Friday, 20 February 2026

PROGRAM JUMUISHI YA MALEZI,MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO YAENDELEA KUIMARIKA KISHAPU

Na Sumai Salum- Kishapu
Afisa Ustawi wa Jamii wilayani Kishapu mkoani Shinyanga  Mwajuma Abeid akizungumza wakati akifungua kikao cha utekelezaji wa PJT-MMMAM mwezi Oktoba-Disemba 2025, kwa niaba ya Mganga Mkuu wilayani humo chenye lengo la kupata uelewa wa kadi alama ya tathmini ya maendeleo ya awali ya Mtoto (ECD), Changamoto zilizotambuliwa na njia za kutatua changamoto hizo zinazoikabili programu hiyo Februari 19,2026

Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeendelea kutekeleza Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT–MMMAM) kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata malezi bora tangu wakiwa katika hatua za awali za maisha. 


Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa programu hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025 Mratibu wa PJT–MMMAM wilayani humo,Paul Lupolaso, kwenye kikoa chenye lengo la kupata uelewa wa kadi alama ya tathmini ya maendeleo ya awali ya Mtoto (ECD), Changamoto zilizotambuliwa na njia za kutatua changamoto hizo Februari 19,2026.


Katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo utoaji wa elimu ya afya na lishe kwa jamii, kampeni za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, jitihada za kukabiliana na udumavu, pamoja na utoaji wa elimu ya kuzuia ukatili dhidi ya watoto. 

"Katika kipindi hiki tumeweza kutoa vidonge vya madini chuma kwa wanawake wajawzito na kufikia 91%, elimu ya kinamama kujifungulia vituo vya afya 90%, Watoto kunyonya maziwa ya mama pekee wenye umri wa miezi 0 mpaka miezi 6 kwa 98%" ameongeza Lupolaso

Aidha,  ameongeza kuwa elimu ya usalama wa mtoto imeendelea kutolewa katika shule za msingi 128 zilizopo ndani ya Wilaya ya Kishapu. Hata hivyo, amebainisha kuwa utekelezaji wa programu hiyo umekumbana na changamoto kadhaa ikiwemo upungufu wa watumishi katika kitengo cha lishe, ushiriki mdogo wa wanaume katika masuala ya afya na lishe ya familia, pamoja na uhitaji wa kuimarisha usimamizi elekezi katika vituo vya kutolea huduma za afya. 

Kutokana na changamoto hizo, Halmashauri imeweka mikakati ya kuimarisha utekelezaji wake kwa kufanya kikao cha Kamati ya Lishe kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata, kuhimiza maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe (SaLiki), kufanya usimamizi elekezi katika vituo vya afya na zahanati, kuongeza uhamasishaji wa jamii kuhusu usafi wa mazingira na umuhimu wa kinamama kujifungulia katika vituo vya afya, pamoja na kutoa mafunzo kazini kwa watoa huduma kuhusu huduma za dharura kwa mama na mtoto. 

Baada ya uwasilishaji wa taarifa hiyo, wajumbe walitoa maoni mbalimbali ya kuboresha programu hiyo, wakisisitiza umuhimu wa kuongeza mikakati ya kuwahusisha wanaume katika kliniki za wajawazito na masuala ya lishe ili kuimarisha uwajibikaji wa familia, kuanzisha vikundi vya wazazi katika ngazi ya jamii vitakavyosaidia kutoa elimu ya malezi chanya, pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia katika upangaji na utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya mtoto. 

Sambamba na hayo, Halmashauri pia imeendelea kutoa shukrani kwa wadau wanaoiunga mkono katika utekelezaji wa programu hiyo wakiwemo World Vision, THPS, Marie Stopes, AMREF, Kivulini na REDESO kwa mchango wao katika kuboresha ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa Serikali ilizindua rasmi programu hiyo mwezi Desemba 2021 ikiwa na dhamira ya kuimarisha mfumo jumuishi wa malezi ya mtoto unaojikita katika maeneo ya afya bora, lishe, malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto.
Mratibu wa PJT–MMMAM wilayani humo,Paul Lupolaso akizungumza kwenye kikao cha utekelezaji wa PJT-MMMAM mwezi Oktoba-Disemba 2025, chenye lengo la kupata uelewa wa kadi alama ya tathmini ya maendeleo ya awali ya Mtoto (ECD), mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazoikabili programu hiyo na ku Februari 19,2026
















 
Share:

Thursday, 19 February 2026

SERIKALI YATOA FURSA KWA WASANII KAHAMA KUPITIA MIKOPO YA UTAMADUNI NA SANAA

 

Na Neema Nkumbi, Kahama

Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni tano kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kwa ajili ya kuwakopesha wasanii nchini, hatua inayolenga kuinua vipaji, kukuza sekta ya ubunifu na kuwawezesha vijana kiuchumi.

Akizungumza katika mafunzo ya uelimishaji kuhusu namna ya kupata mikopo hiyo yaliyofanyika leo februari 18, 2026 katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Afisa wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Jovita Godwin, amesema mfuko huo unatoa fursa kwa wasanii wa nyanja mbalimbali ikiwemo muziki, filamu, sanaa za maonyesho, fasihi na ufundi wa kazi za sanaa ili waweze kukuza kazi zao na kufikia malengo yao ya kisanaa na kibiashara.

Amesema serikali imekusudia kuona sekta ya sanaa inakuwa chanzo cha ajira na mapato kwa vijana wengi, hivyo amewahimiza wasanii wa Kahama kujitokeza kwa wingi na kuzingatia vigezo vilivyowekwa ili wanufaike na mikopo hiyo.

Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Kahama, Martha Kapela, amesema halmashauri imejipanga kuibua na kukuza vipaji kupitia matamasha, makongamano na ziara katika kata mbalimbali kwa lengo la kuwatambua wasanii na kuwaunganisha na fursa zinazotolewa na serikali.

Naye Meya wa Manispaa ya Kahama, Kaniki Mataluma, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kiuchumi kwa vijana, akiwataka wasanii kutumia mikopo hiyo kama chachu ya maendeleo yao binafsi na ya taifa.

Baadhi ya wasanii waliohudhuria mafunzo hayo wameishukuru serikali kwa kuanzisha mfuko huo wakisema utawasaidia kupanua shughuli zao za kisanaa, huku wakiiomba serikali kuendelea kuboresha masharti ya mikopo ili kuwafikia wasanii wengi zaidi.


Share:

SHUWASA YATWAA TUZO YA MDAU SHUPAVU KANDA YA ZIWA


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imeibuka mshindi wa Tuzo ya Mamlaka Bora inayosimamia upatikanaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika Tuzo za Wadau Shupavu Kanda ya Ziwa, zilizofanyika Jumatatu tarehe 16 Februari 2026.

Tuzo hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, katika hafla iliyofanyika Hoteli ya  Golden Crest, jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa utambulisho, Mhandisi Katopola alisema SHUWASA imetekeleza kwa vitendo jitihada za kumtua mwanamke ndoo kichwani kwa kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa majisafi kwa wastani wa saa 23 kila siku.

Aliongeza kuwa juhudi hizo, sambamba na usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira, zimeifanya Manispaa ya Shinyanga kuwa kinara wa usafi kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo.

SHUWASA inatoa huduma katika eneo lote la Manispaa ya Shinyanga pamoja na miji midogo ya Didia, Tinde na Iselamagazi, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. 

Mhandisi Katopola alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya Mamlaka na wadau wake, hususan wateja na wananchi, kwa kulipia ankara za maji kwa wakati na kutoa taarifa za uvujaji au uharibifu wa miundombinu.

Aidha Mhandisi Katopola alimshukuru Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Hamidu Aweso kwa maelekezo yake ya mara kwa mara katika kuhakikisha Mamlaka za Maji nchini zinatoa huduma bora za maji safi na usafi wa mazingira kwa wananchi katika maeneo yao ya huduma.

Tuzo hii ni chachu ya kuendelea kuboresha huduma na kudumisha viwango bora vya maji safi na usafi wa mazingira kwa maendeleo ya wananchi wa Tinde, Didia, Iselamagazi na Manispaa ya Shinyanga.  












Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger