Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi jana amewasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2020/2021.
Wizara hiyo imeliomba Bunge liiidhinishie jumla ya Shilingi bilioni mia moja tisini na tisa, milioni mia saba hamsini, laki sita themanini na nne elfu (199,750,684,000) zikiwa ni fedha kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na bajeti ya miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha makadirio hayo, Mhe. Prof. Kabudi alielezea mafaniko ambayo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeyapata katika kipindi hiki cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano 2015-2020.
==>>Mafanikio hayo ni:
* Ufunguzi wa Balozi mpya nane katika nchi za Qatar; Uturuki; Sudan; Cuba; Israel; Algeria; Jamhuri ya Korea; na Namibia;
* Kuifanya lugha ya Kiswahili kutumika katika Jumuiya ya Kimataifa na nchi mbalimbali;
* Kufanikisha kufanyika kwa viwango vya juu Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Dar es Salaam mwezi Agosti 2019;
*Kuhamasisha watalii kuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii;
*Kufanikisha uenyekiti wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo mwezi Machi 2016 nchi yetu iliteuliwa kwa mara ya pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo;
*Kuratibu Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic (Africa - Nordic Foreign Ministers’ Meeting) uliofanyika kwa mafanikio makubwa mwezi Novemba 2019 jijini Dar es Salaam;
*Kufanikisha ujumuishwaji wa miradi ya Tanzania katika miradi ya kipaumbele ya miundombinu iliyoidhinishwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
*Kutekeleza Itifaki ya Umoja wa Forodha na Itifaki ya Soko la Pamoja za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
*Kuratibu upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato jijini Dodoma na upatikanaji wa mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 180 kutoka Benki hiyo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya pete katika jiji la Dodoma na
* Kushawishi nchi marafiki kutufutia madeni, kuyapunguza au kuweka masharti nafuu ya kuyalipa.
0 comments:
Post a Comment