Monday, 2 September 2019
Sunday, 1 September 2019
WAANDISHI WA HABARI WATAMBULISHA KUNDI LA 'STRONG DADAZ JOURNALIST' ...DC MAHUNDI ATIA NENO
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya,Mhandisi MaryPrisa Mahundi akiwa katika picha ya pamoja na kikundi cha Strong Dadaz Journalist
Na Esther Macha,Chunya
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya,Mhandisi MaryPrisa Mahundi amewataka wanawake kuendelea kujituma kufanya kazi ili kuongeza thamani yao katika maisha badala ya kutegemea kuolewa.
Akizungumza na waandishi wa habari wanawake waliomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kutambulisha kikundi chao kinachojulikana Strong Dadaz Journalist kilichopo Mkoani Mbeya.
Mhandisi Mahundi aliwataka wanapofanya kazi pia kazi wajitahidi kumtanguliza mungu wakati wanafanya kazi zao za kila siku ili waweze kufanikiwa katika shughuli zao.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa pia wajiongozee dhamani pamoja na kusaidiana wenyewe kwa wenyewe ili kufikia malengo waliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kupendana.
“Siri ya Mwanamke ni kujishughulisha katika maisha msikate tama wanawake wenzangu kitendo cha nyie kuamua kuwa na umoja wenu ni faraja tosha kwenu”alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha Mhandisi Mahundi alitoa kiasi cha shilingi laki tano kwa ajili ya kusaidia kikundi hicho cha Strong Dadaz Journalist ili kiweze kusajili Online Tv ambayo kikundi hicho kimedhamiria kufungua ili kuboresha huduma za kihabari kwa wanawake katika kurahisisha upatikanaji wa habari kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bomba Fm Radio ,Fredy Herbert aliahidi kuchangia kikundi hicho sh.100,000/= katika kusaidia kukamilisha usajili wa Online tv.
“Mhe. mimi nitakuwa na waandishi hawa pindi watakapohitaji msaada wa jambo lolote nitakuwa nao karibu katika kuwasaidia ",alisema Mkurugenzi huyo.
BASI LA MWENDOKASI LATEKETEA NA MOTO KIMARA JIJINI DAR ES SALAAM
Basi la usafiri wa haraka (Mwendokasi) la kampuni ya UDART la limeshika moto na kuteketea eneo la Kimara, jijini Dar es Salaam usiku huu.
Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na pia hakuna taarifa kuhusu majeruhi ama vifo kwenye moto huo.
JISAJILI KUSHIRIKI MKUTANO WA KIBIASHA NA MAONESHO KATI YA TANZANIA NA UGANDA SEPT 6-7, 2019 JIJINI DAR ES SALAAM
• Sisi ni Zaidi ya Ujirani
• Sisi ni ndugu wa Damu
Tanzania na Uganda katika meza moja ili kukuza na kujenga Uchumi imara na madhubuti!
#TZUGBusinessForum19
#SisiNiTanzaniaMpyA+ ya Wazalendo, Waadilifu, Waaminifu, Wachapa Kazi!
PAPA FRANCIS AKWAMA KWENYE LIFTI DAKIKA 25 BAADA YA UMEME KUKATIKA AKIWAHI KANISANI
Papa Francis ameomba radhi kwa kuchelewa misa katika kanisa la Mt. Petro na kusema kuwa alikwama kwenye lifti akiwa anaelekea kanisani.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 alikwama kwenye lifti kwa dakia 25 mara baada ya umeme kukatika na kuweza kutoka kabla ya kikosi cha wazima moto hakijawasili.
"Ninapaswa kuomba radhi kwa kuchelewa," Papa huyo aliawaeleza waumini wake huku akitabasamu.
Na kuwataka waumini wote kuwapongeza wazima moto kwa kazi kubwa waliofanya .
Papa akiwahutubia umati wa watu kusema "kumekuwa na itilafu ya umeme hivyo lifti ilisimama".
"Namshukuru Mungu na kikosi cha zima moto kilifika kwa wakati"
Televisheni inayorusha matangazo ya moja kwa moja ya sala hiyo walihisi papa huyo amechelewa kufika katika misa kutokana na sababu za kiafya, shirika la habari la AFP limeripoti.
Papa huyo alitangaza pia kuwa mwezi ujao, atatangaza makadinari 10 wapya wa kanisa katoliki.
Chanzo - BBC
FAIZA ALLY AFUNGUKA BAADA YA SUGU KUOA MWANAMKE MWINGINE
Mzazi mwenza wa Mbunge wa Mbeya Mjini Sugu, Faiza Ally amesema amependezwa na tukio la kufunga ndoa kwa Joseph Mbilinyi, na anaamini sasa Mbunge huyo anaenda kuwa na maisha ya furaha zaidi.
Faiza ametoa kauli hiyo ikiwa saa chache baada ya Mbunge Sugu kufunga ndoa na mkewe Happines Msonga, ambapo kupitia mtandao wake wa Instagram, amesema licha ya Sugu kuoa bado ana mapenzi na yeye.
"Kuna mtu anayenipemnda sana alinipa ratiba nzima mwezi mmoja kabla ya ndoa na kabla ya hapo nilijua kama wataoana ila siku ya tukio ni siku ya tofauti, hata mwanzoni nilipotaka kufanya jambo nilijikuta nakosa hisia za kufanya kwa sababu sina tena majonzi juu ya baba Sasha.", amesema Faiza.
Ameendelea kusema, "nikimwangalia baba Sasha na mke wake sioni mtu wa kuniliza na najiuliza nilikosea wapi, kwa sababu nilikuwa mpenzi bora, nilikuwa mama bora kwahiyo sijapata mwanaume tu wa kunielewa mimi. Anaoa lakini najua bado ananipenda mimi".
Mapema jana Agosti 31, 2019 Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi 'Mr.II Sugu' alifunga ndoa na mpenzi wake Happiness Msonga, katika kanisa Katoliki, Ruanda jijini Mbeya.
ALIYENASWA AKIFANYA MAPENZI NA MWANAFUNZI NDANI YA CHUMBA CHA MAMA YAKE ATUPWA JELA MIAKA 30
Mkazi wa Kata ya Mikumbi, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Abdull Mohamedi (30) amehukumiwa kifungo cha miaka (30) Gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na hatia ya kujihusisha kimapenzi na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa Mahakama ya Mkoa huo, James Karymaha baada ya kuthibitisha bila shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Hakimu Karyamaha akitoa hukumu katika kesi hiyo namba 08/2019 kupitia kifungu cha Sheria namba 130 kifungu kidogo (1) na (2) na 131 kifungu cha (2) amesema kutokana na kubanwa na Sheria amemuhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwanasheria wa Serikali Abdulaha Madi Mohamedi kuwa mshitakiwa alikamatwa na mama mzazi wa mwanafunzi huyo Salma Salum, Julai 05, 2019, akiwa chumbani ndani ya nyumba yake na mtoto wake akishiriki mapenzi.
Mwanasheria huyo wa Serikali, amesema baada ya Mama mzazi kumkuta mshtakiwa akiwa na mtoto wake alitoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Mtaa na Kata yao na majirani, ambao walifika na kufanikiwa kumkamata na kumfikisha kituo cha Polisi.
Kabla ya Jaji Ngwembe hajatoa adhabu hiyo, mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea na kuomba imuonee huruma kwa kutompa adhabu kali, kwa madai ni mkosaji wa mara ya kwanza na pia shetani mbaya wa mapenzi alimpitia.
Chanzo - EATV
TAZAMA PICHA ZA BARABARA YA KYAKA-BUGENE
Picha zikionesha Sehemu mbalimbali za Barabara ya Kyaka-Bugene mkoani Kagera. Barabara hiyo yenye Urefu wa Kilometa 59.1 ni kichocheo kikubwa cha Uchumi katika Mikoa ya Kanda ya ziwa pia huunganisha nchi ya Tanzania na nchi jirani za Rwanda na Burundi. PICHA NA IKULU
Sehemu ya Barabara ya Kyaka- Bugene katika eneo la Kishoju Karagwe mkoani Kagera.
WAZIRI LUGOLA AAGIZA BODABODA ZOTE ZISAJILIWE..., AWATAKA TRAFIKI KUACHA VISINGIZIO
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati), akimsikiliza Katibu wa Chama cha Wamiliki na Waendesha Bajaj na Bodaboda Mkoa wa Kilimanjaro (CWBK), Rashid Omary, alipokuwa anatoa pongezi kwa Waziri huyo, kuwasaidia kupata eneo la maegesho ya Bajaj na Bodaboda Shairifu, Mjini Moshi, leo. Mwezi uliopita, Lugola alitatua mgogoro uliopo kati ya Manispaa ya Moshi na CWBK kuhusiana na maeneo ya maegesho. Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Khamis Issa, na wapili kulia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani humo, Zauda Mohammed. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (aliyevaa Kaunda suti), akikagua eneo la maegesho ya Bodaboda na Bajaj, Sharifu, Mjini Moshi, leo. Lugola aliambatana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Khamis Issa (kulia), kukagua maeneo ya Aghakan na Shairifu ambalo lilileta mgogoro kati ya Manispaa ya Moshi na Chama cha Wamiliki na Waendesha Bajaj na Bajaj Mkoani humo (CWBK), na kutatuliwa na Waziri huyo mwezi uliopita, mjini humo. Wapili kushoto ni Katibu wa CWBK, Rashid Omary. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia), akimuaga Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki na Waendesha Bajaj na Bodaboda Mkoa wa Kilimanjaro (CWBK), Rashid Omary, mara baada ya kumaliza kukagua vituo vya Sharif una Aghakan vya maegesho ya Bodaboda na Bajaj, Mjini Moshi, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akimuaga Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, Zauda Mohammed (kushoto), mara baada ya Waziri huyo, kumaliza kukagua vituo vya Sharif una Aghakan vya maegesho ya Bodaboda na Bajaj, Mjini Moshi, leo. Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa huo, Khamis Issa. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………………………………………..
Na Felix Mwagara, Moshi (MOHA).
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amelitaka Jeshi la Polisi Kikosi Usalama Barabarani washirikiane na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuzisajili bodaboda na bajaj zote nchini ili ziweze kudhibitiwa katika ukusanyaji wa faini pamoja na matukio mbalimbali ya kiuhalifu zinapofanya makosa.
Lugola alisema ushirikiano kati ya viongozi au askari waliopo chini ya halmashauri nchini ipo ndani ya sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi Sura namba 322, hivyo Jeshi lake linapaswa kushirikiana na Polisi Wasaidizi waliopo chini ya halmashauri ya Miji, Wilaya, Manispaa na Jiji kwa mujibu wa sheria.
Waziri Lugola ameyasema hayo Mjini Moshi, leo, wakati alipokuwa anakagua vituo vya bodaboda na bajaj mjini humo ambapo mwezi uliopita alifanya mkutano na wamiliki na waendesha bodaboda na bajaj mkoani humo kwa lengo la kutatua migogoro mbalimbali waliokuwa wanailalamikia Manispaa ya Moshi kuwanyanyasa pamoja na kuwafukuza kuegesha kituo cha Sharif una Aghakan mjini humo ambapo Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabara Mkoani humo aliwaelekeza wawepo katika eneo hilo.
“Askari wa usalama barabarani, muache visingizio kuwa ukamataji wa bodaboda ni mgumu hasa mnapowaandikia makosa walipe baada ya siku saba, mara usingizia bodaboda hazipo katika mfumo wa TRA kama magari, tukiziachia tuzipate wapi, nilishawaelekeza mshirikiane na viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijijini, Miji, Manispaa na Jiji kuanzisha kanzi data, kwenye mfumo wa kuwasajili waendesha bodaboda wote sehemu mbalimbali nchini, na taarifa za bodaboda hizo endapo zinafanya makosa inakua rahisi kuzikamata kwasababu zipo kwenye mfumo,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kuwa, lengo la usajili wa bodaboda huo, ni kutokana na kuepuka kuzikamata hovyo na kuziweka vituoni jambo ambalo analipinga kuepusha mlundikano wa boaboda vituoni na pia kuwasababishia bodaboda hao kuwaongezea umaskini zaidi.
“Naomba niendelee kurudia tena agizo hili, bodaboda zinazopaswa kuwepo vituo vya polisi ni za aina tatu, moja bodaboda zilizotumika katika matukio ya uhalifu, mbili zilizohusika katika ajali, na tatu bodaboda zilizookotwa, mbali na makundi hayo zinapaswa kulipwa faini,” alisema Lugola.
Pia Lugola aliwataka baadhi askari na wananchi kuacha tabia ya kuwatuhumu viongozi wanapowatetea waendesha bodaboda wanaambiwa kuwa wanasiasa ndiyo wanasababisha ajali kuongezeka.
Amesema kauli hiyo sio sahihi, kwani wanaosababisha ajali asilimia 76 kwa mujibu wa utafiti wa ajali zinazotokea barabarani zinasababishwa na makosa ya wanadamu na sio bajaj na bodaboda peke yao, na asilimia 24 za ajali zinatokea zinasababishwa na ubovu wa miundombinu.
“Kumekuwa na dhana potofu kwamba wanasiasa kama mimi tunasababisha ajali za bodaboda, kwasababu tunawatumia bodaboda kwa mgongo wa siasa, sasa nataka niwaambie, wanaosababisha ajali barabarani ni asilimia 76 ni makosa ya wanadamu ambao ni wanadamu watembea kwa miguu, waendesha baiskeli, wenye mikokoteni, wanafuga mifugo barabarani na madereva ndio wanasababisha ajali, na sio bodaboda wala bajaj peke yao,” alisema Lugola.
Lugola amesema hakuna mahali popote ambayo tumesema baodaboda wakifanya makosa wasikamatwe, tunachosema na kusimamia nikupunguza umaskini kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo inaelekeza Bodaboda na Bajaj wafanye biashara ili wapunguze umaskini.
Aidha, Lugola amesema Serikali ya Magufuli inataka wananchi Watanzania wajiajiri hivyo sekta ya bodaboda lazima iheshimika kwakua nao wanatafuta ridhiki kama ilivyo kwa watanzania wengine.
OPARESHENI YA KIJANI YATUA KIGOMA..... WAZEE WATAKIWA KUPISHA VIJANA NAFASI ZA UONGOZI
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Wazee wametakiwa kutoa nafasi kwa vijana waweze kugombea katika nafasi za uongozi na kuacha tabia ya kuwatisha na kuwazuia vijana ili kuwajengea msingi mzuri na kuwapima katika nafasi mbalimbali ili kujenga viongozi watakaoongoza kwa hekima na busara.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi taifa (UVCCM) Kheri James mkoani Kigoma wakati wa uzinduzi wa 'Oparesheni ya Kigoma ya Kijani'.
James alisema nchi inahitaji utayari wa vijana na uongozi wa vijana hivyo lazima wazeee wawaachie vijana kugombea na wasiwanyime nafasi ili waweze kuwapima na kuwajengea weledi wa uongozi na busara kwa kipindi hiki ambacho bado kuna wazee wenye busara ili waweze kuwapa busara hizo na waweze kubaki viongozi wazuri.
Alisema vijana wakipewa nafasi kwa kipindi hiki ambacho bado kuna wazee wa kuwapima kutokana na busara zao namna gani ya kuongoza, itasaidia kutengeneza taifa lenye uongozi ulio bora na unaozingatia misingi ya waasisi wa Taifa la Tanzania na kuepuka kuacha taifa la watu wanaofanya maamuzi bila kutumia busara.
Aidha James aliwataka wananchi wa mkoa wa Kigoma kuwapuuza wanasiasa wanaotumiwa na watu wa nje kuivuruga nchi, kwa kusema kwamb Tanzania kuna matatizo na hakuna kilichofanyika jambo ambalo sio kweli kwa kuwa mambo yaliyofanywa na Serikali iliyopo madarakani yanaonekana.
Alisema Siasa hazifai kutweza juhudi zinazofanywa na serikali kwa maslahi ya Taifa letu, hivyo wanasiasa wanatakiwa kujua kazi yao ni kukosoa pale jambo linapoonekana haliendi sawa na kupongeza pale serikali inapofanya vizuri na sio kutumiwa na watu wa nje kuwakatisha tamaa viongozi wanaoifanya nchi isonge mbele kwa kuwa uchumi.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kigoma, Amandus Nzamba alisema watajitahidi kutoa nafasi kwa vijana, ili na wao waweze kujifunza namna ya kuongoza na kuiletea nchi maendeleo.
Aidha aliwaomba vijana kujitokeza kwa wingi kugombea uongozi kuanzia ngazi ya serikali za mitaa hadi uongozi wa juu, kwa kuwa vijana wengi wanaogopa kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali hivyo sasa ni wakati wao.
Nae katibu wa Umoja wa Vijana(UVCCM) Kigoma Rashidi Semindu alisema Vijana Kigoma wamejipanga katika chaguzi zinazokuja ikiwa ni pamoja na kulirudisha jimbo la kigoma mjini kwa chama cha mapinduzi na kuhakikisha vijana wote wanajitokeza na kupambana na upinzani kwa Mkoa wa Kigoma.
Alisema wamefanikiwa kuwarudisha kwenye Chama Cha Mapinduzi vijana 82 wakiwemo waliokuwa Viongozi wa chama cha ACT wazalendo, wataendelea kuwashawishi vijana kutokana na mambo Makubwa yanayofanywa na viongozi wa CCM Kwa kuleta maendeleo Tanzania.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM)Taifa Kheri James pembeni ni Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kigoma Silvia Sigula akikaribishwa Mkoani Kigoma.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM)Taifa Kheri James pembeni ni Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kigoma Silvia Sigula akikaribishwa Mkoani Kigoma.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM)Taifa Kheri James pembeni ni Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kigoma Silvia Sigula akikaribishwa Mkoani Kigoma.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM)Taifa Kheri James pembeni ni Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kigoma Silvia Sigula akikaribishwa Mkoani Kigoma.
RAIS MAGUFULI NA MKEWE WAMESHIRIKI MISA TAKATIFU DOMINIKA YA 22 MWAKA 'C' KATIKA KANISA KATOLIKI LA MTAKATIFU PETRO PAROKIA YA OYSTERBAY DAR
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mkewe Janeth Magufuli, Mama Marry Majaliwa (Mke wa Waziri mkuu Mhe. Kassim Majaliwa) pamoja na Waumini wengine wa Kanisa Katoliki wakishiriki Misa Takatifu Dominika ya 22 ya Mwaka “C” iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay jijini Dar es Salaam. Ibada iliyoongozwa na Paroko Msaidizi Padre Dkt. Alista Makubi, Septemba 01,2019.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mkewe Janeth Magufuli, Mama Marry Majaliwa (Mke wa Waziri mkuu Mhe. Kassim Majaliwa) pamoja na Waumini wengine wa Kanisa Katoliki wakishiriki Misa Takatifu Dominika ya 22 ya Mwaka “C” iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay jijini Dar es Salaam. Ibada iliyoongozwa na Paroko Msaidizi Padre Dkt. Alista Makubi, Septemba 01,2019.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisali katika Misa Takatifu Dominika ya 22 ya Mwaka “C” iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay jijini Dar es Salaam. Ibada iliyoongozwa na Paroko Msaidizi Padre Dkt. Alista Makubi, Septemba 01,2019.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisali katika Misa Takatifu Dominika ya 22 ya Mwaka “C” iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay jijini Dar es Salaam. Ibada iliyoongozwa na Paroko Msaidizi Padre Dkt. Alista Makubi, Septemba 01,2019.
Picha zote na IKULU
TAASISI NUNUZI ZASISITIZWA KUJIUNGA NA MFUMO WA MANUNUZI YA UMMA KWA NJIA YA MTANDAO (TANePS)
Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo akikabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo kwa mmoja wa washiriki.
Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo akiwahutubia washiriki wa mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo wa TANePS yaliyofanyika jijini Arusha.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika mafunzo kwa vitendo kuhusu matumizi ya mfumo wa TANePS .
Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imetoa wito kwa Taasisi nunuzi kuwaruhusu watumishi wa vitengo vya usimamizi wa manunuzi pamoja na mifumo ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kushiriki kwenye mafunzo kuhusu matumizi ya Mfumo wa Manunuzi ya Umma kwa njia ya Mtandao ili ziweze kuunganishwa na kufanya manunuzi yake kwa kutumia mfumo huo.
Wito huo umetolewa jijini Arusha na Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo, alipokuwa akifunga mafunzo ya siku sita kuhusu matumizi ya Mfumo huo unaojulikana kwa jina TANePS (Tanzania National e-Procurement System) kwa maafisa 110 wa vitengo vya usimamizi wa manunuzi na Tehama kutoka Taasisi 44.
Mhandisi Kapongo amezisisitiza Taasisi nunuzi kuhakikisha zinaunganishwa na kisha kufanya manunuzi yake kwa kutumia mfumo huo wa TANePS ili kukidhi matakwa ya sheria ya manunuzi ya umma pamoja na uamuzi wa Serikali kutaka taasisi zote za umma kuunganishwa na TANePS ili ziweze kufanya manunuzi yote kupitia mfumo huo kwa lengo la kurahisisha michakato ya manunuzi kufanyika kwa ufanisi na tija zaidi na kuhakikisha upatikanaji wa thamani halisi ya fedha.
Amezitaja baadhi ya faida za mfumo wa TANePS unaosimamiwa na PPRA kuwa ni kupunguza gharama na muda kwenye michakato ya manunuzi serikalini pamoja na kuongeza uwazi, ushindani na usawa kwa wazabuni na watoa huduma wanaoshindania zabuni mbalimbali zinazotangazwa na Taasisi za Umma.
“TANePS inawezesha mchakato wote wa manunuzi serikalini kufanyika kielektroniki ambapo hakutakuwa na sababu ya wazabuni kutumia muda mwingi kutembelea ofisi za Taasisi za Umma pale wanapotaka kushindania zabuni, pia hawawezi kukutana ana kwa ana na watumishi wa taasisi za umma kwa kuwa kila kitu kinafanyika mtandaoni,”alisema Mhandisi Kapongo.
Aidha, Mhandisi Kapongo ametoa wito kwa wafanyabiashara, wazabuni na watoa huduma kuhakikisha wanajisajili kwenye mfumo huo ili waweze kushiriki au kushindania zabuni mbalimbali zinazotangazwa na taasisi za umma.
Tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti, 2019, wataalamu kutoka PPRA wamepiga kambi jijini Arusha kwa ajili ya kutoa mafunzo kuhusu matumizi ya TANePS kwa awamu tofauti, programu inayotarajiwa kuwa endelevu ili kutoa fursa kwa wataalamu wa manunuzi kwenye taasisi zote za umma kupata fursa ya mafunzo hayo. Tangu kuanza kwa programu hii kabambe jumla ya watumishi 204 kutoka taasisi za umma 75 wameshapatiwa mafunzo hayo, ambapo wahusika wanapaswa kutembelea tovuti ya mfumo (www.taneps.go.tz) au tovuti ya PPRA (www.ppra.go.tz) ili kupata zaidi maelezo ya namna kujisajili kushiriki.
Mafunzo haya yanagharamiwa na Serikali pamoja na ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).