Na Stella Theopist, DAR ES SALAAM
YANGA SC imefuta uteja uliodumu kwa miaka minne mbele ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC baada ya ushindi wa 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Shujaa wa Yanga SC ni leo kiungo mshambuliaji Mghana, Bernard Morrison aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 44 kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 25.
Morrison, mchezaji wa zamani wa Heart of Lions, Ashanti Gold za kwao Ghana, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Delhi Dynamos FC ya India na Orlando Pirates ya Afrika Kusini alifunga bao hilo baada ya yeye mwenyewe kuchezewa rafu na kungo Jonas Gerlad Mkude.
Na Yanga walipata bao hilo baada ya beki tegemeo wa kati wa Simba SC, Erasto Edward Nyoni kuumia na kushindwa na kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Kennedy Juma Wilson dakika ya 23 tu.
Pamoja na Yanga kumaliza dakika 45 za kwanza ikiwa inaongoza, lakini ni Simba SC waliotawala zaidi mchezo huo na kutengeneza nafasi nzuri zaidi za kufunga, wakashindwa kuzitumia.
Na sifa zimuendee mlinda mlango, Metacha Boniphace Mnata aliyeokoa michomo mingi ya hatari, ingawa na walinzi wake wanastahili sifa kwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu.
Kipindi cha pili Simba SC waliingia kwa kasi zaidi na kuendelea kusukuma mashambulizi langoni mwa Yanga, lakini kikwazo kikawa kile kile – kupoteza nafasi ama kwa wapinzani kuokoa, au kupiga nje.
Mfungaji wa bao la Yanga, Morrison naye akashindwa kuendelea na mchezo baada ya takriban saa moja, kufuatia kuumia pia na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Sibomana.
Kwa sehemu kubwa ya kipindi cha pili, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji Luc Eymael anayesadiwa na mzawa, Charles Boniface Mkwasa ilicheza kwa kijihami na kushambulia kwa kushitukiza.
Dakika ya 70, kocha wa Simba SC, Mbelgiji pia Sven Ludwig Vandenbroeck anayesaidiwa na mzawa pia, Suleiman Matola alimpumzisha mshambuliaji wake wake wa kimataifa wa Rwanda, Medde Kagere na kumuingiza kiungo Hassan Dilunga.
Bado haikuizuia Simba kuendelea kushambulia lango la Yanga, lakini pamoja na umakini wa wapinzani wao – bahati pia ililalia upande wa Jangwani leo.
Mchezo wa leo umehudhuriwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad na Wenyekiti wa klabu zote, Dk. Mshindo Msolla wa Yanga na Mohamed ‘Mo’ Dewji wa Simba.
Yanga inafikisha pointi 50 baada ya ushindi wa leo katika mchezo wa 25 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya tatu, sasa ikizidiwa pointi moja Azam FC inayoshika nafasi ya pili ingawa mecheza mechi mbili zaidi.
Mabingwa watetezi, Simba SC wanaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa mbali, wakiwa na pointi 68 baada ya kucheza mechi 27.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohammed, Lamine Moro, Said Juma ‘Makapu’, Feisal Salum/Kelvin Yondan dk90+4, Papy Tshishimbi, Haruna Niyonzima, Bernard Morrison/Patrick Sibomana dk56, Ditram Nchimbi na Balama Mapinduzi/Deus Kaseke dk86.
Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni/Kennedy Wilson dk23, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone, Clatous Chama, Meddie Kagere/Hassan Dilunga dk70, John Bocco na Francis Kahata/Deo Kanda dk62.
Chanzo - Binzubeiry
0 comments:
Post a Comment