Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma, imewahoji wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaomaliza muda wao, Livingstone Lusinde (Mtera) na Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini) kwa tuhuma za kuhusika kugawa rushwa kwa wajumbe ili waweze kuungwa mkono kugombea tena ubunge.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sostenes Kibwengo, alithibitisha kushikiliwa na kuhojiwa wabunge hao wakihusishwa na tuhuma za rushwa kwa kushawishi wajumbe ili waweze kuwania tena ubunge katika majimbo yao.
Kibwengo alidai kuwa Julai 7, mwaka huu majira ya mchana, waliwakamata watu 20 ambao ni wanachama wa CCM wakiwa nyumbani kwa Lusinde eneo la Mvumi, Wilaya ya Chamwino.
Alidai uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba watu hao na wengine waliofanikiwa kutoroka walifika nyumbani kwa mbunge huyo kupatiwa fedha ili wamsaidie wakati wa vikao vya uchaguzi.
Kibwengo alithibitisha pia kushikiliwa na kuhojiwa kwa Serukamba kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wanachama wa CCM ili kushawishi mambo yanayohusina na uchaguzi.
Alisema Serukamba pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na pia ni mtia nia ya ubunge katika Jimbo la Kigoma Kaskazini.
0 comments:
Post a Comment