Thursday, 2 April 2026

POLISI YAJIDHATITI KUHAKIKISHA USALAMA NA UTULIVU WAKATI WOTE WA SIKUKUU ZA PASAKA

...

Na mwandishi wetu

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema limejipanga vyema kuanzia ngazi ya Kata na kwa kushirikiana na Kamati za ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa usalama na utulivu unadumishwa wakati wote wa kipindi cha kuhitimisha mfungo wa Kwaresma na sikukuu za pasaka kwa waumini wa dini ya Kikristo wakati wote wa ibada Kanisani na majumbani mwao.

Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime kuhusu kuimarishwa kwa hali ya usalama kuelekea sikukuu za Pasaka iliyotolewa leo Alhamisi Machi 02, 2026 kwa Vyombo vya habari, imetoa wito pia kwa kila mmoja wakati wa ibada na sherehe za pasaka kuhakikisha makazi yanakuwa chini ya uangalizi badala ya kuacha makazi yao bila ya usimamizi.

"Aidha kama tutaruhusu watoto wetu kutoka kwaajili ya kwenda kusherehekea sikukuu hizi katika maeneo stahiki na salama, kila mmoja ahakikishe wanakuwa na uangalizi wa mtu mzima na mwenye akili timamu. Pia tunatoa wito kwa kila mmoja kuzingatia sheria, kanuni na ishara za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazotokana au zinazosababishwa na uzembe pamoja na kuendesha chombo cha moto katika hali ya ulevi."amesema Kamanda Misime.

Polisi pia katika taarifa yake imesisitiza umuhimu wa kila mmoja kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha, wakisisitiza kuacha na kujiepusha na tabia za kupita sehemu ambazo maji mengi yametuama au yanayotiririka suala ambalo si salama kwa binadamu.

"Tunarudia tena kutoa tahadhari hii kwasababu tumeshuhudia baadhi ya watanzania wenzetu wanaopoteza maisha walipojaribu kuvuka sehemu hatarishi ambazo zimejaa maji, tumeshuhudia pia watoto waliopoteza maisha kutokana na kusombwa na maji na wengine kutumbukia kwenye mashimo yaliyochimbwa na kuachwa wazi,

Wazazi/walezi tuwalinde watoto wetu dhidi ya madhara hayo na kwa wale waliochimba mashimo na kuyaacha wazi wayafunike au kuyafukia." Amekaririwa Kamanda Misime katika taarifa yake.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger