Wednesday, 1 April 2026
PROF. SHEMDOE AWASILISHA RANDAMA YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI OFISI YA WAZIRI MKUU 2026/2027
Machi 31, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewasilisha randama ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Mhe. Prof. Shemdoe amewasilisha randama hiyo yenye mafungu 37 kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye anatarajia kusoma rasmi makadirio hayo kesho tarehe 01 Aprili, 2026 katika kikao cha pili cha mkutano wa tatu wa Bunge la Bajeti, ambapo Wabunge watapata fursa ya kujadili mipango na matumizi ya fedha ya ofisi hiyo.

Tuesday, 31 March 2026
Tanzia : BWEGE AFARIKI DUNIA

Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza kwa masikitiko kifo cha mwanachama wake, Ndugu Seleman Bungara maarufu kama Bwege, kilichotokea ghafla wakati akiwa hospitalini akipatiwa matibabu ya kusafisha figo (dialysis).
Kupitia taarifa iliyotolewa na kiongozi wa chama, Dorothy Semu, chama kimetoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wanachama wote walioguswa na msiba huo.
ACT Wazalendo imemtaja marehemu Bungara kama mwanasiasa wa upinzani aliyekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki na demokrasia nchini.
Chama hicho kimesema kitashiriki kikamilifu katika mazishi na kuwataka wanachama kuungana na familia katika kipindi hiki kigumu.

WMA YATOA MSAADA WA VIFAA VYA UJENZI KWA WAHITAJI DODOMA
Katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Wakala wa Vipimo (WMA) imetoa misaada ya vifaa vya ujenzi wa jiko la kisasa katika Kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalumu Cha RAHMAN ORPHANAGE CENTER kilichopo Chang'ombe jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya kutoa misaada hiyo Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma Said Ibrahimu amesema suala la mazingira safi ya kupikia ni haki ya kila mmoja ndio maana wameamua kama Wakala kutoa misaada hiyo itakayowezesha upishi wa kisasa katika mazingira safi na salama ikiwemo usalama wa chakula kwani kituo hicho wamekuwa wakipika kwa kutumia kuni na mazingira ya Nje ambayo sio salama kwa afya ya watoto hao.
"tunamuunga mkono Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha nishati safi ya kupikia inakuwa katika mazingira safi na salama ndio maana leo kwa niaba ya wafanyakazi wa WMA tumekabidhi Sementi, Marumaru na vifaa vingine vitakavyosaidia ujenzi wa jiko hilo, "amesema Meneja Said
Kadhalika, Mkurugenzi wa kituo hicho Bi. Rukia Abdallah ameishukuru WMA kwa misaada hiyo itakayokwenda kuboresha mazingira ya mapishi katika Kituo hicho chenye idadi ya watoto 120 huku akiomba wadau wengine kujitokeza kuchangia kituo hicho ikiwemo suala la usafiri ili watoto hao waweze kutembelea maeneo mbalimbali kwa ajili ya kujifunza zaidi.
Mmoja wa watoto wanaolelewa katika Kituo hicho Hazra Ramadhan ameipongeza Wakala wa Vipimo kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia na kuwaomba kuendelea kuwakumbuka kila mara ili waweze kutimiza malengo yao.











