Saturday, 14 March 2020

MKUCHIKA -HALMASHAURI ZIJIFUNZE URASIMISHAJI SINGIDA

...
Afisa  Biashara  wa Manispaa ya Singida, Erick Sinkwembe  akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu kituo cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara.(Picha na John Mapepele)

Kwaya ya Chuo cha Utumishi wa  Umma  ikitumbuiza  mbele ya ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa walipotembelea Kampasi ya Singida.(Picha na John Mapepele)

Wanafunzi wa  Sekondari ya Mwenge Mjini Singida wakiwasikiliza wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Selikali za Mitaa.(Picha na John Mapepele)

Meneja wa TARURA, Manispaa ya Singida, Injinia Lombert Bayona (mwenye koti jekundu) akitoa maelezo kwa Kamati kuhusu ujenzi wa Barabara .(Picha na John Mapepele)

Na John Mapepele,Singida

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, George Huruma Mkuchika amezielekeza Halmashauri za Wilaya zote nchini kwa kushirikiana na Mpango wa Kurasimisha Raslimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kuanzisha Vituo vya Urasimishaji na Uendelezaji Biashara (One Stop Business Formalization and Development Centers) katika maeneo yao kwa nia ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara ili biashara zao ziwe rasmi na kuendesha kwenye mfumo unaotambulika kisheria.



Mkuchika ameyasema hayo akiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Selikari za Mitaa wakati wakikagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na kamati hiyo kwenye ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Singida, kwenye kituo cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara kilichoanzishwa na Manispaa ya Singida kwa kushirikiana na MKURABITA wakati alipokuwa akiongea na wafanyabiashara na vikundi vya wajasiliamali mbalimbali wa Singida.

Amesema amefurahishwa na ubunifu uliofanywa na Manispaa ya Singida kwa kuanzisha kituo hicho ambacho ni msaada mkubwa kwa ajili ya kuwakwamua wafanyabiashara na kuzitaka Halmashauri nyingine kuja kujifunza namna ya kuanzisha vituo hivyo kutoka Manispaa ya Singida kwa kuwa kimekuwa kikifanya kazi zake vizuri.

“Niseme wazi tumefurahishwa sana na ubunifu mlioufanya kwa kuanzisha kituo hiki kwa kuwa ni jambo muhimu sana linalotakiwa kwa wakati wa sasa kwa maendeleo ya taifa letu”alisisitiza Mkuchika

Akitoa taarifa ya kituo hicho mbele ya Kamati, Afisa Biashara wa Manispaa ya Singida, Erick Sinkwembe amesema katika mwaka 2018/2019 Manispaa ya Singida kwa kushirikiana na MKURABITA wamefanya urasimishaji biashara kwa njia ya kujenga uwezo kwa wafanyabiashara 777.

Amesema lengo kuu la kuanzisha kituo hicho ni kufanya mchakato mzima wa urasimishaji wa biashara kuwa wa haraka ,rahisi na wa gharama nafuu kwa mfanyabiashara ambapo aliongeza kwamba shughuli za urasimishaji biashara kwenye Manispaa ya Singida zimefanywa kwa kushirikiana na wadau kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.

Amezitaja taasisi hizo kuwa ni Benki ya NBC,CRDB na NMB,BRELA,NSSF,SIDO,TCCIA,NIC, TRA pamoja na NHIF na kwamba shughuli za Kituo hicho zilianza rasmi tarehe 10/12/2019 ambapo Ofisi ya Biashara ya Manispaa pia ilihamishiwa hapo ili kurahisisha utendaji kazi

Amesema awali jengo hilo ambalo linatumika kama kituo lilikuwa ukumbi wa Manispaa na baada ya kukarabatiwa na Manispaa kwa jumla ya shilingi 17,349,960/= na MKURABITA kuwezesha vitendea kazi (Komputa, UPS,Scanner na Printa) vyenye jumla ya gharama ya shilingi 4,071,000/= limeweza kufanya kazi ambapo amesema kilichobaki ni kuunganisha mfumo wa TEHEMA utakaogharimu jumla ya shilingi 3,995,000/=, kazi ambayo amesema itakamilika katika siku chache zijazo.

Mratibu wa Programu ya MKURABITA nchini, Dkt. Seraphia Mgembe ameitaka Ofisi ya Biashara ya Manispaa ya Singida kuwa kiungo kikuu baina ya wadau katika mnyororo mzima wa urasimishaji na uendelezaji wa biashara kwenye Manispaa hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Jasson Rweikiza amesema Kamati yake imeridhishwa na kazi inayofanywa na Kituo hicho na kuwataka wafanya biashara kutumia fursa hiyo vizuri kupata mikopo katika Taasisi za kifedha ili kuziendeleza biashara zao.

Kwa nyakati tofauti wajasiliamali na wafanyabishara wameomba kamati kuangalia namna ambavyo Serikali itakavyowapunguzia kodi ambapo pia waliomba watumishi wa taasisi zote kuwepo katika kituo hicho ili kuwarahisishia kupata huduma zote kwa wakati mmoja na kwa haraka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi ameishukuru Kamati kwa michango yao waliyotoa ili kuboresha kituo na miradi yote waliyoikagua katika ziara yao ya siku mbili ambapo amesema Mkoa umepokea na utafanyia kazi kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa ili kuwaletea maendeleo ya haraka wananchi wa mkoa wa Singida kama kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu!

Katibu Tawala Mkoa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi amesema katika ziara hiyo kamati imeweza kukagua miradi mbalimbali ambayo ni Ukarabati wa Shule ya Sekondari Mwenge kupitia mpango wa ukarabati wa shule kongwe za Serikali (89),Mradi wa Timiza Malengo unaosimimamiwa na kufadhiliwa na TASAF, Kituo cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara, Eneo la ujenzi wa Chuo Cha Utumishi wa Umma (Mungumaji) Kampasi ya Singida na Ujenzi wa barabara kiwango cha lami unaofanywa na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA).



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger