Sakata la bati 1346 za msaada zilizotolewa katika maafa ya mvua ya barafu mwakata mwaka 2015 limezua mjadala baada ya fedha zaidi ya Tsh. milioni 12 zilizotokana na kuuzwa kwa bati hizo kukosa mwelekeo huku Diwani Mstaafu wa Kata ya Mwakata Ibrahim Six Masanja akihusishwa na ubadhilifu huo.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Julai ,9,2020 katika kijiji cha Mwakata halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga ,baadhi ya wananchi wa kijiji hicho akiwemo Mathias Mtonja ,Richard Maganga wamehoji kupatikana muafaka wa fedha hizo zilizotokana na kuuzwa kwa bati za msaada kwani kuna zaidi ya Milioni 12 hazijulikani zilipo huku akaunti ya kijiji cha Mwakata ikiwa na salio la Tsh.Laki moja tu hadi sasa.
Wakijibu hoja hizo za Wananchi ,Mwenyekiti mteule wa kijiji cha Mwakata Mseka Mathias amesema hajui matumizi ya fedha zilizotokana na kuuzwa kwa bati na kuahidi kulipeleka ngazi za juu huku mtendaji wa kijiji hicho Mfikwa Andrew pia naye akishindwa kujibu hoja hizo za bati.
Wananchi hawakuridhishwa na majibu ya afisa Mtendaji wa kijiji cha Mwakata Mfika Andrew kwani wamedai kuwa yeye alikuwa mjumbe wa ODC na atakuwa anajua fedha za bati zilikoenda ,hali iliyosababisha mvutano katika mkutano huo.
Akihitimisha mkutano huo Mwenyekiti wa kijiji cha Mwakata ,Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga Mseka Mathias amependekeza kuunda tume ya watu wawili na kuendelea ili kwenda kwa mkuu wa Wilaya ya Kahama Ana Mringi Masha kuomba kuitisha mkutano utakaohusisha Diwani Mstaafu Ibrahim Six Masanja pamoja na viongozi wengine wastaafu ili kuweza kujibu tuhuma hizo mbele ya Wananchi.
Hata hivyo Mtandao huu umezungumza na Diwani Mstaafu wa kata ya Mwakata Ibrahim Six Masanja ambapo amesema kuwa bati hizo ziliuzwa kwa kutangaziwa wananchi na waliandika barua Kwa Mkurugenzi mtendaji ili kupata idhini ya kuuza bati hizo.
0 comments:
Post a Comment