka Vijana nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za ajira zinazotolewa na Serikali.

Vilevile, amewasisitiza vijana wanaokidhi vigezo kuchangamkia nafasi za kazi 500, Kada ya Uuguzi kwa kutuma Maombi yao kupitia tovuti ya www.jobs.kazi.go.tz ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingia makubaliano na Serikali ya Saudi Arabia pamoja na nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusu ajira za watanzania katika nchi hizo, mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 31 Disemba, 2023.

Share:

Video Mpya : SHITUNGULU - UTANIKUMBUKA

Msanii Shitungulu anakualika kutazama Video ya wimbo wake mpya unaitwa Utanikumbuka
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO ALHAMISI DESEMBA 28,2023




Share:

Wednesday 27 December 2023

DCEA YAKAMATA DAWA ZA KULEVYA ZILIZOFUNGASHWA KAMA KAHAWA NA MAJANI YA CHAI DAR NA IRINGA...YATOA ONYO ZITO


Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 27,2023 Jijini Dar es Salaam 


TAARIFA KWA UMMA

UKAMATAJI WA KILOGRAMU 3,182 ZA DAWA ZA KULEVYA

Dar es Salaam, - 27 Disemba, 2023

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 3,182 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine katika operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam na Iringa kati ya tarehe 5 hadi 23 mwezi Disemba, 2023. Watu saba wamekamatwa kuhusika na dawa hizo ambapo wawili kati yao wana asili ya Asia.

Kiasi hiki cha dawa za kulevya kinajumuisha kilogramu 2,180.29 za dawa aina ya methamphetamine na kilogramu 1001.71 aina ya heroin zilizokamatwa katika wilaya za Kigamboni, Ubungo na Kinondoni jijini Dar es Salaam pamoja na wilaya ya Iringa mkoani Iringa.

Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya. Hivyo, watuhumiwa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani.

Aidha, dawa hizi zilizozikamata zilikuwa zimefungashwa kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbalimbali za kahawa na majani ya chai. Mbinu hii inatumika kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wake na kukwepa kubainika.

Ukiacha dawa ya heroin inayotengenezwa kwa mchanganyiko wa kemikali kutoka kwenye mimea ya afyuni (opium popy) inayolimwa katika nchi za Asia na baadhi ya kutoka Amerika, dawa aina ya methamphetamine ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi sawa na cocaine. Dawa hii huwa kwenye mfumo wa vidonge, unga au chembechembe mithili ya chumvi ang’avu yenye rangi mbalimbali ambayo huzalishwa kwenye maabara bubu kwa kuchanganya aina mbalimbali za kemikali bashirifu.

Dawa hii ni hatari kwa afya ya mtumiaji, madhara yake ni makubwa na hayatibiti kirahisi kwani mtumiaji hupata madhara ya kudumu kwenye ubongo na hivyo hupunguza uwezo wa kutunza kumbukumbu, kusababisha uraibu na kuathiri mfumo mzima wa fahamu.

Kiasi cha dawa za kulevya zilizokamatwa, endapo zingefanikiwa kuingia mtaani zingeweza kuathiri zaidi ya watu 76,368,000 kwa siku. Hivyo, ukamataji huu umeokoa nguvu kazi ambayo ingeangamia kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa a Kulevya, inatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka kwani mafanikio haya yametokana na ushirikiano unaotokana na wananchi wanaotoa taarifa juu ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na weledi na uzalendo mkubwa wa maafisa wa Mamlaka katika udhibiti wa biashara ya dawa za kulevya.

Pia, Mamlaka inatoa onyo kwa wote wanaoendelea kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya hapa nchini kuacha badala yake wajikite kwenye biashara nyingine halali kwani Mamlaka imejizatiti kukomesha biashara ya dawa za kulevya kwa kufanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, Mamlaka inaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha katika kutekeleza kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Tukishirikiana, kwa umoja wetu tutaweza kuokoa vizazi vyetu na taifa letu dhidi ya tatizo la dawa za kulevya.

Imetolewa na,

 

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA

NA DAWA ZA KULEVYA.






Share:

3,182 KG ZA DAWA ZA KULEVYA AINA YA HEROIN NA METHAMPHETAMINE ZAKAMATWA NCHINI


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini( DCEA) imefanikiwa kukamata jumla ya Kilogramu 3,182 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine katika operesheni maalum iliyofanyika Jijini Dar es Salaam na Iringa.

Katika Operesheni hiyo ambayo imefanyika Disemba 5 hadi 23,2023, jumla ya watu saba wamekamatwa kuhusika na dawa hizo ambapo wawili kati yao wana asili ya Asia.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 27,2023 Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. Aretas Lyimo amesema kiasi hicho cha dawa za kulevya kinajumuisha kilogramu 2,180.29 za dawa aina ya methamphetamine na kilogramu 1001.71 aina ya heroin zilizokamatwa katika wilaya ya Kigamboni, Ubungo na Kinondoni Jijini Dar es Salaam pamoja na Wilaya ya Iringa mkoani Iringa.

Aidha amesema kuwa aina ya dawa ambazo wamezikamata zilikuwa zimefungashwa kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbalimbali za kahawa na majani ya chai.

“Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya. Hivyo, watuhumiwa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani”. Amesema

Amesema kuwa kiasi cha dawa zilizokamatwa, endapo zingefanikiwa kuingia mtaani zingewza kuathiri zaidi ya watu 76,368,000 kwa siku.

“Ukamataji huu umeokoa nguvu kazi ambayo ingeangamia kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi”. Amesema

Pamoja na hayo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka kwani mafanikio haya yametokana na ushirikiano unaotokana na wananchi wanaotoa taarifa juu ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na weledi na uzalendo mkubwa wa maafisa wa Mamlaka katika udhibiti wa bishara ya dawa za kulevya.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger