Wednesday, 6 May 2020

Serikali Yaendelea Kushughulikia Changamoto Zinazojitokeza Mipakani

...
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema changamoto zinazojitokeza katika mipaka mbalimbali ya Tanzania wakati wa usafirishaji wa bidhaa hususan katika kipindi hiki cha janga la COVID-19 zinaendelea kutatuliwa kwa majadiliano.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert Ibuge ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania Nchini Zambia Mhe. Benson Keith Chali ili kuangalia namna ya kutatua changamoto mbalimbali za usafirishaji wa bidhaa hususani zile zinazotoka katika bandari ya Dar es Salaam kuelekea katika nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC.

Ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha janga la COVID – 19 unaosababishwa na virusi vya Corona changamoto mbalimbali zimejitokeza katika utoaji wa huduma za usafirishaji wa huduma na bidhaa mbalimbali na hivyo serikali inafanya jitihada za majadiliano na baadhi ya nchi katika mipaka ili kutatua changamoto zinazojitkeza na kuwezesha huduma ya usafirishaji kuendelea bila ya vikwazo.

Nae Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Mhe. Chali amemuahidi Balozi Kanali Ibuge kuwa Serikali ya Zambia imeshaanza kuzifanyia kazi changamoto zinazojitokeza. "Suala hili limeshaanza kufanyiwa kazi na kila kitu kitakuwa sawa hivi karibuni," amesema Balozi, Chali. 

Katika tukio jingine Balozi Kanali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi ambapo katika mazungumzo hayo wameongelea zaidi namna ya kushirikiana na kuwezesha kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa wawekezaji wadogo na wakati wa Tanzania na kuwa na ubia na wawekezaji wakubwa hususani katika kipindi hiki cha COVID – 19 na baada ya COVID – 19 ili kuunusuru uchumi wa Taifa kuanguka.

"Tumekubaliana kuongea ushirikiano katika sekta za afya, maji, maendeleo na uwekezaji …….kwa hili tunawashukuru sana UNDP kwa kazi wanayoifanya lakini pia hata katika ushirikiano wa kisera tumekuwa tukishirikiana nao jambo ambalo linazidi kuimarisha uhusiano wetu hasa katika wakati huu wa COVID - 19 kwani jambo hili linasaidia kunusuru uchumi wa taifa kuanguka," amesema Balozi, Kanali Ibuge.

Katika hatua nyingine, Balozi Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Balozi wa Uingereza nchini Bi. Sarah Cooke pamoja na Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania Bw. Zlatan Milišić ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano hususani katika kipindi hiki cha janga la COVID – 19.

Tarehe 6 Aprili, 2020 ulifanyika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulijadili janga la COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona. Mkutano huo ulihusisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha,Viwanda,Biashara, Utalii, Mambo ya Ndani na Uchukuzi, kutoka nchi 16 wanachama wa SADC. 

Katika mkutano huo, Baraza la Mawaziri lilitoa mwongozo kuhusu Usafirishaji wa Bidhaa Muhimu na Huduma katika Nchi za SADC katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona. Mwongozo huu unatumika katika kipindi hiki unalenga kupunguza safari zisizo za lazima na kuwezesa usafirishaji wa bidhaa muhimu wakati huu wa janga la COVID - 19.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger