Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema ana matumaini makubwa na mradi wa Mwongozo wa Masuala ya Uvuvi Mdogo (Small Scale Fisheries Guidelines) kwa kuwa mbali na kushughulika na wavuvi wadogo unalenga pia katika kuhakikisha wanawake wanahusishwa kikamilifu katika mnyororo wa uzalishaji kuanzia ngazi za awali.
Akizungumza jana majira ya jioni (11.03.2020) katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi ndogo za wizara hiyo katika jengo la NBC jijini Dodoma, kilichohusisha baadhi ya wajumbe wa timu ya kitaifa inayoratibu utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Naibu Waziri Ulega amesema serikali imekuwa ikitaka kuona namna wavuvi wadogo wanavyonufaika kupitia sekta ya uvuvi wakiwemo wanawake.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amesema wafadhili wa mradi huo wako tayari na wanaichukulia Tanzania kama mfano utakaotumika katika nchi nyingine katika bara la Afrika.
Ili kutimiza malengo hayo, timu hii ya kitaifa (National Task Team) inalenga kukusanya maoni ya wadau wote ikianzia na watunga sera, viongozi wakuu katika sekta ya uvuvi, mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi na wavuvi.
Wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti Alhaj Yahya Mgawe wameeleza kuwa ili uvuvi mdogo ambao unahusisha zaidi ya asilimia 90 ya uvuvi wote duniani uweze kuwa na tija ni lazima wavuvi wawezeshwe kwa kutumia mkakati uliokubaliwa na mataifa yote duniani.
Malengo ya mkakati huo ni kuondoa umasikini, matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi na kuhakikisha usalama wa chakula.
Timu ya kitaifa inayoratibu utekelezaji wa mradi wa Mwongozo wa Masuala ya Uvuvi Mdogo (Small Scale Fisheries Guidelines) unaofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), iko katika hatua ya kukusanya maoni ya kuandaa mpango mkakati wa kitaifa ili kufikia malengo hayo.
Maoni na michango ya mawazo yataisaidia nchi kuandaa mpango wa utekelezaji na kuhakikisha maisha ya wavuvi wadogo yanaboreshwa na sekta ya uvuvi inachangia kukua kwa uchumi wa nchi.
0 comments:
Post a Comment