Saturday, 11 July 2020

JPM KUJENGAvKIWANDA KIKUBWA CHA KUKU NA KLINIKI YA KISASA YA MIFUGO SINGIDA

...

Waziri wa Mifugo na Uvuvi (mwenye kofia nyeusi) Luhaga Mpina akishiriki katika zoezi la uchanjaji wa mifugo kitaifa pamoja na wataalam wa mifugo lililofanyika leo kwenye kijiji cha Kinyangiri wilayani Mkalama mkoani Singida ambapo Serikali imeahidi kuwezesha kujenga kiwanda kikubwa cha machinjio ya kisasa kitakacholisha Tanzania na nchi mbalimbali duniani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi (mwenye kofia nyeusi) Luhaga Mpina wa kwanza kulia akifuatiwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Injinia Jackson Masaka na Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida ndugu Beatus Choaji wakiwa kwenye sherehe za uzinduzi wa uchanjaji wa mifugo kitaifa pamoja na wataalam wa mifugo lililofanyika leo kwenye kijiji cha Kinyangiri wilayani Mkalama mkoani Singida.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi (mwenye kofia nyeusi) Luhaga akionyeshwa kifaa maalum cha kuchanjia mifugo wakati wa zoezi la uchanjaji wa mifugo kitaifa pamoja na wataalam wa mifugo lililofanyika leo kwenye kijiji cha Kinyangiri wilayani Mkalama mkoani Singida.


WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi (mwenye kofia nyeusi) Luhaga akihutubia umati wa wadau wa mifugo wakati wa zoezi la uchanjaji wa mifugo kitaifa pamoja na wataalam wa mifugo lililofanyika leo kwenye kijiji cha Kinyangiri wilayani Mkalama mkoani Singida.
Umati wa wadau wa mifugo wakati wa zoezi la uchanjaji wa mifugo kitaifa pamoja na wataalam wa mifugo lililofanyika leo kwenye kijiji cha Kinyangiri wilayani Mkalama mkoani Singida.


Na John Mapepele, Singida

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina amesema Serikali inakusudia kuwezesha kujenga kiwanda kikubwa cha kisasa cha kuchakata nyama ya kuku kwenye Mkoa wa Singida kitakacholisha Tanzania na nchi mbalimbali duniani ambacho kitakuwa kinafanya uzalishaji ifikapo Desemba mwaka huu ili kuinua hali za wafugaji wa kuku wa Singida na kuongeza pato la taifa.

Mbali na kiwanda hicho, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kujenga Kliniki bora ya kisasa ya mifugo kwenye Halmashauri ya Mkalama. 


Kliniki hiyo ni miongoni mwa Kliniki 30 ambazo zinazijengwa nchi nzima na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kwenye Halmashauri mbalimbali.

Waziri Mpina ameyasema haya kwenye hotuba yake ya uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo za Mifugo Kitaifa kwenye kijiji cha Kinyangiri katika Wilaya ya Makalama mkoani Singida ambayo imelenga kutokomeza magonjwa mbalimbali ya mifugo (hususan magonjwa 13 ya kipaombele) ambayo yamekuwa kikwazo katika uzalishaji na biashara ya mifugo ndani na nje ya Tanzania.

“Tumeona hapa uzalishaji mkubwa sana wa kuku Singida, sasa ninaagiza mambo makubwa mawili Bodi ya Nyama na Dawati la linaloshughulikia Sekta Binafsi katika Wizara yangu kuwezesha kujenga kiwanda cha kuchakata nyama ya kuku na tutakizindua kikiwa kinatoa huduma ifikapo Desemba mwaka huu"Alisema

"Lakini la pili ninamuagiza Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko na Dawati la Sekta Binafsi kuunda vikundi na kuwaletea vitotoleshi vya kisasa ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa kuku ili kuwezesha upatikanaji wa malighafi za kiwanda kwa uhakika” alisisitiza Waziri Mpina.

Mpina amesema magonjwa mengi ya mifugo ni yale ya kuambikiza hususani yanayotokea kwa mlipuko na kusabisha vifo na hasara kubwa kwa wafugaji na kufafanua kuwa hadi sasa tayari, Serikali imekiimarisha kiwanda cha chanjo cha Tanzania Vaccine Institute (TVI) na kinazalisha aina sita (6) ya chanjo za kipaumbele na kitaanza kuzalisha aina nyingine tatu kufikia mwezi Desemba, 2020.

Mbali na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanza kutengeneza chanjo sita Mpina amesema mapinduzi na mageuzi makubwa yamefanyika ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Mifugo inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na kwa mwananchi mmoja mmoja tofauti na awali ambapo sekta hiyo na wafugaji walidharaulika sana.

Ametaja baadhi ya mambo yaliyoboreshwa kwenye eneo la chanjo hapa nchini kuwa ni pamoja na Wizara yake kupitisha Mpango wa Ununuzi wa Chanjo za Mifugo kwa Pamoja (Vaccine Bulk Procurement Plan);

Serikali kutangaza Bei Elekezi ya chanjo aina 13 za magonjwa ya kipaumbele ambapo chanjo zimepungua bei kwa zaidi ya asilimia 60;

Amebainisha kuwa, Katika mwaka 2019/2020, Serikali katika kiwanda cha TVI imezalisha jumla ya dozi 53,851,850 za chanjo za magonjwa ya mlipuko na yanayovuka mipaka na chanjo hizi zote zimechanja mifugo.

Pia, Wizara imevutia wawekezaji na kiwanda kikubwa cha Hester Biosciences Africa Limited kinajengwa na kitakapokamilika kitakuwa kinazalisha aina 37 ya chanjo za wanyama.

Ameongeza kuwa katika mwaka 2019/2020, utoaji wa chanjo umeimarika ambapo Halmashauri 103 kati ya 185 sawa na asilimia 56 zimeshiriki kikamilifu katika kutoa chanjo kwa mifugo

Aidha Mpina amesema kutokana na mikakati ya Wizara yake ya kudhibiti utoroshaji wa mifugo kutoka nchni kwenda nchi za nje na udhibiti wa uingizaji holela wa bidhaa za mifugo nchini kupitia “Operesheni Nzagamba” Serikali ya awamu wa Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliweza kukusanya zaidi ya bilioni 50 kwa mwaka ukilinganisha na Shilingi bilioni 9.5 zilizokuwa zikikusanywa katika kipindi cha nyuma kwa mwaka.

Akitoa maelekezo kwa wataalam Waziri Mpina amewataka wataalmu wote wa mifugo ngazi ya Wizara, Mikoa, Wilaya na Kata kuhakikisha uchanjaji wa mifugo unatekelezwa kikamilifu kulingana na kalenda ya chanjo kwa kuwa ni suala la kisheria ambapo amemtaka Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo (DVS) kuhakikisha unasimamia jukumu hili na yeye kupatiwa ripoti ya chanjo hizo kila mwezi.

Pia amewataka Wataalamu wote wa mifugo kuhakikisha wanatoa elimu ya chanjo kwa wafugaji ili watambue umuhimu na faida za kuchanja mifugo yao na kwamba, Serikali imeshaandaa mazingira wezeshi ya upatikanaji wa chanjo kila mahali na kwa bei elekezi.

Amesema kulingana na Kalenda ya chanjo kitaifa, mwezi Juni mpaka Augosti, 2020 ni msimu wa chanjo za Homa ya Mapafu ya Ng'ombe, Homa ya Mapafu ya Mbuzi, Sotoka ya Mbuzi na Kondoo, Ugonjwa wa kutupa mimba na Ugonjwa wa Miguu na Midomo.

Hivyo, ametoa wito kwa madaktari wa mifugo wote nchini kuhakikisha kwamba chanjo hizi zinatolewa kikamilifu.

Aidha ameziagiza Halmashauri zote ambazo hazitowi huduma ya chanjo kwa mifugo yao kufanya hivyo mara moja kuanzia mwezi huu wa Julai, 2020.


Ripoti ya idadi ya mifugo na aina ya chanjo inayotolewa iwe inaletwa kwa Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo (DVS) kila wiki.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger