Tuesday, 23 December 2025
UZALENDO WA KWELI HUPIMWA KWA VITENDO VYA KULINDA TAIFA

Vijana wamehimizwa kutambua kuwa mzalendo wa kweli hupimwa kwa vitendo vya kulinda taifa.
Jackline Mwafongo, mkazi wa Mbeya, ameeleza kuwa vurugu huleta hofu na uharibifu wa mali, jambo ambalo huathiri moja kwa moja ustawi wa vijana na sekta binafsi.
Badala ya kujihusisha na miito ya uasi, wananchi wameaswa kuiga mifano ya ubunifu kama ule wa kukodisha power bank uliozinduliwa na kijana Thomas Ryoba, ambao unalenga kutatua changamoto za jamii na kuongeza kipato.
Jackline amesema hayo wakati Jeshi la Polisi likitoa taarifa ya kuimarika kwa usalama kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka,ambnapo limewataka vijana na raia nchini kupuuza taarifa za uchochezi zinazotoka nje ya nchi na kujikita na maisha yenye tija.
Wananchi wameonya kuwa taarifa nyingi mtandaoni zinalenga kupandikiza mgawanyiko na kudhoofisha uchumi wa taifa kupitia maandamano na vurugu ambazo hazizingatii historia na utulivu wa Tanzania wa zaidi ya miaka 60.
Maoni ya wananchi yamesisitiza kuwa sauti ya utulivu imeshinda kelele za chuki, na kutoa wito kwa kila mmoja kutambua thamani ya amani kama nyenzo kuu ya kufanya shughuli halali.
Aidha, msisitizo umetolewa kuwa usalama wa mali na miundombinu ya biashara ni jukumu la pamoja, kwani uharibifu wowote unarudisha nyuma jitihada za serikali za kukuza uchumi jumuishi. Kupitia kampeni ya "Nchi Kwanza," vijana wametakiwa kuendelea kuwa nguzo ya amani ili kuhakikisha uwekezaji na ajira nchini vinazidi kuongezeka bila bughudha.
UBUNIFU WA "SMART CHAJA" WAANGAZIA FURSA ZA VIJANA KATIKA MAZINGIRA YA AMANI
Katika hali inayoshiria kukomaa kwa fikra za kimaendeleo miongoni mwa vijana, mbunifu Thomas Ryoba amezindua huduma ya vituo vya kukodi kuchaji simu iitwayo “Smart Chaja,” mfumo unaomwezesha mteja kukodi power bank kupitia programu tumizi ya simu pindi anapopata dharura.
Ryoba amesisitiza kuwa huduma hiyo itapatikana katika maeneo rasmi kama ofisi, hospitali, na kumbi za starehe, huku akiwahimiza vijana wenzake kuchangamkia fursa za ubunifu ili kujipatia kipato na kufikia ndoto zao.
Hata hivyo, wadau wa maendeleo wamebainisha kuwa ubunifu kama huu wa Ryoba unahitaji mazingira tulivu na salama ili uweze kustawi na kuvutia wateja.
Maoni ya wananchi mtandaoni yamepongeza hatua hiyo kama "akili kubwa," yakisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia teknolojia kujenga uchumi badala ya kuitumia kama chombo cha kuvuruga utulivu. Amani imetajwa kuwa nguzo muhimu inayowezesha sekta binafsi na wabunifu wadogo kukua na kuchangia katika malengo ya serikali ya kukuza viwanda na ajira.
Wananchi wamehimizwa kulinda amani ili kutoa nafasi kwa wabunifu hawa kufanya kazi bila hofu ya uharibifu wa mali kama ilivyowahi kutokea mnamo Oktoba 29, ambapo baadhi ya makampuni yalichomwa moto wakati wa vurugu.
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama ni shwari, jambo linalotoa fursa kwa biashara na ubunifu mpya kama wa "Smart Chaja" kuendelea msimu huu wa sikukuu.






