Friday, 19 April 2024
DORIS MOLLEL FOUNDATION, ORXY GAS WAINGIA MAKUBALIANO KUWEZESHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA WAUGUZI 1000
Mkurugenzi wa Kampuni ya gesi ya oryx Araman Benoite na Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel , Doris Mollel wakimkabidhi mtungi wa kupikia wa gesi ya Orxy mmoja wa wauguzi katika hospitali ya rufaa ya Mwananyamala Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini makubalino kati ya kampuni ya Orxy Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation kuwezesha nishati safi ya kupikia kwa wauguzi na madaktari 1000 kutoka mikoa 10 nchini watakabidhi mitungi ya kupikia ya Orxy Gas lengo likiwa kuliwezesha kundi hilo la sekta ya afya kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa. Hafla hiyo imefanyika leo Aprili 19, 2024.
******************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Orxy Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation wameingia makubaliano kuwezesha nishati safi ya kupikia kwa wauguzi na madaktari 1000 kutoka mikoa 10 nchini watakabidhi mitungi ya kupikia ya Orxy Gas lengo likiwa kuliwezesha kundi hilo la sekta ya afya kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Akizungumza wakati wakikabidhi mitungi ya gesi ya kupikia ya Orxy 50 kwa wauguzi katika hospitali ya rufaa ya Mwananyamala kati ya mitungi 1000 itakayotolewa na Kampuni hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya gesi ya oryx Araman Benoite amesema makubaliano hayo yanalenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watanzania.
Amesema katika kampeni hiyo ya kuwezesha watanzania kuingia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, mpaka sasa tayari wameshatoa mitungi kwa wananchi zaidi ya elfu 32 ili kusaidia lengo la kufikia asilimia 80 ya watumiaji wa nishati safi.
Amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia inasaidia kuondoa hatari za kiafya kwa watumiaji wa kuni na mkaa kama nishati ya kupikia lakini pia hatari za kimazingira na ustawi wa jamii.
"Takribani watu 33,000 wanapoteza maisha nchini Tanzania kwa maradhi yanayotokana na kuvuta moshi unaotokana na mkaa au kuni hiyo ndio sababu ya Oryx gas kuja na suluhisho la kuwahamasisha wananchi kutumia gesi kwa matumizi ya kupikia", amesema Benoite
Ameeleza kuwa matumizi ya gesi yanaepusha wamama na watoto kuumika kubeba kuni hivyo kuepuka kujeuriwa na wanyama wakali wakiwa katika harakati za kutafuta kuni pia kuimarisha maisha ya wanawake na kuwalinda dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.
“Kuanzia mwezi wa saba mwaka 2021 tumekuwa mstari wa mbele kuunga mkono utekelezaji wa mkakati wa serikali uliopewa nguvu na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania , Dk. Samia Suluhu Hassan kwa lengo kwamba ifikapo mwaka 2033 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia”, ameeleza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel , Doris Mollel amesema katika makubaliano waliosaini na oryx watawafikia waguzi 1000 ambapo watawapa mitungi na majiko ya gesi kama mabalozi kwa kina mama waweze kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni programu ya miaka miwili.
Amesema mitungi hiyo itakwenda kwa wauguzi walioko maeneo magumu ambapo watakuwa wanawatembelea kwenye vituo vya afya na zahanati ili kuweza kuwafikia wafanyakazi ambao ni wauguzi wanaofanya kazi kubwa ya kuokoa maisha hususani ya mama na mtoto.
Awali Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala mkoani Dar es Salaam Dk.Zavery Benela amesema hospitali hiyo inakabiliwa na ongezeko la wagonjwa wa mifumo ya hewa.Kati ya wagonjwa wa nje 500 wanaofika kuonwa na madaktari bingwa asilimia 30 ya wagonjwa hao ni wa matatizo ya mfumo wa hali ya hewa .
Amesema matatizo hayo ya upumuaji kwa sehemu kubwa yanasababishwa na hali ya hewa pamoja na mazingira ya kuandaa chakula kutokna na kuni na mkaa.
Aidha Dk.Benela amesema magonjwa ya mfumo wa hali wa hewa yamekuwa changamoto hasa kwa watu wazima na watoto wa umri wa chini ya miaka 5.
WAZIRI JERRY SILAA KUONGOZA KLINIKI YA ARDHI TANGA
WAZIRI wa Ardhi,Nyumba na Mendeleo ya Makazi Jerry Silaa anatarajiwa kuongoza Kliniki ya Ardhi kwa mkoa wa Tanga itakayofanyika kuanzia Aprili 22 mpaka 28 mwaka huu ikifanyika kwenye maeneo mawili Kijiji cha Miaka 21 Chumbageni Tanga na Korogwe.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tanga Tumaini Gwakisa alisema zoezi hilo litafanyika kwenye maeneo mawili ambapo litaanzia Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Tanga eneo la Kijiji cha miaka 21 Chumbageni kuanzia Aprili 22 mpaka 25 mwaka huu.
Alisema baada ya kumaliza kwa Tanga wataelekea wilayani Korogwe ambapo litafanyika kuanzia Aprili 26 mpaka 28 mwaka hu na uendeshwaji wa program hiyo utasimaiwa na itaongozwa na Waziri wa Ardhi Jerry Silaa akiwa na wataalamu wa Wizara hiyo.
“Nichukue nafasi hii kwaalika wananchi wote wa mkoa wa Tanga kuhudhuria na kupata huduma mbalimbali za sekta ya ardhi katika maeneo ambayo kliniki hiyo itafanyika kwani kutakuwa na utatuzi wa migogoro ya ardhi ambapo Waziri atasikiliza kero mbalimbali za Migogoro hiyo”Alisema
Alisema pia kutakuwa na utolewaji wa elimu kuhusu usimamizi wa ardhi pamoja na uwepo wa kituo jumuishi kitakachotoa huduma ya kupokea maoni mbalimbali na utoaji hati miliki ,ukadiriaji wa kodi ya ardhi na ulipaji wa kodi ya ardhi.
Gwakisa aliwataka wananchi wa mkoa wa Tanga kuhudhuria na kushiriki ambapo Waziri atakuwepo na wataalamu kutoka Wizarani