Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka waratibu na wadau wa Programu wa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba “Greenhouse” ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wakandarasi ambao walijenga vitalu nyumba kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa mafunzo hayo ili yawe na ubora zaidi.
Waziri Mhagama ameyasema hayo jana Machi 11, 2020 wakati wa kikao kilichowakutanisha Waratibu hao pamoja vijana kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha mafunzo ya Kilimo hicho kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba.
Alieleza kuwa kuimarishwa usimamizi na uendeshaji wa programu ya mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba “Greenhouse” kutachangia kuongeza ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo.
“Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndio yenye dhamana na masuala ya vijana iliamua kupitia ilani ya uchaguzi ibara ya 6 kifungu (a) inayosema kuhamasisha kilimo kupitia kauli mbiu ya Kilimo Kwanza kwa kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao, ambao ulipelekea kutambua umuhimu wa mchango wa vijana hasa waliopo vijijini ndipo mradi huu wa Kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba ulianzishwa kwa lengo la kuwezesha vijana,” alisema Mhagama.
Aliongeza kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ina nia ya dhati ya kuwawezesha vijana kupitia programu mbalimbali inazoazisha kwa lengo la kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto ya ajira.
“Serikali ina lengo la kufikisha ujuzi huo wa kilimo cha kisasa katika halmashauri zote za Tanzania bara kwa kuwa asilimia 63 ya fursa za ajira zinapatikana kwenye kilimo na tena maeneo ya vijijini,” alisema Mhagama
“Mataifa makubwa mengi yaliyoendelea wamekuwa wakitumia kilimo cha aina hiyo kwa lengo la kulima kisasa, kuongeza thamani ya mazao, kupata masoko endelevu na la uhakika na kulima kwa tija, hivyo tukiwawezesha vijana wetu watanufaika na kilimo hicho na sekta hiyo italeta tija katika kukuza uchumi wa nchi,” alieleza Mhagama.
Sambamba na hayo Mheshimiwa Mhagama alitoa maagizo yafuatayo (i) Kufanyika maamuzi ya haraka yatakayowezesha vijana katika halmashauri ambazo bado mradi huo haujafika wanafikiwa (ii) Fedha zote zilizokusanywa na vijana katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo zikaguliwe na vijana washirikishwe ili waweze kutoa taarifa ya idadi ya mazao waliyozalisha na kiwango walichoweza kuuza (iii) kuanzishwa mfumo wa ufuatiliaji ambao utakuwa na taarifa ya utekelezaji wa majukumu (iv) Kuwezesha upatikanaji wa mikopo ambayo itawasaidia vijana hao kuanzisha vitalu nyumba vyao (v) kutengeneza mfumo wa ukusanyaji mapato na matumizi (vi) Wakandarasi waliojenga vitalu nyumba katika halmashauri 84 awamu ya kwanza kufanyia marekebisho vitalu nyumba ambavyo vimekuwa na matatizo.
Aidha Waziri Mhagama amewataka vijana kutumia ujuzi waliopata katika mafunzo hayo ili waweze kusimamia mradi huo vizuri na wajenge moyo wa kuthubutu katika kuwasaidia vijana wenzao kupata ujuzi wa mafunzo hayo ya kilimo cha kisasa.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe alikiri kupokea maagizo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili programu hiyo ya mafunzo ya kilimo cha kisasa iweze kuwa endelevu.
“Ofisi ya Waziri Mkuu iliona umuhimu wa kushirikiana na , Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, wakandarasi pamoja na Vijana ili kutathmini utekelezaji wa mradi huo na kuona namna ya kukabili changamoto ambazo zilijitokeza, mafanikio yaliyopatikana ili kuona namna bora ya kuimarisha mafunzo hayo,” alisema Massawe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ally Msaki alielezea maazimio waliyofikia pamoja na wadau katika kuimaarisha usimamizi na uendeshaji wa mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na kuangalia namna bora ya kuendesha mafunzo hayo, uwepo wa utaratibu maalum wa makusanyo, utunzaji na matumizi ya fedha, kuwezesha vijana kuwa na ujuzi wa kuongeza thamani ya mazao, kuelezea wananchi mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo wa kilimo cha Kitalu nyumba,kuwezesha vijana kufanya kilimo biashara na uwepo wa muendelezo wa kutoa mafunzo na kuongeza vitalu nyumba katika kila halmashauri.
Naye Mmoja wa wanufaika wa Programu hiyo Bw. Festo Masiba ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewajengea ujuzi mkubwa wa kuweza kulima kwa tija.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuamini sisi vijana na kutuwezesha kupata mafunzo ya Kilimo bora kwa kutumia eneo dogo na upatikanaji wa mazao ni mwingi, tumeweza kukua kiuchumi na tunaujuzi wa kuwajengea wadau wengine vitalu nyumba,” alisema Masiba
0 comments:
Post a Comment