Monday, 6 April 2020

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Yakabidhiwa Magari 12 Kwa Ajili ya Maandalizi Ya Uchaguzi

...
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amekabidhi magari 12 kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo ni sehemu ya magari 20 yalionunuliwa na tume ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi magari hayo, Aprili 4,2020 Mhagama amesema Serikali itahakikisha kwamba NEC inawezeshwa kufanya kazi zake kwa mujibu wa Katiba na Sheria ili iweze kuendesha uchaguzi ulio huru na wa haki.

“Kwetu sisi kama Serikali wajibu wetu wa kwanza ni kuhakikisha kwamba Tume haikwami katika kutekeleza majukumu yake, hata fedha zinazohitajika katika shughuli zote za uchaguzi zinatengwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali,” amesema Mhagama.

Mhagama ameipongeza NEC kwa weledi katika utendaji kazi na kusema kwamba msingi wa uhuru wa Tume uliowekwa na Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 utaendelea kuheshimiwa na Serikali.

“Nchi kama Malawi na nchi nyingine zinakuja kujifunza kwenye Tume hii, nakupongeza sana Mwenyekiti (wa Tume) na wafanyakazi wote. Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ametamka kwamba mwaka huu tuna uchaguzi na ametamka kwamba uchaguzi huo lazima uwe huru na haki. Magari haya 12 mmepata, mtapata magari mengine nane (8) na sio magari tu bali vifaa vyote vya uchaguzi vimeshafikia hatua nzuri ya manunuzi, fedha zimeshatengwa,” amesema Mhagama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa (NEC) Jaji Semistocles Kaijage ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa Tume ili iweze kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba na Kisheria.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger