Na. Immaculate Makilika - MAELEZO
Serikali imesema nchi iko salama dhidi ya ugonjwa wa CORONA na tayari imechukua hatua kadhaa za tahadhari ili kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo hapa nchini.
Serikali imesema nchi iko salama dhidi ya ugonjwa wa CORONA na tayari imechukua hatua kadhaa za tahadhari ili kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo hapa nchini.
Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kwamba ugonjwa huo sio tu hauingii nchini, lakini pia kuzuia kusambaa kwa maambukizi endapo utaingia.
“Zipo hatua zinazochukuliwa ndani ya Taasisi na Wizara moja moja, lakini pia zipo hatua za kitaifa za kukabiliana na ugonjwa huu, na hivyo naomba kuwatoa hofu watanzania kuhusu ugonjwa huu” alisema Dkt. Abbasi
Akifafanua hatua ya kwanza ya kukabiliana na ugonjwa huo, Dkt. Abbasi alisema, Serikali imeandaa utaratibu maalum katika maeneo ya Viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani, ambapo watu hawapimwi ugonjwa wa corona bali joto la mwili ili kuangalia endapo joto limezidi kiwango cha kawaida cha binadamu.
“Watanzania waendelee kuchukua tahadhari kama Rais Magufuli alivyoeleza na wazingatie maelekezo ya namna ya kujikinga yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Afya kupitia wataalamu wake” alisema Msemaji wa Serikali
Dkt. Abbasi amefafanua kuwa katika hatua ya pili, Serikali imeandaa vituo maalum vya kuwatenga washukiwa, na kuna vifaa vyote vya kupima huu ugonjwa. Aidha, hatua ya tatu ni kuwepo kwa hospitali maalum katika kanda zote nchini, ambazo zimetengwa na zitatangazwa endapo atatokea mgonjwa wa CORONA.
Vilevile, Serikali inaendelea kufanya jitihada katika kupambana na ugonjwa huo ikiwemo kusitisha safari za ndege katika nchi za China na Italia na safari ya timu ya Taifa ya mpira wa miguu iliyokuwa iende nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo uliokuwa ufanyike hivi karibuni .
Dkt. Abbasi amevipongeza Vyombo vya Habari nchini kwa kuitikia wito wa Rais wa kuhabarisha umma kuhusu ugonjwa huu, na kuwataka kuzingatia maelekezo ya wataalamu.
0 comments:
Post a Comment