Sunday, 4 September 2022

RAIS SAMIA AGUSWA NA JITIHADA ZA BENKI YA NBC UWEZESHAJI JAMII KIUCHUMI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu akisalimiana na wanachama wa Saccos ya Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar wakiongozwa na Mwenyekiti wa Saccos hiyo Bw Said Hamad Ramadhan (wa pili kushoto) wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa jengo la ofisi za Saccos hiyo iliyoambatana na upokeaji wa samani mbalimbali kutoka Benki ya NBC kwa ajili ya saccos hiyo. Wengine ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi. Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki visiwani Zanzibar


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu (katikati) akijipongeza na baadhi ya viongozi serikali, chama na benki ya NBC mara baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa ofisi za Saccos ya Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja wakati wa hafla fupi iliyoambatana upokeaji wa samani mbalimbali zilizotolewa na Benki ya NBC kwa ajili ya saccos hiyo. Pamoja nae ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Haroun Ali Suleiman (Kulia), Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid ( wa pili kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa tatu kushoto) na Mratibu wa Saccos hiyo Bw Said Ramadhani Mgeni (wa pili kushoto)


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu (wa tatu kushoto) akijipongeza na baadhi ya viongozi serikali, chama na benki ya NBC mara baada ya kuzindua ofisi ya Saccos ya Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja wakati wa hafla fupi iliyoambatana upokeaji wa samani mbalimbali zilizotolewa na Benki ya NBC kwa ajili ya saccos hiyo. Pamoja nae ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Haroun Ali Suleiman (wa pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid ( kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa pili kulia).


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu (alieketi) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi akifafanua kuhusu mchango wa benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za serikali katika kujenga mfumo jumuishi wa fedha (Financial Inclusion) na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi wakati wakati hafla fupi ya uzinduzi wa ofisi ya Saccos ya Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja iliyoambatana upokeaji wa samani mbalimbali zilizotolewa na Benki ya NBC kwa kwa ajili ya saccos hiyo mwishoni mwa wiki.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu (Katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw Theobald Sabi wakati hafla fupi ya uzinduzi wa ofisi ya Saccos ya Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja iliyoambatana upokeaji wa samani mbalimbali zilizotolewa na Benki ya NBC kwa kwa ajili ya saccos hiyo mwishoni mwa wiki.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu akizungumza na wakazi wa Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja wakati hafla fupi ya uzinduzi wa ofisi ya Saccos ya Kizimkazi Mkunguni iliyoambatana upokeaji wa samani mbalimbali zilizotolewa na Benki ya NBC kwa kwa ajili ya saccos hiyo mwishoni mwa wiki.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu akisalimiana na baadhi ya maofisa waandamizi wa benki ya NBC wakati hafla fupi ya uzinduzi wa ofisi ya Saccos ya Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja iliyoambatana upokeaji wa samani mbalimbali zilizotolewa na Benki ya NBC kwa kwa ajili ya saccos hiyo mwishoni mwa wiki.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw Theobald Sabi (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wanachama wa Saccos ya Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar wakiongozwa na Mwenyekiti wa Saccos hiyo Bw Said Hamad Ramadhan (wa pili kushoto walioketi) wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa ofisi za Saccos hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki ikiambatana na upokeaji wa samani mbalimbali kwa ajili ya saccos hiyo zilizotolewa na Benki ya NBC mwishoni mwa wiki.

Na Mwandishi Wetu-Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu amezipongeza taasisi za fedha nchini ikiwemo benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa namna zinavyoendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga mfumo jumuishi wa fedha (Financial Inclusion) huku akionesha kuguswa na jitihada za taasisi hizo katika uwezeshaji wa jamii kiuchumi hususani makundi ya wanawake na vijana.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa jengo la ofisi ya Saccos ya Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar iliyoenda sambamba na upokeaji wa samani mbalimbali zilizotolewa na Benki ya NBC kwa ajili ya saccos hiyo, Rais Samia alionesha kuguswa na namna taasisi za kifedha zilivyo mstari wa mbele katika kuchochea uchumi jumuishi huku pia zikitumia vema sehemu ya mapato yao kurejesha kwa jamii kupitia misaada mbalimbali inayoendelea kutolewa na taasisi hizo.

“Naamini kupitia Saccoss hii ya Kizimkazi wananchi wengi wa eneo hili watafikiwa na huduma muhimu za kifedha na hivyo kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa kaya nyingi za eneo hili. Nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Benki ya NBC kwa namna ilivyoguswa na jitihada za wakazi hawa wa Kizimkazi na hivyo kuamua kuwaunga mkono kwa kuwapatia msaada wa samani za ndani ikiwemo viti na meza kwa ajili ya ofisi yao…hongereni sana benki ya NBC,’’ alisema Rais Samia.

Rais Samia alitoa wito kwa wananchi kutumia vema ushirikiano unaotolewa na taasisi hizo katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya, michezo na kiuchumi ili waweze kujikwamua kiuchumi na kijamii kwa kuhakikisha wanaitumia vema misaada hiyo ili iweze kuwanufaisha wananchi wengi na kwa muda mrefu zaidi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi alisema msaada huo ni mwendelezo wa jitihada za benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za serikali katika kujenga mfumo jumuishi wa fedha (Financial Inclusion) na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

“Kupitia Saccoss hii wananchi wengi wanakwenda kufikiwa na huduma za kifedha wakiwemo vijana, wazee na kina mama hatua ambayo itawawezesha kupata mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji yao ya kibiashara na kujiongezea kipato kwa faida ya uchumi wao na familia zao. Benki ya NBC tumekuwa mstari wa mbele kuunga mkono kila jitihada zinazofanywa na wananchi kibiashara na kiuchumi kwa kuwa tuna malengo yanayofanana,’’ alibainisha.

Alisema si mara ya kwanza kwa benki hiyo kushirikiana na wakazi wa Kizimkazi katika miradi ya maendeleo huku akitolea mfano wa ujenzi wa madarasa kwa ajiili ya shule ya awali ya Kizimkazi-Mkunguni ulioambatana na utoaji wa msaada wa gari maalum la tiba yaani (Mobile Clinics) inayotoa bure huduma kwa ajili ya Mama na Mtoto kwa maeneo mbalimbali visiwani Zanzibar.

“Misaada yote imekuwa matokeo chanya kwa jamii hii na sisi kama Benki na mdau wa maendeleo, tunajivunia sana kuwa sehemu ya suluhu ya changamoto za jamii yetu.’’ Alisema

Awali akitoa taarifa fupi kuhusu Saccos hiyo, Mratibu wa Saccos ya Kimzikazi Bw Said Ramadhani Mgeni alisema licha ya ujenzi wa jengo hilo kuanza mwaka 2015 ulikwama kuendelea kutokana na kukosekana kwa fedha hadi pale Rais Samia ambae pia ni Mwanachama wa Saccos hiyo aliposaidia juhudi hizo kwa kuchangia fedha kiasi cha sh milioni 55 iliyosaidia kukamilisha mradi huo.

“Kukamilika kwa mradi huu kunatoa fursa kwa wananchama na wakazi wa vijiji jirani kuihifadhi fedha karibu kabisa na makazi yao huku pia ujenzi wa ofisi hiyo ukitarajiwa kutoa huduma ya ukumbi kwa wakazi kizimkazi pindi tutakapokuwa na mikutano yetu na kwenye hili tunawashukuru sana Benki ya NBC kwa msaada wao wa samani za ndani ikiwemo viti na meza ambavyo tunaahidi kuvitunza na kuvilinda’’ alisema.
Share:

KAMATI YA BUNGE YAITAKA OSHA KUONGEZA ELIMU KWA UMMA


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Naghenjwa Kaboyoka (kushoto) akizungumza na Wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na Viongozi wa OSHA wakati mafunzo ya usalama na afya yaliyotolewa na OSHA kwa Kamati hiyo ambayo yalienda sambamba na zoezi la ukaguzi wa jengo jipya la Ofisi za OSHA jijini Dodoma. Aliokaa nao meza kuu ni Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Meru na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda.


Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda (kulia) akitoa maelezo ya awali kuhusu Taasisi ya OSHA mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati hiyo katika Ofisi za OSHA jijini Dodoma iliyolenga kujifunza kuhusu masuala mbalimbali ya usalama na afya mahali pa kazi. Waliokaa katika meza kuu ni Mwenyekiti wa Bodi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Meru (wapili kulia), Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Mhe. Naghenjwa Kaboyoka na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Japhet Hasunga.


Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya OSHA, Dkt.Adelhelm Meru (aliyesimama) akitoa neno la ukaribisho kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) wakati wa kikao kifupi mara baada ya Wajumbe hao kufika katika Ofisi za OSHA jijini Dodoma.


Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) wakifuatilia mada mbali mbali zilizowasilishwa na watalaam wa OSHA wakati mafunzo na zoezi la upimaji afya kwa Wajumbe wa Kamati hiyo katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma.


Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) wakishiriki zoezi la uchunguzi wa afya lililoendeshwa na wakaguzi wa afya wa OSHA kwa Wajumbe hao katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma.


Mbunge wa Viti Maalam wa Mkoa wa Morogoro na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Aleksia Kamguna (aliyesimama), akichangia mada wakati wa majadiliano kati ya OSHA na Kamati hiyo kuhusu masuala mbalimbali ya usalama na afya mahali pa kazi.


Mbunge wa Jimbo la Katavi na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Isack Kamwelwe, akifanyiwa kipimo cha usikivu (audiometry test) na Mkaguzi wa Afya wa OSHA, Dkt. Kihama Kilele. Zoezi hilo lilifanyika kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali sambamba na mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi.

**************************

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeutaka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuongeza uelewa wa masuala ya usalama na afya miongoni mwa Watanzania ili kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyotokea kwenye maeneo ya kazi.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Naghenjwa Kaboyoka, alipozungumza baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo ya usalama na afya pamoja na zoezi la upimaji afya lililoandaliwa na OSHA kwa Kamati hiyo.

“Wajumbe wangu kwakweli wamefurahi sana maana wamejua mambo mengi sana kupitia mada nzuri zilizowasilishwa na watalaam wa OSHA. Tathmini ambayo tunatoka nayo baada ya mafunzo haya ni kwamba OSHA inafanya kazi nzuri lakini tunawashauri kujitangaza na kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili kuwasaidia waajiri na wafanyakazi kujua wajibu wao kuhusiana na usalama na afya mahali pa kazi,” ameeleza Naghenjwa Kaboyoka, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali.

Mafunzo hayo yaliyofanyika leo (Septemba 03, 2022) katika jengo jipya la OSHA la Dodoma, yalilenga kuwajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya wabunge hao ikiwa ni mkakati wa Taasisi wa kuyafikia makundi mbali mbali katika jamii.

Aidha, pamoja na kupatiwa mafunzo hayo muhimu, watunga sera hao walikuwa na lengo la kukagua jengo jipya la OSHA ili kujiridhisha endapo ujenzi huo umezingatia viwango stahiki ambapo wameleza kuridhishwa na kiwango cha jengo hilo pamoja na kiasi cha fedha za umma zilizotumika.

Awali, menejimenti ya OSHA iliwasilisha mada mbali mbali mbele ya Kamati hiyo ikiwemo namna ilivyotekeleza mradi huo wa jengo la ofisi la ghorofa nne kwa muda wa miezi nane (8) na kutumia kiasi cha bilioni 4.8 chini ya bajeti ya bilioni 6.5 pamoja na kodi.

Wakizungumza mara baada ya kuhitimisha mafunzo, baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza OSHA kwa kusimamia vyema mradi huo na kuokoa fedha nyingi za serikali ambapo wamezitaka Taasisi nyingine za serikali kuiga mfano wa OSHA.

“Tumepata mafunzo mazuri sana, kule nje wengine tulikuwa tunasikia tu OSHA bila kujua namna wanavyofanya kazi lakini leo tumejifunza kwamba OSHA wanafanya kazi kwa kuzingatia taratibu zote walizoelekezwa kisheria.

Aidha, jambo kubwa lililotufurahisha zaidi ni kuhusu ujenzi wa jengo hili. Kiuhalisia mimi kama mjumbe wa kamati ya PAC nimeona thamani halisi ya fedha katika jengo (value for money). Jengo limejengwa vizuri na limezingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu na taratibu zote za usalama na afya. Tunatoa wito kwa Taasisi nyingine kuiga mfano huu,” amesema Emmanuel Shangai, Mjumbe wa Kamati na Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro.



Kwa upande wao Mwenyekiti wa Bodi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Meru na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, wameeleza dhumuni la kuandaa mafunzo hayo na kuahidi kutekeleza ushauri uliotolewa na Kamati hiyo yenye wajibu wa kusimamia nidhamu katika matumizi ya fedha za serikali.

Kwetu OSHA, imekuwa siku nzuri sana ambapo tumepata fursa ya kukutana na wajumbe wa Kamati hii. Kama tunavyofahamu wabunge ni wawakilishi wa wananchi ambao ni wadau wetu hivyo kukutana nao na kujadiliana kuhusu masuala haya muhimu kutawezesha wadau wetu kupata elimu ya masuala haya kupitia wabunge katika majimbo yao,” amesema Dkt. Adelhelm Meru, Mwenyekiti Bodi ya OSHA.

“Sisi kama watendaji tumefarijika sana kupata fursa ya kuwashirikisha waheshimiwa wabunge masuala haya ya usalama na afya mahali pa kazi kwani wao ndio wanaotunga sera na kuishauri serikali hivyo wakiyafahamu vema majukumu yetu ndivyo watakavyoweza kuishauri vizuri serikali,” amesema Bi. Khadija Mwenda, Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Ziara hiyo imefanyika sambamba na mafunzo ya Usalama na Afya kwa wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na zoezi la uchunguzi wa afya zao ili kuwawezesha kufahamu kwa undani shughuli zinazofanyika na Taasisi ya OSHA na hivyo kuwa mabalozi kwa wananchi wanaowawakilisha.
Share:

ASKOFU ALIYETAMANI KIFO AFARIKI BAADA YA KUMALIZA KUHUBIRI MSIBANI...KAHUDUMU UASKOFU SIKU 5 TU


Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa George Chiteto amefariki dunia jana mchana mara baada ya kumaliza kuhubiri katika mazishi ya mke wa Askofu Lugendo wa Dayosisi ya Mbeya Bi. Hilda Lugendo yaliyofanyika wilayani Muheza mkoani Tanga.


Tukio hilo la huzuni limekuja ghafla mara baada ya kumaliza mahubiri katika msiba huo, Askofu George Chiteto alirudi kukaa kwenye kiti ili taratibu zingine za ibada ziendelee, alianza kujisikia vibaya, akaishiwa nguvu kisha kupoteza fahamu.


Utaratibu wa kumkimbiza hospitali ulifanyika haraka na kufikishwa katika hospitali teule ya wilaya ya Muheza Tanga na saa chache akaaga dunia.


Askofu George aliwekwa wakfu Jumapili iliyopita Agosti 28, 2022 kuwa Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa iliyopo wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma na Septemba 03, 2022 akawa ameaga dunia akihudumu nafasi hiyo ya uaskofu wa Dayosisi hiyo kwa takribani siku kati ya tano tu.


Askofu mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, aliyekuwepo katika ibada hiyo ya mazishi jijini Tanga, ndie aliyetangaza msiba huo uliolikumba kanisa hilo.


Katika mahubiri ya leo na ya mwisho Marehemu Askofu George Chiteto amehubiri ujumbe unaosema "JITAHIDI UINGIE KATIKA ULE MJI MTAKATIFU" ambapo alitolea mfano ya kuwa, hata yeye angetamani kifo cha amani.


Askofu Chiteto alipata Ushemasi mwaka 1987 na Daraja la Ukasisi mwaka 1988, ana Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Theolojia (Masters of Arts in Theology) kutoka Chuo Kikuu cha St. John’s - Dodoma aliyoipata mwaka 2012.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI SEPTEMBA 4,2022


Magazetini leo Jumapili September 4,2022













Share:

HUYU NDIYE BINADAMU WA KWANZA KUUZA MAISHA YAKE KAMA BIASHARA


Mike Merrill amekuwa binadamu wa kwanza Duniani kuuza uhai wake


Mike Merrill

MIKE Merrill ndiye mtu pekee duniani anayeuzwa hadharani. Tangu 2008, maisha yake yameelekezwa kwa wanahisa wake, ambao wamenunua hisa ndani yake na kupiga kura juu ya mustakabali wake katika maisha yake kiujumla.


Kwenye maamuzi tata ya kibinafsi kama vile uzazi, ushirikiano wa kitaaluma, kazi, siasa, na hata maisha yake ya uchumba huamuliwa na wenyehisa wake ambao ni pamoja na wafanyakazi wenzake, wapenzi, rafiki wa kike wa zamani pamoja na marafiki.

Baada ya kutajwa kwa vyombo vya habari katika “The Atlantic”, “Wired” sasa amekuwa maarufu na watu wengi kutaka kuwekeza kwenye maisha yake.
Share:

Saturday, 3 September 2022

KINANA AWAKINGIA KIFUA WAKULIMA WA KAHAWA NA VANILA KAGERA, ATAKA WALIPWE FEDHA ZAO KWA WAKATI



Makamu Mwenyekiti  wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Mh. Abdulrahman Kinana akizungumza na wananchi katika ukumbi wa Lina's uliopo kata ya Bilele Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Mh. Abdulrahman Kinana katika ukumbi wa Lina's Bukoba


Na Mbuke Shilagi Kagera.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Mh. Abdulrahman Kinana amewakingia kifua wakulima wa zao la Kahawa na Vanila Mkoani Kagera na kutaka walipwe fedha zao kwa wakati.

Ameyasema hayo Jana Septemba 2,2022 katika ziara yeke mkoani humo wakati akizungumza na wananchi katika ukumbi wa Lina's uliopo kata ya Bilele Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.

 Amesema kuwa Wakulima wanapouza mazao yao wapewe fedha na sio makaratasi wala mikopo.

"Mtu anachukua Kahawa yako anakupa karatasi mimi sijaja hapa kwa karatasi mimi nimekuja na rupia nakupa Kahawa wewe unanipa Fedha" Amesema Mh. Kinana.

Ameongeza kuwa atafurahi kuona Wakulima wanalima mazao yao na kuwauzia watu binafsi wenye kuweza kulipa kwa wakati ili kuepusha usumbufu wanaokutana nao katika mashirika.

Sambamba na hayo ameongeza kuwa atatafuta soko la vanila katika nchi ya China kwani nchi hiyo inanunua na ina uhitaji wa zao la Vanila hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Albert Chalamila atamuunganisha na aliyepo ubalozini China ili kutafuta masoko huko.
Share:

BARABARA ZA TARURA ZALETA SHANGWE HAI WANANCHI WAMPONGEZA RAIS SAMIA



Ujenzi wa barabara za Makoa Darajani-Mferejini (7.3 KM) na Kwasadala -Longoi (6.0 KM) kwa kiwango cha changalawe umeleta faraja na furaha kubwa kwa wananchi wa kata ya Narumu na maeneo mengine ya jirani wilayani Hai, Kilimanjaro kwa kuwaondolea kero kubwa ya barabara iliyodumu kwa muda mrefu.


Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa barabara hizo mbele ya Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Babara Vijijini na Mijini (TARURA) meneja wa TARURA wilaya ya Hai mhandisi Pickson Lema alisema ujenzi wa barabara hizo uliogharimu shilingi 950,000,000.00 utawawezesha wananchi kuzifikia huduma muhimu za kijamii kama shule, hospitali, nyumba za ibada na masoko kiurahisi.

Alibainisha pia barabara hizo zitawezesha usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara kiurahisi.

Diwani wa Kata ya Narumu Mhe John Lengai alisema kuwa anamshukuru Rais Smia Suluhu Hassan kwa mambo mazuri anayoyatekeleza na mojawapo likiwa ni hilo la barabara ukiachilia mbali vituo vya afya, zahanati na madarasa anayojenga, akamwomba mwenyekiti wa bodi kufikisha salamu hizo kwa Rais kwa kuwatendea makuu.

Kwa upande wake katibu wa mbunge wa Hai ndugu Benson Lema alisema kuwa anatoa shukurani za dhati kwa bodi ya ushauri ya TARURA pamoja na TARURA mkoa na wilaya kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja.

“Lakini shukurani za dhati ziende kwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan. Kwakweli ametupendelea kwa upekee kabisa kwani barabara hii kutokana na ubovu wake ilikuwa inaitwa barabara ya Ngómbe lakini sasa na sisi tunaonekana watu kwa barabara safi kabisa,” alisema Benson

Marry Shirima mtendaji wa kata ya Narumu alisema kuwa kwa niamba ya mbunge na wananchi wa kata yake wanamshukuru sana Rais Samia suluhu Hassan pamoja na TARURA kwa barabara hizo zinazojengwa.

“Mimi ni mtendaji wa kata hii na ninaposafiri ukinikuta utafikiri nimetoka kuvuna kumbe ni kwasababu nimepita kwenye maeneo magumu ambapo kulikuwa hakuna usafiri unaweza kufika kwenye hili eneo, lakini kwa sasa bodaboda zipo za kutosha na magari yatakuwa yakutosha pia,”alisema Marry.

Aidha alimkabizi mwenyekiti wa bodi kahawa pamoja na mkungu wa ndizi kama ishara ya ukarimu na moyo wa upendo kutoka kwa wananchi kwa barabara nzuri walizojenga.

Mwenyekiti wa bodi ya Ushauri ya TARURA mhandisi Florian Kabaka kwa upande wake alisema kuwa wamefika wilayani hapo kwa lengo la kukagua barabara ili kuona kama imejengwa kwa ufanisi badala ya kukaa ofisini na kuangalia kwenye makaratasi.

“Ninashukuru kuona kwamba kuna kitu kizuri kinatekelezwa hapa kutokana na furaha na shangwe mliyoionesha hapa, nia njema ya Rais wetu ni kuona tunawafikia wananchi ili wapate miundombinu bora itakayowawezesha kuzifikia huduma muhimu na maeneo ya biashara na kukuza uchumi wao,” alisema mhandisi Kabaka.
Share:

AJALI YA BASI LA SUPER NAJIMUNISA YAUA WATU WATANO, KUJERUHI 54 SHINYANGA

 

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

WATU watano wamepoteza maisha huku 54 wakijeruhiwa ajali ya Basi na Fuso kugongana uso kwa uso eneo la Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga.


Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi Septemba 3,2022 majira ya Saa 8 usiku, ikihusisha basi  Kampuni ya Super Najimunisa yenye namba za usajili T.413 DAY likitokea Dar es salaam kuelekea Jijini Mwanza, na Fuso yenye namba za usajili T.123 DJH likitokea Mwanza kwenda Dar es salaam likiwa na mzigo wa dagaa.


Manusura wa ajali hiyo Fred Mahina, amesema dereva wa basi hilo alikuwa akiendesha mwendokasi na walipokuwa wakimzuia aliwajibu wangetaka usafiri wa raha wangepanda ndege, huku akiwaambia wasali sana ili wafike salama.


"Tulipofika Morogoro dereva akiwa mwendokasi alikwaruza Roli tukapona kuanguka, lakini akazidi kuendesha mwendokasi abiria tulipokuwa tukipiga kelele apunguze mwendo, aligoma na kutuambia tusali ,ndipo tulipofika hapa Shinyanga na kupata ajali," anasema Mahina.


Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Leonard Nyandahu ambaye alikuwa eneo la ajali hiyo, amesema chanzo ni uzembe wa Dereva wa basi kwa kutozingatia vibao vya usalama Barabarani na kuendesha mwendokasi.


Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga Dk. Luzila John amethibitisha kupokea Vifo vya watu watano pamoja na majeruhi 54 ambao wanaendelea na matibabu.


Amesema watu hao ambao wamepoteza maisha bado hawajatambuliwa majina yao, na wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitalini hapo.

Share:

ASKOFU MACHIMU AMPONGEZA RAIS SAMIA ,KWA KUTOA RUZUKU YA MBOLEA KWA WAKULIMA

Askofu Raphael Machimu akiwasihi waumini kuliombea Taifa la Tanzania na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima.
Askofu Raphael Machimu akizungumza kanisani

Askofu wa Kanisa la EAGT Ushirika Makimbilio Healing Center mjini Shinyanga, Raphael Machimu amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku ya mbolea.


Askofu Machimu amesema hayo leo Ijumaa Septemba 2,2022 wakati wa ibada iliyoambatana na zoezi la kuhitimisha kongamano la kurugenzi ya kusifu na kuabudu kongamano lililohusisha zaidi ya vijana elfu moja kutoka katika Kanda za maziwa makuu inayojumuisha mikoa nane ya Kigoma ,Kagera,Geita,Mwanza,Simiyu ,Shinyanga ,Mara na Tabora.



Amesema nivyema wananchi wakawekeza katika sekita ya kilimo hali itakayo wawezesha kunufaika na ruzuku ya mbolea iliyotolewa na serikali.


Askofu Machimu amesema ni wajibu wa waumini wa kanisa hilo na madhehebu mengine kuedelea kusali na kuomba katika familia zao wakiliombea Taifa na viongozi wake maana pasipo amani na utulivu waumini hawawezi kupata nafasi ya kufanya shughuli zao ikiwemo kusifu na kuabudu.


Aidha Askofu Machimu amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa uhuru wa kuabudu hali inayo wapa viongozi wadini kufanya kazi ya kulitangaza neno la Mungu kwa uhuru.


“Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kudumisha amani ya nchi na kuya ruhusu madhehebu mbalimbali kufanya shughuli zake kwa uhuru maana kuna baadhi ya nchi zinazo kosa uhuru huo”,amesema Askofu Machimu.


Pia Machimu, amewashukuru waimbaji kwa kuendelea kuhubiri na kulitangaza neno la mungu kwa njia ya nyimbo huku akiwasii waimbaji kuyaishi yale wanayo imba katika nyimbo zao.


Naye mkurugenzi wa Idara ya kusifu na kuabudu Taifa kutoka Nyanda za juu kusini jimbo la Mbalari mch. Gidion Malatila amebainisha kuwa katika kongamano hilo wamewasii waimbaji kutenda matendo yanayo mpendeza mwenyezi mungu wakati wa utume wao.


Kwa upande wao badhi ya waimbaji walio hudhuria kongamano hilo lililo dumu kwa mda wa siku tano wameahidi kuyazingati amaagizo naUshauri uliotolewa na Askofu kwa kuyaishi yale wanayo imba katika nyumba zaibada ikiwemo kuendelea kuomba na kusali wakiliombea Taifa la Tanzania na viongozi wake.
Viongozi wakiendelea kusifu na kuabudu.
Viongozi wa kurugenzi wa idara ya kusifu na kuabudu kanda za maziwa makuu.
Mkurugenzi wa idara ya kusifu na kuabudu taifa kutoka nyanda za juu kusini jimbo la Mbalali Mch. Gidion Malatila.
Wanakwaya wakisifu kwenye kongamano hilo.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger