Sunday, 9 April 2023

KAMA RIPOTI YA CAG NI NZURI, RAIS NI MZURI



Na Mwandishi Wetu

MJADALA wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) unaoendelea baada ya kuwasilishwa kwake bungeni Dodoma wiki hii, umeacha nje jambo moja – nafasi na umuhimu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye jambo hilo.

Ni rahisi kuelewa kwa nini macho na masikio ya wengi yataelekezwa kwenye taarifa kuhusu kinachoonekana kama matumizi mabaya na upotevu mkubwa wa mali ya umma yaliyomo kwenye ripoti hiyo. Mara nyingi taarifa ya CAG huumiza na kukera wengi. 

Wakati akipokea taarifa hiyo ya CAG wiki mbili zilizopita, Rais Samia hakutofautiana na wengi na – kwa kuonyesha namna alivyokerwa na yaliyomo, alitumia lugha kali ambayo Watanzania hawajazoea kumsikia akizungumza hadharani.

Lakini huo ni upande mmoja wa shilingi. Upande wa pili wa shilingi ni kwamba kama Rais Samia angetaka kuficha madudu yaliyomo serikalini kwake, angeweza kufanya hivyo kama ilivyo kwa viongozi wengine wa Kiafrika na duniani wasiopenda dhana ya uwajibikaji ndani ya serikali zao.

Katika dunia ya sasa, desturi kwa viongozi wakubwa wa dunia ni kuingia madarakani kihalali na kuanza kupambana na vyombo na taasisi zinazoweza kubana mamlaka ya watawala au kuibua uozo uliomo serikalini na kwenye maisha ya watawala.

Njia wanazotumia viongozi wengi ni kuviondolea uhalali vyombo na watu waliojitolea kupambana na uozo, kuvipunguzia bajeti ili visitimize majukumu yake na wakati mwingine kuvifuta kabisa.

Mdhibiti Mkuu kwenye Siasa za Tanzania

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni taasisi ambayo iko kikatiba. Hata hivyo, katika miaka walau 40 ya kwanza ya Uhuru, nafasi ya CAG (ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa NAOT), haikuwa na umaarufu wala ushawishi ilionao sasa.CAG wa kwanza Mzalendo, Mohamed Aboud, alidumu kwenye nafasi hiyo kuanzia mwaka 1969 hadi 1996. Alifuatiwa na Thomas Kiama aliyeanza mwaka 1996 hadi alipostaafu mwaka 2005.Ofisi hiyo ilianza kubadilika mwaka 2005 wakati alipoingia Ludovick Utouh. 

Ukizungumza na Watanzania wengi, utadhani kwamba Utouh ndiye alikuwa CAG wa kwanza hapa nchini. Hata hivyo, Utouh alikuwa vile alivyokuwa kwa sababu moja tu; Jakaya Kikwete.Rais Kikwete ndiye aliyeibadili ofisi ya NAOT kisheria na kimajukumu kufanya inachofanya sasa. 

Aliongeza bajeti kubwa iliyofanya ofisi hiyo kuongeza idadi ya wafanyakazi na utaalamu kiasi kwamba kufikia mwishoni mwa utawala wake, ofisi hiyo ilipewa kazi ya kukagua vitabu vya hesabu vya Umoja wa Mataifa (UN).

Isingewezekana kwa CAG Utouh kufanya yote aliyofanya bila Kikwete.

Kama Rais huyo wa nne wa Tanzania asingetaka, NAOT ingeweza tu kuendelea na shughuli zake kama ilivyozoea au kama ilivyo kwenye nchi nyingi za kiafrika ambako haina meno.

Kama kulikuwa na migogoro yoyote baina ya Utouh na Serikali ya Kikwete hatukuwahi kuisikia.

Tulichokuwa tunasikia ni kuwa bajeti ya CAG ilikuwa inaongezeka kila mwaka na majukumu ya kikaguzi kuongezeka ndani na nje ya nchi.

Alipoingia madarakani hayati Rais John Magufuli, kulikuwa na migongano ya wazi baina yake na Profesa Mussa Assad aliyechukua nafasi ya Utouh baada ya kustaafu kwake. 

Miaka mitatu tu baada ya kuingia madarakani, bajeti ya CAG ilikatwa kutoka shilingi bilioni 69.1 mpaka shilingi bilioni 61.4. 

Mafunzo zaidi kwa watumishi wa ofisi hiyo yakaanza kuadimika na mawanda ya ukaguzi yakapunguzwa. 

Hali ikawa mbaya kiasi kwamba ikafikia wakati Bunge likakataa kufanya kazi naye – pengine kwa maelekezo ya Mkuu wa Nchi na mwishowe Assad akaondolewa kwenye wadhifa huo kinyume cha taratibu. 

Kama kuna funzo moja la kudumu kwenye historia ya Tanzania ni kwamba uimara na uhuru wa CAG kwenye kutimiza majukumu yake unaendana moja kwa moja na Rais aliye madarakani. Kama Rais anataka ripoti ya CAG iwe imara na thabiti, ripoti ya CAG itakuwa imara na yenye weledi.

Rais Samia na CAG

Wakati Rais Samia anaingia madarakani mwaka 2021, nchi ilikuwa inapita katika kipindi kigumu kiuchumi kutokana na athari za ugonjwa wa Uviko-19 uliosababisha kuyumba kwa uchumi wa dunia.

Pamoja na hayo, miongoni mwa hatua za awali alizochukua – katika mazingira hayo magumu, ilikuwa ni kuongeza bajeti ya ofisi ya CAG kutoka shilingi bilioni 80 alizokuta hadi bilioni 80.9. 

Zaidi ya hapo, tangu siku yake ya kwanza madarakani, Rais amekuwa akitoa ujumbe wa mara kwa mara wa kutaka taasisi za uwajibikaji na zile za utoaji haki kutimiza majukumu yao waliyopewa kikatiba.

Kwa kufanya hivyo, alikuwa anamtia moyo CAG Charles Kicheere, kuwa anachotakiwa kufanya ni kutimiza wajibu wake. 

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha takribani miaka minne iliyopita, CAG aliruhusiwa kufanya ukaguzi katika maeneo kama ya manunuzi ya ndege za serikali ambayo yalikuwa ‘kaa la moto’ kuyajadili wakati wa zama za mtangulizi wake.

Kwa sababu ya kuwepo kwa uhuru wa kutosha wa wanasiasa, wanaharakati, wabunge na waandishi wa habari, ina maana ripoti ya CAG ya safari hii itakuwa na mwangwi mkubwa pengine kuliko ilivyokuwa miaka michache nyuma.

Lakini Watanzania sasa wanajua kwamba haya yote ni matunda ya utawala wa Rais Samia. 

Kama angeamua kufuata nyayo za mtangulizi wake, tungesikia na kujadili yale tu ambayo watawala wangetaka tuyasikie na kuyajadili. 

Kama tunasikia vitendo vya ubadhirifu na ufisadi, maana yake ni kwamba Rais Samia anataka kujua wapi panapovuja ili hatua zichukuliwe. 

Hata hivyo, ni hatari sana kumlazimisha Rais aanze kuchukua hatua tu kwa sababu amekerwa na alichokisoma na kuambiwa.

Ili tusirudi tulikotoka na kumfanya Rais abaki kuvipa nguvu vyombo vyake, ni muhimu mchakato na taratibu za kihasibu na kisheria kufuatwa ili kwamba kama mtu atakutwa na hatia, aadhibiwe baada ya kukamilika kwa mchakato wa uchunguzi.

Wale wote wanaotaka Rais achukue hatua za papo kwa papo sasa hivi bila ya uchunguzi wa makini kwa sababu ya ripoti hii, hawaitakii mema nchi yetu.

Tunataka Rais ambaye anachukua hatua kwa kufuata katiba, sheria, kanuni na utaratibu (due process) baada ya uchunguzi kukamilika na hakuna anayeonewa. 

Wafanyakazi wa NAOT ni wanadamu na hivyo wanaweza kukosea hapa na pale.

Kama tunataka Rais wetu apate kile anachokitaka kutoka kwenye ripoti hizi na sisi wananchi tuendelee kuwa salama kwa sababu ya kuwa na Mkuu wa Nchi anayependa kufuatwa kwa taratibu zote, ni muhimu kuacha michakato iende mpaka mwisho.

Lakini katika yote, tusisahau jambo moja katika mijadala yetu, kwamba kama tumefurahi kuwa ripoti ya CAG imeshiba taarifa na inatoa picha halisi ya mahali tulipo kwenye uwajibikaji wa mali ya umma, tujue kwamba kuna mkono wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye hilo. 

Historia inatuonesha kuwa asili ya ripoti ya CAG ni kufichua madudu. Kwa vile watumishi wa umma ni wanadamu, jambo hilo halitabadilika. Kitakachobadilika ni Rais.

Kwa sababu hiyo, ni muhimu kutambua bahati tuliyonayo sasa ya kuwa na Rais anayetaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali atimize majukumu yake,.

Mwisho
Share:

Video Mpya : NELEMI MBASANDO ACHA KUNIZOEA

Share:

Ngoma Mpyaaa!! BHUDAGALA - GEREJI

 

Share:

Saturday, 8 April 2023

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI APRILI 9,2023

















Share:

AJIUA CHUMBANI AKIACHA MKEKA WA MADENI ANAYODAIWA



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Mwanaume aitwaye Ally Hamis (48) amejiua kwa kujinyonga ndani ya nyumba yake katika kijiji cha Itwangi Wilaya ya Shinyanga huku akiacha ujumbe kuhusu madeni anayodaiwa ndugu zake wayalipe.

Inaelezwa kuwa tukio hilo limebainika kutokea leo Jumamois Aprili 8,2023 majira ya asubuhi baada ya familia kumkuta Ally Hamis amejinyonga ndani ya nyumba yake.


Mwenyekiti wa kijiji cha Itwangi Kisendi Lubinza amesema Ally ameacha ujumbe kwa kuorodhesha madeni anayodaiwa na kuwaomba ndugu zake kulipa madeni hayo likiwemo deni la baskeli yake aliyokuwa anadaiwa sh 40,000/= , baba yake mdogo alipwe laki tatu na mwingine alipwe debe moja la mahindi.


"Kwenye wosia wake pia ameandika kwamba ‘nimeamua kujiua mimi mwenyewe asishikiliwe mtu yoyote nimeamua kwa moyo wangu, nimeamua kumfuata Mama yangu aliyetangulia mbele za haki miaka mingi iliyopita", ameeleza Mwenyekiti huyo wa kijiji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.


“Ni kweli mtu huyo alijinyonga na akaacha ujumbe kuwa ana madeni kwa hiyo askari wameshaenda wakakagua eneo la tukio walikuwa na daktari mwili umefanyiwa uchunguzi na walikabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishu”, amesema Kamanda Magomi
Share:

MIAKA MIWILI YA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN TARURA MKOA WA RUVUMA KAZI INAENDELEA


KATIKA kipindi cha miaka mwili ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mtandao wa barabara za vijijini na mijini kwa Mkoa wa Ruvuma zimeimarika maradufu.

Hatua hii imetokana na uamuzi wa dhati wa Rais Samia wa kuongeza bajeti kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Ruvuka kwa zaidi ya mara mara tatu.

TARURA Mkoa wa Ruvuma inahudumia jumla ya kilomita 7,146.202 za barabara, kati ya hizo kilomita 2,312.83 sawa na asilimia 32.36 ni za mjazio, kilomita 3,873.85 sawa na asilimia 52,85 ni mkusanyo na kilomita 959.52 sawa na asilimia 13.43 ya mtandao mzima wa mkoa ni za jamii/kijiji.

Anapozungumzia mafanikio ya miaka miwili ya Mheshimiwa Rais Samia, Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Wahabu Nyamzungu anasema mwaka 2020/21 mkoa ulitengewa Sh bilioni 7.973 za Mfuko wa barabara zilizotumika kufanya matengenezo ya kawaida ya kilomita 549.61 kwa Sh bilioni 1.356, sehemu korofi kilomita 137.29 kwa Sh bilioni 1.165, madaraja madogo 4, boksi kalavati 17, makalavati 11, madrifti 5 na mifereji ya maji yenye urefu wa mita 2,000 kwa gharama ya Sh bilioni 1.113,

Anasema hali ya mtandao wa barabara ulikuwa na kilomita 890.449 za barabara za changarawe sawa na asilimia 12.46, kilomita 93.635 barabara za lami sawa na asilimia 1.31, kilomita 3.92 barabara za zege na kilomita 6,159.19 zilikuwa barabara za udongo ambazo ni asilimia 12.46.

Anasema kuwa barabara zenye hali nzuri zilikuwa ni kilomita 1,391.453, hali ya kuridhisha kilomita 1,572.083, hali isiyoridhisha kilomita 4,182.667, madaraja 471, makaravati 1,940 na drifti 63.

“ Kwa kweli hali ya utekelezaji wa miradi ya barabara ilikuwa changamoto kubwa kwa kuwa bajeti ya utekelezaji wa miradi kwa mwaka ilikuwa finyu.”

Mhandisi Nyamzungu anasema kuwa mwaka 2021/22 ikiwa ni ndani ya miaka mwili ya uongozi wa Rais Samia TARURA Mkoa wa Ruvuma ulitengewa Sh bilioni 20.166 ambazo za tozo ya mafuta ni Sh bilioni 7, fedha za jimbo Sh bilioni 4.5, mfuko wa barabara Sh bilioni 7.383 na mfuko wa maendeleo Sh bilioni 1.283.

Anasema kwa mwaka 2022/23 Mkoa wa Ruvuma imetengewa bajeti ya Sh bilioni 23.757 na kati ya hizo fedha za tozo ya mafuta ni Sh bilioni 10.025, mfuko wa barabara ni Sh bilioni 6.918, fedha za miradi ya maendeleo ni Sh bilioni 1.39 na fedha za majimbo Sh bilioni 4.5.

“ Hivyo kwa miaka mwili ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan TARURA Mkoa wa Ruvuma tumepokea shilingi bilioni 43.924 zikiwa ni fedha za matengenezo ya barabara na madaraja.”

Anasema baada ya ongezeko la bajeti hali ya barabara kwa Mkoa wa Ruvuma imeimarika zaidi ambapo kilomita 1,372.581 ni barabara za changarawe, kilomita 118.688 ni barabara za lami, kilomita 6.92 ni barabara za zege na kilomita 5,658.41 ni barabara za udongo.

“Kwa sasa barabara zinazopitika kwa mwaka mzima zimefikia asilimia 35. Pia barabara zenye hali nzuri ni kilomita 2.250.387, zenye hali ya kuridhisha ni kilomita 1,767.889 na zile zilizo katika hali isiyoridhisha ni kilomita 3,127.913 na kuna madaraja 511, makalavati 2,130 na drifti 63.”

Anasema pia utekelezaji wa miradi ya barabara kwa sasa imeimarika ambapo ndani ya miaka mwili TARURA Mkoa wa Ruvuma umefanya matengenezo ya barabara kwa kiwango cha changarawe kilomita 482.132, ujenzi wa barabara za lami kilomita 25.053, ujenzi wa madaraja 40, ujenzi wa mifereji ya maji ya mua urefu wa mita 3,400.

Pia ujenzi wa barabara za zege katika maeneo yenye miinuko na miteremko kilomita 6.92, ufunguzi wa barabara mpya kilomita 500.03 ambazo hazijawahi kufunguliwa tangu tupate uhuru na kupunguza kiwango cha barabara za udongo kutoka kilomita 6,159.19 hadi kufikia kilomita 5,658.41.

Aidha, ongezeko la uwekaji wa taa za barabarani imeongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka idai ya taa 34- hadi kufikia taa 383 ikiwa bado idadi ya taa zinazotarajiwa kuweka mpaka kufikia Juni mwaka huu kufikia taa 420.

Mhandisi Nyamzungu anataja baadhi ya miradi ya kimkakati ambayo TARURA Mkoa wa Ruvuma imeitekeleza katika kipindi hicho ni ujenzi wa barabara ya Luhindo-Mpepo-darpori kwa kiwango cha changarawe urefu wa kilomita 27.52.

“Barabara hii imeongeza tija kwa wakulima wa kahawa na sekta ya usafiri na usafirishaji kwani kabla ya maboresho gari zilizokuwa zikitumiwa na wananchi wa Kata ya Mpepo ni landrover pekee lakini sasa basi za abiria zimeweza kufika.”

Mhandisi Nyamzungu anasema pia kufungua barabara za fukwe za Ziwa Nyasa kwa ajili ya kuhamasisha utalii katika Wilaya ya Nyasa ambazo zimeboreshwa kwa fedha za tozo za mafuta.

“Eneo la fukwe za Nyasa kata ya Kilosa na Mbamba Bay halikuwa na barabara zilizoboreshwa lakini katika kipindi cha miaka mwili ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tumeweza kufungua kilomita 14 za barabara za changarawe, barabara hizi zitaboresha na kuleta hamasa katika sekta ya utalii wa picha na kufutia wawekezaji wa ufukweni.”

Mhandisi Nyamzungu anasema pia kuondoa vikwazo kwa kujengwa madaraja na makalavati, kujenga barabara za lami kwenye katika miji na makao makuu ya kila wilaya, kufungua barabara mpya hasa katika maeneo ya uwekezaji mkubwa wa sekta ya kilimo na uchimbaji wa makaa ya mawe.

Kuendeleza barabara za mitaa kwa kiwango cha changarawe na kuweka taa katika miji mbalimbali kwenye maeneo ya miji.

“Tunachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuongoza kwa mafanikio hasa katika sekta ya mundombini na kuondoa vikwazo vya usafiri na usafirishaji wa mazao vijijini.”

“ Kwa kuongeza fedha kumeongeza ufanisi kwenye utekelezaji wa miradi, kuinua uchumi kwa wananachi wa kawaida hasa wakulima kwa kuwawezesha kusafirisha mazao ya kwa urahisi kuyafikia masoko na hatimaye kukidhi mahitaji yao kwa urahisi.”

Mhandisi Nyamzungu anaongeza: “tunamwomba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kutuwezesha TARURA ili tuweze kutimia kauli mbiu yetu isemayo ‘Tunakufungulia barabara kufika kusiko fikika’.”
Share:

LORI LAUA WAENDESHA BODABODA ZAIDI YA 10 KIJIWENI


Watu kadhaa wamepoteza maisha baada ya lori lililokuwa likisafirisha changarawe kupoteza mwelekeo na kugonga kundi la bodaboda waliokuwa wameegesha eneo lao (kijiweni) mjini Migori nchini Kenya.

Tukio hilo la asubuhi ya Jumamosi - Aprili 8,2023 limeshuhudia umati mkubwa wa watu ukimiminika eneo la tukio ili kuwanusuru majeruhi na kuwakimbiza hospitalini kwa matibabu. 

Kwa mujibu wa raia mmoja aliyeshuhudia na kuzungumza na runinga ya TV47, breki za lori hilo zilifeli na kuingia katika kundi hilo la bodaboda ambao walikuwa wanasubiri abiria. 

Ajali hiyo imefanyika karibu na shule ya msingi ya Migori. Eneo la tukio lilikuwa limejaa damu na miili. 

Vyuma pia vilikuwa vimetapakaa eneo hilo.

Eneo la tukio linaripotiwa kuwa na zaidi ya miili kumi huku ambulansi na wazima moto kutoka kwa serikali ya kaunti ya Migori wakifika eneo la ajali hiyo.
Share:

RIPOTI ZA CAG: UFISADI HAUJAZIDI NCHINI, KILICHOZIDI NI UHURU


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) zimeibua mjadala mkubwa na mpana nchini tangu zitolewe hadharani siku chache zilizopita.


Ripoti hizo za mwaka wa fedha wa 2021-2022 zimeweka bayana kasoro mbalimbali kwenye serikali kuu, tawala za mikoa na serikali za mitaa pamoja na mashirika ya umma.


Kasoro hizo ni pamoja na tuhuma za ubadhirifu wa pesa za umma na uendeshaji wa hasara wa baadhi ya mashirika ya umma.


Lakini, mambo yaliyoibuliwa na ripoti hizi mpya za CAG siyo mapya na siyo ishara ya kuongezeka kwa ufisadi nchini.


Mfuatiliaji yoyote makini wa ripoti za CAG atabaini kuwa mambo yaliyoibuliwa kwenye ripoti za mwaka huu yamekuwa yakiibuliwa pia kwenye ripoti za awamu zilizotangulia kwa miaka kadhaa sasa.


Kuna tofauti kuu saba zifuatazo kati ya mazingira ya utoaji wa ripoti za CAG chini ya Awamu ya Tano na utoaji wa ripoti za CAG kwenye Awamu hii ya Sita:


1. Kuongezeka kwa uhuru wa CAG


Tangu aliyekuwa CAG, Profesa Mussa Assad, kung’olewa kazini na utawala wa Awamu ya Tano kinyume na katiba kwa kusema ukweli na kusimamia kile anachokiamini, ofisi ya CAG imekosa uhuru wa kufanya kazi yake, hadi ilipoingia madarakani Serikali ya Awamu ya Sita na kurejesha uhuru huo kwa CAG.


Kwenye awamu iliyopita, CAG hakuwa na uhuru wa kukagua na kutoa ripoti za miradi ya kimkakati ya maendeleo, ikiwemo reli ya SGR, ununuzi wa ndege za ATCL, TTCL na ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa JNHPP, tofauti na sasa kwenye Awamu ya Sita ambapo amepewa uhuru kufanya ukaguzi na kubaini kasoro kadhaa kwenye miradi hiyo.


2. Kuongezeka kwa uhuru wa vyombo vya habari


Uhuru wa habari umeimarika kwenye Awamu ya Sita na kuvipa vyombo vya habari fursa ya kuripoti tuhuma zilizoibuliwa na CAG bila woga wa kufungiwa au kushughulikiwa na watu wasiojulikana.


Maana yake ni kwamba, maudhui yaliyomo kwenye ripoti za CAG yameripotiwa kwa uzito mkubwa na vyombo vya habari tofauti na hali ilivyokuwa chini ya Awamu ya Tano, ambapo wanahabari waliogopa kuripoti taarifa hizo.


3. Kuongezeka kwa uhuru wa vyama vya upinzani

Awamu ya Sita imerejesha uhuru wa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, na hiyo imewapa fursa viongozi wa upinzani kuzunguka nchi nzima kuzungumzia ripoti za CAG kwenye majukwaa ya siasa na hivyo basi kusambaza mjadala huo kila kona ya nchi.


Kiongozi mmoja wa chama kimoja cha upinzani alisikika akisema juzi kwenye mkutano wa hadhara kuwa angekuwepo aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, wote waliotajwa kwenye ripoti za CAG “wasingekuwepo.”


Kauli hiyo imewashangaza hata wafuasi wa chama hicho, kwani kiongozi huyo huyo wa upinzani alikimbia nchi kusalimisha maisha yake kwenye utawala wa Awamu ya Tano na mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani ilipigwa marufuku, ambapo asingeweza kuwa na jukwaa la hadhara la kuzungumzia ripoti za CAG.


4. Kuongezeka kwa uhuru wa wanaharakati

Taasisi zisizo za kiserikali pamoja na wanaharakati wamepata uhuru zaidi kwenye Awamu ya Sita kuzungumzia mambo mbalimbali, ikiwemo ripoti za CAG, tofauti na hali ilivyokuwa kwenye awamu iliyopita.


5. Kuongezeka kwa uhuru wa wabunge wa CCM

Wabunge wa chama tawala, ambao kwenye awamu iliyopita walizibwa mdomo na hawakuwa na uhuru wa kuikosoa serikali ndani na nje ya Bunge, sasa wanatumia uhuru wao chini ya Serikali ya Awamu ya Sita kupaza sauti zao juu ya kasoro zilizotajwa na CAG.


6. Kuongezeka kwa uhuru wa wastaafu

Viongozi mbalimbali wastaafu ambao kwenye Awamu ya Tano waliambiwa wakae kimya waache “kuwashwa washwa” sasa hivi wana uhuru wa kuongea, kushauri na hata kuikosoa serikali bila hofu yoyote.


7. Kuongezeka kwa uhuru wa kuongea wa wananchi


Tofauti na hali ilivyokuwa kwenye Awamu ya Tano ambapo wananchi walikosa uhuru wa kuongea na kuikosoa serikali, wananchi sasa wamerejeshewa uhuru huo chini ya Awamu ya Sita na wanautumia kujadili ripoti za CAG kwa uwazi bila woga.


Wachambuzi wa masuala ya utawala wanasema kuwa uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kurejesha tunu za taifa za uhuru na haki kwa kiasi kikubwa utachochea utulivu wa kisiasa na maendeleo endelevu nchini.


Mjadala unaoendelea wa ripoti za CAG umedhihirisha kuwa kilichozidi nchini siyo ufisadi wala uendeshaji mbovu wa mashirika ya umma, bali kilichozidi kwenye Awamu ya Sita kulinganisha na awamu iliyopita ni uhuru. Na hili ni jambo jema sana kwa mustakabali wa taifa letu.

Share:

Friday, 7 April 2023

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI APRILI 8,2023



























Share:

YESU WA TONGAREN AGOMA KUSULUBISHWA


Eliud Wekesa almaarufu yesu wa Tongaren kutoka kaunti ya Bungoma nchini Kenya ameonekana kuwajibu watu waliotaka asulubishwe wakati huu wa pasaka jinsi Yesu Kristo alivyofanyiwa.

Katika Video iliyosambazwa mtandaoni yesu wa Tongaren anasikika akisema kuwa katika maandiko yake na kuelewa kwake kwa kitabu kitakatifu hakuna mahali ambapo yesu alisulubishwa mara mbili.

"Sijawahi kuona mahali popote hata katika chuo changu cha mbinguni kwamba waliandika yesu atasulubiwa mara ya pili," Yesu wa Tongaren alisema. 

Yesu wa Tongaren alisema kuwa imeandikwa kuwa yesu atakaporudi atakuwa sawa na bali hatorejelea tena katika usulubissho aliopitia kuwakomboa wanadamu.

Yesu wa Tongaren ameongoza ibada ya maombi ya siku kuu ya pasaka katika kanisa lake na kusema kuwa watafunga kwa kwa siku tatu wakiomba.
Share:

AUAWA KWA KUCHOMA KISU BAADA YA KUOMBA MAJI YA KUNYWA TANGA

Jeshi la Polisi Mkoani Tanga linamshikilia Hassan Nyundo (25) Mkazi wa Kijiji cha Vue kata ya Mowa Wilayani Mkinga kwa tuhuma za kumchoma kisu Amiri Mohamed (30) huku ikidaiwa kwamba sababu mojawapo ya ugomvi ni kitendo cha Amiri kumuomba maji ya kunywa wakati akifahamu kuwa Hassan amefunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

RPC Henry Mwaibambe amesema kuwa 05/04/2023 majira ya saa sita mchana Amiri na Mtuhumiwa walikuwa wakiishi nyumba moja hivyo hadi mauti yanamkuta Amiri alimshinikiza Mtuhumiwa kumpatia maji ya kunywa kitendo kilichomchukiza Hassan (Mtuhumiwa) na kusababisha ugomvi uliopolekea kumchoma kisu kulikosababisha kufia njiani wakati akiwaishwa Hospitali.

Kamanda Mwaibambe amesema hadi sasa kuna taarifa mbili juu ya tukio hilo ambapo wengine wanasema Mtuhumiwa alichukizwa na kitendo cha Amiri kumuomba maji pamoja na kunywa maji wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani lakini wengine wanasema ni ugomvi wa kawaida.

“Kwakweli hadi sasa chanzo kamili cha tukio hilo bado hakijajulikana kwani hawa wawili ni ndugu waliokuwa wakiishi nyumba moja, ni mauaji ya kusikitisha sana haiwezekani ugomvi wa maji tu unachomoa kisu una mchoma mwenzako, kwakweli huu ni mmomonyoko mkubwa wa maadili”.
Share:

LEMBELI ATEMBELEA MAENEO YA KIHISTORIA NEW YORK - MAREKANI..ASEMA TANZANIA INALIPA KIPAUMBELE SUALA LA UHIFADHI NA ULINZI WA MAZINGIRA


Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jane Goodall Tanzania Bw. James Lembeli ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo nchini Marekani na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kahama akiwa katika Bustani ya New York City Park.
**
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jane Goodall Tanzania Bw. James Lembeli ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo nchini Marekani na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kahama amesema Tanzania,kama ilivyo kwa nchi nyingine inalipa kipaumbele suala la ulinzi wa mazingira na uhifadhi kuepusha janga linaloweza kutokea kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambazo tayari katika nchi nyingine zimeanza kuleta madhara makubwa.


Ametaja madhara hayo ni mafuriko,vimbunga,joto kali na kuyeyuka kwa theluji huko antaktika na ktk vilele vya milima ikiwemo kilimanjaro kuwa ni mifano halisi.


Lembeli amesema hayo juzi mjini New York wakati akiongea na wadau wa masuala ya mazingira kutoka sehemu mbambali za Dunia wakati wa ghahla ya kumpongeza mwanzilishi taasisi ya Jane Goodall kutimiza miaka 89 na miaka karibu miaka 63 tangu atue Kigoma,Tanzania kuanza kazi ya utafitiwa wa Sokwe na wanyama wengine aina ya Nyani.


Amesema,Kwa kutambua msimamo wa Tanzania ktika sekta za mazingira na uhifadhi,serikali ya Marekani kupitia shirika lake la misaada USAID ilitoa msaada wa Dola milioni 20 kwa ajili ya mradi wa kuimarisha na kuboresha mazingira katika mikoa ya Kigoma na Katavi ulioanza mwaka 2013 na ambao utamalizika novemba mwaka huu.


Mradi huo umejikita hususani katika elimu ya kuhifadhi misitu ya asili katika maeneo hayo,afya na elimu ya kujitegemea hususani Amina mama na vijana vijiji.


Taasisi ya Jane Goodall ambayo chimbuko lake ni Gombe, Kigoma Tanzania ambako muasisi wake (Jane Goodall) alifika kuanza kazi ya utafiti wa Sokwe na wanyama aina ya nyani inafanya kazi ktk nchi zaidi ya 60 ulimwenguni ikiwa imejikita kuhusani katika suala la elimu ya uhifadhi wa mazingira kupitia programu yake ya vijana ya Roots and Shoot-lengo likiwa ni kuiponya Dunia na tatizo la uharibifu wa mazingira hivyo kuwa sehemu Bora ya kuishi wanadamu na viumbe vingine.


Akiwa New York,lembeli licha ya kuhudhuria kikao cha Bodi ya Wakurungenzi ya Jane Goodall-Marekani pia alipata fursa ya kukutana na watu mbalimbali na kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria ikiwa pamoja na kanisa Kuu katoliki la Mtakatifu Patrick ambapo alipata fursa ya kuingia na kusali, Bustani kubwa ya mjini New York, New York Central Park, Makumbusho ya Brooklyn na Lockfeller Center.


Sherehe ya miaka 89 ya kuzaliwa Jane ilifanyika katika hoteli maarufu ya mjini New York Litz Calton.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jane Goodall Tanzania Bw. James Lembeli ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo nchini Marekani na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kahama akiwa katika Bustani ya New York City Park
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jane Goodall Tanzania Bw. James Lembeli ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo nchini Marekani na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kahama akiwa katika Bustani ya New York City Park
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jane Goodall Tanzania Bw. James Lembeli ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo nchini Marekani na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kahama akiwa katika  kanisa kuu la Mtakatifu Patrick-New York
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jane Goodall Tanzania Bw. James Lembeli ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo nchini Marekani na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kahama akiwa katika  kanisa kuu la Mtakatifu Patrick-New York
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jane Goodall Tanzania Bw. James Lembeli ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo nchini Marekani na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kahama akiwa katika Rockefeller Center
Studio za radio na NBC tv
Share:

PROGRAMU YA TAIFA YA KUKUZA UJUZI YAWAKUNA WABUNGE


Mbunge wa Kigoma Mjini Mhe. Kilumbe Ng'enda ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna inavyoshoghulikia changamoto ya ajira kwa vijana nchini kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambayo imekuwa chachu ya vijana kujiajiri na kuajiri wenzao. 

Akichangia Aprili 6, 2023 bungeni mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, Mbunge huyo amesema programu hiyo iwe endelevu kwa kuwa ina manufaa yenye tija kwa nguvukazi ya Taifa kupata ujuzi unaowawezesha kujiajiri sambamba na kujikwamua kiuchumi.

 "Nimetembelea Chuo cha VETA Kigoma nimeshuhudia kijana ameweza kutengeneza redio na anarusha matangazo mwenyewe katika jamii inayomzunguka, hivyo kijana huyo akiendelezwa anaweza kufanya mambo makubwa sana," amesema. 

Vilevile, amesema uwepo utaratibu wa kuwawezesha vitendea kazi vijana hao wanapomaliza mafunzo yao ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. 

Pia, ameshauri serikali kuweka utaratibu maalum wa kuendeleza vipaji vya vijana wabunifu ambao wamenufaika na programu hiyo.
Share:

WAZIRI MHAGAMA,SIMBACHAWENE WAKABIDHIANA OFISI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Watumishi wa Ofisi hiyo (hawapo pichani)  wakati wa makabidhiano ya Ofisi kati yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi  wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene yaliyofanyika Jijini Dodoma..





Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene  ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi  wa Umma na Utawala Bora akimkabidhi nyaraka  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)  Mhe. Jenista Mhagama  wakati wa hafla ya  makabidhiano ya Ofisi  kati yao.  Kulia ni Katibu  Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi katika Ukumbi wa Ofisi hiyo  Aprili 06, 2023 Jijini Dodoma.


Na Mwandishi wetu, DODOMA.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amewataka watumishi wa umma kutekeleza  majukumu yao ipasavyo  kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo wakati wa hafla ya makabidhiano  kati ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya uteuzi uliyofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia  Suluhu Hassan  Aprili 01 mwaka 2023.

Waziri  Mhagama  amesema dhamira ya mtumishi wa umma Nchini ni kuhakikisha anatimiza wajibu wake kikamilifu katika kuwahudumia wananchi mahali na kwa nafasi yoyote anayopangwa  kwa kuzingatia miongozo na taratibu  zilizopo.

“Mara zote dhamira ya mtumishi wa umma  Nchini ni kuhakikisha kila unapopangwa unafanya kazi kwa nguvu zako zote pamoja na utii  na kuwa tayari kutumikia Taifa mahali popote kwahiyo kurudi kwangu hapa najihesabu ni sehemu yenu pia kama mtumishi wa umma,” Amesema Mhe. Jenista.

Pia amebainisha kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ina jukumu la kuratibu shughuli za Serikali haiwezi kufanikiwa ikiwa watumishi wake watashindwa kujidhatiti na kufanya kazi kwa moyo kwa kuzingatia mazingira husika.

“Msingi wa tija katika utendaji wa kazi Serikalini  unatutaka  kuwa na uratibu mzuri unaozingatia sera, miongozo na kanuni zilizopo kwa kuzingatia jukumu kubwa la Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu shughuli zote za Serikali na tuna jukumu la kusimamia Bunge kama mhimili mwingine ndani ya Nchi hivyo bila kuwa na ushirikiano hatutafikia malengo tunayokusudia,” Ameeleza.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amemshukuru  Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa  kumuamini na kumpa  fursa ya kulitumikia Taifa pamoja na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu  kwa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.

“Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini  kuendelea  kuwatumikia wananchi katika nafasi hii na watumishi pia nawashukuru kwa ushirikiano mlionipatia na kuwezesha kufanikisha shughuli za uratibu kwa kipindi chote,” Ameshukuru Mhe. Simbachawene.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amemshukuru Mhe. Simbachawene kwa utumishi wake mwema katika Ofisi hiyo.

Aidha ametumia nafasi hiyo kumkaribisha Mhe. Waziri Mhagama katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuahidi kumpa ushirikiano ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananachi.

 

 

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger