Saturday, 6 November 2021

LORI LA MAFUTA LAUA WATU ZAIDI YA 80 SIERRA LEONE

...



Takriban watu 84 wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya mlipuko mkubwa kutokea katika mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown. Mlipuko huo ulitokea baada ya lori la mafuta lenye urefu wa futi 40 kugongana na gari jingine kwenye makutano yenye shughuli nyingi jijini humo.

Picha za video zilizorushwa na vyombo vya habari vya ndani zilionesha miili iliyoungua vibaya. Rais Julius Maada Bio alisema “amesikitishwa sana na moto huo mbaya na vifo vya kutisha vya watu”. Katika ukurasa wake wa twitter, alisema serikali yake itafanya “kila kitu kusaidia familia zilizoathirika”.

Meya wa Freetown Yvonne Aki-Sawyerr alieleza kuwa aliona picha “za kutisha” lakini akasema ukubwa wa athari za tukio hilo hazijafahamika


Katika chapisho lake wenye ukurasa wa Facebook alisema kulikuwa na “uvumi kwamba zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha”, ingawa bado hakuna idadi rasmi ya vifo. Chumba cha kuhifadhia maiti kinachosimamiwa na serikali kimepokea miili 91 hadi sasa, meneja wake ameliambia shirika la habari la Reuters.

Mlipuko huo unaaminika ulitokea kwenye makutano nje ya Duka Kuu la Choitram lililo na shughuli nyingi katika eneo la Wellington mjini siku ya Ijumaa. Ripoti moja ilisema basi lililojaa watu liliteketea kabisa, huku maduka ya karibu na maduka ya soko yalishika moto huo wakati mafuta yalipomwagika barabarani.



Brima Bureh Sesay, mkuu wa Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga la Sierre Leone, aliviambia vyombo vya habari kuwa tukio hilo lilikuwa “ajali mbaya”.


Mji huo wa bandari, ambao ni makazi ya watu zaidi ya milioni moja, umekabiliwa na majanga kadhaa makubwa katika miaka ya hivi karibuni.



Mwezi Machi, zaidi ya watu 80 walijeruhiwa baada ya moto mkubwa katika mojawapo ya vitongoji duni vya jiji hilo kuwaacha zaidi ya watu 5,000 kuyahama makazi yao.



Na mwaka 2017 zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha maporomoko ya matope yaliyokumba jiji hilo, na kuwaacha karibu watu 3,000 bila makazi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger