Tuesday, 6 September 2022
Monday, 5 September 2022
TBS YATOA MAFUNZO KWAWATUMISHI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA PWANI
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bi.Zuwena Jiri akifungua mafunzo kwa Watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mkoani Pwani kujifunza mwongozo wa utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) yaliyofanyika leo Septemba 5,2022 Kibaha mkoani Pwani. Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bi.Zuwena Jiri akizungumza katika mafunzo kwa Watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mkoani Pwani kujifunza mwongozo wa utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) yaliyofanyika leo Septemba 5,2022 Kibaha mkoani Pwani.Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Yusuph Ngenya akikisitiza jambo wakati akizungumza katika mafunzo kwa Watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mkoani Pwani kujifunza mwongozo wa utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) yaliyofanyika leo Septemba 5,2022 Kibaha mkoani Pwani. Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Yusuph Ngenya akizungumza katika mafunzo kwa Watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mkoani Pwani kujifunza mwongozo wa utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) yaliyofanyika leo Septemba 5,2022 Kibaha mkoani Pwani. Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bi.Zuwena Jiri akipata picha ya pamoja na Watendaji wa halmashauri tisa za Mkoa wa Pwani wakati wa ufunguzi wa mafunzo juu ya kujifunza mwongozo wa utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) leo Septemba 5,2022.
(PICHA ZOTE EMMANUEL MBATILO)
*************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Pwani Bi.Zuwena Jiri amesema Serikali imeazimia kwa dhati kuendeleza biashara kwa kuhakikisha bidhaa za chakula na vipodozi zinakidhi matakwa ya viwango vya ubora na usalama.
Ameyasema hayo leo Septemba 5,2022 wakati akifungua Mafunzo mafunzo kwa Watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mkoani Pwani ambapo ametoa rai kwa watumishi wa serikali kuwa majukumu waliyopewa yawe chachu ya kutumikia umma kwa bidii bila ubaguzi, kuwashauri na kuwasaidia kitaalamu pale inapohitajika (tusibweteke), ili bidhaa zetu ziwe bora na salama na uchumi wetu uendelee kukua.
Amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaelimisha watumishi kutoka ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhusu Sheria, Kanuni na miongozo inayohusika na utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano baina ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na TAMISEMI.
Aidha amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa inakuwa na mtandao mkubwa unaoshughulikia shughuli za udhibiti wa ubora na usalama wa chakula na vipodozi.
"Kwa kulitekeleza hili Serikali imeamua kuwatumia wakaguzi walio chini ya ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika shughuli za udhibiti wa bidhaa husika ili kulinda afya za watumiaji katika maeneo yao. Kwa kufanya hivi, itasaidia kuhakikisha shughuli za udhibiti zinafanyika kwa haraka na ufanisi zaidi'. Amesema RAS Zuwena.
Hata hivyo amesema mafunzo hayo ni njia muafaka ya kuleta tija zaidi katika juhudi za kuleta maendeleo katika udhibiti wa bidhaa za chakula na vipodozi katika mkoa na Taifa kwa ujumla pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wanahudumiwa kwa haraka pale inapohitajika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Yusuph Ngenya amewataka Wafanyakazi wanaopatiwa mafunzo hayo kufanya kazi kwa weledi kwa kuwapa elimu ya kutosha wafanyabishara na wahusika wote ili huduma ziweze kuwafikia wahitaji wa chini.
"Sisi tunaenda kuwahudumia wananchi wa chini kwenye huduma za chakula na vipodozi kwa hawa wanaopatiwa mafunzo leo hivyo tuwaelimishe Wafanyabishara na siyo kusukumana polisi vile hivyo tuelimishane kama kuna mfanyabiashara atakuwa haijakidhi viwango ili aweze kukidhi viwango husika". Amesema Ngenya.
KAMBI YA TFS YAVAMIWA WAWILI WAUAWA, SITA WAJERUHIWA
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Filemon Makungu (wa pili kushoto) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na kuuawa kwa watu wawili na wengine sita kujeruhiwa na wafugaji katika kijiji cha Mvinza wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WATU wawili wamekufa na wengine sita kujeruhiwa baada ya watu wanaoaminika kuwa wafugaji kuvamia kambi ya Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) kwenye kijiji cha Mvinza wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma,Filemon Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma leo amesema kuwa uvamizi huo ulifanyika kwenye kambi hiyo iliyopo kwenye hifadhi ya msitu wa Makere Kusini mkoani Kigoma mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kamanda Makungu aliwataja waliokufa kuwa ni pamoja na Mkazi wa kijiji cha Mvinza aliyejulikana kwa jina moja la Salvatory ambaye alikuwa kibarua kwenye shamba hilo la miti la TFS ambaye alichomwa na vitu vyenye ncha kali na kufariki dunia wakati wa uvamizi huo.
Aidha alisema kuwa jana polisi wakiwa kwenye ukaguzi wa eneo hilo kuangalia athari ya tukio hilo maiti ya mtu mwingine ilipatikana ambaye alitambulika kwa jina la Thomas Alfred aliyekuwa akifanya kazi za vibarua kwenye kambi hiyo ya TFS mwili wake ukiwa na majeraha makubwa shingoni.
Aliwataja waliojeruhiwa kwenye tukio hilo kuwa ni pamoja na Dora Nicolaus na David Lazaro ambao ni watumishi wa Suma JKT wakiwa kwenye kazi ya ulinzi ya kambi hiyo, Amon Moshi Mtunza Bustani, Ndayishimiye Haruna Mkulima wa bustani na Elcado Enos Mkulima.
Sambamba na mauaji na watu hao kujeruhiwa pia vitu mbalimbali vimeteketezwa kwa moto likiwemo trekta mali ya TFS,nyumba moja ya tofali za kuchoma iliyoezekwa na bati ikitumika kama ofisi, pikipiki sita za watuhumiwa waliokamatwa kwa kuingia kwenye hifadhi yam situ kinyume cha sheria, gunia 20 za maharage, gunia 70 za mahindi, gunia 30 muhogo na gunia 20 za mtama.
“Taarifa za awali zinaonyesha kuwa siku za karibuni kuna ng’ombe ambao idadi bado haijajulikana ya wafugaji walikamatwa na kuchukuliwa na maafisa wa TFS kwa tuhuma za ng’ombe hao kuingizwa kwenye hifadhi ya msitu kwa ajili ya malisho, hivyo vurugu hizo zimekuja kama nia ya watu hao kulipiza kisasi kwa mifugo yao kukamatwa na ndiyo maafa hayo yametokea,”alisema Kamanda Makungu.
Hadi sasa watu watatu ambao wanaaminika ni sehemu ya wafugaji hao wamekamatwa na wanashikiliwa na polisi wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea kuhusiana na tukio hilo.
BARRICK NORTH MARA YAANDAA LIGI YA SOKA YA ‘MAHUSIANO CUP’ TARIME…VIONGOZI, WANANCHI WAIPONGEZA KULETA BURUDANI
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (mwenye kofia mbele) na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara wakikagua timu wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Mahusiano Cup
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko (aliyesimama) akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mashindano hayo
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (kulia) akizungumza na timu za Kewanja FC na Mosege FC wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo.
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (kushoto) akishiriki kucheza ngoma ya asili wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, (mwenye kofia) akikagua timu ya waamuzi wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo
Wananchi wakishiriki mashindano mbalimbali wakati wa uzinduzi huo
Wananchi wakishiriki mashindano mbalimbali wakati wa uzinduzi huo
Wananchi wakishiriki mashindano mbalimbali wakati wa uzinduzi huo
Wananchi wakishiriki mashindano mbalimbali wakati wa uzinduzi huo
***
-Viongozi, Wananchi waipongeza kwa kuleta burudani katika maeneo yao
Mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, umeandaa mashindano ya soka ya kuwania kombe la ‘Mahusiano Cup’ yanayojumuisha vijiji 16 vinavyozunguka mgodi huo ambayo yalizinduliwa rasmi jana katika viwanja vya shule ya sekondari ya Ingwe wilayani Tarime.
Mashindano haya yenye kauli mbiu ya “Mahusiano bora kwa uwekezaji Endelevu” yaliwashirikisha wananchi kutoka vijiji mbalimbali na wafanyakazi wa Barrick North Mara, ambapo waliburudika kwa kucheza michezo ya aina mbalimbali. Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa ni Mkuu wa wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mtenjele, aliyeongozana na viongozi mbalimbali wa Serikali wilayani humo.
Vijiji ambavyo timu zake zinashiriki katika mashindano hayo ni Genkuru, Msege, Komarera, Nyamwanga, Kewanja, Nyakunguru, Kerende, Nyabichume, Mji Kati, Matongo, Nyangoto, Mrito, Keisangoro na Nyarwana.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, alisema michezo ni nyenzo muhimu katika kujenga na kudumisha uhusiano katika jamii “Bila mahusiano bora na jamii inayotuzunguka sisi kama kampuni hatuwezi kufanya kazi kwa utulivu,hali ambayo inaweza kusababisha uwekezaji wetu usiletee manufaa katika pande zote mbili”,alisema.
Mkuu wa wilaya ya Tarime, Kanali Mntenjele, aliwataka washiriki wa mashindano hayo kucheza kwa amani na wasimamizi husika kutenda haki bila kupendelea timu yoyote.
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, aliipongeza Barrick North Mara, kwa kuandaa mashindano hayo,alisema yatahamasisha ushirikiano kutoka kwa jamii inayozunguka Mgodi huo ili kuwezesha kila upande kunufaika.
Wakiongelea kuhusu mashindano haya, baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliipongeza Barrick North Mara, kwa kuleta mabadiliko chanya mbalimbali kupitia uwekezaji wake ikiwemo kuwapatia wananchi burudani kupitia mabonanza ambayo yamekuwa yakiandaliwa na kufadhiliwa na mgodi huo.
JESHI LA POLISI LAMKAMATA MWANAMKE ALIYEMFANYIA UKATILI MTOTO WAKE
JESHI la Polisi nchini Uganda, linamshikilia Dorothy Nabulime (22) mkazi wa mji mdogo wa Busula, nje kidogo ya jiji la Kampala kwa tuhuma za kumpiga na kumfanyia ukatili mwanae wa kike mwenye umri wa miaka miwili.
Dorothy mama wa watoto watatu alirekodiwa video akimpiga mwanae huyo bila huruma na kumuangusha kwenye beseni alilokua anaogea.
Mwanae mkubwa ana miaka 5 ambaye alimzaa akiwa na miaka 17. Wa pili ana umri wa mitatu na wa mwisho ana miaka miwili ambaye ndiye aliyerekodiwa akimpiga. Dorothy ni “single mother” ambaye anadaiwa kupitia unyanyasaji wa kijinsia katika malezi yake, na anawalea watoto wote watatu peke yake kwa biashara ndogondogo.
Amefunguliwa kesi ya shambulio la kudhuru mwili (assault causing bodily harm) na unyanyasaji wa mtoto (child abuse) na anatarajiwa kupandishwa kizimbani kesho, jumatatu kujibu tuhuma zinazomkabili. Kwa sasa anashikiliwa kituo cha polisi Luwero, huko Busula na amefunguliwa kesi nambari SD/RF/06/03/09/2022.
Ikiwa atapatikana na hatia anaweza kufungwa kati ya miaka miwili hadi mitano Gerezani.!
BENKI YA CRDB YAZINDUA PROMOSHENI YA TISHA NA TEMBO CARD JIJINI DODOMA
MENEJA wa Benki ya CRDB Kanda ya Kati,Chabu Mishwaro,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Promosheni Maalum ya Matumizi ya Kadi iliyopewa jina la ''Tisha na TemboCard'' kwa Kanda ya Kati iliyofanyika leo Septemba 2,2022 jijini Dodoma.
MENEJA wa Biashara Kanda ya Kati Jane Maganga,akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Promosheni Maalum ya Matumizi ya Kadi iliyopewa jina la ''Tisha na TemboCard'' kwa Kanda ya Kati iliyofanyika leo Septemba 2,2022 jijini Dodoma.
MENEJA wa Benki ya CRDB Kanda ya Kati,Chabu Mishwaro (Kusoto) akizindua Promosheni Maalum ya Matumizi ya Kadi iliyopewa jina la ''Tisha na TemboCard'' kwa Kanda ya Kati.Kulia ni Meneja Mwandamizi Malipo ya Kadi kutoka CRDB Bw.Victor Makere hafla iliyofanyika leo Septemba 2,2022 jijini Dodoma.
MENEJA Mwandamizi Kitengo cha Kadi kutoka CRDB Bw.Karington Chahe,akielezea jinsi promosheni hiyo itakavyokuwa inafanyika mara baada ya kuzinduliwa kwa Promosheni Maalum ya Matumizi ya Kadi iliyopewa jina la ''Tisha na TemboCard'' kwa Kanda ya Kati iliyofanyika leo Septemba 2,2022 jijini Dodoma. Dodoma.
MTEJA wa CRDB Husna Mchana,ambaye ni mhudumu kutoka Kampuni ya Afroil Investment Pump,akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Promosheni Maalum ya Matumizi ya Kadi iliyopewa jina la ''Tisha na TemboCard'' kwa Kanda ya Kati iliyofanyika leo Septemba 2,2022 jijini Dodoma.
MENEJA wa Benki ya CRDB Kanda ya Kati,Chabu Mishwaro,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua Promosheni Maalum ya Matumizi ya Kadi iliyopewa jina la ''Tisha na TemboCard'' kwa Kanda ya Kati iliyofanyika leo Septemba 2,2022 jijini Dodoma.
MENEJA wa Benki ya CRDB Kanda ya Kati,Chabu Mishwaro,akicheza burudani na wafanyakazi wa CRDB mara baada ya kuzindua Promosheni Maalum ya Matumizi ya Kadi iliyopewa jina la ''Tisha na TemboCard'' kwa Kanda ya Kati iliyofanyika leo Septemba 2,2022 jijini Dodoma.
***************
BENKI ya CRDB imezindua Promosheni maalum ya matumizi ya kadi iliyopewa jina la “Tisha na TemboCard” kwa Kanda ya Kati itakayoendeshwa kwa kipindi cha miezi 3 kuanzia ilivyozinduliwa rasmi Kitaifa jijini Dar-es-Salaam mnamo Agosti 18,mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo leo Septemba 2,2022 jijini Dodoma Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kati,Chabu Mishwaro,amesema lengo la Promosheni hiyo ni kuwahamasisha wateja na Watanzania kujenga utamaduni wa kutumia kadi zao kufanya manunuzi na malipo ya huduma.
Bi.Mishwaro amesema kuwa bado watanzania wengi hawana mwamko wa kutosha juu ya matumizi ya kadi.
“Promosheni hii ina lengo la kuwahamasisha wateja na watanzania kujenga utamaduni wa kutumia kadi zao kufanya manunuzi na malipo ya huduma huku wakijishindia zawadi,”amesema .
Aidha amezitaja zawadi hizo ni fedha taslimu kila mwezi kwa wateja watatu ambapo watajishindia Sh.Milioni moja kwa mshindi wa kwanza, wengine washindi wawili watapata Sh.500,000 .
“Na kubwa zaidi ni safari ya kwenda nchini Qatar iliyolipiwa kila kitu kwa wateja wanne wa TemboCard, washindi ni wale tu watakaokuwa na miamala mingi kupitia kadi zao za TemboCard,”alisema.
Bi.Misharo amesema kadi hizo zinatumika kupitia ATMs, matawi, CRDB Wakala, Mashine za malipo za (POS) na kufanya manunuzi na malipo kwa njia ya mtandao ndani na nje ya nchi.
''Ni matumaini yangu kuwa kampeni hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga utamaduni wa watu kutumia kadi zao kufanya malipo na manunuzi.''amesema
Hata hivyo amewasihi wateja wote wenye kadi za TemboCard kufurahia urahisi wa kufanya malipo popote pale walipo huku wakijiwekea nafasi ya kushinda zawadi.
Amesema kuwa wateja ambao hawana akaunti katika Benki ya CRDB huu ndio wakati wa kufungua akaunti na kuanza kuweka fedha ili kurahisisha kufanya miamala kupitia TemboCard zao ambazo watapewa baada ya kufungua akaunti.
Naye , Meneja Biashara Kanda ya Kati, Jane Maganga, amesema kuwa promosheni hiyo ni ubunifu wa CRDB katika kuwarahisishia wateja wake kupata huduma mbalimbali.
“Hii promosheni ya Tisha na TemboCard ni shindano ambalo litampa mabadiliko mteja, atakuwa akihitaji huduma au bidhaa anatumia kadi yake kuchanja tu na kulipia badala ya kutoa burungutu la fedha,”amesema Maganga
Sunday, 4 September 2022
WANANCHI MOROGORO WAASWA KUKAMATA FURSA ZA MTANDAONI
Na Mwandishi Wetu
Ili kupata manufaa ya huduma za teknolojia ya Habari na Mawasiliano wakazi wa Morogoro wamesisitizwa kutumia fursa za mtandaoni kujinufaisha katika kukuza shughuli za kilimo, ujasiriamali, elimu na ukuzaji tija katika Maendeleo binafsi na ya taifa.Afisa wa TCRA Bi. Rehema Kihiyo akiwahudumia wajasiriamali wadogo katika soko la gulio la SabaSaba, mjini Morogoro. PICHA: TCRA
Hayo yalibainishwa na Afisa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wakati akitoa elimu kwa wananchi waliofika kujipatia mahitaji mbalimbali katika soko la mnada wa Jumapili ‘gulio’ ambalo hufanyika kila Jumapili mjini Morogoro eneo la Sabasaba.
Mamlaka ya Mawasiliano ilifika kwenye soko hilo la mnada kuwapa wananchi elimu juu ya matumizi ya huduma za Mawasiliano ikiwemo fursa zinazopatikana katika anga la kimtandao “the cyber space”. Ulikaye aliwaeleza wananchi kuwa TCRA kupitia kampeni yao ya Kwea Kidijitali wanalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu stahiki ya matumizi sahihi na salama ya mtandao, ikiwa ni Pamoja na kung’amua fursa zilizomo kwenye anga la kimtandao.
“Mitandao ina fursa lukuki zikiwemo kupata elimu kwa wanafunzi, kujifunza na kupata masoko ya shughuli zako za ujasiriamali, kilimo, biashara na nyingine nyingi zinazokuwezesha Kukwea Kidijitali; TCRA tunasisitiza unapotumia mitandao hiyo hakikisha umehakiki usajili wa laini zako za simu kwa kubofya *106#, kisha ufuate maelekezo,” alisisitiza Ulikaye.
Alibainisha kuwa unapobaini namba usiyoifahamu fika kwa mtoa huduma wako na kuiondoa mara moja. Aidha, alisisitiza kuwa kutoa taarifa kwa kikosi kazi kinachohusisha Jeshi la Polisi, mtumiaji wa huduma za Mawasiliano mara anapopokea ujumbe wa kitapeli, anapaswa kuiripoti namba iliyomtumia ujumbe huo kwenda namba 15040, huduma aliyosisitiza kuwa haitozwi gharama zozote kwa mtumiaji wa huduma anaetoa taarifa.
Katika kazi hiyo ya kuwaelimisha wananchi kuhusu Mawasiliano TCRA iliambatana na watoa huduma wote wa Mawasiliano ya simu Pamoja na Jeshi la Polisi, kwa shabaha ya kuwapatia wananchi wa Morogoro huduma zilizokamilika kuhusu Mawasiliano.
Akizungumzia ushiriki wa Jeshi la Polisi kwenye kampeni hiyo ya elimu kwa umma, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ambae pia anasimamia Kitengo cha Mitandao Fadhili Ally Magombela alibainisha lengo la Jeshi hilo kuhakikisha wananchi wanapata elimu kwa kina kuhusu usalama wao wanapokuwa kwenye anga la mtandao.
“Maisha kwenye mtandao hayatofautiani sana na Maisha katika ulimwengu wa kawaida, kwa hiyo tunapenda kuwasisitiza wananchi, wakati wote kuhakikisha wanakuwa makini wanapokuwa kwenye mazingira ya kimtandao, kwa kuwa uhalifu huko ni halisi, aidha tunawaasa wananchi ukitapeliwa au kunusurika katika utapeli mtandaoni hakikisha unatoa taarifa katika kituo cha Polisi Jirani yako ili hatua zichukuliwe” alibainisha Afisa huyo wa Polisi.
MFAHAMU ASKOFU CHITETO ALIYEFARIKI BAADA YA MAHUBIRI MSIBANI
MFAHAMU KWA UFUPI MAREHEMU ASKOFU CANON, CAPT, GEORGE YORAM CHITETO, DAYOSISI YA MPWAPWA KANISA ANGLIKANA TANZANIA
Na Maiko Luoga +255 762 705 839
Mhashamu Baba Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Maimbo Mndolwa, kwa masikitiko amewajulisha Waumini wa Dayosisi ya Mpwapwa na Tanzania kwa ujumla Taarifa za kifo cha CAPT. GEORGE YORAM CHITETO, Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Mpwapwa kilichotokea Septemba 03, 2022.
Askofu Chiteto alifariki Dunia muda mfupi baada ya kutoa Mahubiri katika Misa ya kuaga mwili wa Hilda Lugendo aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Ushirika wa Mama wa Kikristo (UMAKI), Kanisa Anglikana Tanzania, iliyo fanyika katika Kanisa Anglikana Kristo Mfalme Muheza Dayosisi ya Tanga.
Katika Mahubiri yake Askofu Chiteto alitembea na ujumbe wenye kichwa cha neno uliosema JITAHIDI KUINGIA, alifafanua ujumbe huo kutoka Kitabu cha Injili kama alivyoiandika Luka Mtakatifu sura ya 13 aya ya 24 inayoeleza “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba kwa maana wengi watatamani kuingia lakini hawataweza”
Kupitia ujumbe huo aliwashauri Wakristo kufanya bidi ya kumtumikia Mungu ili kujijengea heshima au hadhi mbele za Mungu ili wanapomaliza kazi na kufariki Dunia, Mungu awapokee katika ufalme wa Mbingu,
Aidha alitoa mfano wa Mama mmoja aliyekuwa akiuugua na kuweweseka katika hatua za mwisho za kufariki ndipo Askofu Chiteto alialikwa kwenda kumfanyia maombi alipofika hapo alimwambia mama huyo kuwa aseme japo neno moja la kutubu kwa Mungu ili aweze kuingia katika mlango mwembamba lakini Mama huyo hakutaka kutubu hadi alipofariki Dunia.
“Nilipofika Hospital mama yule alikuwa anahangaika anawaambia Madakitari kuwa anaona giza anawataka wafungue mapazia, mimi nilipofika nilimwambia Mama ebu sema japo neno moja la kutubu ili Mungu akusamehe uingie mbinguni lakini hakutaka akaishia kunitukana hadi alipofariki katika mazingira hayo ya kutukana”
Alitoa mfano wa pili akimzungumzia kijana mwimbaji wa Kwaya ambae alienda kumuongoza maombi kuwa Kijana huyo alimweleza Askofu Chiteto kuwa anaona mlango umefunguka malaika wanapanda na kushuka na Yesu amesimama pembeni kisha Kijana huyo akafumba macho na kufariki Dunia hivyo alisema anaamini Kijana huyo alikufa kifo kizuri.
“Niliona kijana yule ana hadhi kubwa, mimi palepale nikasema na Mungu kifo changu kiwe hivihivi yaani isibadilike hata sentesi moja, yaani unapokuja kuniita mlango uwe umefunguka sio kusema fungua fungua, Tujiulize sote kama tuna hadhi au wenye hadhi ni wachache?” alihoji Askofu George Chiteto dakika chache kabla ya kufariki Dunia.
Mara baada ya kumaliza kutoa mahubiri kwenye Ibada hiyo, Dakika chache baadae Askofu Chiteto Alijisikia vibaya na kukimbizwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga ambapo alifariki Dunia wakati jitihada za kuokoa uhai wake zikiendelea, Taarifa ya kifo chake ilithibitishwa na Madaktari kwa Askofu Mkuu ambae aliwatangazia waumini Msiba huo.
Marehemu Askofu CAPT. GEORGE YORAM CHITETO aliwekwa wakfu na kuwekwa kitini kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa, Kanisa Anglikana Tanzania siku ya BWANA ya tarehe 28 Agosti mwaka huu 2022 katika Kanisa la Watakatifu wote Mpwapwa.
Alizaliwa tarehe 7 Desemba, mwaka 1962 katika kijiji cha Inzomvu Wilaya ya Mpwapwa, Alisoma shule ya msingi Inzomvu mwaka 1975 hadi mwaka 1981, Baada ya hapo akajiunga na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Chisalu kwa kozi ya Kilimo na ufugaji mwaka 1981, Mwaka 1984 – 1985 alijiunga na Chuo cha Jeshi la Kanisa (Church Army) Nairobi nchini Kenya.
Mwaka 1987 aliamuriwa kwa daraja la Ushemasi akatumika katika daraja hilo kwa muda wa mwaka mmoja, mwaka 1988 aliamuriwa daraja la Ukasisi, Mwaka 1994 alijiunga na Chuo cha Mt. Filipo Kongwa kwa kozi ya Stashahada ya Theologia na kuhitimu mwaka 1996.
Mwaka 2005 alijiunga na Chuo kikuu cha Gloucestershire kwa kozi ya Stashahada ya juu, Mwaka 2007-2010 alijiunga na Chuo Kikuu cha Mt. Yohana Dodoma na kuhitimu katika Shahada ya Sanaa ya Theologia na Elimu, Mwaka 2010 – 2011 alihitimu katika Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Theologia kutoka Chuo cha Mtakatifu Yohana.
Askofu George Yoram Chiteto ameacha mke Mama Monica Chiteto na watoto sita, Ibada ya kuaga mwili wake itafanyika Septemba 05, 2022 kuanzia saa nane mchana katika Kanisa Anglikana Madaba – Muheza kisha siku hiyo jioni safari itaanza kutoka Muheza Mkoani Tanga kuelekea Mpwapwa mkoani Dodoma kwaajili ya mazishi yatakayofanyika siku ya tarehe 7 Septemba, mwaka huu 2022.
Enzi za uhai wake Askofu George Chiteto atakumbukwa zaidi kwa utumishi wake uliotukuka ndani ya Kanisa akipita katika maeneo ya mjini na Vijijini akihubiri na kuwaokoa wengi walio mkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wao kupitia utumishi wa Marehemu Askofu Chiteto.
Pia atakumbukwa zaidi kwa Hotuba yake nzuri aliyoitoa agosti 28, 2022 mbele ya Mgeni Rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Utaratibu George Simbachawene aliye mwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kushiriki tukio hilo ambalo baada ya kuwekwa Wakfu Askofu Chiteto amehudumu kama Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa kwa muda wa siku sita pekee.
Katika Ibada hiyo ya kuwekwa Wakfu Marehemu George Chiteto kuwa Askofu wa tatu wa Dayosisi ya Mpapwa ilifanyika Changizo dogo iliyoongozwa na Waziri Simbachawene ya kupata fedha ili kufanikisha ununuzi wa Gari la Askofu na jumla ya Shilingi milioni 21 zilipatikana ambazo ni ahadi pamoja na fedha taslimu na zoezi hilo linaendelea.
Kufuatia Msiba huo Wakristo wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa na Tanzania kwa ujumla wameeleza kupokea msiba huo kwa mshituko na masikitiko makubwa kwakuwa Askofu hakuonesha hali ya ugonjwa hadi alipofariki Ghafla baada ya kumaliza kazi ya kuwahubiria waumini.
“Tumesikitishwa na tukio hili la kifo cha Baba Askofu maana alikuwa mzima, amehubiri hapa Kanisani tumependa mahubiri yake wengi tumefurahi na kushangilia lakini ghafla tukaona anatolewa nje na kukimbizwa Hospitali, mwishoni wa ibada Baba Askofu Mkuu alitangaza taarifa za kifo chake tumeumia sana” walieleza.
Kanisa linatoa pole kwa familia ya Baba Askofu Chiteto, mkewe na watoto, wahudumu na Wakristo wote wa Dayosisi ya Mpwapwa na Kanisa Anglikana Tanzania, Raha ya Milele umjalie Ee Bwana, na Mwanga wa Daima umwangazie. Roho ya Baba Askofu CAPT. GEORGE YORAM CHITETO na roho zao wote waaminifu waliofariki katika imani zipumzike kwa Amani. Amen.