Tuesday, 10 March 2020

Waziri Mkuu Majaliwa Kufungua Mkutano wa Mawaziri SADC kwa Njia ya Video

...
Na Erick Msuya- MAELEZO.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kufungua kikao cha Baraza la Mawaziri wa Nchi wanachama wa jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wanaoshughulikia Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha Uchumi pamoja na viwanda na Biashara Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Machi kwa njia ya Video kufuatia tishio la virusi vya Corona. 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Kanali Wilbert Ibuge katika kituo cha mikutano Mwalimu Nyerere (JNICC) baada ya kutoa taarifa fupi ya kikao cha dharura cha Mawaziri wa SADC sekta ya Afya kilichojadili hali halisi ya Ugonjwa wa Corona  (CODIV- 19)  katika Nchi za SADC. 

Amesema Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na kuendeshwa kwa  njia ya mfumo wa  Video (Video Conference) kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Corona (CODIV-19) ulioikumba nchi ya Afrika ya Kusini ambayo pia ni Nchi mwananchama wa Jumuiya ya SADC. 

“Kufatia Ushauri uliotolewa katika maazimio ya kikao cha Mawaziri wa  Afya wa SADC, kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC sasa hivi kitafanyika kwa njia ya video  tofauti na ilivyozoeleka, hivyo kila Nchi mwanachama wa SADC atakuwa nchini kwake huku tukijadili kwa njia ya video” alisema Balozi Ibuge. 

Kwa upande wake  Naibu Katibu Mtendaji wa Maswala ya Ushirikiano wa Kikanda (SADC) Thembinkosi Mhlongo amesema kuna haja ya Nchi wanachama wa SADC kutumia hati ya kusafiria (Pasport) inayoweza kukumruhusu kila Mwanachama kusafiri na kufanya Shughuli za maendelo katika umoja wa SADC bila bugudha. 

“Umoja wa Mataifa na jumuiya nyingine mengine wana Hati zao za kusafiria, na sisi tunahaja ya kuwa na hati zetu za kusafiria tukiwa kama SADC, katika jumuiya yetu kuna watu watafanyakazi kwa muingiliano wa kikanda hivyo ni muhimu kutumia hati moja” Alisema Mhlongo. 

Miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni mazingira wezeshi ya maendeleo ya viwanda, masuala ya fedha na Michango ya Jumuiya, hati za kusafiria za SADC, na uanzishwaji wa shirika la utalii kwa nchi za kusini mwa Afrika.
Mwisho.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger