Sunday, 4 July 2021
SERIKALI YA TANZANIA YATOA MWONGOZO WA UDHIBITI WA MAAMBUKIZI YA COVID - 19 KATIKA SHULE, VYUO NA TAASISI ZA ELIMU
NAIBU KATIBU MKUU NISHATI, VIWANDA WATEMBELEA BANDA LA PURA MAONESHO YA SABA SABA 2021
EVIH , NYOTA MPYA KUTOKA NIGERIA ANAYEKUJA KUUSHANGAZA ULIMWENGU WA MUZIKI AFRIKA MASHARIKI
Evih amewahi kufanya kazi kadhaa na moja ya kazi yake iliyofanya vizuri alishirikiana na msanii wa muziki kutoka Nigeria na mshindi wa tuzo ya BET katika kipengele cha Best international Act miaka kadhaa iliyopita,David Adeleke maarufu kwa jina la DAVIDO.
Licha ya kazi hiyo kufanya vizuri Evih ameamua kutanua wigo wa mashabiki zake kutoka Naijeria mpaka Afrika ya Mashariki kwa kuachia kazi yake aliyoipa jina la FOREIGN (SO WAVY) Ambayo inaambatana na safari yake nchini Tanzania na kenya kwaajili ya kuzuru katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni Afrika Mashariki akianzia Nchini Tanzania.
Unaweza kufutatilia kazi zake kupitia chaneli yake ya youtube na pia kuwa karibu naezaidi kwa kumfuata kupitia ukurasa wake wa Instagram na twitter kwa jina la @evihofficial.
Changamkieni Kupata Hati Katika Maonesho Ya Sabasaba-Dkt Mabula
Na Munir Shemweta, WANMM
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula amewataka wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani waliorasimishiwa makazi yao kutumia fursa ya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa kujipatia hatimiliki za ardhi zinazopatikana ndani ya siku moja katika maonesho hayo.
Akizungumza wakati wa kutembelea Banda la Wizara ya Ardhi katika maonesho hayo mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Mw. Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa Dar es Salaam Dkt Mabula alisema maonesho ya Sabasaba ni fursa nzuri kwa wananchi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani kujipatia hatimiliki za ardhi pamoja na huduma nyingine za sekta hiyo kwa uharaka zaidi.
Katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya mwaka huu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatoa hatimiliki za ardhi kwa wale wananchi waliorasimishiwa makazi yao na kuwa na nyaraka muhimu kupata hati ndani ya siku moja
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, kasi ya serikali ya awamu ya sita ni kubwa na sasa hatimiliki ya ardhi inapatikana kwa siku moja tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo pamoja na mmiliki kuwa nyaraka zote lakini kupata hati ilikuwa vigumu.
"Kasi ya serikali ya awamu ya sita ni kubwa sana katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inapatiwa ufumbuzi na kwa kuwa hivi sasa tuko katika mfumo wa kidigitali hatimiliki ya ardhi unaweza kuipata ndani ya muda mfupi kwenye banda la wizara hapa sabasaba tofauti kabisa na miaka ya nyuma" alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri Dkt Mabula ambaye alikabidhi hati za ardhi kwa baadhi ya wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Ardhi katika maonesho hayo ya 45 ya Biashara ya Kimataifa alisema, hata wale wananchi wenye migogoro ya ardhi wanaweza kupata ufumbuzi wa migogoro papo hapo kupitia wataalamu wa sekta ya ardhi waliopo kwenye maonesho.
Akielezea zaidi utendaji wa Wizara yake, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema kuwa, Wizara ya Ardhi imejipanga vizuri kuhudumia wananchi kutokana na huduma za sekta hiyo kupatikana kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
‘’ Yeyote mwenye changamoto ya ardhi kwa sababu huduma zinafanyiika hapa kwa karibu afike katika maonesho ya SABASABA atapata ufumbuzi wa suala lake maana watumishi wapo kwa ajili ya kufanya kazi na hata waliopo mikoani huduma inatolewa huko ambako ni sawa na Wizara ya ardhi’’ alisema Mhe. Dkt Angeline Mabula.
Baadhi ya wananchi waliopata hatimiliki za ardhi zilizotokana na zoezi la urasimishaji katika maonesho hayo walipongeza Wizara ya Ardhi kwa kufanikisha kutoa hati ndani ya muda mfupi katika maonesho ya Sabasaba na kutaka kazi hiyo iendelee na kwenye mikoa mingine hata baada ya maonesho hayo.
‘’Hatua hii ya kutoa hati ndani ya muda mfupi ni nzuri sana na inatakiwa iwe endelevi isiwe katika maonesho pekee na ifanyike pia katika mikoa mingine ili kuwaondolea usumbufu wanannchi wanaotaka kupata hati’’ alisema Ally Ismail mkazi wa Gongolamboto.
Serikali Yaanza Safari Utoaji Tuzo Za Habari, Sanaa, Utamaduni Na Michezo
Serikali imeanza safari ya utoaji tuzo mbalimbali kwa wadau wa sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo zitakazoenzi vipaji na mafanikio katika sekta hizo.
Hayo yameelezwa jana usiku wa Julai 3, 2021, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliyemwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Mhe Innocent Bashungwa.
Dkt. Abbasi alikuwa akitoa nasaha katika usiku wa tuzo mbalimbali kwa wanafunzi wa vyuo vikuu katika sanaa mbalimbali, tuzo zilizoandaliwa na taasisi ya UniAwards kwa kushirikiana na Wizara ya Habari na Sanaa.
“Tuzo za leo ambazo tumeshirikiana na wadau wa sekta binafsi ni mwanzo wa mwaka huu kuwa wa kurejesha tuzo nyingine mbalimbali ambazo zitaenzi na kutambua umahiri katika sekta zote nne za wizara yetu,” alisema.
Tuzo hizo zimehudhuriwa na mastaa mbalimbali wa muziki na filamu wakiwemo Kala Jeremire, Baker Flavour, Jay Melody, Rapture na Lissa wake, Davina, Batuli, Joti na wengine wengi.
ULEGA ATAJA MKAKATI WA KUTHAMINISHA ZAIDI DAGAA
Afisa Mfawidhi Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) Kanda ya Ziwa Victoria Bw. Roman Mkenda akifafanua utendaji kazi wa kituo hicho katika kulinda rasilimali za uvuvi zilizopo ndani ya Ziwa Victoria wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya uvuvi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria kilichofanyika katika Maabara ya Taifa ya Uvuvi jijini Mwanza. (03.07.2021)
Na. Edward Kondela
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema serikali imejipanga kuhakikisha inaboresha uvuvi wa dagaa hasusan katika Ziwa Victoria ili kuliongezea thamani zao hilo.
Mhe. Ulega amesema hayo wakati wa mkutano na wadau wa Sekta ya Uvuvi wanaohusika na uchakataji wa minofu ya samaki na wavuvi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita na Simiyu na kusisistiza kuwa serikali imejipanga kuipa thamani uvuvi wa dagaa ili kuongeza uwekezaji wa zao hilo.
“Tunataka tupate vichanja vya kutosha katika kuanika dagaa sio dagaa wanamwagwa tu inatakiwa wawekwe kwenye Vichanja’’ amesema Mhe. Ulega.
Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaongea na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na wadau mbalimbali ili kuwekeza katika uvuvi wa dagaa.
Ameongeza kuwa dagaa wanatakiwa kupelekwa maeneo mbalimbali nchini na kusaidia kuondokana na tatizo la utapia mlo kwa kuwa dagaa wana madini mengi ya kutosha katika kuupatia mwili afya na kushauri viwanda mbalimbali kuhakikisha vinachakata dagaa vyema na kuuza ndani na nje ya nchi.
Naibu waziri Ulega amesema uvuvi wa dagaa umeleta ajira kwa watu wengi sana hususan akinamama hivyo ni muhimu kuhakikisha zao hilo linaendelea kuongeza tija zaidi katika kukuza pato la taifa na mtu mmoja mmoja.
Amewatadharisha pia wavuvi wa dagaa na sangara wasije kujiingiza katika mgogoro kama wa wakulima na wafugaji katika kugombania uvunaji wa rasilimali za uvuvi, hivyo serikali itahakikisha inaweka mazingira mazuri zaidi ya uvunaji wa rasilimali hizo baina yao.
Mhe. Ulega amewaomba pia wamiliki wa viwanda vya kuchakata minofu ya samaki kuhakikisha wanawalipa wavuvi stahiki zao kwa wakati ili waweze kuendelea kufanya nao biashara ya kuwauzia samaki kutokana na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wavuvi kudai kuwa wamekuwa hawalipwi kwa wakati wanapopeleka samaki viwandani na kuamua kuuza katika masoko ya ndani.
Pia alibainisha kuwa katika Bajeti ya Mwaka wa fedha 2020/2021 kupitia Sekta ya Uvuvi wamefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 22.6 ambapo serikali ilipanga kukusanya Shilingi Bilioni 33 na kwamba asilimia 80 ya mapato hayo yametokana na Ziwa Victoria.
Naibu waziri huyo amewataka wadau wa uvuvi wawe wanaishauri serikali kuhusiana na sekta hiyo na kwamba lengo la serikali ni pamoja na kudhibiti maeneo ya mazalia ya samaki ili kupata mazao mengi.
Nao baadhi ya uvuvi wakichangia katika mkutano huo wameiomba serikali iwasaidie katika utoaji wa taarifa ya bei elekezi ili kupunguza kubadilika badilika kwa bei za samaki zinazonunuliwa viwandani.
Wameiomba pia serikali iwasaidie wavuvi katika utungaji wa Sera za Uvuvi pamoja na kutaka soko la samaki kuwa huru ili waweze na kujiongezea kipato.
Baadhi ya wavuvi hao pia wameiomba serikali kusaidia katika upatikanaji wa zana za uvuvi pamoja na pamoja na kudhibiti upatikanaji wa nyavu zisizotakiwa ambazo zinavua samaki wadogo.
DKT KALEMANI ATOA MWEZI MMOJA KWA SHIRIKA LA TPDC KUANZA UTEKELEZAJI WA UJENZI WA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA
WAZIRI wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza wakati wa kikao kazi cha maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Bomba la mafuta kilichofanyika Jijini Tanga.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Godfrey Mwambe akizungumza katika kikao hicho.
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kagahe akizungumza wakati wa kikao hicho.
KURUGENZI wa Shirika la Maendeleo ya Petrolium Tanzania (TPDC) Dkt James Mataragio akizungumza katika kikao hicho.
Mtoa mada wa fursa za Mradi wa EACOP Sipiel Msomvu ambaye ni mtaalamu kwenye mradi huo aliyeshiriki kwenye majadiliano.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati Dastan Kitandula akizungumza wakati wa kikao hicho.
KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Tanga Hashim Mgandilwa akizungumza wakati wa kikao hicho.
Mtaalamu aliyeshiriki kwenye majadiliano ya mradi huo kutoka EWURA Peneli Kagama akieleza jambo kwenye kikao hicho.
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Slivestry Koka akizungumza wakati wa kikao hicho
Mkurugenzi Mtendaji TPSF, Francis Nanai kushoto akifuatilia kwa umakini hotuba ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani wakati wa kikao hicho kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga (CCM) Mhandisi Mwanaisha Ulenge.
Wadau mbalimbali wakifuatilia kikao hicho.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ametoa mwezi moja Shirika la maendeleo la petrol nchini TPDC kuanza utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Bomba la mafuta ghafi kutoka nchi Uganda hadi Chongoleani Jijini Tanga.
Rai hiyo alilitoa leo wakati wa kikao kazi cha maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Bomba la mafuta kilichofanyika Jijini Tanga alisema kuwa muda wa vikao kwa ajili ya majadiliano umekwishwa na kinachotakiwa kwa sasa kuanza utekelezaji wake.
Alisema kuwa sekta binafsi ipo tayari kwa ajili ya kuchangamkia fursa za ujenzi hivyo aliitaka TPDC kuanza maandalizi ya ujenzi wa Mradi huo ili kutoa fursa kwa wananchi kuweza kupata ajira na hivyo kuinua uchumi wao.
“Niwaombe TPDC hii iwe mkutano wa mwisho tunataka kuja kuitwa kwenye vikao vya kujadili namna ambavyo kazi zimefanyika kwani sasa wananchi wanataka kuona namna ambavyo wanashiriki katika Mradi huo” alisema Waziri Kalemani.
Alisema kuwa kuwa Mradi huo unatarajiwa kuwekeza zaidi ya sh Tril 8.4 ambazo lengo la Serikali ni kuhakikisha fursa hiyo ya uwekezaji inawanufaisha sekta binafsi ili kuongeza wingo wa kiuchumi.
Waziri Kalemani alisema wakati wa kazi za ufundi na nyengine kwenye haya matenki na hakuna sehemu nyengine itajengwa mradi huo tofauti na hapa Tanga hiyo itachukua ajira za hapa hapa nchini hatarajii watoke nje ya nchi.
Alisema katika utekelezaji wa mradi huo watanzania wengi wataajiriwaa na itachukua wafanyakazi wengi sana hivyo watanzania wengi wahakikishe wanajipanga kuchangamkia fursa zitakazokuwepo.
“Nitoe tamko kwamba watanzania wanaweza hata mabomba yatakayojenga mradi huo serikali kupitia Rais Samia Suluhu wanataka yaweza kutoka hapa nchini kama ni muda wa kujipanga na kujiandaa muanze leo haiwezi kuingia akilini mabomba ya kupikia mafuta yatokea nje maana yake manufaa yanaendelea kupungua”Alisema
Waziri huyo aitoa rai kwa watanzania wengi uwezo kuchangamkia fursa za mikopo kwenye mabenki kupata fedha waweze kujenga viwanda vya mabomba hapa nchini hayo ndio manufaa tunayoyataka .
“Hivyo fursa hii watanzania tuiifumbie macho…Agizo langu Kampuni itakayojenga mradi huo wakandarasi mtakaowapa kazi mhakikishe vifaa ujenzi vinatoka hapa nchini”Alisema
Hata hivyo alisema suala la pili manufaa makubwa yatatokana na ajira watanzania wasiopungua efu 15,000 wataajiriwa kwenye mradi huo hivyo mjiandae kuchangamkia fursa hizo.
Awali akizungumza katika semina hiyo Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt James Mataragio alisema kikao hicho lengo lake ni kuweza kukutana kuweza kushirikishana habari za mradi wa (EACOP) wamefikia wapi na wanaendelea wapi na fursa zilizopo.
Alisema Shirika hilo ni Taasisi ambayo inaweza kusimamia mradi huo na kuhakikisha unasimamia maslahi mapama ya Taifa yanatekelezwa na kulindwa ili kuweza kuleta tija kubwa .
Mkurugenzi huyo alisema EACOP ni moja ya miradi 16 ambayo ni ya kielelezo kama utakumbuka wiki iliyopita Waziri Mkuu alizindua mpango wa tatu wa maendeleo ya miaka mitano katika huo mpango na hiyo mradi huo ni miongoni mwao.
SERIKALI IMEDHAMIRIA KUIMARISHA USHIRIKA
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akiongea na Wanaushirika wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani Julai 03,2021 katika Viwanja vya Nanenane, Mkoani Tabora
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akiuliza jambo katika mabanda ya maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani, (kulia) ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) Bi. Theresia Chitumbi katika Viwanja vya Nanenane, Mkoani Tabora
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani mkoani Tabora.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinaimarika na wakulima wanapata tija na manufaa ya shughuli za uchumi zinazoendeshwa kwenye Vyama vya ushirika.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani Julai 03, 2021 yaliyozinduliwa Julai 29, 2021 viwanja vya Nanenane Ipuli Mkoani Tabora.
Mhe. Kassim Majaliwa ameeleza kuwa Ushirika ni Sekta muhimu yenye mchango mkubwa kwa Taifa ambayo inahusisha shughuli za uchumi ikiwemo Kilimo, uvuvi, ufugaji na Nyanja nyingine za uchumi ambazo zote hutoa ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa. Hivyo, amewataka Viongozi na watendaji wa Sekta ya Ushirika kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinaendeshwa kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu na kusimamia Vyama kwa misingi ya uadilifu ili kuondokana na changamoto ambazo zimekuwepo zinazoharibu taswira ya Ushirika.
“Lazima tuzilinde mali za Ushirika jukumu tulilonalo viongozi wa Ushirika ni kusimamia mali za Ushirika na kuheshimu dhamana tulizopewa na wanaushirika,” alisema Waziri Mkuu
Akizungumzia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala Waziri Mkuu amesema mfumo huo ni mkombozi kwa wakulima kwani mkulima anapata fursa ya kupata bei yenye ushindani kupitia minada ya ununuzi ambayo mara nyingi ni ngumu kuipata kwa walanguzi. Hivyo, ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuendeleza juhudi za kuelimisha kuhusu mfumo huu na kuhakikisha hata maeneo yenye changamoto na mfumo elimu itolewe ili wakulima waelewe manufaa ya mfumo.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amesema Tume inaendelea kuunga mkono Juhudi za kufufua viwanda ili kuongeza thamani za mazao yanayozalishwa na wakulima. Ameongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka jana tayari viwanda vitatu vinavyomilikiwa na Vyama vya Ushirika vimeanza kufanya kazi akivitaja viwanda vinavyomilikiwa na KACU, Chato na Mbogwe jambo ambalo linasaidia kuongeza bei ya mazao na ushindani wa soko.
Aidha, Dkt. Ndiege ametoa wito kwa vyama vya Ushirika kuitumia Benki ya Ushirika ya KCBL ambayo tayari imeanza kazi kuanzia Novemba mwaka jana. Mrajis ameongeza kuwa Benki hiyo ni mahususi kwaajili ya wanaushirika na tayari imeanza kupata faida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) Bi. Theresia Chitumbi ameeleza Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika duniani 2021 isemayo “Ushirika tujijenge upya kwa ubora na tija” inalenga kuonesha ustahimilivu wa Vyama vya Ushirika katika kusaidia na kutoa michango ya utu kwa jamii katika kipindi cha majanga mbalimbali kama mabadiliko ya tabia nchi, uharibifu wa mazingira na hali ya hewa. Kauli mbiu hiyo inalenga kuchochea vyama vya ushirika kutumia nguvu yake ya umoja, maadili yake na tunu katika kutafuta suluhu ya changamoto.
Mwenyekiti huyo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuamini ushirika kama taasisi zenye uwezo wa kuchochea maendeleo ya uchumi pamoja na jitihada kubwa za urejeshaji wa mali za Ushirika zilizokuwa zimeuzwa na kuporwa kiholela zimechukuliwa bila utaratibu zikiwemo nyumba za makazi, maghala, viwanda na viwanja. Akiongeza kuwa wanaushirika wanaimani kuwa Serikali itaendelea na zoezi hilo la kutafuta na kuzirudisha mali za ushirika ni endelevu.
Akielezea baadhi ya Changamoto inayovikabili Vyama vya Ushirika wa akiba na Mikopo (SACCOS) mwenyekiti amesema Vyama hivi hupokea hisa, akiba, na amana za wanachama kupitia makato ya mishahara ya watumishi husika. Hata hivyo, fedha hizo hukatwa tozo la gharama la gharama (processing fees) kwa asilimia mbili na vyama hupokea fedha pungufu za wanachama kwa kiasi cha asilimia hizo lakini hulazimika kunjazia mwanachama fedha kamili kwenye taarifa zake hivyo kusababisha vyama kuingia hasara. Pamoja na ucheleweshaji wa marejesho kutoka kwa waajiri.
Ofisi ya Waziri Mkuu yaagiza miradi ya Afya yenye ufadhili wa Global Fund Tanga na Kilimanjaro kukamilika iweze kuhudumia wananchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, imetembelea na kukagua kasi ya utekelezaji wa miradi ya Afya inayohusisha ujenzi majengo pamoja na mifumo ya utoaji huduma za afya kwa wananchi, inayofadhiliwa na serikali pamoja na Mfuko wa Dunia -Global Fund katika mikoa ya Tanga na Killimanjaro na kuagiza miradi yote iliyosimama ujenzi ikamilike haraka iweze kutoa huduma kwa wananchi
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Bw. Kaspar Kaspar Mmuya alitoa agizo hilo alipofanya ziara ya ukaguzi miradi hivi karibuni na kubaini kuwapo changamoto mbalimbali za kiutendaji zilizosababisha miradi kuchelewa na kushindwa kukamilika kwa wakati hadi kusimama ujenzi. Aliwataka watendaji wote wanaohusika katika ujenzi wa miradi hiyo kufuatilia haraka na kwa karibu changamoto zote zilizojitokeza katika utekelezaji miradi na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kuwezesha miradi kukamilika na kuanza kazi
Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo Mratibu wa utekelezaji wa miradi hiyo ya ujenzi na utoaji huduma za afya inayofadhiliwa na Mfuko wa Dunia- Global Fund, inayolenga kupambana na magonjwa ya Kifua Kikuu, UKIMWI, Malaria pamoja na kuboresha Mifumo Endelevu ya Utoaji wa Huduma za Afya. Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw.Tixon Nzunda,
ndiye Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Kitaifa inayoratibu Matumizi ya fedha zinazotolewa na mfuko wa Dunia.
Hivyo, katika ziara hiyo ya ukaguzi ya siku tano, Naibu Katibu Mkuu Mmuya alimuwakilisha Katibu Mkuu na aliambatana na timu ya Wataalam kutoka Ofisi yake ya Waziri Mkuu; Ofisi ya Rais TAMISEMI; Wizara ya Afya, ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; na Sekretarieti ya Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) ya Global Fund ambao walitembelea mikoa ya Tanga na Kilimanjaro kwa lengo la kubaini kiini cha changamoto zilizopo zinazosababisha miradi kukwama ujenzi
Miradi iliyotembelewa, kukaguliwa na kutolewa maagizo na Naibu Katibu Mkuu Mmuya katika awamu hii ya kwanza akiwa na timu yake ya wataalamu ni pamoja na ujenzi ni jengo la ghorofa moja la Wazazi (Mama na Mtoto) katika hospitali ya halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, na majengo mawili yanayojengwa katika hospitali ya ya rufaa ya mkoa- Mawezi, mkoani Kilimanjaro moja likiwa la kawaida litakalotoa huduma za dharura (Emergency Medicine Department-EMD) na jengo la ghorofa nne la Mama na Mtoto (Martenity Block)
Wakati wa zoezi la ukaguzi watendaji katika miradi hiyo, kwa wakati tofauti, walimueleza Naibu Katibu Mkuu na ujumbe wake kuwa miradi hiyo ya ujenzi pamoja na uboreshaji wa mifumo endelevu ya utoaji wa huduma za afya kwa umma haijakamilika kwa wakati kutokana na changamoto za kiutendaji katika kutekeleza majukumu ikiwa ni pamoja na kuchelelewa vibali vya kuruhusu kupata fedha kuweza kuikamilisha miradi kwa wakati. Miradi yote aliyotembelea na kuikagua Naibu Katibu Mkuu Mmuya kama mratibu, akiwa na wataalamu wake aliishuhudia ikiwa haijakamilika kwa muda uliopangwa na imesimama ujenzi.
Akiongea baada ya ukaguzi wa Miradi Naibu katibu Mkuu Mmuya aliwapongeza watendaji kwa namna walivyoweza kusimamia uwepo wa miradi hiyo na kufikia hatua ilivyo na kuwahimiza kuendelea kuisimamia huku wakifuatilia kwa kasi ufumbuzi kwa changamoto zilizopo na kuhakikisha miradi inakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
“Nawapongeza watendaji wote katika miradi hii kwa jitihada zenu kuhakikisha miradi hii inakuwepo na inafikia hatua hizi nzuri katika ujenzi. Miradi hii ni ya lazima na muhimu sana kwa wananchi, hivyo haina budi kusimamiwa kwa weledi na ufanisi na kutatua changamoto zinazojitokeza kukwamisha miradi kukamilika kwa wakati na kuifanya isiweze kutoa huduma kwa wananchi” alisema Naibu Katibu Mkuu Kaspar Mmuya na kuongeza kuwa: “Ofisi ya Waziri Mkuu kama Mratibu imedhamiria kufuatilia na kuratibu kwa ufaisi miradi hii ya ujenzi katika sekta ya afya yenye ufadhiliwa wa pamoja na Mfuko wa Dunia iweze kuleta tija”
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Kaimu Mganga Mkuu Dkt. Gasto Stephen alitoa taarifa kwa Naibu Katibu Mkuu Mmuya kuhusu maendeleo ya ujenzi wa jengo la ghoofa la ‘Mama na Mtoto’ akisema jengo hilo halijakamilika na limesimama ujenzi kwa sasa. Alisema lilianza kujengwa Juni 1, 2020 na lilipaswa kukamilika, Marchi 1, 2021. Aidha alisema Mfuko wa Dunia -Global Fund ulitoa shilingi za kitanzania 400,000.000/- mwezi Mei mwaka 2019 kukamilisha ujenzi na jengo hilo ambalo likikamilika litaweza kutoa huduma za upasuaji za dharura kwa akina mama , huduma za mama wajawazito wanaosubiri kujifungua , huduma za kujifungua, huduma baada ya mama kujifungua na huduma za watoto njiti.
changamoto zilizopelekea mradi huo kukwama kukamilika zilielezwakuwa ni pamoja na mabadiliko ya ramani ya mwanzo ya jengo hilo la ‘Mama na Mtoto’ ambapo lilikuwa jengo la kawaida lakini kutokana na ufinyu na jiofrafia ya eneo la hospitali ya wilaya ilipendekezwa kuwa jengo la ghorofa ili kupata nafasi ya kutosha ya utoaji huduma zote zilizotajwa.
Aidha alielezwa changamoto ya bajeti ndogo kulingana na tathmini ya mradi, ongezeko la gharama za ujenzi kutokana na mabadiliko ya bei ya vifaa vya ujenzi, na wazabuni wa vifaa hivyo kuwa wachache, kutopatikana kokoto za mashine katika eneo la Lushoto, upatikanaji wa nondo na bati kutoka kiwandani uliohitaji kusubiri kwa muda pamoja na kuwapo mvua za mara.
Changamoto nyingine zilizoelezwa kuchelewesha jengo kukamilika ni mchakato wa manunuzi wakati wa kuomba ondoleo la kodi pamoja na mchango wa Halmashauri kupitia mapato ya ndani kuathiriwa na mabadiliko ya Tabianchi pamoja na ugonjwa wa unaosababishwa na virusi vya Korona (UVIKO 19) hivyo, kusababisha jengo kutokamilika kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Lushoto Bibi Ikupa Harrison Mwasyoge alimweleza Naibu Katibu Mkuu Kaspar na timu yake ya wataalamu kuwa kutokana na changamoto zilizojitokeza za ukusanyaji wa mapato ya ndani, Halmashauri yake iliomba kuongezwa bajeti ya shilingi za kitanzania 364,907,640.1/- ili kumalizia mradi wa jengo hilo la ‘Mama na Mtoto’ ndani ya mwezi Julai, 2021.
Taarifa aliyopewa Naibu Katibu Mkuu kuhusu fedha kwa ajili ya mradi huu iliainisha kuwa jumla ya fedha zinazohitajika sasa kukamilisha mradi huo wa ujenzi wa jengo la ‘Mama na Mtoto’ baada ya makadirio mapya ni shilingi zipatazo 810,848,342.10 ambapo fedha za ujenzi wa jengo ni shs. 694,582.778 na fedha za vifaa tiba ni sh.116,265,564. Hadi Mwezi Mei, 2021 jumla ya matumizi ya fedha yalikuwa shs. 439,417,222 ambapo kazi ya ujenzi imefikia asilimia 78 na muda uliotumika ni asilimia 94.
Akitoa Maagizo, Naibu Katibu Mkuu Mmuya alimuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuandika barua kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kupata majibu ya barua yake ya mwaka 2020 kuhusu maombi ya fedha za kukamilisha mradi huo na kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kufanya uchambuzi wa mahitaji halisi ya kukamilisha ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto na kuyawasilisha Ofisi ya Rais -TAMISEMI ili jengo likamilike kwa wakati na kuitaka Halmashauri pia iwasilishe maombi Ofisi ya Rais, UTUMISHI ya kujaza nafasi za wakuu wa zinazokaimiwa ili kuongeza ufanisi katika shughuli zake.
Mkoani Kilimanjaro, katika majumuisho ya ziara yake Naibu Katibu Mkuu aliagiza hatua za utekelezaji kutatua changamoto zilizokwamisha ujenzi wa majengo kwa kumuelekeza Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Abdallah Seif Shekalaghe kufuatilia kwa karibu na haraka upatikanaji wa kibali cha msamaha wa kodi kwa manunuzi ya vifaa vya ujenzi (GN- Government Notice) wa jengo la huduma za dharura ili kuhakikisha manunuzi yanafanyika mapema iwezekanavyo.
“Fuatilieni haraka hiyo GN kuweza kupata msamaha wa kodi. Andaeni pia mkakati mahsusi wa kusimamia hospitali za rufaa za mikoa na kanda badala ya kusimamiwa na Wizara ya Afya moja kwa moja” Naibu Katibu Mkuu alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro na timu yake ya wataalamu wakati wa kikao cha majumuisho kilichofanyika ofisi kwake.
Awali Naibu Katibu Mkuu Mmuya alikagua miradi hiyo ya ujenzi majengo katika hospitali Kongwe ya mkoa–Mawenzi, Mkoani Kilimanjaro ambapo alipewa taarifa na Mganga Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt Credianus Mgimba kuwa ujenzi wa jengo la huduma za dharura (Emergency Medicine Department) umekwama kukamilika na kwamba changamoto zilizopo katika utelekezaji ujenzi ni pamoja na kibali cha msamaha wa kodi kwa ajili ya manunuzi ya vifaa vya ujenzi (GN) kuchukua muda mrefu.
Kwa mujibu wa Dkt. Mgimba, jengo hilo la huduma za dharura likikamilika litasaidia kuboresha huduma za dharura pale wanapopokea wagonjwa wa dharura kwa wakati mmoja na kuweza kutoa huduma kwa wakati, kuboresha huduma za wagonjwa mahututi, kuboresha utoaji huduma wa vipimo vya dharura pamoja na kutatua changamoto ya msongamano wa wagonjwa.
Ujenzi wa mradi wa jengo la huduma za dharura ulianza mwezi Machi, 2020 na ulitarajia kukamilika mwezi Machi, 2021, na sasa unategemewa kukamilika ifikapo mwezi Augusti, 2021. Makadirio ya ghrama za mradi huu ni shilingi 764,995,974.
Aidha alielezea mchanganuo wa mapokezi na matumizi ya fedha za ujenzi wa jengo hilo katika kipindi cha utekeezaji cha mwaka 2019/2021 kuwa hadi sasa fedha zimepokelewa toka Global fund kwa awamu mbili, awamu ya kwanza Tshs 262,400000(mwezi Juni 2019) na awamu ya pili zilipokelewa shilingi 514,083,631.31 (Mwezi Disemba 2020) .Mradi umefika asilimia 84 ya utekelezaji.
Kuhusu mradi wa ujenzi jengo la ‘Mama na Mtoto’ (Martenity Block Complex), Naibu Katibu Mkuu Kaspar alielezwa kuwa changamoto zilizokwamisha ujenzi kukamilika kwa wakati ni muda mrefu kwa upatikanaji kibali cha msamaha wa kodi na suala la kutotenganisha utendaji wa majukumu ya kimkataba kama vile shughuli za fundi mkuu na mshauri elekezi zinafanywa na mtaalamu wa aina moja na kusababisha ugumu katika udhibiti ubora na uwajibikaji katika utekelezaji wa mradi.
Mradi huu ukikamilika ujenzi utasaidia kuboresha huduma za Mama na Mtoto na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto chini ya miaka mitano. Pia jengo litasaidia kutatua changamoto ya msongamano wa wagonjwa katika wodi ya wazazi inayotumika sasa, kusaidia kuboresha huduma za wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) pamoja na kupunguza rufaa zisizo lazima kwenda hospitaliya rufaa KCMC, kuboreshwa kwa huduma za vipimo kama vile CT-Scan, MRI, Xray na Ultrasound kuboresha kuduma za upasuaji ambapo zitafanyika kwa ubora na kwa wakati kutokana na uwepo wa vyumba upasuaji vya kutosha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mganga mkuu wa Mkoa kwa Naibu Katibu Mkuu Mmuya, Ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto ulianza mwaka wa fedha 2009/2010 na Mkandarasi binafsi ambapo mwaka 2016 alikabidhiwa kwa wakala wa Majengo-Tanzania Building Agency (TBA) kuendela na ujenzi chini ya usimamizi wa ofisi ya Katibu Tawala-(RAS) mkoa wa Kilimanjaro ambapo makadirio ya ujenzi wote ilikuwa shilling 10.5 bilioni . Aidha utekelezaji wa mradi huu umefanyika kwa awamu 7 , awamu ya kwanza hadi ya sita ulikuwa chini ya Katibu Tawala wa Mkoa na awamu ya saba unafanyika chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na watoto ambapo katika awamu ya saba mradi umetekelezwa kwa asilimia 43 kulingana na kazi zilizofanyika na Wakala wa majengo Tanzania(TBA).
Mchanganuo wa mapokezi na matumizi ya fedha za ujenzi wa jengo hili la Wazazi mwaka 2008/2009 hadi 2019/2020 katika hospitali kongwe ya Mawezi ulionesha kwamba awamu ya kwanza ya ujenzi hadi awamu ya sita katika mwaka 2008/2009 hadi 2017/2018 chanzo cha fedha ilikuwa ruzuku kutoka serikali kuu. Hadi sas ujenzi jengo hili la Mama na Mtoto umekamilika asilimia 70. Na tangu jengo lilipokabidhiwa wizara ya afya (awamu ya 7) ujenzi umekamilika kwa asilimia 43% ya lengo la ujenzi katika awamu hiyo.
Aidha tangu ujenzi wa mradi wa jengo la Mama na mtoto ulipoanza mwaka 2009 hadi sasa zimetumika jumla ya shilingi Bilioni 6.4 na bado shilingi Bilion 4.1 kukamilisha ujenzi kwa mujibu wa makadirio ya awali mwaka 2009.
Naibu Katibu Mkuu Mmuya alielezwa na Dkt. Mgimbi kuwa katika awamu ya saba wamepokea kiasi cha shilingi 1,778059098/- kutoka Global Fund na fedha zilizotumika ni sh. 1,667,637,689/- kati ya fedha hizo kiasi cha sh.550,219921.15 zimetumika kumlipa TEMESA na shilingi 172,686,326.48 zimetumika kumlipa mjenzi TBA na shilingi 944,731447 zimetumia kwa ajii ya vifaa vya ujenzi.
Yanga Yaitungua Simba Bao 1-0
Klabu ya Yanga imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Watani wao wa Jadi, Simba SC katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa ukishududiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan .
Bao pekee la Yanga SC lilifungwa na Kiungo wa Klabu hiyo, Zawadi Mauya dakika ya 11 ya mchezo baada ya kupiga shuti kali lililomgonga Beki wa Simba SC, Shomari Kapombe na kutinga wavuni likiwaacha Simba wakishangaa dakika za mwazo za mchezo huo.
Yanga SC walionekana kuzuia kwa kuwa wengi golini kwao dakika zote huku wakitumia mchezo wa kushambulia kwa kushtukiza .
Mabeki wa pembeni wa Yanga SC, Kibwana Shomari na Adeyum Salehe walionekana kumbana vilivyo Mchezaji wa Simba SC, Bernard Morrison na kukosa nafasi ya kufurukuta katika mchezo huo licha ya ubora wa safu ya Kiungo kikiongozwa na Clatous Chama.
Simba SC imeshindwa kutangaza Ubingwa wa Ligi Kuu Bara (VPL) mbele ya Yanga SC sasa itasubiri michezo yake iliyobaki katika Ligi hiyo dhidi ya Azam FC, Namungo FC, Coastal Union na KMC FC.
Waziri Prof. Mkumbo : Serikali Itaongeza Nguvu Katika Uzalishaji Ili Kukabili Changamoto Ya Upungufu Wa Malighafi Za Viwanda Nchini.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ameeleza kuwa Serikali itaongeza nguvu ya uzalishashi katika Kilimo, Mifugo, uvuvi na vyuma ili kukabili changamoto ya upungufu malighafi inayokabili viwanda vingi nchini na kusababisha viwanda hivyo kuzalisha chini ya uwezo na kiwango cha uzalishaji.
Waziri Prof. Mkumbo ameyasema hayo Julai 03, 2021 Dar es salaam alipotembelea kiwanda cha OK Plast Ltd kinachozalisha bidhaa za nyaya za umeme Pamoja na mikeka na kukuta kuna changamoto ya upungufu wa malighafi ya mabaki ya shaba kwa ajiri ya kiwanda hicho.
“Nikili kwamba moja ya changamoto kubwa katika viwanda vya Tanzania kwa sasa ni malighafi sio idadi ya viwanda, idadi ya viwanda ipo ya kutosha lakini viwanda vyetu vingi vinazalisha chini ya uwezo kwa sababu ya kukosekana kwa malighafi kwahiyo tuna kazi kubwa ya kuongeza uzalishaji katika kilimo, mifugo, uvuvi na vyuma” ameeleza Prof. Kitila Mkumbo
Aidha, Waziri Prof. Mkumbo ameeleza kuwa atakutana na Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira ili kujadili na kuona namna ya kusaidia kiwanda hicho na viwanda vingine vyenye changamoto ya malighafi ya mabaki ya shaba na chuma ili kuona namna ya kusaidia mabaki hayo kuuzwa kwa viwanda vya ndani kuliko kusafilishwa kwenda nje.
Waziri Prof. Mkumbo amtumia nafasi hiyo kuwahimiza watanzania kununua bidhaa zilizozalishwa hapa nchi na zilizodhibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania maana kwa sasa viwanda vya ndani vinazalisha bidhaa bora na zenye viwango.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Sheria na Uzingatiaji Sheria wa Kiwanda cha OK Plast Ltd, Bw. Anackreto Pereilla ameishukuru Serikali kuwa kusikiza Changamoto yao ya upungufu wa malighafi ambayo imekuwa adimu kutokana na malighafi hiyo kusafirishwa kwenda nje, hivyo amewaomba mawaziri wenye dhamana kuona namna ya kuzuia malighafi hiyo kwenda nje ambayo imesababisha uzalishaji kupungua na kupelekea kupunguzwa wafanyakazi katika kiwanda hicho.
Majaliwa: Wizara Ya Kilimo Hakikisheni Ushirika Unakuwa Endelevu
Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo isimamie kikamilifu changamoto mbalimbali zinazodumaza vyama vya ushirika nchini ili kujenga ushirika imara unaokuwa na endelevu.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza wizara hiyo ihakikishe inavijengea vyama vya ushirika uwezo wa kujiendesha kiushindani na kuimarisha utafutaji wa masoko ya ndani na nje.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana (Jumamosi, Julai 3, 2021) kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika viwanja vya lipuli, Tabora.
Amesema ushirika ni chombo ambacho kinajenga imani kwa wakulima na wanaushirika na kwa kuwa Serikali inaweka nguvu katika jambo hilo kwa lengo la kuona ushirika unaleta manufaa.
“Natambua kuwa ushirika ndicho chombo madhubuti cha kuwauunganisha wakulima, wafugaji na wavuvi na kuwapa uwezo na nguvu ya kutatua matatizo yao ya kiuchumi na kijamii.”
Amesema wizara hiyo inatakiwa iimarishe usimamizi na udhibiti wa vyama hivyo sambamba na kuviwezesha kusimamia mifumo rasmi ya masoko ukiwemo wa Stakabadhi ghalani.
Amesema utoaji wa elimu na mafunzo ya ushirika kwa wanachama, viongozi na watendaji ni vema ukaimarishwa ili waweze kuelewa vizuri dhana ya ushirika, misingi, kanuni na taratibu.
Kadhalika, Waziri Mkuu ameliagiza Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) libadilishe mfumo wa ukaguzi na lihakikishe linatoa taarifa sahihi kwa wakulima.
Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imefanya ukaguzi wa ndani wa vyama vya ushirika 4,494 kati ya 9,185.
Pia, Waziri Mkuu amewataka Warajisi wote wahakikishe kila ushirika katika maeneo yao unakuwa na kanzi data za wanaushirika wote. “Lazima uwe na takwimu za wanaushirika wote.”
Amesema lengo la kuwa na takwimu hizo ni kuweza kufanya makadirio ya kupeleka mahitaji mbalimbali kwa wakulima ikiwa ni pamoja na mbegu, mbolea na dawa za kuulia wadudu.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Majaliwa kwa jitihada zake za kufufua na kuendeleza vyama vya ushirika nchini.
“Wewe binafsi Mh. Waziri Mkuu umesimamia shughuliza ushirika kwa moyo mmoja. Umetusaidia kurudisha mali za vyama vya ushirika ambazo zilitoka kinyume na utaratibu.”
“Kwa juhudi hizi Mhe. Waziri Mkuu umetusaidia sana kurudisha imani kwa wana-ushirika kwamba wakiwa kwenye ushirika mali zao haziwezi kufanyiwa ubadhilifu wa aina yoyote.”
Waziri huyo ametaja vyama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimamia urejeshwaji wa mali zake kuwa ni pamoja na mali za NCU-Mwanza, SHIRECU-Shinyanga, KNCU, KCU.
Pia, Waziri huyo amemuahidi Waziri Mkuu kwamba wataendelea kusimamia ushirika nchini na kuhakikisha unaendeshwa kwa weledi, uwajibikaji na uwazi ili watu wengi wapende kujiunga.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Wananchi Wasisitizwa Kufanya Uhakiki Wa Laini Za Simu
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ametoa rai kwa wananchi kuendelea kufanya uhakiki wa laini za simu kwa lengo la kutambua laini zilizosajiliwa kwa majina yao ili kuepuka kuhusishwa na makosa ya utapeli mitandaoni.
Hayo ameyazungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa tovuti na Mpango mkakati wa Wizara hiyo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2025/26 uliofanyika jijini Dodoma
Amesema kuwa ni muhimu kwa kila mwananchi kuepuka kusajili laini kwa kuweka alama ya kidole zaidi ya mara moja ili kuzuia usajili wa laini nyingine za ziada ambazo zinaweza kutumika kufanya uhalifu mitandaoni
“Wananchi wengi wamekuwa wahanga wa utapeli mitandaoni hivyo Wizara imejipanga kuimarisha mifumo ya kulinda faragha na taarifa binafsi ili zisitumike vibaya na watu wasiokuwa na nia njema”, alizungumza Dkt. Ndugulile
Aidha, amewaasa wananchi kuacha kutoa taarifa binafsi au kufuata maelekezo yeyote kwa watu wanaopiga simu na kujitambulisha wanatoka dawati la huduma kwa mteja katika makampuni ya simu ili kuepuka kutapeliwa
Ameongeza kuwa namba wanayotakiwa kupigiwa na makampuni ya simu ni namba 100 na sio kupigiwa na namba kutoka mitandao tofauti na mitandao wanayotumia huku wakijitambulisha wametoka huduma kwamteja na kuomba taarifa zao za kifedha au kutaka kujua salio lililopo katika laini zao za simu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Dkt. Nchemba Aagiza Fedha Za Maendeleo Zipewe Kipaumbele Kwenye Utekelezaji Wa Bajeti
Na. Josephine Majura, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewaagiza watendaji wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa hakuna Wizara ama taasisi itakayopelekewa chini ya asilimia 50 ya bajeti yake ya maendeleo katika bajeti ya Serikali iliyooanza kutelezwa kuanzia Julai mosi mwaka huu.
Ametoa Maagizo hayo wakati akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine ametoa mwelekeo wa utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2021/2022.
“Nataka mkasimaie ugawaji wa rasilimaji fedha kwa kila Wizara ili tukirudi tena bungeni kuelezea utekelezaji wa bajeti kusiwe na mahali ambapo fedha za maendeleo zitakuwa zimepelekwa chini ya asilimia 50” Alisisitiza Dkt. Nchemba.
Aidha, aliwaagiza watumishi hao kujiwekea utaratibu wa kufuatilia kwa umakini utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotokana na fedha zinakazotolewa na Serikali ili kuona utekelezaji wake na kama zimetumika kama ilivyokusudiwa kwa kuwa itasaidia miradi kukamilika kwa wakati.
Aidha, aliwataka watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia maadili, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma.
Dkt. Mwigulu aliongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan anaitegemea wizara katika masuala yote ya uchumi hivyo ni jukumu la Wizara kuhakikisha inatoa ushauri mbalimbali wa kitaalamu kuhusu masuala ya uchumi kwa maendeleo ya nchi.
Vile vile Dkt. Mwigulu aliwataka watumishi hao kuwa wabunifu hususan katika kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuisaidia Serikali katika kukuza uchumi wa nchi.
Alitoa wito kwa watumishi kuendelea kutumia fursa za mafunzo zilizopo ili kujiongezea ujuzi, lakini pia aliagiza kuwepo na utaratibu mzuri ambao kila mtumishi atapata nafasi ya kuhudhuria mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ili kuongeza ujuzi kwenye taaluma zao.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, aliwapongeza watumishi kwa ufanyaji kazi na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha jukumu la kusimamia uchumi wa nchi inatekelezwa kwa ufanisi zaidi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, alisema kuwa Wizara inaendelea kusimamia uchapaji kazi, maadili na maslahi ya watumishi ambapo watumishi wamepandishwa vyeo na kupandishwa madaraja.
“Tumewapandisha madaraja na kuwabadilishia miundo watumishi 529 baada ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza watumishi wote wapandishwe madaraja wakati wa Siku ya wafanyakazi Mei Mosi na pia tumewathibitisha kazini watumishi 31” alisema Bw. Tutuba
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia Utawala Dkt. Khatibu Kazungu alimhakikisha Waziri wa Fedha na Mipango kwamba atasimamia utaribu wa mafunzo kwa watumishi ili kuwajengea uwezo katika taaluma zao na kuwaongezea ufanisi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia Uchumi Bw. Adolf Ndunguru alisema kuwa Wizara itaimarisha eneo la utafiti ili kuiwezesha Wizara kusimamia uchumi wa nchi.