Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula ameipongeza Wizara ya ardhi kwa kuwezesha kwa kiasi kikubwa katika mchango wa Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kwani wizara hiyo imejitahidi sana katika kutenga maeneo ya viwanda ambavyo vimejengwa kwa kasi.
Mhe. Mabula amesema hayo wakati akitembelea banda la Wizara ya Ardhi kwenye Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya SABASABA na kufuraishwa na huduma zinazotolewa kwa wananchi ambapo yeye mwenyewe alipata fursa ya kugawa hati kwa wananchi waliojitokeza katika banda hilo.
Aidha Dkt Mabula ameipongeza Wizara ya ardhi kwa kutoa huduma mbalimbali kwa kushirikiana na idara zilizo chini ya Wizara hiyo kwani wamefanikiwa kutoa hati za kielektroniki kumi ambapo wananchi waliweza kulipia na kupata ndani ya siku moja katika maonesho hayo.
“Katika swala zima la upimaji na uandaaji miji Wizara inahakikisha inatenga maeneo ya viwanda kwani tumeziagiaza Halmashauri zote kuhakikisha zinapima maeneo ya viwanda ili kuwezesha wawekezaji kufanya shughuri zao za kuendeleza uchumi bila kuingiliana na wananchi “ Amesema Dkt. Mabula.
Dkt. Mabula pia ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kutoa huduma ya matibabu ya kuvunja mawe kwenye figo na mfumo wa haja ndogo kwa njia ya mawimbi (mshituko kwa kitaalam) bila kufanya upasuaji.
Amesema kuanzishwa kwa matibabu hayo ni mwendelezo wa kutekeleza juhudi za Serikali za kuboresha huduma bobezi za kibingwa nchini ili kuongeza wigo wa huduma ambazo hapo awali zilikuwa hazipatikani hapa nchini kutokana na kutokuwepo kwa wataalamu, vifaa tiba au vyote viwili.
Huduma hii inafanywa kwa kutumia mashine ambayo inatoa mawimbi sauti yanayosafiri kupitia ngozi hadi kwenye figo sehemu yenye jiwe au mawe. Mawimbi hayo hugeuka kuwa nishati yenye uwezo wa kuvunja mawe kuwa madogo mithili ya mchanga ambapo yakishasagwa yanatoka kwa njia ya haja ndogo ( mkojo).
Pia, amelipongeza Sirika la Viwanada Vidogovidogo (SIDO) pamoja na kuwataka wajasiriamali wadogowadogo wanashirikiana na SIDO kuhakikisha wanakuwa wabunifu Zaidi katika kutengeneza bidhaa zao ili ziendane na kasi ya uchumi wa kati kwani Wizara ya Ardhi imetenga maeneo ya kutosha kwa ajili yao.
Ameipongeza pia JWTZ kwa kuanzisha miradi mbalimbali inayowafanya kuwawezesha vijana wanaomaliza mafunzo kuliko kuwaacha waende mtaani hali inayowafanya vijana hao kushindwa kijiajili hivyo, kwa kuwawezesha huku katika uendelezaji miradi inayofanywa na JWTZ itawanufaisha vijana wengi.
0 comments:
Post a Comment