INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Wednesday, 1 June 2016
Magufuli: Serikali Itakomesha Watumishi na Wanafunzi Hewa
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
RAIS
John Magufuli (pichani) amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga
kumaliza makosa yote yaliyojitokeza huko nyuma ikiwemo tatizo la
watumishi na wanafunzi hewa lililoibuka hivi karibuni.
Amewataka
Watanzania kuacha kuingiza siasa kwenye makosa yanapojitokeza, hasa
yale yanayogusa sehemu nyeti kama elimu, kwani yakiachwa kuna uwezekano
wa kutengeneza taifa la watu wa ajabu.
Alisema
tangu aingie madarakani amekumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo
matatizo ya rushwa, ukwepaji kodi, watumishi hewa na sasa amekumbana na
tatizo la wanafunzi hewa.
“Nchi
yetu ina changamoto na mambo mengi sana hata mimi nimekumbana na
changamoto naziona mwenyewe, nikigeuka hivi watumishi hewa ambao hadi
sasa wamefikia 10,500, nikigeuka hivi kuna wanafunzi hewa,” alisisitiza.
Alisema
ni Tanzania pekee ambayo mtu anaweza kupata daraja la nne kidato cha
nne katika elimu ya sekondari, halafu akapata fursa ya kujiunga na chuo
kikuu na kupatiwa mkopo wa serikali, wakati mhitimu aliyefaulu kidato
cha sita akikosa fursa hiyo.
Alisema
endapo kulifanyika makosa lazima yarekebishwe, kwani inafahamika fika
mtu akimaliza kidato cha nne akifeli ataanzia ngazi ya Astashahada,
Stashahada ndio apate nafasi ya kujiunga chuo kikuu.
“Sasa hapa kwetu ni tofauti ukifeli kidato cha nne unajiunga chuo kikuu,” alihoji
na kuwataka watu waache siasa kwenye makosa kwani mambo kama hayo
yakiachwa kuna hatari ya nchi kutengeneza taifa la ajabu.
Hivi
karibuni, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo Ufundi,
Profesa Joyce Ndalichako aliivunja Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na
kuwasimamisha kazi viongozi wanne waandamizi kwa tuhuma za kudahili
wanafunzi wasio na sifa.
Aidha,
Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Awadh Mawenya naye alisimamishwa kazi kwa
kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliodahili wanafunzi hao
wasio na sifa.
Profesa
Ndalichako alichukua hatua hizo baada ya TCU kudahili wanafunzi 489
waliopata daraja la 4.32 katika mitihani yao ya kidato cha nne lakini
walijiunga na chuo kikuu na kupatiwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni
784.
Mauaji ya Kutisha: Watu 8 Wakamatwa Kwa Mwenyekiti wa Kitongoji na Kuchinjwa Kinyama
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
MAUAJI
ya Watanzania kwa njia ya kuchinjwa yanaendelea kushika kasi baada ya
usiku wa kuamkia jana wakazi wanane wa kitongoji cha Kibatini, kata ya
Mzizima jijini Tanga kukusanywa kwa mwenyekiti wa kitongoji na kisha
kuuawa kwa kuchinjwa shingo na watu wasiojulikana.
Watu
hao ambao inadaiwa kuwa ni majambazi walivamia usiku wa kuamkia jana
kwa kuvunja milango ya nyumba tatu ambazo wakazi hao walikuwa wamelala
na kuwachinja kisha kuiba biskuti, mchele na sukari na kutokomea navyo
kusikojulikana.
Wauaji
hao inadaiwa wana uhusiano na wahalifu ambao wamekuwa wakijificha ndani
ya mapango ya Majimoto na kujihusisha na matukio kadhaa ya uvamizi ili
kupora vyakula na kusababisha mauaji ya wakazi wa Jiji la Tanga, ikiwamo
katika duka kuu la Central Bakery mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
Mmoja
wa shuhuda wa mauaji hayo, Kea Leonard (70) ambaye pia ni mkazi wa
Kibatini, katika mahojiano jana alisema wanaamini kwamba chanzo cha
mauaji ya wenzao ni kulipiza kisasi.
“Wiki
iliyopita majira ya saa tano asubuhi hapa tulikamata vijana saba kati
ya wanane wenye umri wa kama miaka 13 ambao walikuwa wakiranda randa
hapa kitongojini ili kutafuta namna ya kuvuka mto kwenda ng’ambo ya pili
na ndipo mmoja wao alipotutoroka,” alieleza Leonard na kuongeza:
“Watoto
hao tulipowaweka chini ya ulinzi na kuwahoji tukaanza kuwatilia shaka
hivyo mwenyekiti aliamua kuripoti Polisi na ndipo hao wakawachukua kwa
ajili ya mahojiano na hatukufuatilia tena kujua kwamba waliachiwa au la
kwa sababu hao watoto sio wenyeji wala wakazi wa eneo hili.”
Aliongeza
kwamba wakati wahalifu hao wanavamia nyumba ya mjumbe wa serikali ya
kitongoji kabla ya kumtoa nje walisikia mmoja wa watu hao akimhoji
kuhusu mahali walipopelekwa watoto saba.
Diwani
wa Kata ya Mzizima, Fredrick Charles alizungumza na waandishi wa habari
na kuthibitisha kwamba kati ya watu waliokufa mmoja ni Mjumbe wa
Serikali ya Mtaa wa Mleni uliopo kwenye kata hiyo.
“Hali
ya usalama hapa kwetu Mzizima si shwari kwa sababu wananchi wangu wa
Kibatini wamevamiwa na kuchinjwa usiku wa kuamkia jana majira ya saa
sita usiku,” alisema Chiluba.
Naye
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mleni kilichopo kitongoji hicho,
Shabani Amani alisema wamepatwa na hofu kubwa kuhusu matukio hayo.
“Tunadhani
kuna mapungufu katika suala la ulinzi hapa kwa sababu baada ya kutokea
matukio kadhaa eneo letu hasa baada ya kudaiwa kwamba mapango
waliyojificha wahalifu yako hapa jirani na kwetu kikosikazi cha
mchanganyiko wa askari polisi na wa JWTZ wanafanya doria kwa saa 24
lakini tunashangaa kwa nini matukio yanaendelea,” alisema Amani.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul alithibitisha mauaji hayo. “Mei 30, mwaka huu majambazi waliokuwa na visu na mapanga walivamia kaya tatu na kuua wananchi majira ya saa saba usiku,” alisema Kamanda Paul.
Aliwataja
waliouawa ni Issa Hussein (50) ambaye ni mmiliki wa kaya hiyo pamoja na
kuibwa biskuti, mchele na sukari katika duka dogo. Wa kaya nyingine ni
Mkola Hussein (40) na Hamis Issa (20), Hamis Issa (20) na aliyemtaja kwa
jina la Mikidadi (70).
Kamanda
aliwataja marehemu wengine ni Mahamud (35) ambaye ni mkwe wa Mikidadi,
Issa Ramadhani (25), Kadir (25) na Salum ambao ni wachunga ng’ombe
kijijini humo.
Hata
hivyo, mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mke wa marehemu Mkola aitwaye
Aisha Saidi, alisema walipofika nyumbani hapo waligonga mlango na kumtoa
nje Mkola na kuondoka naye.
“Nimeachwa
mjane na watoto sita... Baada ya hao watu kuingia walimkamata Mkola na
kumdai aeleze kwamba watoto wao saba wamepelekwa wapi na alipojibu sijui
wakamtoa nje na kumkusanya pamoja na wanakijiji hao wengine na
kuwachinja eti tu kwa sababu hawakutaja mahali walipopelekwa watoto,” alisema Aisha.
Katika
hatua nyingine, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)
imesikitishwa kupokea taarifa za vitendo vya mauaji ya kikatili
vinavyoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali nchini.
“Wimbi
hili la matukio ya vitendo vya mauaji na ukatili uliojitokeza kwa
kufuatana mwezi Mei 2016 yanavunja haki ya kuishi ambayo ndio msingi wa
haki zote za binadamu kwa ujumla wake.
"Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inalaani vikali mauaji haya yote na
matendo yote ya kikatili dhidi ya mwanadamu yanapotokea popote nchini,” ilieleza taarifa ya Mwenyekiti wa Tume, Bahame Nyanduga.
Tume
iliishauri serikali kupitia Jeshi la Polisi ichukue hatua mahsusi
kuhakikisha ulinzi wa wananchi dhidi ya mauaji na vitendo hivi, kwani
jukumu la kwanza la kuhakikisha usalama wa wananchi ni jukumu la
serikali.
Jeshi la Polisi lihakikishe watu wote waliohusika kutekeleza mauaji haya wanakamatwa ili sheria ichukue mkondo wake, ilieleza.
Shein: Hakuna Mtu Wala Nchi Yakuweza Kuniondoa Madarakani
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
RAIS
wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema hakuna nchi au jumuiya za
kimataifa zitakazomwondoa madarakani yeye kwa sababu amechaguliwa
kihalali na wananchi kwa kura nyingi kwa mujibu wa Katiba.
Dk
Shein alisema hayo wakati akizungumza na wanachama na wafuasi wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) katika matawi ya Wesha Tibirinzi, Pembeni Shengejuu
na Maziwa Ng’ombe, Micheweni katika ziara ya kuwafariji kutokana na
matukio ya hujuma zilizofanywa na wapinzani huko Pemba.
Aliwataka
wafuasi wa CCM na wanachama wake waliopo Pemba, wasibabaishwe na kauli
zinazotolewa na viongozi wa vyama vya siasa wanaopita na kudai kwamba
uchaguzi mwingine unakuja.
“Mimi
ndiye Rais halali wa Zanzibar nimechaguliwa katika uchaguzi ulioitishwa
na Tume ya Uchaguzi... wananchi msisikilize uvumi na kauli za wapinzani
zenye lengo la kuwababaisha na kuwayumbisha katika shughuli zenu za
maendeleo,” alieleza Dk Shein.
Dk Shein alisema amesikitishwa na kauli za uchochezi zinazotolewa na viongozi wa vyama vya siasa zenye malengo ya kuishawishi jamii kutengana na kugombana na kususiana hata katika shughuli za jamii ikiwemo misiba.
Alisema
kiongozi anayefanya vitendo vyenye lengo la kuwagawa wananchi kwa
malengo ya kisiasa huyo ameishiwa na hana nafasi katika jamii.
“Huyo kiongozi anayewashawishi wananchi kususia shughuli za jamii na maendeleo basi huyo ameishiwa kisiasa na hana nafasi katika jamii ya wananchi na ninyi mpuuzeni.Alikuwa na nafasi ya kushiriki katika uchaguzi lakini alisusa,” alieleza.
Alisema viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wameishiwa hoja kwa sasa na hawana la kufanya baada ya kugomea kushiriki katika uchaguzi halali wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu ambao umetoa nafasi kwa CCM kushinda katika uchaguzi wa kishindo.
“Huyo kiongozi anayewashawishi wananchi kususia shughuli za jamii na maendeleo basi huyo ameishiwa kisiasa na hana nafasi katika jamii ya wananchi na ninyi mpuuzeni.Alikuwa na nafasi ya kushiriki katika uchaguzi lakini alisusa,” alieleza.
Alisema viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wameishiwa hoja kwa sasa na hawana la kufanya baada ya kugomea kushiriki katika uchaguzi halali wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu ambao umetoa nafasi kwa CCM kushinda katika uchaguzi wa kishindo.
Mapema
Dk Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM aliwataka wanachama wa
chama hicho kutembea kifua mbele na kuachana na unyonge kwa sababu chama
chao ndiyo kilichoshika dola na kuunda serikali.
Akizungumzia yanayotokea Pemba, Dk Shein alisema, “Nimesikitishwa
na taarifa za matukio mbalimbali yanayofanyika huku Pemba ikiwemo watu
kususiwa maiti, kushushwa katika gari za abiria baada ya kuwa na itikadi
tofauti......haya matukio hayakubaliki na yanakwenda kinyume cha
maamrisho ya dini zote.”
Aliwataka
viongozi waliopewa majukumu kwa mujibu wa Katiba kufanya kazi zao na
kupambana na vitendo vya ubaguzi ikiwemo vya kuonewa kiholela wananchi.
Waziri Mkuu: Serikali Itahakikisha Inaendelea Kulinda Rasilimali Za Nchi Ikiwemo Urithi Wa Dunia
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
SERIKALI
ya awamu ya tano imesema kuwa itaendeleza jitihada za kutunza na
kulinda urithi wa dunia ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi
maeneo ya uhifadhi ili watanzania wote waweze kunufaikana rasilimali za
nchi .
Hayo
yalisemwa na waziri mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akifungua mkutano
wa kulinda urithi wa dunia wa Afrika kama nyenzo ya maendeleo endelevu
unaoendelea jijini Arusha
Majaliwa
alisema kuwa rasilimali zilizopo ni za watanzania na ili kuhakikisha
kuwa wananufaika nazo serikali itahakikisha inatunza na kulinda
uhifadhi ili yawe endelevu na kusaidia vizazi vijavyo.
Alisema
kuwa Tanzania ni moja ya nchi tajiri yenye urithi na hivyo ili
kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika haswa waishio maeneo ya uhifadhi
serikali itatoa elimu ya kutosha ili waepuke kuchangia uharibifu wa
mazingira unaotokea kwenye hifadhi za taifa .
“Rasilimali
hizi ni zetu na hivyo hata wanaoishi maeneo ya hifadhi watusaidie kwa
wale wanaoingilia na kuharibu kwani hata hizo mali asili zinatusaidia
sote na ndiyo sababu tumewekea mikakati ya kutunza maeneo hayo ili yawe
endelevu" alisema
Kwa upande wake mwenyekiti wa mkutano huo ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Mali asili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema
kuwa madhumuni ya mkutano huo ni kutambua changamoto na mambo ambayo
yanatishia na kuathiri uhifadhi bora wa maeneo ya urithi wa dunia
katika afrika .
Aidha
mkutano huo utapendekeza suluhisho kwa kupitia upya shughuli
zinazotekelezwa katika eneo la urithi wa dunia na kuangalia mchango wa
miradi ya jamii za kiafrika na kuandaa muelekeo wa miaka kumi ijayo.
Milanzi
alisema kuwa mkutano huo utapendekeza suluhisho kwa kushawishi wanawake
kuongeza ushiriki wao katika miradi inayoendana na uhifadhi wa urithi
na maendeleo endelevu pamoja kuchunguza jinsi mitafaruku inayotokea
kwenye maeneo ya urithi wa dunia kutokana na makundi ya kigaidi na
kutunza amani utamaduni na uridhi asilia.
Aliongeza
kuwa pia mkutano huo umejikita kwenye sera ya UNESCO ya mwaka 2015
inayohusu kujumuisha maendeleo endelevu kwenye mkataba wa uridhi wa
dunia.
“Mkutano
huo pamoja na matokeao tegemewa kisayansi, pia utakuwa na manufaa kwa
taifa na sio tu kuitangaza Tanzania kutalii na kisasa bali pia ni fursa
muhimu ya kiuchumi kutokana na idadi ya wageni watakao huthudhuria
mkutano huu pamoja na kuanzisha mitandao wa kitaaluma na kujenga mitaji
wa kijamii” alisema Malinzi
Aidha
pia mara baada ya mkutano huu na kupata muafaka wa yote kutakuwa na
tamko lililotokana na majadiliano yaliyokuwa yakifanyika siku zote za
mkutano na tamko hili linatarajiwa kutolewa katika hifadhi ya taifa ya
Ngorongoro
Wahadhiri UDOM Wataja Kiini cha Mgomo Kilichosababisha Wanafunzi 7802 Warudishwe Nyumbani
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
JUMUIYA
ya Wanataaluma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) imesema kilichotokea
si walimu kugoma kufundisha programu ya Stashahada Maalumu ya Elimu,
Sayansi, Hisabati na Tehama, bali tatizo ni kutoelewana na Menejimenti
ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo
chuoni hapo.
Aidha,
imelaani kitendo cha wanafunzi 7,802 wa Programu Maalumu ya Ualimu wa
Msingi na Sekondari, waliorudishwa nyumbani bila kupewa muda wa kutosha
kujiandaa kwa kuzingatia umri wao na mazingira waliyokuwa wanaishi, hali
inayofanya wazagae mitaani huku wakiwa hawana pa kwenda.
Hayo
yako kwenye tamko lililotolewa jana na Katibu wa jumuiya hiyo, Lameck
Thomas, ambalo lilieleza kuwa lawama zimekuwa zikitupwa kwa walimu
kutokana na taarifa hizo kutolewa na upande mmoja, ambao ni Menejimenti
ya chuo kwenda serikalini bila kuwepo na taarifa yoyote kutoka kwa
walimu kupitia jumuiya yao.
Thomas
alisema si kweli kama walimu waligoma kufundisha lakini tatizo kubwa ni
kutoelewana kati ya walimu na Menejimenti ya chuo kutokana na mazingira
mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo chuoni hapo.
"Hatuzungumzii
fedha zaidi tunazungumzia suala la kuboresha elimu ili taifa lipate
walimu wa baadaye katika kufundisha Sayansi, Hisabati na Tehama, vifaa
vya kufundishia navyo ni changamoto kubwa,” alisema.
Katibu
huyo alisema kama Jumuiya ya Wanataaluma wanapata hisia kwamba Wizara
ya Elimu, imeamua kwa makusudi kushirikiana na uongozi wa chuo kupotosha
uhalisia wa jambo hilo kwani hakuna hata wakati moja ambao wamefanya
mawasiliano na walimu wenyewe kupata ukweli kutoka upande wao.
“Alichosema
waziri bungeni juzi ni taarifa ya upande mmoja ambayo haitatupeleka
kwenye utatuzi wa kudumu wa suala hili kutokana na ukweli kwamba walimu
nao wana mengi ya kuzungumza,” alisema katibu huyo.
Alisema
serikali imejenga desturi ya kuonana na menejimenti za vyuo pindi
yanapotokea matatizo bila kupata taarifa kutoka vyanzo vingine hali
ambayo imekuwa inasababisha vyanzo sahihi vya matatizo kutojulikana kwa
uwazi.
Alisema
changamoto za ufundishaji kutokana na uhaba na walimu kulingana na
idadi ya wanafunzi waliopo. Akitoa mfano alisema kwa sasa Chuo cha
Sayansi Asilia na Hesabu, kina upungufu wa walimu 128 waliokuwa
wanahitajika kufundisha programu hiyo kwa ufanisi; na kwa muhula
uliopita walimu 72 tu ndio walibeba mzigo wa upungufu huo na muhula huu
hali ilikuwa inaelekea kuwa mbaya zaidi.
“Wingi
wa wanafunzi na uhaba huu wa walimu ulisababisha upangaji wa ratiba na
kufundisha kutokana na ukweli kwamba kozi ziligawanywa katika mikondo
mingi ambayo walimu walilazimishwa kuifundisha huku wakiwa na majukumu
ya kufundisha kozi za shahada na majukumu mengine,” alifafanua.
Alisema
chuo kimekuwa na desturi ya kupokea wanafunzi wengi bila kuzingatia
idadi ya walimu waliopo na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na
hiyo si mara ya kwanza kwa chuo kufanya hivyo, kwani mwaka 2008 walileta
wanafunzi wengi ambao matokeo yake walimu kufundisha masomo mengi
kuliko uwezo wao wa kazi.
Alisema
taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma
ilipotoshwa, kwani haijaeleza ukweli wa madai uliowasilishwa na chuo
husika.
Alisema
katika Chuo cha Sayansi Asilia na Hesabu taarifa inasema
yaliyowasilishwa ni madai ya Sh milioni 367.8 na kupungua mpaka Sh
milioni 90 wakati uhalisia ni kwamba madai hayo hata yangebanwa namna
gani yasingepungua mpaka chini ya Sh milioni 223.7.
Alisema
mfano mwingine ni Chuo cha Elimu Masafa na Sayansi za Kompyuta ambao
taarifa inasema waliwasilisha madai yanayozidi Sh milioni 100 wakati
taarifa ya chuo inasema ni madai ya Sh milioni 53.7 tu.
Mwenyekiti
wa jumuiya hiyo, Edson Baradyana alisikitishwa na yaliyotokea na
kuitaka serikali kufanya jitihada za makusudi ili kumaliza mgogoro huo
na hilo litawezekana kama walimu, wanafunzi na Menejimenti kukaa pamoja.
Baradyana
alisema wanafunzi hawakutendewa haki kwani ilitolewa notisi ya ghafla
ya kuondoka chuoni huku wengine wakiwa hawana nauli na hawakujua pa
kwenda hali inayofanya waendelee kuzurura mitaani.
Alisema
wanaamini kama Menejimenti ya chuo ingeonesha ushirikiano wa karibu kwa
walimu wanaofundisha programu hiyo na kushirikiana, hayo yasingetokea
au yasingekuwa makubwa kiasi hicho.
“Lazima
kuangaliwa na kutatuliwa kwa changamoto nyingine zilizoibuliwa na
wanataaluma na wanafunzi katika uendeshaji wa programu hiyo badala ya
kujikita kwenye suala la malipo tu, serikali iwe na utaratibu wa
kuwasiliana na walimu na wanafunzi mara kunapotokea matatizo vyuoni ili
kupata taarifa toshelezi kutoka pande zote,” alisema Mwenyekiti wa Udomasa.
Aidha,
wakati wa kurejeshwa nyumbani kwa wanafunzi hao wa Udom kukibebwa
kisiasa na vyama vya upinzani, taarifa ya serikali imeeleza kuwa
wahadhiri waliogoma, walitaka kulipwa posho ya zaidi ya Sh milioni 900.
Akitoa
taarifa ya pili bungeni juzi usiku, Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema
wanafunzi hao si sehemu ya kazi zilizoko katika mikataba ya ajira ya
wahadhiri hao, ila ni sehemu ya kazi ya ziada.
Kwa
kuwa kazi hiyo ni ya ziada, Profesa Ndalichako alisema walikubaliana
walipwe posho ya kazi ya nyongeza ambayo uongozi wa Chuo Kikuu cha
Dodoma ulikuwa tayari kutoa zaidi ya Sh milioni 200.
Kwa
mujibu wa Profesa Ndalichako, wahadhiri hao walisisitiza kuwa wanataka
posho hiyo iwe zaidi ya Sh milioni 900, jambo lililokataliwa na Mkaguzi
wa Ndani wa Mahesabu wa Udom aliyesema kuwa kiwango hicho ni kikubwa
kuliko uhalisia wa kazi yenyewe.
Kutokana
na kutokubaliana kati ya wahadhiri hao na uongozi wa Udom, wahadhiri
hao ndio wakaitisha mgomo wa kufundisha wanafunzi hao huku wakiendelea
na kazi za kufundisha walio katika programu za shahada ya kwanza na
kuendelea.
Profesa
Ndalichako alisema kwa uamuzi huo wa wahadhiri, serikali isingeweza
kuwachukulia hatua kwa kuwa wamegomea kazi ya ziada na si kazi
waliyoajiriwa na kuingia mkataba na chuo.
Kwa
hali hiyo, Profesa Ndalichako alisema serikali ililazimika kuingilia
kati ambapo Mei 10, mwaka huu Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia
na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alikwenda chuoni hapo kutafuta
suluhu.
Mbali
na Naibu Waziri, alisema hata makatibu wakuu wa wizara hiyo nao
walikwenda kuzungumza na wahadhiri hao bila mafanikio, huku wanafunzi
hao wakikaa chuoni bila kuingia darasani kwa wiki ya tatu.
Profesa
Ndalichako alisema mbali na madai ya wahadhiri hao, pia wakati wa
kutafuta suluhu ya jambo hilo, walitazama suala la tija kwa wanafunzi
hao wa diploma maalumu ambao ni zaidi ya 7,800 na pia kwa wanafunzi wa
shahada ya kwanza ambao pia wanapaswa kufundishwa na wahadhiri hao.
Kutokana
na kukosa masomo kwa wiki tatu mfululizo na kuwepo kwa uwezekano wa
kukosekana tija katika ufundishaji, Profesa Ndalichako alisema ndio
uamuzi wa kuwarudisha nyumbani wanafunzi hao ukafanyika ili serikali
iangalie upya utaratibu wenye tija zaidi wa kuwaendeleza wanafunzi hao.
Aidha,
Profesa Ndalichako alisema wakati wanafunzi hao wakitakiwa kurudi
nyumbani, walizingatia hali yao ya kipato, kwa kuwa tayari walikuwa
wameshapewa fedha za kujikimu za siku 60 tangu Aprili 21, mwaka huu.
Profesa
Ndalichako aliwataka wanafunzi hao kuvuta subira wakati serikali
inatafuta namna bora ya kuwapatia elimu hiyo kwa kuzingatia tija kwao.
Waziri Mkuu: Wataalamu Wa Malikale na uhifadhi wa urithi Kuweni Wabunifu
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wataalamu wa mambo ya malikale na
uhifadhi wa urithi asilia (natural heritage) watafute mbinu
zitakazoimarisha utunzaji wa rasilmali hizo bila kuathiri mifumo ya
uchumi ya nchi zinazoendelea.
Ametoa
wito huo jana (Jumanne, Mei 31, 2016), wakati akifungua Mkutano wa
Kimataifa wa siku nne unaojadili Uhifadhi wa Urithi wa Dunia wa Afrika
kama Nyenzo ya kuleta Maendeleo Endelevu ulioanza leo kwenye ukumbi wa
mikutano wa kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Waziri
Mkuu alisema kuna baadhi ya nchi ambazo ni maskini sana lakini
zimebarikiwa kuwa na rasilmali kama madini na gesi asilia lakini kwa
sababu rasilmali hizo ziko karibu sana na vivutio vya urithi asilia wa
dunia, watu wa nchi hizo wanazuiwa kuchuma rasilmali zao ili wasiharibu
vivutio hivyo.
“Tunatambua
umuhimu wa kutunza rasilmali na vivutio vya urithi asilia. Hivi ni kwa
nini zisitafutwe teknolojia zinazofaa ambazo zitaruhusu uvunaji wa gesi
asilia na madini bila kuathiri uhifadhi wa vivutio vya urithi asilia wa
dunia (world heritage sites)?”, alihoji Waziri Mkuu.
“Serikali
za nchi za Kiafrika zinahitaji suluhisho kama hili wakati zikiendelea
kutafuta njia sahihi za kuwianisha uhifadhi wa vivutio vya urithi wa
dunia na changamoto ya kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake,” amesema.
“Sisi
viongozi ambao wengi wetu ni wanasiasa, hatukatai ushauri wa wataalamu
lakini tunawasihi baadhi yenu ambao mnashiriki mkutano huu muhimu,
mtafute njia mbadala za kufumbua tatizo hili badala ya kuendelea
kutegemea njia za kizamani za kukabiliana na changamoto kama hizi ili
sote tuweze kunufaika na rasilmali zilizopo ikiwa ni pamoja na kutunza
vivutio vya urithi asilia wa dunia,” aliongeza.
Alisema
kama rasilmali hizo zitachambuliwa vizuri na kwa njia sahihi bila
kuathiri vivutio vya urithi wa dunia, ni dhahiri kuwa zitaingiza mapato
ambayo kiuchumi yatasaidia kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi ambao
pia watasaidia kwenye uhifadhi wa vivutio hivyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu
alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilmali nyingi zikiwemo za
ardhini (madini), misitu, wanyama na maeneo ya kihistoria na kusisitiza
kuwa Watanzania wana jukumu la kuzilinda ili zilete tija kwa wananchi
wote.
“Tukizitunza
rasilmali zetu zitasaidia kupata mapato kutokana na utalii Serikali
itapeleka sehemu ya mapato haya katika miradi mbalimbali na hivyo
kuchangia kwenye pato la Taifa,” amesema.
Kwa
upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe
amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na UNESCO hasa katika masuala
yanayohusu uhifadhi wa vivutio vya dunia kutokana na umuhimu wake kwenye
maendeleo endelevu.
Alisema
wizara yake imelenga kusimamia, kuendeleza na kuimarisha utunzaji wa
maliasili na uhifadhi wa vivutio asilia na vya kiutamaduni (natural and
cultural heritage) kwa kushirikiana na wadau wengine hapa nchini.
Naye
Mkurugenzi wa Uhifadhi Malikale wa UNESCO, Dk. Mechtild Rossler
aliwataka washiriki wa mkutano huo kutoka nchi mbalimbali duniani wawe
tayari kupitia upya shughuli zinazotekelezwa katika eneo la urithi wa
dunia na kuangalia wajibu wa nchi za Kiafrika katika kuandaa mwelekeo wa
miaka ijayo.
Alisema
katika miaka 40 ya utendaji wa UNESCO, idadi ya vivutio vya urithi wa
dunia imeongezeka na kufikia 89 ambapo kati ya hivyo viko baadhi
vinakavyobiliwa na changamoto ya kufutika kutokana na athari za kigaidi,
matukio ya kivita na kazi za kibinadamu.
“Vivutio
16 kati ya 48 viko katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la
Sahara na hivi vinakabiliwa na tishio la kupotea kutokana na vita,
harakati za kigaidi na shughuli za kiuchumi za kibinadamu zikiwemo
uchimbaji wa madini na gesi asilia,” alisema.
Aliwataka
washiriki wa mkutano huo wakumbuke kuwa vivutio vya urithi wa dunia ni
vielelezo vya jamii na pia huchangia uchumi kwa kutoa ajira kwenye jamii
husika.
Mkutano
huo unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 150 kutoka nchi mbalimbali
duniani, unajumuisha washiriki kutoka nchi 36 zikiwemo nchi 12 ambazo ni
za nje ya bara la Afrika.
Waziri Mkuu amerejea mjini Dodoma jana mchana kuendelea na vikao vya Bunge.
Serikali Yaitaka RITA Kutoa Elimu Kwa Wananchi Kuhusu Umuhimu Kuandika Wosia Wa Mirathi
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
SERIKALI imeitaka wakala wa usajili,Ufilisi na Udhamini, RITA, kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuelewa umuhimu wa kuandika wosia na mirathi ,ili kuondoa migogoro kwa familia wakati wa kugawa mirathi ya marehemu.
SERIKALI imeitaka wakala wa usajili,Ufilisi na Udhamini, RITA, kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuelewa umuhimu wa kuandika wosia na mirathi ,ili kuondoa migogoro kwa familia wakati wa kugawa mirathi ya marehemu.
Rai hiyo imetolewa jana na mkuu wa wilaya ya Arusha, Fadhili Nkurlu, alipokuwa akifungua kampeni ya siku nne
ya kisheria inayotolewa bure na RITA, kuhusu kuandika mirathi na wosia
na kuwaelekeza eneo salama la kuhifadhi wosia ukisha andikwa na
mhusika ili kuondoa migogoro mingi kwa familia pindi mhusika
anapofariki dunia.
Mkuu
huyo wa wilaya, alisema,wananchi wengi hawana elimu juu ya wosia na
mirathi hivyo RITA, ambayo ni wakala wa serikali ina jukumu kubwa la
kuhakikisha elimu inawafikia wengi na hivyo kuwezesha wajane na watoto
ambao ndio waathirika kupata mirathi .
Alisema
wosia unasaidia kutatua migogoro ambayo ingelijitokeza wakati wa kugawa
mirathi ya marehemu na mtu kuandika wosia sio uchuro bali ni kuweka
utaratibu wa mali za muhusika zitakavyogawiwa pindi akisha fariki dunia.
Aliikumbusha
jamii kuwa msimamizi wa mirathi sio mrithi wa mali ya marehemu bali
jukumuake ni kukusanya mali yote na madeni yote ya marehemu na kusimamia
ugawaji na ulipaji wake na kamwe msimamizi yeyote asijihusishe na
urithi .
Jamii
nyingi zimekuwa zikiingia kwenye migogoro ya kugawana mirathi kutokana
na kutokuwa na elimu ya kutosha ya kuandika wosia kabla ya kifo na
matokeo yake wanaoathirika ni wajane na watoto ambao hukosa haki yao .
Awali
mratibu wa kampeni hiyo,msajili na wosia kutoka makao makuu ya RITA,
Augostino Mbuya, alisema migogoro mingi imekuwa ikijitokeza kwenye
familia wakati wa kugawa mirathi kutokana na kutokuwepo kwa wosia ambao
ni mwongozo wa jinsi ya kuigawa mali ya marehemu kwa wahusika na matokeo
yake watoto na wajane hukosa haki yao ya kurithi.
Alisema
kutokana na hali hiyo RITA, ipo tayari kutoa elimu kwa umma kuhusu
huduma hiyo ya kuandika wosia kutokana na wananchi wengi kutokuwa na
elimu na kufahamu wapi watapata huduma hiyo ya kuandika wosia na ugawaji
wa mirathi za marehemu
Mbuya,alisema
mkakati uliopo ni kusogeza huduma ya kuandika wosia na mirathi ngazi za
mikoa na wilaya pamoja na kuhakikisha wanakuwepo wanasheria wa kutosha
lengo ni kuiwezesha jamii kuondokana na migogoro ambayo inaweza kuepukwa
wakati wa kugawa mali za marehemu.
Alisema
tangia kuanzishwa kwa huduma hiyo ya Rita, imeweza kusajili wosia zaidi
ya 300 na 30 kati yake zimeshachukuliwakwa utekelezaji .
Akisoma
taarifa ya kazi za Rita, msajili wa mirathi na wosia, kutoka makao
makuu ya Rita, Joseph Mwakatobe amesema mahakama kuu imeiteua RITA,
kusimamia utatuzi wa migogoro ya urithi na uandishi wa wosia lngo ni
kuondoa migogoro inayojitokeza pindi mtu anaofariki dunia.
Alisema
Rita, itaendesha kampeni hiyo ya kuhamasisha wananchi kuhusu kuandika
mirathi na wosia katika mkoa wote wa Arusha,ili kuwezesha wajane na
watoto wanapata haki yao ya kurithi mali za marehemu .
Aliongeza
kuwa kuandka wosia ni swala lahiari ya mtu,na Rita, imekuwa ikikumbana
na changamoto mbaimbali zkiwemo za kutokuwepo na wosia wakati wa mirathi
.
Aliongeza
kuwa mirathi inatolewa kulingana na sheria za dini ya kiislamu, mila na
sheria ya India ya mwaka 1865 ambayo inahusisha makundi yote ambayo
hayapo kwenye makundi ya kidini na mila.
Taarifa toka Ikulu kuhusu uteuzi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
TAARIFA KWA UMMA
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli,
amemteua Dkt. Alex L. Kyaruzi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Kufuatia
uteuzi huo, Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Profesa Sospeter M.
Muhongo (Mb.), amewateua wafuatao kuwa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa
TANESCO kuanzia tarehe 31/5/2016 hadi tarehe 30/5/2019;
1. Dkt. Samwel Nyantahe
2. Dkt. Lugano Wilson
3. Bw. David Elias Alal
4. Mhandisi Stephen Peter Mabada
5. Mhandisi Leonard R. Masanja
Aidha,
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Profesa Sospeter Muhongo (Mb)
amekamilisha uteuzi wa Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO), kuanzia tarehe 30/5/2016 hadi 29/5/2019 wajumbe hao ni :
Bw. Abdalah H. Musa
Dkt. Coretha Komba
Bw. Felix M. Maagi
Dkt. Lightness Mnzava
Bw. John B. Seka
Uzinduzi
wa Bodi hizo utafanyika Makao Makuu ya Mashiriki hayo Siku ya Alhamisi
tarehe 2 Juni, 2016, saa 4:00 asubuhi kwa Bodi ya STAMICO na saa 8:00
mchana kwa Bodi ya TANESCO.
Imetolewa na;
KATIBU MKUU
31 MEI, 2016
Rais Magufuli Awatangazia Vita Wafanyabiashara ‘Wajanja’
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Rais
John Magufuli amesema Serikali yake itaendelea kupambana na wanaoingiza
bidhaa zilizochini ya kiwango na wale wanaokwepa kodi.
Amesema kwa kufanya hivyo, wanachangia kuviua viwanda vya ndani ya nchi.
Rais
Magufuli ameyasema hayo jana kwenye hafla ya utaoji wa Tuzo ya Rais ya
wazalishaji bora wa viwandani kwa mwaka 2015 zilizofanyika jijini Dar es
Salaam.
Tuzo hizo zimeandaliwa na Shirika la Wenye Viwanda Nchini (CTI).
Rais
amesema pia hatawavumilia watendaji wote watakao wakwamisha
wafanyabiashara wenye nia ya kuanzisha viwanda nchini kwa sababu zisizo
za msingi na kuwaahidi kuwasaidia waweze kufanikisha ndoto zao.
Pia,
amesema ni vizuri wafanyabiashara wote nchini wakatumia fursa
zipatikanazo katika awamu hii ya uongozi wake, ili wasije kuzijutia
baadaye.
“Nasema kwa dhati kutoka moyoni, you have my support, mkishindwa katika kipindi cha awamu ya tano basi hamtaweza tena,” alisema.
Rais
Magufuli alisema nchi inapokuwa na viwanda vingi vitatoa ajira kwa
Watanzania, vitaongeza mapato kwa Serikali na kuingiza fedha za kigeni
kwa kuuza bidhaa nje ya nchi.
“Nina
dhamira ya dhati ndani ya moyo wangu kuwasaidia wenye nia ya kuanzisha
ya viwanda, siwachukii matajiri nawapenda matajiri,” alisema.
Rais Magufuli aliwapa moyo wafanyabiashara wenye viwanda kuanzisha vingine ili Serikali iweze kunufaika zaidi.
Alisema
Tanzania ina rasilimali nyingi kama maliasili na madini na
akawahakikishia wawekezaji kuwa lipo soko kubwa la bidhaa
watakazozitengeza lenye watu milioni 160 katika nchi za Afrika Mashariki
na Kati.
Magufuli
alisema sekta ya viwanda ni muhimili mkubwa wa uchumi katika nchi huku
akitolea mfano wa nchi za China, India, Korea Kusini, Malaysia, Thailand
na Vietnam ambazo zimekuwa kwa kasi kwa sababu ya uwepo wa viwanda.
Alisema
viwanda vinapoanzishwa nchini badala ya kuuza mali ghafi kwa bei ndogo
zitatengenezwa bidhaa ambazo zitauzwa nje ya nchi na kutoa ajira kwa
Watanzania.
“Badala ya kuuza ngozi tutengeneze viatu hapa hapa nchini au badala ya kuuza ng’ombe Comoro tumepeke nyama iliyosindikwa,” alisema.
Alisema nchi kama ya Sudan Kusini ina mahitaji makubwa ya unga wa mahindi.
“Lakini
wanaofaidika na soko hilo ni Wakenya ambao wanakuja nchini wananunua
mahindi, wanasaga na kuyapeleka huko,hivi wafanyabiashara tunashindwa
hata kuanzisha viwanda vya kusaga mahindi,” alisema
Alisema
Mkoa wa Arusha una ng’ombe wa maziwa lakini yananunuliwa na Wakenya
ambao wanayasindika kwenye viwanda vyao na kuja kuyauza hapa nchini.
Hata
hivyo, alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha benki ya
maendeleo ya viwanda kwa lengo la kutoa mikopo yenye masharti nafuu na
riba ndogo.
Kuhusu
kuondoa kwa changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo ya viwanda
nchini, Magufuli alisema Serikali imeshatenga Sh1trilioni katika mwaka
wa fedha ujao kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa ajili ya
kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Pia, Serikali imeunda kamati maalumu itakayoangalia mazingira ya ufanyaji biashara nchini ikiwamo kodi na tozo mbalimbali.
“Nchi yetu inakuwa na kodi za ajabu ajabu, mfano zao la kahawa kulikua na zaidi ya kodi 30. Haya ndiyo tunayoyaangalia,” alisema.
Kuhusu
upatikanaji wa mitaji na riba kubwa zinazotozwa na benki, alisema
katika kukabiliana na matatizo hayo Serikali inajiandaa kuanzisha benki
ya viwanda itakayowasaidia wenye wawekezaji.
Kwa
upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
alisema Serikali imejikita katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda vingi
zaidi nchini.
“Tumeandaa mkakati wa pamba hadi inakuwa nguo, alizeti hadi mafuta na tunaendelea kufufua viwanda vilivyokufa,” alisema.
Akizungumzia
changamoto zinazowakabiri wenye viwanda nchini, mwenyekiti wa
Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Samuel Nyantahe alisema uchakavu wa
miundombinu ya umeme na miundombinu ya barabara imekuwa ikiongeza
gharama za uzalishaji.
Pia,
alilalamikia uwapo wa utitiri wa kodi, mamlaka za usimamiaji biashara
na uwapo wa bidhaa bandia zinazotishia bidhaa za ndani.