*Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na wataalam wa Sekta ya Mifugo wa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kikao cha wataalam wa Sekta ya Mifugo kilichofanyika kwenye ukumbi wa TVLA Jijini Dar es, (04/06/2021)*
*Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar Bi. Maryam Juma Saadalla akiongea wakati wa kufunga kikao cha ushirikiano cha wataalam wa Sekta ya Mifugo wa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kilichofanyika kwenye ukumbi wa TVLA Jijini Dar es Salaam. (04//06/2021)*
*Makatibu wakuu wa Sekta ya Mifugo (wa pili kutoka kushoto mbele ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel, wa tatu kutoka kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar Bi. Maryam Juma Saadalla wakiwa kwenye picha ya pamoja na wataalam wa Sekta hiyo mara baada ya kikao cha ushirikiano Kati ya Serikali hizo mbili kilichofanyika kwenye ukumbi wa TVLA Jijini Dar es Salaam (04/06/2021).*
Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar zimekubaliana kuendeleza ushirikiano na kutatua changamoto za kiutendaji katika ngazi za idara na taasisi zikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Zanzibar (ZALIRI).
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel alisema hayo wakati wa mapitio ya taarifa ya kikao cha wataalam wa sekta ya Mifugo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichofanyika Juni 04, 2021 Jijini Dar es salaam.
Alisema utaandaliwa mkakati wa pamoja wa mawasiliano katika sekta hizo za pande mbili ili wadau pia watambue ushirikiano huo ambao umelenga kukuza uzalishaji katika sekta ya Mifugo hapa nchini.
Alisema pamoja na mambo mengine wataangalia namna ya kuwepo kwa urahisi wa utekelezaji wa vibali vya mazao ya mifugo ili vibali ambavyo vimetolewa Zanzibar vitambulike bara na vilivyotolewa bara vitambulike Zanzibar.
"Utaandaliwa mkakati wa pamoja wa mawasiliano katika sekta hizi za pande mbili ili wadau pia watambue ushirikiano huo ambao umelenga kukuza uzalishaji katika sekta ya Mifugo nchini pamoja na kuwepo kwa urahisi wa utekelezaji wa vibali vya mazao ya mifugo" alisema Prof. Elisante
Aliongeza kuwa uamuzi huo umekusudia kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ili kuleta manufaa ya kiuchumi kwa muungano na kwamba utaratibu na kukuza ubora wa wataalam wa mifugo.
Kadhalika alibainisha suala la tozo ya maziwa yaliyokuwa yakitoka Zanzibar (maziwa ya unga) ambapo mnufaika wa nafuu ya tozo hiyo ni Azam kwa makubaliano ya kuhakikisha anawezesha wazalishaji wa maziwa Zanzibar kuendelea na waliazimia aendelee na tozo iliyoazimiwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Maryam Juma Sadalla alisema matayarisho ya sheria ya mifugo ni muhimu lifanyike kwa wakati kama walivyokubaliana ili kukuza sekta ya mifugo Nchini.
Alisema kukamilika kwa sheria hiyo kutasaidi kuwepo kwa udhibiti wa magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa yakisumbua mifugo hasa homa ya mafua ya ndege ambayo imekuwa changamoto kubwa kwa upande wa Zanzibar
“Nashukuru hatua iliyochukuliwa kuendeleza sekta yetu ya kilimo ambayo imeleta faraja kwa kutuongezea ajira kwa vijana ambao wamepata fursa ya kuzalisha vifaranga kupitia vibali maalum kwa sababu ya changamoto ya mafua ya ndege” alisema Bi. Maryam.
0 comments:
Post a Comment