Sunday, 15 March 2020

Wakurugenzi simamieni ukusanyaji wa Mapato

...
Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wameagizwa kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa Mapato ya ndani ili kutimiza malengo yaliyopangwa na Serikali katika mwaka wa fedha wa 2019/2020

Agizo hilo limetolewa leo na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga alipokuwa akikagua  miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.

Ameseama kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepangiwa kukusanya  zaidi ya shilingi bilioni 765 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 lakini hadi kufikia Februari, 2020 Mamlaka hizo zimeweza kukusanya mapato kwa asilimi 61 ya malengo ya mwaka.

“Inasikitisha kuona baadhi ya maeneo fedha za makusanyo ya mapato zinaingia mifukoni mwa watu, unakuta wanakusanya fedha lakini haziingii kwenye akaunti za Halmashauri, jambo hili linaisababishia Serikali kupoteza Mapato”Amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.

Mhandisi Nyamhanga ameendelea kwa kusema kuwa ili Halmashauri ziweze kutekeleza mipango yake  na kufikia malengo waliojiwekea katika mwaka ni wajibu wa wakurugenzi wote kuweka nguvu katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuzitumia fedha hizo  kwa kazi zilizopangwa.

 “Ongezeni kasi ya kukusanya mapato ya ndani, hakikisheni malengo mliyoweka ya ukusanyaji wa mapato yanatimizwa, zibeni mianya ya upotevu wa mapato hasa kwa watumishi wanaosimamia ukusanyaji huo, jambo hili linatia doa na kusababisha Halmashauri nyingi kutokamilisha  miradi ya maendeleo kwa wakati” Amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.

Kuhusu matumizi ya fedha za ndani na ruzuku za Serikali Mhandisi Nyamhanga amesema Serikali inatoa fedha nyingi sana  katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ni wajibu wa Wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanasimamia matumizi ya fedha.

Amesema kuwa baadhi ya Halmashauri fedha hizo zinakusanywa lakini zinaanza kutumika kabla hazijaingizwa kwenye akaunti za Halmashauri, hii ni sawasawa na kutumia fedha mbichi hivyo naelekeza fedha hizo zikusanywe na kuingizwa kwenye akaunti ndipo zianze kutumika

Amefafanua kuwa Fedha nyingi zinakusanywa katika Halmashauri lakini haziingii kwenye Akaunti, Wakurugenzi hakikisheni  mnatumia mifumo ya kielektroniki kukusanya mapato na kuhakikisha fedha hizo zinaingia kwenye Halmashauri

Mhadisi nyamhanga amesema kuwa Halmashauri hazina budi  kuongeza kasi  ya ukusanyaji wa mapato ya ndani  lakini kupanga matumizi  mazuri ya fedha hizo  kama yalivyopangwa  kwenye bajeti zao .

Aidha amesisitiza kuwa Serikali imesambaza mashine  7227  kwenye Halmashauri mbalimbali nchini  kwa ajili ya kuboresha  ukusanyaji wa mapato ambapo ugawaji umeenda sambamba  na  uwezo wa Halmashauri katika kukusanya mapato.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema kuwa wameweza kudhibiti wizi wa mapato ya ndani kwa kuhakikisha matapeli wote wa Mapato wanatafutwa na kuzirudisha fedha hizo

Wakati huohuo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga  amefanya ziara ya siku moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na kutembelea  mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Mvomero na mradi wa ujenzi wa Sekondari ya kumbukumbu ya Sokoine..

Na. Angela Msimbira MVOMERO


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger