Thursday, 16 July 2020

DR HUSSEIN MWINYI APOKELEWA KWA KISHINDO ZANZIBAR

...

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Mwinyi, jana alipata mapokezi ya kishindo kutoka kwa wanachama wa chama hicho, alipowasili Zanzibar.


Mgombea huyo ambaye aliteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa CCM jijini Dodoma Ijumaa kisha kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho Jumamosi, aliwasili Zanzibar akitokea jijini Dodoma, vilikofanyika vikao vya CCM.

Dk. Mwinyi alipokelewa na umati uliojitokeza kumpokea katika Uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume hadi ofisi kuu za CCM Kisiwandui.

Mapokezi hayo yalisababisha baadhi ya huduma za kijamii kusimama kwa takribani saa tatu kupisha ujio wa mgombea huyo, huku rangi za kijani na njano zikiwa zimetanda katika maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar.

Mapokezi hayo yalipambwa na burudani mbalimbali za ngoma za asili, taarabu na wasanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, akiwamo msanii Ali Kiba alietumbuiza.

Dk. Mwinyi aliwasili uwanja wa ndege majira ya saa 5:30 asubuhi ambapo alitembea kwa gari la wazi na kuwasili Kisiwandui saa 7:00 mchana.

Baada ya kufika ofisi kuu za CCM alizuru kaburi la Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume na kupata tambiko kutoka kwa wazee wa CCM.

Akimtambulisha mgombea huyo kwa wanachama wa CCM, Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema Dk. Mwinyi ni mzaliwa wa Zanzibar na wale wanaosema kuwa sio kwao Zanzibar waache kasumba hizo.

Aliwataka baadhi ya wananchi na wanasiasa kuacha kufanya siasa za ‘kufilisika’ kwa kumchafua mgombea wa urais wa Zanzibar kwa kumhusisha na mambo ambayo hayamhusu.

Alieleza kuwa Mwinyi ana sifa zote za kuwa Rais wa Zanzibar pia ni mtu mtiifu, mwadilifu mwenye hekima na busara.

Kwa upande wake, Dk. Mwinyi aliahidi kuendeleza na kuimarisha umoja wa kitaifa wa Wazanzibari wote na kuyalinda Mapinduzi na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger