Friday, 8 May 2020

Marekani Yaondoa Mifumo Yake Ya Makombora Saud Arabia

...
Marekani imeanza kuondoa katika ardhi ya Saudi Arabia mifumo yake ya makombora ya Patriot na zana zingine za kijeshi, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza uungaji mkono wake wa kijeshi kwa utawala huo wa kifalme.

Katika ripoti ya jana Alhamisi, jarida la The Wall Street Journal lilinukuu maafisa wa serikali ya Washington ambao hawakutaka kutaja majina yao waliosema kuwa, mifumo minne ya makombora ya ardhini hadi angani ya Patriot, zana nyinginezo za kijeshi pamoja na maafisa wa kijeshi wa Marekani wataondolewa kutoka kwenye vituo vya mafuta vya Saudia.

Kadhalika maafisa hao wamesema Marekani inatazamiwa kupunguza vikosi vyake vya baharini katika Ghuba ya Uajemi karibuni hivi, na kwamba tayari ndege mbili za kivita za US zimeshaondolewa katika eneo hili.

Zana hizo za kijeshi za Marekani zilipelekwa Saudia mwezi Septemba mwaka jana, baada ya kujiri wimbi la mashambulizi ya makombora dhidi ya vituo vya mafuta vya Riyadh pamoja na hofu ya kuibuka vita iliyokuwepo kati ya Marekani na Iran

Mapema mwezi uliopita wa Aprili, Rais Donald Trump alitishia kwamba, Washington itasitisha uungaji mkono wake wa kijeshi kwa Saudia, iwapo utawala huo wa kifalme hautasitisha mvutano baina yake na Russia juu ya bei ya mafuta.

Trump alitoa vitisho hivyo katika mazungumzo ya simu na Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, ambapo alisema kuwa Marekani haitakuwa na budi ila kuanza kuondoa vikosi vyake Saudia iwapo utawala wa Riyadh hautapunguza kiwango cha mafuta unachozalisha.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger