Wednesday, 26 March 2025
COSTECH WAKABIDHI RASMI ENEO LA MRADI KWA MKANDARASI KWA AJILI YA UJENZI WA JENGO JIPYA LA STI JIJINI DODOMA
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imekabidhi rasmi eneo la mradi kwa mkandarasi TIL Construction Limited kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo jipya la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STI) jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya kukabidhi eneo hilo la mradi Machi 25,2025 jijini Dodoma Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kutoka COSTECH, Dkt. Aloyce Andrew, amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha utoaji wa huduma kwa wadau wa taasisi hiyo.
"COSTECH ina jengo Dar es Salaam lakini tumeamua kujenga Dodoma kwa ajili ya kuwahudumia wadau wetu kwa ukaribu zaidi...,Jengo hili litakuwa na sehemu ya kuhudumia wabunifu, kuatamia kampuni changa, na kuratibu masuala ya utafiti," amesema Dkt. Andrew.
Amesema ujenzi wa jengo hilo, ambalo litajengwa eneo la Azina jijini humo lenye mita za mraba 4,800, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 kufuatia kusainiwa kwa mkataba Machi 24, 2025.
Kwa upande wake, Mshauri Elekezi wa mradi huo kutoka Kampuni ya MEKON, Benedict Martin, amesema wamekuwa wakihusika katika usanifu wa jengo hilo tangu mwaka jana (2024) baada ya kushinda zabuni kutoka COSTECH.
"Tulishirikiana na COSTECH kuhakikisha jengo hili linakidhi mahitaji yao yote. Pia tuna uhakika kwamba mkandarasi tuliyempata ana uwezo wa kutekeleza mradi huu kwa ubora unaotakiwa," alisema Martin.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TIL Construction Limited, Ding Fubing, ameahidi kwamba kazi itafanyika kwa ufanisi na kumalizika kwa wakati.
"Tunaanza rasmi kesho kwa kulisafisha eneo lote, na baada ya wiki mbili hadi tatu, tutaingia kwenye ujenzi wenyewe. Tunaahidi kufanya kazi nzuri na kukamilisha mradi kwa muda uliopangwa au hata kabla," alisema Fubing.
Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa COSTECH, Imanuel Mgonja, amesema taasisi hiyo ina imani na mshauri elekezi pamoja na mkandarasi, akiwashukuru kwa kujitolea kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora unaohitajika..
SIMBACHAWENE AWATAKA WATENDAJI WA SERIKALI KUWAHESHIMU WAKAGUZI WA NDANI
Tuesday, 25 March 2025
MBUNGE ELIBARIKI KINGU AKABIDHI PIKIPIKI, BATI, TILES NA FEDHA KWA UVCCM SINGIDA
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, ameonesha uongozi wa kipekee kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa UVCCM Mkoa wa Singida.
Katika hafla iliyofanyika Machi 24, 2025, katika Ukumbi wa RC Mission, Mkoani Singida, Kingu alikabidhi pikipiki 6 kwa makatibu wa UVCCM katika Wilaya zote sita za Mkoa wa Singida.Aidha, ametoa bati 120 yenye thamani ya milioni 3.1 kwa UWT Mkoa wa Singida na tiles za milioni 7 kwa Ofisi ya CCM Wilaya ya Ikungi. Kingu pia ametoa shilingi milioni 3 kwa Jumuiya za Wilaya ya Ikungi.
Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Kawaida, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amekabidhi gari la jumuiya hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa. Pikipiki sita zilizotolewa na Mbunge Kingu zilikabidhiwa kwa UVCCM Wilaya ya Singida Magharibi.
Mbunge Kingu amekumbusha ahadi aliyotoa kwa vijana wa Mkoa wa Singida kwamba atawasaidia kwa vifaa vya kazi ili kuhakikisha wanapata fursa za maendeleo.
Amesisitiza kuwa, kwa kushikamana na vijana wake, ataendelea kuwaunga mkono kwa uwezo wake wote na kurejesha heshima kwa chama chake.
Kingu ameongeza kuwa aliagiza pikipiki hizo kutoka Uingereza na kusema alitumia fedha taslimu kiasi cha milioni 16.2 kwa ununuzi wa pikipiki 6, ambazo zimesajiliwa kwa jina la UVCCM na tayari zimelipiwa kodi zote.
Hafla hiyo imekamilika kwa risiti ya ununuzi wa pikipiki hizo, ambayo Kingu alikabidhi kwa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Kawaida, kama uthibitisho wa malipo yaliyofanywa.























