UONGOZI wa Manispaa ya Tabora umetakiwa kuhakikisha Wakandarasi wanaojenga majengo ya Hospitali ya Wilaya na yale ya Kituo cha Afya Tumbi wanakamilisha kwa ubora unatakiwa na ya muda waliopewa katika mkataba ili wananchi waweze kupata huduma kwa karibu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati wakati wa ziara yake katika Manispaa ya Tabora ya kukagua miradi ya maendeleo.
Alisema kiasi cha shilingi milioni 700 zilizotolewa na Serikali ni lazima zionekane katika miundo mbinu itakayojengwa na iwe msaada kwa wananchi kupata huduma bora kwa gharama nafuu.
Dkt. Sengati alisema hatasita kuwachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kutumia fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo wananchi wayonge kwa maslahi binafsi.
Aliwataka watendaji wanaopewa majukumu ya kusimamia miradi kuwa wazalendo na waaminifu ili siku moja nao wawe sehemu ya mafanikio hayo.
Naye Katibu wa Ujenzi wa Hospitali ya Manispaa ya Tabora Joseph Kashushula alisema Mwezi Mei mwaka huu walipokea shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa majengo matatu ambapo yote yameanza.
Alisema majengo hayo ni Jengo la Wagonjwa wa Nje(OPD), Maabara na kichoma taka na yote yanatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu kama ilivyo kwenye mkataba.
Kashushula alisema kiasi hicho ni sehemu ya fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambapo ndani ya mwaka wa fedha huu wanatarajia kupata kiasi cha shilingi bilioni 1 ili kukamilisha majengo ambayo yatakuwa yamebaki.
Kwa upande wa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Tumbi Charles Ngussa alisema walipokea kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo wa Nje (OPD) na vyoo.
Alisema hadi hivi sasa wameshatumia shilingi milioni 113.1 na zimebaki shilingi milioni 86.8.
Ngussa alisema kati ya fedha zilizotumika wameweza kununua vifaa vyote vinatakiwa ikiwemo bati na rangi.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora mara baada ya kuwasili ofisini kwake jana alianza kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa dhana ya hapa kazi.
mwisho
0 comments:
Post a Comment