Monday, 9 March 2020

Laini zote ambazo hazijasajiliwa kuzimwa Jumamosi

...
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kazi ya kuzima laini zote za simu, ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa (NIDA), itakamilika Jumamosi ijayo. Itakamilika ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea na mambo mengine ya kitaifa, ukiwemo Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Uzimaji huo wa laini ulianza mwishoni mwa Januari mwaka huu, baada ya Rais John Magufuli kuongeza siku 20, ili kutoa fursa kwa wananchi, ambao walikuwa hawajasajili laini zao, wakamilishe usajili huo kwa alama za vidole.

Mbali na kuzima laini hizo, TCRA pia imesema kuanzia Juni 30, mwaka huu, kila mmiliki wa laini atatakiwa kumiliki laini moja tu ya simu kwa kila mtandao.

Kama kuna mtu anamiliki laini zaidi ya moja katika mtandao mmoja, atalazimika kuchagua laini moja anayoihitaji ili zilizobaki zizimwe.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa TCRA, Frederick Ntobi, amelieleza HabariLeo kuwa ifikapo Machi 14, mwaka huu watoa huduma ambao ni kampuni za simu za mkononi, watatakiwa kuzizima laini zote, ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole kwa kutumia kitambulisho cha NIDA.

“Kutakuwa na awamu mbili za uzimaji wa laini zilizokuwa zimesajiliwa awali kwa kutumia Kitambulisho cha Mpiga Kura na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, ambapo laini za simu 8,722,527 zilizobakia hadi tarehe 02/03/2020 zitafikia ukomo wake rasmi tarehe 14/03/2020,” alisema Ntobi.

Katika hilo, alifafanua kuwa laini milioni tatu zilizimwa jana Machi 8 ; na awamu ya pili ambayo ni ya mwisho, laini milioni tano zilizobaki, zitazimwa Jumamosi ya wiki hii.

Alisema awamu hizo mbili, zitakuwa zimefanya kazi ya kuzima laini zilizosajiliwa kwa kutumia Kitambulisho cha Mpiga Kura na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kufikia tamati, ambapo jumla ya laini za simu 8,722,527 zitakuwa zimezimwa.

Ntobi alisema watoa huduma, wanatakiwa kuwasimamia vizuri na kwa weledi mawakala wao wa usajili wa laini za simu ili wafuate sheria na utaratibu katika usajili kwa kutumia alama za vidole. Alisema mpaka sasa laini 35,044,629 zimeshasajiliwa kwa alama za vidole, sawa na asilimia 80.1.

Hadi kufikia Machi 2, mwaka huu, jumla ya laini zote za simu zilizounganishwa mitandaoni ni 43,767,156. Laini moja kwa mtandao mmoja.

Kwa mujibu wa Ntobi, Kanuni ya 18 na 19 ya Sheria za Kielektroniki na Mawasiliano ya Posta (Usajili wa Laini) ya mwaka 2020, kila mtu atatakiwa kumiliki laini moja kwa mtandao mmoja wa simu kuanzia Juni 30, mwaka huu.

Endapo mtu anamiliki laini zaidi ya moja kwenye mtandao mmoja, atalazimika kuchagua laini anayoihitaji kati ya hizo. Zilizobaki zitazimwa.

Wanaotumia CCTV
Sambamba na hilo, watu wanaotumia mawasiliano ya mashine kwa mashine, kama vile kamera za CCTV watatakiwa kumiliki laini nne tu na laini hizo hazipaswi kuhamishwa kwenda kwenye matumizi mengine, isipokuwa kwa yale tu yaliyoainishwa wakati wa uombaji na usajili.

Vivyo hivyo, kwa watu waliosajili laini kwa ajili ya matumizi ya ‘moderm’ nao hawapaswi kuzitumia kwa matumizi mengine yoyote.

Suala la akina ‘Tuma Pesa’
Kutokana na matapeli kuendelea kuwatumia watu ujumbe usemao ‘Tuma Pesa Kwenye Namba Hii’ au wengine kuwapigia watu simu, wakijifanya ni wafanyakazi wa kampuni za simu au wengine namba zao kutumika katika uhalifu mwingine wowote, TCRA ilisema atakayebainika, namba yake ya NIDA itafungwa na hataweza kupata huduma katika kampuni yoyote ya simu nchini.

Ntobi alisema wananchi wanaopokea jumbe hizo za kitapeli, au kupigiwa simu na matapeli, wanapaswa kutoa taarifa za namba hizo kwenye kampuni ya simu husika, ili namba ya NIDA ya tapeli huyo ifungwe moja kwa moja.

Waliowasajilia laini wengine, wageni Kuhusu watu waliowasajilia watu wengine, alisema wajiandae kukabiliana na taratibu za sheria, pale laini hizo zitakapobainika kuhusika kwenye matatizo.

Na wale ambao wamewasajilia wageni kutoka nje ya nchi kinyume cha utaratibu, wajue kuwa ni kosa la jinai, nao namba zao za NIDA zitafungwa moja kwa moja.

Chanzo: Habari Leo


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger