Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga imeanza kusikiliza maombi ya dhamana dhidi ya Kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleiman Masoud Nchambi (CCM) mara baada ya Mahakama ya wilaya ya Shinyanga mahali kesi ilipo kutokuwa na uwezo wa kutoa dhamana kesi za uhujumu uchumi.
Maombi hayo yameanza kusikilizwa leo Jumatano Mei 13,2020 kwa Njia ya Mfumo wa Mtandao katika mahakama hiyo chini ya Jaji Phocus Mkeha, ambapo Wakili wa Mbunge huyo Frank Mwalongo amewasilisha Hati ya Maombi ya kupewa dhamana kwa mteja wake katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga baada ya Mahakama ya wilaya kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za Uhujumu Uchumi na kutoa dhamana.
Baada ya Jaji huyo kusikiliza maombi hayo kwa upande wa Wakili wa mtuhumiwa Frank Mwalongo, pamoja na Mkuu wa Mashitaka wa Serikali Magreth Ndaweka, ambaye alikuwa akipinga Mbunge huyo asipewe dhamana kwa sababu akitoka ataharibu upelelezi, alisema maamuzi ya utoaji wa dhamana hiyo atatoa Mei 15 mwaka huu.
Mei 11 mwaka huu Mahakama ya wilaya ya Shinyanga, ilishindwa kutoa dhamana ya Mbunge huyo, kwa maelezo kuwa haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi wala utoaji wa dhamana kwa makosa yasiyozidi Shilingi Milioni 10, ambapo hati ya mashitaka ya Mbunge huyo haijataja thamani na kuambiwa waombe dhamana kwenye mahakama kuu.
Mbunge huyo kwa mara ya kwanza alipandishwa kizimbani Mei 8 mwaka huu katika mahakama ya wilaya ya Shinyanga na kusomewa mashitaka 12 ya Uhujumu Uchumi kwa kumiliki silaha na risasi kinyume cha Sheria, na kufunguliwa kesi namba 10 ya mwaka 2020.
Mbunge huyo na mke wake Aisha Khalfan Soud wapo katika gereza la Mhumbu wakisubiri hatma ya dhamana.
0 comments:
Post a Comment