Friday, 6 March 2020

Mbowe Azungumzia Waliofanya Vurugu Kwenye Mkutano Wake

...
Mwenyekiti  wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, amesema kikundi cha watu waliomzomea katika mkutano wake wa kibunge uliofanyika juzi, kiliandaliwa na kuratibiwa  kwa nia ya kuvuruga mkutano huo.

Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari kwenye ofisi yake wilayani Hai jana, Mbowe alisema kabla mkutano huo wa tano wa kibunge uliofanyika katika Kijiji cha Kikavu, Kata ya Machame Weruweru, walikuwa na taarifa zote kuhusu kikundi hicho.

“Mkutano ulikuwa na taarifa zote za mapema, kwamba kuna mpango unaoratibiwa na baadhi ya viongozi cha chama flani na tuliripoti tukio hili polisi, kwamba kuna taarifa ya watu waliokuwa wakiletwa kutoka maeneo mengine ili kuvuruga mkutano.

“Lakini tulishangaa kuona genge hilo la vijana lilipojitokeza mbele ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya, alionekana kuwalinda na kuwaacha wakivuruga mkutano kwa zaidi ya dakika 15, wakionekana wakipiga kelele na mayowe bila kuchukuliwa hatua yoyote,” alisema Mbowe.

Alisema mpango huo unaonekana ulikuwa wa makusudi kwa kuwa hata polisi hawakutaka kuchukua hatua yoyote kuwadhibiti vijana hao, na wao kama viongozi walilazimika kuwashauri vijana wao ambao walikuwa tayari kuulinda mkutano wasichukue hatua yoyote dhidi ya vijana wale kwa sababu hawakuzoea vurugu.

Mbowe alisema vijana hao walipelekwa eneo la mkutano huo kwa magari manne na wamewapa polisi picha zao, namba za magari hayo na wote wanajulikana kwa kuwa hata polisi wenyewe walipiga picha, hivyo wanategemea kuona polisi wakichukua hatua dhidi ya watu hao.

Alisema hakuna aliyedhurika kwa watu wa pande zote kwa kuwa watu wa Chadema hawakupambana nao kwa kuwa walifahamu kuwa jambo hilo liliratibiwa na kiongozi mmoja ambaye anawalinda wahalifu kwa sababu ametumwa.

“Wananchi wenyewe wa eneo lile wanawajua wahusika kuwa hawakutoka kabisa katika eneo lile wala katika kata ile na waliletwa kwa mabasi, baada ya kupewa pombe ili waende kuvuruga mkutano huo,” alisema Mbowe.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger