Saturday, 22 November 2025

BODI YA TANAPA YATEMBELEA OFISI YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI


Bodi ya wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Novemba 21, 2025 imefanya ziara Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza namna Mamlaka hiyo inavyofanya kazi kama wadau muhimu katika masuala ya uchunguzi wa kisayansi kwa wanyamapori.

Wajumbe wa Bodi hiyo walipokelewa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, na kupewa maelezo kuhusu majukumu yanayofanywa na Mamlaka hiyo yenye jumla ya maabara 7 za vipimo, uchambuzi na utafiti.

Ziara hiyo iliambatana na kutembelea Maabara ya Vinasaba vya Wanyamapori “Wildlife DNA Laboratory” ambapo maabara hiyo ina jukumu la uchunguzi wa vinasaba “DNA” vya wanyamapori, kutoa ushahidi wa kisayansi kwa kesi za ujangili, kutoa mafunzo juu ya ukusanyaji na uhifadhi wa sampuli, kuhifadhi na kusaidia ushirikiano kati ya taasisi hiyo na wadau mbalimbali katika kukabiliana na ujangili.

Share:

TBS WATOA WITO USALAMA WA CHAKULA


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limehimiza wananchi kuzingatia matumizi ya chakula salama pamoja na kuimarisha usafi katika maandalizi ya chakula ili kulinda afya ya mlaji na kupunguza madhara yanayotokana na vyakula visivyo salama.

Akizungumza leo Novemba 21, 2025 Jijini Dar es Salaam, Afisa Udhibiti Ubora Mkuu wa TBS, Bw. Moses Mbambe, amesema usalama wa chakula unategemea kwa kiasi kikubwa maandalizi yanayozingatia usafi na matumizi ya maji salama.

“Chakula salama ni kile kilichoandaliwa katika mazingira safi, kisichokuwa na bakteria au vimelea vinavyoweza kusababisha maradhi kwa mlaji,” amesema Mbambe.

Mbambe amesema matumizi ya maji machafu katika maandalizi ya chakula, pamoja na kupikia katika mazingira yasiyo safi au vyenye maandalizi hafifu, huathiri kwa kiasi kikubwa usalama wa chakula kinachotumika majumbani, kwenye migahawa na katika maeneo ya biashara.

Katika kuongeza usalama wa chakula, TBS imehimiza uhifadhi sahihi wa vyakula hususan nafaka kwa kuzihifadhi kwenye madumu yenye mfuniko ili kuzuia mashambulizi ya sumukuvu, ambayo yana madhara makubwa kiafya.

Vilevile, Mbambe amesisitiza umuhimu wa kutenganisha chakula kilichopikwa na kisichopikwa, pamoja na kupika vyakula kama nyama kwa muda sahihi ili kuua vimelea vya magonjwa.

TBS imeonya pia juu ya matumizi ya vyombo visivyo safi na usambazaji wa chakula kwenye vifungashio visivyo salama ikiwemo chupa zilizotumika awali kuhifadhia juisi, mafuta au bidhaa nyingine.

“Chakula kinapobaki lazima kipashwe angalau nyuzi joto 60°C ili kuua vimelea vinavyoweza kuleta athari kwa afya ya binadamu,” amesema Mbambe.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Tathmini ya Hatari za Chakula TBS, Bi. Immaculatha Justine, amesema vyakula vinavyotokana na mifugo ni muhimu kwa afya ya binadamu lakini vinaweza kuwa hatarishi endapo kanuni bora hazitazingatiwa kuanzia ufugaji, uchinjaji hadi usambazaji.

Ametaja vihatarishi vya kibailojia kama vile virusi vya homa ya manjano, bonde la ufa na minyoo kuwa miongoni mwa vimelea vinavyoweza kusababisha madhara ya kudumu kwa walaji.

Ameongeza kuwa matumizi holela ya dawa za mifugo bila kufuata ushauri wa wataalamu yanaweza kusababisha mabaki ya kemikali hatarishi kubaki katika mazao ya wanyama.

Kwa upande wa samaki wanaofugwa, Bi. Immaculatha ameainisha uwezekano wa kuwepo kwa mabaki ya madini tembo, ambayo husababisha athari za kiafya endapo yataliwa bila kudhibitiwa.

Bi. Immaculatha amehimiza kufuatwa kwa kanuni za usafi katika hatua zote za mnyororo wa thamani wa chakula cha mifugo, na amewataka wananchi kununua bidhaa za mifugo katika maeneo yaliyoidhinishwa na kukaguliwa na mamlaka husika.
Share:

Friday, 21 November 2025

WATANZANIA KATAENI KUVURUGWA DESEMBA 9 – AMANI NDIO RIZIKI YETU!

Katika hali inayoonyesha wasiwasi wa baadhi ya wananchi kuhusu mipango ya uvunjifu wa amani, inayosambazwa mitandaoni hasa ile inayoelezwa kulenga Desemba 9, wito umetolewa kwa Watanzania wote kusimama imara na kukataa ushawishi wa wale wanaotaka kuingiza taifa kwenye machafuko.

Wananchi wamesema amani ni msingi mkuu wa maisha yao ya kila siku, huku wakisisitiza kwamba hakuna kazi wala maendeleo yanayoweza kupatikana bila utulivu.

Amani Huratibu Kazi, Huzima Vurugu

Malugu Nkwabi  mkazi wa Bariadi ambaye ni Afisa Usafirishaji, alitoa msisitizo mkubwa kwa umuhimu wa amani katika ufanisi wake wa kazi.

"Ni lazima Watanzania tushikane kuhakikisha amani ndiyo kila kitu. Amani ndiyo kitu cha muhimu sana kwenye taifa. Maisha yote yanategemea kuwepo kwa amani. Ukiangalia kuanzia saa 12:00 jioni ukifika ni lazima nifanye kazi ili niweze kurudi nyumbani na maisha yangu kuendelea. Huwezi kufanya kazi pasipo kuwepo amani.."

Kauli hii inalenga moja kwa moja wale wanaofikiria kuandamana au kufanya vurugu, ikiwakumbusha kwamba uvunjifu wa amani kwanza unakwenda kuathiri shughuli zao za kujipatia riziki.

Kwa upande wake, Bwana Marco Mahega,kutoka mkoani Simiyu , alieleza masikitiko yake kwa jinsi Watanzania wanavyotaka kuichoma nchi yao na kukumbusha  nchi  zenye migogoro, akisisitiza kuwa amani inalinda hata viwango vya chini vya jamii.

"Sisi wenye familia zetu tukikuta nchi haina amani hatuna kwa kuikimbilia... Tunashukuru Mwenyezi Mungu, tumepewa amani. Naomba tuendelee kuihifadhi. Ukiona nchi haina amani maana yake haina amani hata kwenye familia yako. Tunaangalia nchi nyingi ambazo hazina amani wanatumia muda wao mwingi kuendelea kwenye migogoro. Sisi amani ndiyo kila kitu. Nawaomba Watanzania wenzangu tuendelee kudumisha amani."

Wakati wakikataa vurugu, wananchi pia wanatoa wito kwa viongozi kuwajibika. Bwana Paul Mboyi,alielekeza wito wake kwa viongozi waliochaguliwa hivi karibuni, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi badala ya kuendeleza siasa.

"Kila mtu atimize wajibu wake... Naomba viongozi ambao kwanza wamechaguliwa waanze kufanya yale mambo waliyoahidi.  Tusiishie tu kwenye siasa. Tunaomba viongozi kuwafuata wananchi, wasikae ofisini tu. Mkutano wa mkoa tulinde kwanza kauli ya amani. Kusiwe na makundi."

Wito wa Bwana Mboyi unaonesha kuwa wananchi wanataka kuona uongozi unajikita katika maendeleo, lakini wanakiri kwamba amani lazima ilindwe kwanza kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi.

Share:

TUYAKATAE MAKUNDI YASIYOFAA, YATATUGHARIMU




Na Mwandishi wetu, Dar

Wito umetolewa kwa Vijana kujiepusha na makundi yasiyofaa pamoja na kutofuata kila wanachoambiwa kwenye Mitandao ya Kijamii nchini katika kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kuwepo.

Wito huo umetolewa na Mzee Ally Bomba Omar, Mkazi wa Tandika Mabatini Mkoani Dar Es Salaam, akieleza kuwa tangu kuzaliwa kwake Mwaka 1949 hakuwa kushuhudia vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

"Tangu kipindi cha Mwalimu Nyerere tulikuwa tunaishi kwa amani, matatizo haya yaliyotokea hapa yamenishangaza na watu hawa sijui wametokea wapi. Sisi tusiokuwa nacho na tuliozoea kununua unga nusu kilo nusu kilo tuliteseka sana na bahati mbaya hata ukiwa na visenti unanunua wapi vitu? Maduka yote yalikuwa yamefungwa." Amesema Mzee Bomba.

Mzee huyo amefahamisha kuwa ana amini kwamba kila mmoja ana akili timamu, akisema makundi mabaya yatawapoteza, akisema maandamano yasiyo rasmi yanaleta matatizo mengi ikiwemo vifo, majeraha na uharibifu wa mali na maisha.


Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA NOVEMBA 21,2025

Magazeti
 
Share:

Thursday, 20 November 2025

TUWAKATAE WANAONUFAIKA NA VURUGU- KAZAZI



Na Mwandishi Maalum, Dar

Vijana na Watanzania kwa ujumla wametakiwa kujiepusha na kutumika na watu wachache wenye kutanguliza maslahi yao binafsi ambao wamekuwa wakipata kipato kutokana na uharibifu, vurugu na ghasia wanazozihamasisha kufanywa ndani ya Jamii ya Watanzania.

Wito huo umetolewa na Bw. Juma Rashid Kazazi, Mkazi wa Dar Es Salaam wakati akizungumza kuhusu kadhia ya vurugu, wizi na uharibifu uliotokea Oktoba 29, 2025 na baada ya siku ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania, akisema wapo wanaonufaika na ghasia hizo huku washiriki wa ghasia hizo wakiathirika.

"Ndugu zangu Watanzania sasa tusifikie Vijana tukawa ni sehemu ya kipato cha watu, mtu anakuja kwa maslahi yake. 

Hilo jambo nawasisitiza Vijana wa Kitanzania mjaribu kukaa, mfikirie na si kila jambo ni la kupokea maana katika matukio haya wanatengenezea watu kipato na sisi tunabaki kuumia, kushinda njaa, kupigwa na hata kufa."

"Wao wanafaidika sisi tunaendelea kuumia na ni muhimu tujifunze kwa tukio lile na kama wana nia njema waje na wao tushirikiane kwenye kuandamana badala ya kututanguliza sisi wakati wao wapo nje ya nchi. Niwaombe Vijana hili jambo tuliangalie kwa ukubwa na tuwakatae watu hawa na kile wanachotuambia." Amesema Bw. Kazazi.

Akieleza kuwa ni mara ya kwanza kushuhudia uharibifu na vurugu zile, amewaomba watanzania pia kukemea jambo hilo jipya nchini, akisema ikiwa Watanzania wote watasimama pamoja watafanikisha kuidumisha amani ya Tanzania na kuruhusu kila mmoja kuendelea na shughuli zake za kiuchumi na kijamii.
Share:

Wednesday, 19 November 2025

MKUU WA WILAYA YA KAHAMA AFANYA KIKAO NA VIONGOZI WA DINI KUJADILI NAMNA YA KUIMARISHA AMANI

  

Mkuu wa Wilaya ya Kahama Frank Nkinda, ameongoza kikao maalum na Viongozi wa Dini pamoja na wajumbe wa Baraza la Amani Wilaya ya Kahama, chenye lengo la kujadili hali ya amani na kuweka mikakati ya kuendelea kuilinda amani katika wilaya hiyo.

Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kikihusisha viongozi kutoka madhehebu mbalimbali ya kidini ambao wamekutana kubadilishana mawazo juu ya namna bora ya kudumisha maelewano, mshikamano na utulivu wa jamii.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Dc Nkinda amesisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa ustawi wa wananchi na maendeleo ya wilaya, akibainisha kuwa Serikali inaiona nafasi ya viongozi wa dini kama ya msingi katika kuhamasisha maadili, uwajibikaji na utulivu wa kijamii.

 "Kahama imekuwa mfano wa maeneo yenye utulivu na mshikamano, Ili tufike mbali zaidi, tunahitaji ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na taasisi za dini,  Amani haitokei tu tunaitengeneza na kuilinda kwa pamoja", amesema Mhe. Nkinda.

Kwa upande wao, viongozi wa dini wameipongeza Serikali kwa utaratibu wa kuwaleta pamoja na kuwashirikisha katika masuala muhimu yanayoigusa jamii, huku wakiahidi kuendelea kuwa mstari wa mbele kuhimiza amani, upendo na uvumilivu miongoni mwa waumini na wananchi kwa ujumla.

Baraza la Amani limesema kuwa litaendeleza majadiliano na mikutano ya mara kwa mara ili kuhakikisha changamoto ndogo ndogo zinazoweza kuhatarisha amani zinatambuliwa mapema na kutafutiwa suluhu.

Kikao hicho kimehitimishwa kwa makubaliano ya kuongeza ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini na wadau wengine, kuhakikisha Kahama inasalia kuwa wilaya salama, yenye utulivu na mwelekeo mzuri wa maendeleo.

Share:

RAIS SAMIA AWAAPISHA MAWAZIRI WAPYA IKULU CHAMWINO, DODOMA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaapisha Mawaziri wa Wizara mbalimbali kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 18 Novemba, 2025.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini pamoja na wageni mbalimbali, ikiashiria mwanzo mpya wa safari ya kuimarisha utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Katika hotuba yake mara baada ya uapisho, Rais Samia amewataka viongozi hao wapya kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na uadilifu ili kuhakikisha Serikali inaendelea kutekeleza mipango ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wote.

Amewakumbusha kuzingatia uwajibikaji, ushirikiano na kusimamia vizuri rasilimali za umma.

Uapisho huu unaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuleta matokeo chanya, kuimarisha utawala bora na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger