Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi, SACP Mihayo Msikhela akionesha baadhi ya vielelezo vilivyokamatwa kwenye msako wa kuwatafuta watuhumiwa wa mauaji.
Na Damian Masyenene–Shinyanga Press Club Blog
Wiki chache baada ya tukio la mauaji ya watu wanne katika mgodi wa wachimbaji wadogo uliopo eneo la namba 4, Kijiji cha Wisolele Kata ya Segese Tarafa ya Msalala katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga kwenye Plant ya kuchenjua Dhahabu ya Dakires, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwanasa watuhumiwa 13 na vielelezo mbalimbali.
Tukio hilo la mauaji lilitokea Juni 30, 2020 saa 2:00 usiku, ambapo walinzi wawili wa kampuni ya Sekepa inayolinda Plant hiyo, Juma Jigwasanya na Lusajo Michael pamoja na Mwendesha Mtambo wa Plant, Raphael Kipenya na Msimamizi Mkuu wa plant hiyo,Daniel William waliuawa kwa kugongwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya kichwani na watu wasiojulikana.
Ambapo baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi nchini liliamua kufanya msako kuwasaka watuhumiwa wa uvamizi na mauaji hayo na operesheni hiyo ilikamilika jana Julai 9, 2020 Alfajiri.
Akitangaza matokeo ya msako huo wa siku 10 kwa waandishi wa habari leo Julai 10, 2020 katika kituo cha Polisi Bugarama halmashauri ya Msalala, Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi, SACP Mihayo Msikhela amesema kuwa baada ya taratibu za upelelezi kukamilika watapelekwa mahakamani haraka iwezekanavyo, huku Jeshi hilo likiendelea kuwatafuta baadhi ya watuhumiwa waliokimbia ili nao wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
“Baada ya tukio Jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi lilianza msako wa kuwatafuta wahalifu hao, tutaendelea kufanya operesheni na misako kwenye migodi yote ya uchimbaji madini ili kubaini mtandao wote wa watuhumiwa wanaojihusisha na matukio kama haya,” alisema.
Amesema katika tukio hilo mhanga mmoja, Exavery Mboya (21) ambaye alikuwa mwendesha mitambo kwenye plant hiyo alinusurika baada ya kujeruhiwa na kuwekwa pamoja na marehemu baada ya watuhumiwa kuamini kuwa ameuawa, ambapo majeruhi huyo amelazwa hospitali ya Mji Kahama na afya yake imezidi kuimarika.
SACP Msikhela alitaja vielelezo vilivyokamatwa katika opereseheni hiyo vikihusishwa na tukio hilo la mauaji, kuwa ni mchanga viroba saba visivyo na mnaso wa dhahabu (vimeshachenjuliwa) iliyoibiwa kwenye plant hiyo Kilo 464.76, viroba vinne vya Carbon vyenye dhahabu Kilo 385.34 vikiwa kwenye hatua ya kupelekwa kwenye kinu kwa ajili ya kuchenjuliwa, pikipiki tano zikiwemo nne zilizotumika mzigo na moja ambayo mmoja wa watuhumiwa alikimbia na kuitelekeza.
Vingine ni Bunduki aina ya Shotgun yenye serial namba9025817, namba ya usajili TZCAR103855 ambayo iliporwa kwa mlinzi mmojawapo aliyeuawa siku ya tukio ikiwa na risasi mbili baadae kutelekezwa umbali wa mita 400 kutoka kwenye eneo la tukio.
Kamanda Msikhela amesema pia wamekamata panga moja, ambapo msako huo ulianza Juni 30, mwaka huu na kumalizika juzi (Alhamisi) alfajiri ambao watuhumiwa hao ni wale waliosuka mpango, walioutekeleza, waliosafirisha mizigo na waliohifadhi mizigo.
Hata hivyo Kamanda Msikhela ametoa wito kwa mamlaka zinazoshughulikia utoaji wa nyaraka na vibali vya kusafirisha mchanga kwenda kuuchoma ili kupata dhahabu, ni vyema wakatoa vibali baada ya kujiridhisha uhalali wa mchanga huo hasa kwa kufika kwenye Plant, kubaini mmiliki halali au mchanga husika ili kuepuka kutoa vibali kwa wahalifu.
Viroba vya Carbon ya Dhahabu vilivyokamatwa kwenye operesheni hiyo.
Bunduki aina ya Shot Gun na Panga vilivyokamatwa vikihusishwa na tukio hilo la mauaji.
Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi, SACP Mihayo Msikhela (wa pili kutoka kushoto) akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha Polisi Bugarama halmashauri ya Msalala, kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba.
SACP Msikhela akionyesha baadhi ya vielelezo vinavyohusiana na tukio hilo.
Sehemu ya viroba vilivyonaswa vyenye Carbon ya kuchenjulia Dhahabu
SACP Mihayo Msikhela (kushoto) akionesha risasi mbili zilizokutwa kwenye bunduki aina ya Shot Gun iliyotumika kwenye tukio la mauaji.
SACP Msikhela akionesha sehemu ya vielelezo mbalimbali vilivyonaswa kwenye msako huo zikiwemo pikipiki tano zilizotumiwa na watuhumiwa kutekeleza mpango wao wa uvamizi mgodini.
SACP Msikhela akitoa maelezo mbalimbali kuhusu vielelezo vilivyonaswa kuhusiana na tukio hilo la mauaji.
Picha zote na Damian Masyenene
CHANZO - SHINYANGA PRESS CLUB CLOG
CHANZO - SHINYANGA PRESS CLUB CLOG
0 comments:
Post a Comment