Monday, 24 February 2020

Everton Yatandikwa 3-2 na Arsenal

Kombora la Pierre-Emerick Aubameyang na bao kutoka kwa kinda Eddie Nketiah yalitosha  kwa Arsenal kunyakuwa ushindi wa 3-2 dhidi ya Everton. 

Mechi hiyo ya Jumapili, Februari 23, iliyosakatwa ugani Emirates iliwashuhudia Arsenal wakitoka nyuma na kulaza miamba wa Merseyside. 

Dominic Calvert-Lewin aliiweka Everton kifua mbele, dakika moja tu katika mchezo huo kwa kuvurumisha hadi nyavuni kupitia shuti la Sigurdsson. Hata hivyo, Nketiah, alisawazishia Arsenal dakika ya 27 ambaye alitingisha wavu baada ya kumalizia krosi tamu ya Sala. 
 
Aubameyang alibadilisha matokeo hayo kuwa 2-1 dakika sita baadaye, kwa kumchenga Jordan Pickford. 

Lakini zikiwa zimesalia sekunde kuingia muda wa mapumziko, Everton walisawazisha bao hilo kupitia kwa Richarlison ambaye aliwasiliana na Bernd Leno na kuhakikisha awamu ya kwanza inaisha sare. 

Awamu ya pili ilimshuhudia Aubameyang akiirejeshea Arsenal uongozi kupitia pasi ya Nicolas Pepe kupitia kichwa kutoka upande wa kulia.

 Upande zote mbili zilishindwa kuonja wavu kwa mara nyingine tena huku wenyeji wakiondoka na ushindi wa 3-2.


Share:

Auawa kwa Radi Akinyolewa Saluni Njombe

Martin Nyigu (35) mkazi wa kijiji cha Lusitu, kata ya Luponde, halmashauri ya mji wa Njombe mkoani Njombe,  amefariki dunia kwa kupigwa na radi jana majira ya saa 9 alasiri akiwa ananyoa nywele saluni huku kinyozi na wateja waliokuwa wanasubiri huduma wakiwa salama.

Diwani wa  Luponde, Ulrick Msemwa, amethibitisha ukweli wa taarifa hizo kwa mujibu wa taarifa za awali alizopokea kutoka kwa mtendaji wa kata hiyo, Patrick Mtundu.


Share:

Halima Mdee Agoma Kumpa Mkono aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.Vincent Mashinji

Baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.Vincent Mashinji kuhamia CCM, leo Februari 24, amekutana na viongozi wa CHADEMA katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa ajili ya kesi yao ya uchochezi inayowakabili mahakamani hapo.

Mashinji alifika mahakamani hapo kisha akaanza kusalimiana na viongozi mbalimbali wa CHADEMA ambao wapo katika kesi moja.

Miongoni mwa aliosalimiana nao ni Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Salum Mwalimu.

Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alikataa kupeana mkono na Mashinji.

Pia Dr.Mashinji alionana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe wakiwa ndani ya chumba cha Mahakama licha ya kuwa hawakupeana mikono.

Kesi hiyo imeitishwa leo mahakamani hapo kwa ajili ya kufanya majumuisho ya mwisho kabla ya kutolewa hukumu.


Share:

Wazalishaji watakiwa kuzingatia viwango

Na Mwandishi wetu -Singida,
Wazalishaji wa bidhaa  mbalimbali mkoani Singida wametakiwa kutambua kuwa suala la viwango ni la kisheria hivyo ni lazima kuthibitisha ubora wa bidhaa ili kumlinda mlaji na kupata uhakika wa soko la bidhaa wanazozizalisha.
 
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu  wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt Rehema Nchimbi alipokuwa akifungua mafunzo ya wazalishaji wa bidhaa za vyakula yakiwemo mafuta ya alizeti na wauzaji wa vipodozi na vyakula yaliyofanyika katika ukumbi wa VETA  mkoani Singida.
 
Dkt. Nchimbi alisema suala la ubora wa bidhaa linapaswa kuzingatiwa katika mnyororo wote wa uzalishaji ili  mlaji awe salama  na kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kutozingatia viwango.
 
“Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ndiyo hakikisho la wazalishaji na fursa zinazotengenezwa zitakuwa dhahiri iwapo masuala ya viwango yatazingatiwa, vilevile TBS ni daraja kati ya mzalishaji na soko, hivyo mzalishaji ni lazima kufuata utaratibu,” alisisitiza Dkt. Nchimbi.
 
Alisema maisha  ya binadamu ni chakula hivyo ni muhimu kuzingatia usalama wake, kwani bidhaa  hafifu zinagharimu afya ya walaji  na kwamba magonjwa mengi yanatokana na jinsi tunavyoandaa chakula na tunavyokula, hivyo wazalishaji wanapaswa kuwa waaminifu katika kuzalisha bidhaa yoyote.
 
Dkt. Nchimbi alisema TBS siyo adui  wazalishaji hawapaswi kuichukia  na wajenge  dhana kuwa TBS ni usama hivyo wazalishaji wa Singida wahakikishe kuwa wanazalisha bidhaa bora wakati wote ili kudhidhirisha kauli kwamba Singida ni njema wakati wote.
 
Akizungumzia kwa upande wa TBS, Dkt. Nchimbi alisema Shirika  linapaswa kuangalia namna ya kuongea na wajasiriamali ili kuhakikisha kuwa yale wanayowafundisha wanaelewa kikamilifu. Mafunzo haya yawe na kipimo ili kujua kama yameeleweka vizuri na kwamba watakaopokea  mafunzo ndiyo watakaowapima.
 
Kwa upande wake Meneja wa  Mafunzo na Utafiti kutoka TBS Bw. Hamisi Sudi alisema Shirika litaendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali ili kuhakikisha kuwa wanazalisha bidhaa kwa kuzingatia viwango.
 
Alisema Shirika linatambua  kuwa wajasiriamali wana mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa wananchi walio wengi hivyo Shirika lina mchakato endelevu wa kutoa elimu kwa jamii hasa wajasiriamali kwakuwa ni mojawapo ya majukumu yake ya kila siku.
 
Shirika likiwa mkoani Singida limetoa mafunzo kwa wajasiriamali 221 Katika wilaya za Iramba, Singida na Manyoni, ambayo pia yamewashirikisha watendaji wa Halmashauri wakiwemo maafisa Biashara, Maendeleo ya Jamii na Afya pamoja na Maafisa kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO). 
 
Pia Shirika linatarajia kutoa mafunzo katika wilaya za Kondoa, Kongwa na ikiwa ni muendelezo wa mafunzo katika Kanda ya Kati.
Mwisho.



Share:

Israel Yadai Kuishambulia Syria Kwa Makombora

Israel inadai kuwa imevishambulia vituo vya kijeshi vya kundi lijiitalo Islamic Jihad karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus. 

Taarifa ya jeshi la Israel inasema kuwa ndege zake zilipiga maeneo ya kundi hilo kusini mwa Damascus, kufuatia makombora yaliyorushwa kutoka Ukanda wa Gaza. 

Taarifa hiyo imesema pia kuwa jeshi la Israel lilirusha makombora yake kuelekea Gaza. 

Hata hivyo, shirika la habari la Syria, SANA, limesema kuwa mfumo wa ulinzi wa nchi hiyo ulifanikiwa kuyatunguwa makombora hayo. 

Kundi la Islamic Jihad linaendesha shughuli zake ndani ya Mamlaka ya Palestina na pia nchini Syria, na jana Jumapili lilirusha makombora yapatayo 20 kutokea Ukanda wa Gaza. 

Mashambulizi haya ya Israel yalifanyika muda mchache, baada ya jeshi kumuua kijana mmoja wa Kipalestina liliyedai alikuwa akitega bomu kwenye mpaka, na kisha kuiburuza maiti yake kwa buldoza, hali iliyozusha hasira kubwa kote Palestina.


Share:

Waziri Mkuu: Sekta Ya Madini Kuchangia Asilimia 10 Ya Pato La Taifa Ifikapo 2025

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hatua iliyofikiwa ya kuzuia uvunaji haramu wa rasilimali kwa utaoji wa cheti cha uhalisia kwa madini ya bati, kutaiwezesha sekta ya madini nchini kuchangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Ameyasema hayo jana (Jumapili, Februari 23, 2020) wakati wa kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania wa mwaka 2020 kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Mkutano huo wa siku mbili ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha  Julius Nyerere.

Waziri Mkuu ambaye amezindua utoaji wa cheti cha uhalisia (certificate of origin) kwa madini ya bati kitakachokuwa kinatolewa na Tanzania, amesema cheti hicho ni muhimu kwa Taifa letu na nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maziwa Makuu kwa kuwa kitaweka utaratibu wa kudhibiti madini hayo.

Waziri Mkuu amesema mambo waliyojifunza katika mkutano huo yatasaidia kuongeza kasi ya kukua kwa mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa. “Wizara ya Madini shirikianeni na wadau wengine katika kuhakikisha mkutano huu unaendelea kuboreshwa kila mwaka na kuongeza washiriki ili kupanua uelewa wa pamoja.”

Waziri Mkuu amesema kuwa ni matarajio ya kila mmoja wao kwamba uzinduzi huo walioufanya utasaidia katika kutekeleza Itifaki ya Kuzuia Uvunaji Haramu wa Rasilimali yaani ‘Protocol Against the Illegal Exploitation of Natural Resources’

“…nafahamu kwamba mkutano wa aina hii unaoihusu sekta ya madini unafanyika kwa mara ya pili hapa nchini. Nitoe wito kwa nchi wananchama kuhakikisha mikutano ya aina hii iweze kuandaliwa katika nchi nyingine na iwe endelevu katika kutoa fursa kwa wadau kutambua fursa zilizopo nchi nyingine.”

 Waziri Mkuu amesema Serikali inaridhishwa na kuimarika kwa utendaji kazi wa sekta ya madini nchini kutokana na mafanikio yake ikiwemo kuongezeka kwa mchango wake katika pato la Taifa. “Mathalan, kupitia Taarifa ya Hali ya uchumi ya Mwaka 2019, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/2020, mchango wa Sekta ya Madini ulikua kwa asilimia 13.7.”

Waziri Mkuu amesema kwenye kipindi hicho, sekta ya madini ilikuwa ya pili katika kuchangia pato la Taifa ikitanguliwa na sekta ya ujenzi ambayo ilichangia pato la Taifa kwa asilimia 16.5.

“Katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia sekta ya madini imeweza kukusanya sh. bilioni 242.53 sawa na asilimia 51.5 ya lengo la mwaka la kukusanya sh. bilioni 470.89.Makusanyo hayo yalitokana na mrabaha, ada ya ukaguzi wa madini, huduma za kimaabara, mauzo ya machapisho mbalimbali ya kijiolojia na ada za leseni.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na utoroshwaji wa madini, Serikali iliamua kuanzisha masoko ya madini nchini kwa lengo la kuondoa mianya ya kuweza kufanya biashara ya madini kupitia njia zisizo rasmi. “Hadi sasa tuna jumla ya masoko ya madini 27 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 28 kote nchini.”

Amesema masoko hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji sahihi wa takwimu za madini tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa kwake, hivyo ametumia fursa hiyo kuwafahamisha wadau wa mkutano huo kuwa masoko hayo yapo wazi kwa wadau wa ndani na nje ya nchi.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa nchi ambazo bado hazijaanzisha masoko ya madini kutumia masoko yaliyoko nchini wakati wakijipanga kuanzisha masoko yao.

“Masoko haya yanafanya kazi katika misingi ya kiushindani na uwazi wa kibiashara. Pia, niwahakikishie kuwa masoko yetu yana ulinzi na usalama wa kutosha na sifa zote za kimataifa zinazohitajika katika kuendesha biashara hiyo. Hivyo, yatumieni vizuri masoko haya.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa sambamba na kuanzishwa kwa masoko ya madini, Serikali pia imefanikiwa kuhamasisha wamiliki wa migodi kuchangia zaidi katika huduma za jamii nakuimarisha usimamizi wa shughuli zinazofanywa na wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo wa madini.

“Vilevile, Serikali imefanikiwa kuongeza ushiriki wa moja kwa moja wa Serikali katika kumiliki na kusimamia migodi, ikiwa ni pamoja na kumilikishwa asilimia 16 ya hisa katika migodi;na kufungamanisha sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi.”

Awali, Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema mkutano huo umehudhuriwa na nchi 11 wanachama waJumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) pamoja na wadau wa sekta ya madini wa ndani na nje ya nchi.

Waziri Biteko alisema lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wa madini katika nyanja tofauti tofauti ikiwemo wachimbaji, wanaotengeneza na kuuza tekinolojia, wadau wenye mitaji na wasionayo lakini pia kwa upande wa Serikali kujifunza namna ya kuboresha na kuifanya sekta ya madini kuwa ni sekta yenye kuongeza tija kwa Taifa.


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatatu February 24






















Share:

Sunday, 23 February 2020

ONGEZEKO LA SANGARA ZIWA VICTORIA LAISHTUA CCM,YATOA MAAGIZO MAZITO

 Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba akibeba samaki aina ya sangara mwenye urefu wa  sentimita 90 akiwa na uzito wa kilo 15 baada ya kutembelea Mwalo wa Nyamikoma Busega Simiyu na kushangazwa na mafanikio ya Serikali ya kudhibiti uvuvi haramu
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba akikagua zana haramu zilizokamatwa katika Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega mkoani Simiyu wakati wa ziara ya Wajumbe wa Sekretarieti ya CCM Mkoa Simiyu kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye Sekta ya Uvuvi. Kulia ni Afisa Mfawidhi Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Simiyu na Magu, Samson Mboje.
 Na Mwandishi Wetu, Simiyu


CHAMA cha Mapinduzi kimeshtushwa na ongezeko kubwa la samaki aina ya Sangara ikiwa ni miaka mitatu tu tangu Serikali ya awamu ya tano kuanza operesheni za kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria na kutaka Serikali kuchukua hatua za haraka kutafuta masoko ya uhakika ya samaki ndani na nje ya nchi.


Wakizungumza kwenye ziara ya Wajumbe wa Sektetarieti ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Simiyu baadhi ya Wavuvi katika Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega wamesema awali kabla ya operesheni kuanza walikuwa wakisafirisha wastani wa tani 6 za samaki kwa mwezi lakini tangu Serikali ilipoamua kuchukua hatua za kudhibiti uvuvi haramu samaki wameongezeka na sasa wanasafirisha wastani wa tani 60 kwa mwezi.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi ‘BMU’ Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega mkoani Simiyu , George James alisema ongezeko hilo kubwa la samaki pia limepunguza bei ya Sangara kutoka wastani wa shilingi 9,000  kwa kilo hadi kufikia shilingi 4,000 kwa kilo.


Mbali na mafanikio hayo pia wavuvi hao wameiomba Serikali kuwasaidia kupata mtambo wa kutengeneza barafu katika eneo hilo kwani kwa sasa wanalazimika kusafiri hadi jijini Mwanza umbali wa zaidi ya kilomita 150 kufuata barafu.


Hivyo walimuomba Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu kumfikishia shukrani Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli  kwa uongozi wake imara hasa katika usimamizi wake wa rasilimali za uvuvi na kwamba sasa samaki ni wengi na kwamba ombi lao kubwa ni kusaidiwa kupata soko baada ya ongezeko hilo la samaki.

Akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega, Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba  aliitaka Serikali kupitia Dawati la Sekta Binafsi lililoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufika katika mwalo huo wa Nyamikoma ili kuwaunganisha wavuvi hao na taasisi za kifedha kuweza kupata mtambo wa kutengeza barafu.


Pia ameitaka Serikali kutanua wigo wa kuwatafutia masoko ya samaki wavuvi hao ili kunufaika na fursa kubwa ya ongezeko hilo la samaki aina ya Sangara kwa kupeleka katika masoko ya mikoa ya mbali na Ziwa Victoria pamoja na nchi za jirani za Kongo, Zambia, Burundi, Rwanda, Malawi na Msumbiji.


Kuhusu vita dhidi ya uvuvi haramu, Katibu huyo alisema Ilani ya CCM imeitaka Serikali kudhibiti uvuvi ili kupata uvuvi endelevu na kuongeza kipato cha mwanchi mmoja mmoja na kuiletea fedha za kigeni Serikali kutokana na mauzo ya samaki nje ya nchi na kupongeza juhudi kubwa zilizofanywa na Rais Dk. John Magufuli katika kusimamia rasilimali hizo za uvuvi.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuamua na kusimamia operesheni Sangara ambayo ilisimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi operesheni hii imezaa matunda kama mlivyotoa ushuhuda kwamba operesheni hii mliipinga sana lakini sasa mnaona matokeo yake”alisema.


Aliongeza kuwa CCM inaamini katika kusimamia sheria na kwamba hatua zote zilizochukuliwa na Serikali katika kudhibiti uvuvi haramu zililenga kunufaisha watanzania wengi tofauti na hapo awali ambapo watu wachache ndio waliokuwa wakinufaika kupitia uvuvi haramu.


“Niipongeze sana Serikali yetu kwa kukubali kutukanwa, kuzuliwa maneno mengi kupata kashfa nyingi lakini bado waliendelea kusimamia msimamo wa kulinusuru ziwa letu kwenye ilani yetu tumesema tutahakikisha tunadhibiti uvuvi haramu ili tuweze kupata samaki wa kutosha kwa ajili ya watanzania sisi CCM tunaomba msiishie hapa endeleeni kudhibiti uvuvi haramu ili matunda yazidi kuongezeka siku hadi siku”alisema Katibu wa CCM


Katika hatua nyingine, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Busega, David Palanjo aliongoza zoezi la uteketekezaji wa shehena ya nyavu haramu zilizokamatwa kwenye operesheni hiyo katika wilaya za Magu na Busega na kutoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kudhibiti uvuvi haramu.
Share:

Tangazo la Nafasi za Kazi Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba



==>>Kwa Nafasi Zingine Nyingi Zikiwemo za Mabenk, Makampuni Binafsi <<BOFYA HAPA>>


Share:

Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo




Share:

K-lyinn Adai Kuzuiwa Kuingia Kwenye Kaburi La Reginald Mengi

Takriban mwaka mmoja baada ya kifo cha bilionea wa Tanzania Reginald Mangi, tayari kumeibuka mgogoro katika familia yake, baada ya mkewe Jacqueline Mengi kudai kwamba amenyimwa kuona kaburi la mumewe.

Katika chapisho lake la twitter, Klynn kama anavyofahamika anasema kwamba amenyamaza vyakutosha. Na sasa ameshindwa kuvumilia baada ya yeye na wanawe pacha kuzuiwa kuona kaburi hilo na kwamba walihitaji kuomba ruhusa.

Katika chapisho hilo malkia huyo wa urembo wa zamani anaendelea kusema kwamb; "Mmefikia hatua ya kunizuia mimi na wanangu kuingia kwenye kaburi la mume wangu, tunafukuzwa eti mpaka tuombe ruhusa ya kuingia kwenye kaburi la mume na baba wa watoto wangu! Nimechoka , sitakubali kuendelea kuona wanangu wakisononeka na sitakaa kimya", alisema Klynn.

Reginald Mengi alifariki mwaka jana mwezi Mei tarehe 2 huko Dubai akiwa na umri wa miaka 75. Wawili hao walikuwa wamefunga ndoa mwaka 2015 na kupata watoto wawili.

Familia ya bilionea huyo haijatoa tamko lolote.


Share:

Waziri Mkuu Awataka Watumishi wa Umma Watenge Muda wa Kusikiliza Kero za Wananchi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametaka watumishi wa umma nchini kote kutenga muda wa kusikiliza kero za wananchi.

Alitoa maagizo hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mwanga Community Centre, Manispaa ya Kigoma Ujiji.

“Watumishi mnatakiwa kwenda kwa wananchi na kusikiliza kero na kushirikiana nao kuzipatia ufumbuzi. …hamuendi na kama mngekuwa mnaenda kusingekuwepo na mabango kwani kitendo cha kuwepo mabango ni ishara tosha kuwa hamuendi,” alisema.

Alisema Serikali imepeleka fedha nyingi mkoani Kigoma za kugharamia miradi ya maendeleo zikiwemo sh bilioni 4.6 za ununuzi wa dawa ambapo Manispaa ya Kigoma Ujiji inapata sh milioni 50 kila mwezi hivyo hakuna sababu wananchi kukosa dawa.

Alisema Serikali ya Rais Dk John Magufuli imedhamiria kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya karibu na wananchi zikiwemo za afya ili kuwapunguzia watu, kutembea umbali mrefu hadi hospitali za wilaya au mkoa.

Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kupitia Baraza la Madiwani kusimamia vizuri matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali ili kugharamia miradi ya maendeleo.

Alikemea wananchi katika maeneo mengi ya mkoa wa Kigoma kudai fidia maeneo hata ya mapori na kukwamisha baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali ya kanda.

Awali, Waziri Mkuu alishiriki swala ya Ijumaa katika msikiti wa Mujahidina uliopo eneo la Buzebazeba mijini Kigoma.

Alitumia fursa hiyo kuwausia waumini wa dini ya Kiislam na wananchi kwa ujumla kuendelea kushikamana na kulinda amani. Pia aliwahamasisha walime zao la michikichi


Share:

Katibu Wa UVCMM Kata ya Hananasifu Ahukumiwa Miaka Mitatu Jela Baada ya Kugundulika Sio Raia wa Tanzania

Katibu wa Umoja wa Vijana CCM Kata ya Hananasifu, Mohamed Nyandu amehukumiwa kulipa faini ya Sh1.5 milioni au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kuishi nchini bila kibali.

Nyandu ambaye imeelezwa kuwa ni raia wa Burundi alikiri kutenda kosa hilo la kuishi nchini kinyume na sheria ya uhamiaji na kutoa taarifa za uongo zikihusisha urai wake.

Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya Kinondoni Vicky Mwaikambo amesema kutokana na mshtakiwa huyo kukiri mashtaka yote matatu yanayomkabili hivyo mahakama hiyo imemtia hatiani na kumtaka kulipa faini ya Sh500,000 kila kosa au kwenda jela miaka mitatu na akitoka jela arudishwe nchini Burundi.

Akisomewa hati ya mashtaka na Wakili wa Serikali Idara ya Uhamiaji, Godfrey Ngwijo amedai kuwa tarehe, mwezi na mwaka usiojulikana mshtakiwa huyo ameingia nchini kwa kutumia njia zisizo halali na alikamatwa Januari 20, 2020 na maofisa wa uhamiaji wa wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Amedai kuwa Januari 20, 2020 katika ofisi za uhamiaji wilaya ya Kinondoni mshtakiwa huyo alikamatwa kwa kosa la kuishi nchini isivyo halali wakati akijua yeye ni raia wa Burundi.

Katika shitaka la tatu mshtakiwa huyo alitoa tarifa za uongo zikihusisha uraia wake kwa maofisa wa uhamiaji ili kujipatia kitambulisho cha Taifa cha Tanzania (Nida) wakati akijua yeye si raia wa Tanzania.

Baada ya kumtia hatiani, wakili wa Serikali alidai kuwa hawana rekodi ya makosa ya nyuma hivyo mshitakiwa anavyoonekana amejihusisha na siasa kwa muda mrefu lengo lake ni kitu gani ukizingatia uhalisia wa nchi aliyotoka katika mambo ya usalama.

“Hivyo naiomba mahakama hii impe adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,”alidai Shija.

Hata hivyo baada ya Hakimu Mwaikambo kumuhukumu kulipa faini ya Sh1.5 milioni lakini mshtakiwa huyo alishindwa kulipa faini hivyo ameenda gerezani kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela. Atarudishwa Burundi baada ya kumaliza kifungo.


Share:

UINGEREZA YAPIGA MARUFUKU UHUSIANO WA MAPENZI KATI YA WAFANYAKAZI NA WANAFUNZI

Chuo Kikuu cha London chaanzisha sera ya kupiga marufuku uhusiano wa mapenzi chuoni

Marufuku ya kuwa na uhusiano wa mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha London ni mwamko mpya kwa vyuo vikuu, wachambuzi wamesema.

Makundi ya wanafunzi yamesema kwamba ni imani yao kuwa sera sawia na hiyo zitaanza kutekelezwa na vyuo vingine.

Chuo Kikuu cha London kinaaminika kuwa cha tatu nchini Uingereza kuanzisha marufuku hiyo.

Inasemekana kwamba sera hiyo inalenga kuzuia unyanyasaji kwa walio na madaraka na vitendo vya ngono.

Kelsey Paske, maneja wa kitengo kinachoangazia tabia ya utamaduni, amesema sera hiyo pia inalenga kutatua migogoro ambayo huenda ikazuka kutokana na mahusiano "huenda yakawa na athari mbaya katika mazingira ya kwenye taasisi za masomo".

Sera mpya ya mahusiano katika Chuo Kikuu cha London kwa wafanyakazi, kulingana na gazeti la the Guardian, inakataa "mahusiano ya karibu na ya mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi pale ambapo kuna usimamizi wa moja kwa moja".

Uhusiano wa mapenzi kati ya mfanyakazi na mwanafunzi ambaye hamsimamii kimasomo moja kwa moja ni lazima uwekwe wazi na mfanyakazi.

Sera hiyo pia inakataza mahusiano ya mapenzi na wafanyakazi au wanafunzi wenye umri wa chini ya miaka 18 au watu wazima ambao wako katika hatari mfano, yule ambaye atahitaji usaidizi maalumu kwasababu ya ulemavu.

Kukiuka sera hiyo kutachunguzwa na kitengo cha kukabiliana na utovu wa nidhamu chuoni, ambao ni pamoja na uwezekano wa kuchukuliwa kwa hatua kuanzia kupewa onyo rasmi hadi kufutwa kazi au kufukuzwa chuoni.

Dr Anna Bull, wa shirika moja linalopinga vitendo dhidi ya tabia zinazoendeleza ngono katika taassi za shule za juu, amesema kwamba shirika lake linaunga mkono kikamilifu sera hiyo mpya na ni matumaini yao kwamba vyuo vingine vikuu vitafuata mkondo huo.

Alisema kuwa sera hiyo ni moja ya sheria kali Uingereza ambayo pia inatekelezwa na vyuo vikuu vingine viwili vya Greenwich na Roehampton.

Dr Bull ameongeza kuwa vyuo vingi vina sera ambazo zinakemea vikali uhusiano wa mapenzi kati ya wahadhiri na wanafunzi lakini sheria kama hiyo bado huenda ikatoa mwanya kwa wafanyakazi wanaotaka kuwa na uhusiano na wanafunzi ambapo wafanyakazi wanaweza kuitisha vikao nje ya jengo la chuo au hata kuzungumza na mwanafunzi kwa namna inayoashiria kuwa anatafuta uhusiano wa mapenzi.

"Tunaona kwamba huu ni mwito kwa sekta hii kuanza kuwajibika kwa kuhakikisha wanafunzi wanalindwa dhidi ya wahadhiri kutumia vibaya madaraka yao," amesema.
Share:

TYSON AMTWANGA DEONTAY WILDER RAUNDI YA 7 NA KUWA BINGWA MPYA WA WBC


Tyson Fury ameshinda pambano lake la leo Februari 23, 2020 la uzito wa juu dhidi ya Deontay Wilder kwa TKO raundi ya 7 na kuwa bingwa mpya wa WBC.



Tyson alionyesha umahiri wake katika ulingo baada ya kumaliza ufalme wa Deontay Wilder wa miaka mitano na kuchukuwa mkanda wa WBC katika uzani mzito duniani baada ya kumwangusha binngwa huyo kwa njia ya knockout katika raundi ya saba.

Katika mechi iliochezwa katika Mecca ya ndondi mjini Las Vegas nchini Marekani raia huyo wa Uingereza mwenye umri wa miaka 31 alimshinda mpinzani wake katika pigano ambalo ni wachache wangeweza kutabiri..

Mchanganyiko wa ngumi za kulia na kushoto ambazo Wilder amekuwa akizitumia kuwalambisha sakafu wapinzani wake zilitumika dhidi yake na kuangushwa katika raundi ya tatu na tano.

Fury alihakikisha ametimiza aliyoahidi na kubadili mbinu zake kutoka upigaji hadi mwenendo wake na kumzidia nguvu mpinzani wake ambaye hajawahi kushindwa.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Tyson ameandika: “Nataka kusema Deontay Wilder, ameonyesha weledi wake. Amepigana hadi raundi ya saba. Yeye ni shujaa, atarejea tena kuwa bingwa. “Lakini mfalme amerejea katika kiti chake.”

Tyson Fury akizungumza na BT Sport: “Nilimwambia kila mmoja kwamba mfalme anarejea kwenye kiti chake. katika pigano langu la mwisho karibu kila mmoja alinikashifu. Nilikuwa na uzani wa chini na nilifanya mazoezi kupitiza. Mimi ni muharibifu. lakini sio vibaya kwa mwanamasumbwi.

“Natimiza ninachosema. Nilimwarifu Wilder, timu yake, na dunia nzima. Tulifanya mazoezi ya knockout.

“Ninazungumza hivi kwasababu ninaweza kutoa ushahidi wa ninachokizungumzia. Watu walinisema vibaya, waliangalia kitambi changu na upara wangu na kudhania kwamba siwezi kupigana. Alipigana kwa weledi kadiri ya uwezo wake wote Tyson Fury na kila mmoja yuko katika kipindi chake cha juu.

“Namtarajia [Wilder] aombe pigano la tatu. najua kwamba yeye ni shujaa na mimi nitakuwa na msubiri.”

Fury kisha akasema kwamba anataka pambano la tatu dhidi ya Wilder lifanyike uwanja wa Las Vegas ambao kwa sasa unajengwa na utafunguliwa hivi karibuni.

Kulingana na timu yake, Wilder amepelekwa hospitali kushonwa baada ya kujeruhiwa kwenye sikio.

-BBC


Share:

JAJI KUFUNGULIWA MASHITAKA KWA KUDAIWA KUSHIRIKIANA NA MSHUKIWA WA MAUAJI

Jaji mmoja nchini Kenya anayejulikana kwa jina la Sankale Ole Kantai atafunguliwa mashtaka Mahakamani kufuatia madai kwamba alishirikiana na mshukiwa wa mauaji.

Jaji huyo wa Mahakama ya rufaa, Sankale Ole Kantai alikamatwa na maafisa wa jinai siku ya Ijumaa na kuhojiwa kuhusu uhusiano wake wa karibu na Sara Waimu , mshukiwa mkuu wa mauaji ya raia wa Uholanzi Tob Cohen.

Jaji huyo aliachiliwa siku ya Jumamosi mchana kwa dhamana baada ya kulala katika kituo cha polisi cha Muthaiga ambapo alikuwa anazuiliwa. Atawasilishwa mahakamani siku ya Jumanne.

Idara ya Jinai imethibitisha kwamba jaji huyo atafunguliwa mashtaka ya kuwa na njama ya kuilaghai haki na kuingilia mashahidi.

Mwili wa raia huyo tajiri kutoka Uholanzi ulipatikana katika shimo la maji taka nyumbani kwake jijini Nairobi 2019.

Kwa mujibu wa BBC, Maafisa wa polisi wanasema kwamba wana sababu za kuamini kwamba jaji Sankale alikuwa na uhusiano wa karibu na mshukiwa huyo ambaye amedaiwa kumpa ushauri ili kukabiliana na kesi yake mahakamani.


Share:

Mwanajeshi Mwingine wa Uturuki Auawa Kwa Bomu Na Vikosi Vya Syria Vinavyoungwa Mkono na Urusi

Askari mwingine wa Uturuki ameuawa kwenye shambulio la bomu katika mkoa wa Idlib. 

Huyo ni askari wa 16 kuuawa kwenye mashambulio yanayofanywa na vikosi vya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi. 

Wizara ya ulinzi ya Uturuki imesema mauaji hayo yametokea wakati ambapo mazungumzo ya kusitisha mapigano baina ya Ankara na Moscow yamekwama. 

Kuongezeka kwa vifo vya wanajeshi wa Uturuki, kunaweza kuondoa uwezekano wa kupatikana suluhu ya kusitisha mapigano katika eneo la Kaskazini magharibi mwa Syria. 

Tangu mapema mwezi Desemba, raia karibu milioni moja wa Syria wengi wao ni wanawake na watoto hawana makaazi na hasa katika kipindi hiki cha baridi kutokana na mapigano. 

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan anatarajia kukutana na viongozi wenzake wa Urusi, Ujerumani na Ufaransa Machi 5 kwa ajili ya kuuzungumzia mkoa wa Idlib.

Baada ya syria kukumbwa na vita kwa miaka tisa sasa, vikosi vya serikali ya Syria vinapambana kulidhibiti eneo hilo la mwisho linaloshikiliwa na waasi.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger