Saturday, 7 March 2020

Katibu Mkuu CCM: Tutatumia Dola Kubaki Madarakani

...
Katibu  Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ali, amekiri chama chake kuitumia dola kuhakikisha kinabaki madarakani.

Amesema kama chama chochote kinachoongoza serikali kitashindwa kutumia dola kubaki madarakani, utakuwa uzembe wa chama chenyewe.

Kwa kulitambua hilo, Dk. Bashiru amesema CCM imekuwa ikitumia dola kujihakikishia ushindi wakati wa uchaguzi na mwaka huu wamepanga "kuitumia dola kweli kweli".

Lakini, kiongozi huyo wa CCM akaonya kuwa chama kinachoongoza serikali, hakipaswi kuitumia dola kunyanyasa wapinzani wake.

Dk. Bashiru aliyasema hayo katika mahojiano maalum na vyombo vya habari vya IPP alivyovitembelea jijini Dar es Salaam jana.

"Ukishakuwa chama tawala, kuna dhana inaitwa nafuu ya mwenye madaraka. Ukishindwa kutumia nafuu hiyo, utakuwa kama KANU (chama tawala cha zamani cha Kenya), iliposhindwa kutumia nafuu hiyo, haikuwahi kurudi madarakani au UNIP ya Zambia.

"Unashika dola halafu unatumia dola kubaki madarakani. Akitokea mtu mwenye busara zaidi, akakwambia usitumie dola, ukamsikiliza, siku ukishatoka hurudi!

"Hata kwenye kazi, kazi inatafuta kazi. Kwa hiyo, aliye na dola anatumia dola hiyo kubaki madarakani. Ukweli hata Chadema ikiingia madarakani, kuiondoa kwenye dola itakuwa ni uzembe wake, kwa sababu ana nafuu na faida ya kuwa na dola.

"Kinachotakiwa usitumie dola vibaya kunyanyasa wapinzani wako. Wanaosubiri sisi (CCM) tulegelege kutotumia dola kubaki kwenye dola, watasubiri sana. Huo ndio ukweli, si wa Tanzania, si wa CCM, hata (Donald) Trump (Rais wa Marekani) kumwondoa leo ni ngumu," alisema.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu kauli yake hiyo, Dk. Bashiru alisema: “Watu wakisema unatumia dola, wanadhani unakwenda kuiba, dola ni chombo cha wananchi, kutumia dola ni kutumia wananchi waliokukabidhi dola ili wakubakize kwenye dola, hii ndiyo maana yake tu.

“Hawa wananchi ambao tumeshirikiana wote kutafuta maji, kujenga miundombinu ya barabara kwa kodi zao, hakuna chombo kinachoweza kukusanya kodi ambacho si dola, ndiyo moja ya sifa, sifa kubwa ya dola ni kukusanya kodi, tutatumia kodi za wananchi.

“Ndiyo matumizi ya dola, tutatumia vyombo vya ulinzi na usalama kuwahakikishia wananchi wako salama, ndiyo matumizi ya dola.

“Sasa, wewe ukiwa na dola halafu wahuni wanakwenda Rufiji na Kibiti, si unakumbuka kulikuwa hakupitiki? Tulitumia dola kulinda usalama wa watu. Nimepita mara nyingi wakati mwingine ninashuka kula kuku wa kuchemsha, hayo ndiyo matumizi ya dola ninayosema.”

Dk. Bashiru alisema wanatumia dola kwa sababu wamekabidhiwa dhamana kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha usalama upo.

“Kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana na rushwa, tumevitumia kuwatisha wala rushwa, sasa hayo matumizi mabaya? Tutaitumia kweli kweli.

“Matumizi ya dola ni kuwatumia wananchi wenye dola kwa kuwa dola ni mali ya wananchi, sisi tumekabidhiwa dhamana ya kuiendesha, tukiiendesha vizuri wananchi watatuamini zaidi, tukiiendesha vibaya, wanatuadhibu, wanampa mtu mwingine. Hata hao wengine wanatafuta dola.

“Faida tuliyo nayo tuna dola, wengine wanatafuta, mwenye dola akiishika vizuri, akaitumia vizuri na kufanya yale iliyoahidi, akatumia vizuri kujengea imani wapigakura, hawabadilishi ile dola kumpa mtu mwingine, hii ndiyo faida ya kuwa na dola.

“Mwaka huu kuna uchaguzi, tunakwenda kuomba, yaani tutapiga magoti tukiwa na maelezo mnajua tuliahidi hiki, tumefanya hivi, mmetupa kodi zenu tumefanya haya. Kwa hiyo watu wasitafsiri vibaya, lakini huwezi kuzuia tafsiri kwa kuwa hii ni dhana ya kifalsafa kidogo.

“Mtu anaweza kutumia maneno haya niliyoyasema akatafsiri vingine, maana yake ni hiyo, tutatumia dola kodi, taasisi za serikali kutekeleza ilani, tutatekeleza ahadi na kufika Oktoba, tutakuwa kwenye nafuu zaidi na faida zaidi kubaki madarakani," alifafanua.

KIFO CHA UPINZANI
Alipoulizwa kuhusu madai ya kuwapo mkakati wa chama chake kuhakikisha kinaua upinzani nchini, Dk. Bashiru alisema hakuna dhamira hiyo, lakini kama kuna vyama vitakufa, CCM haiwezi kuzuia.

“Hatuna mpango wa kuzuia kifo, siyo kazi yetu kuzuia kifo cha chama, ni jukumu la chama kutokufa, mtu atakayekaa barabarani kusababisha chama kife kwa kushindwa ni halali yangu, na hili ni jukumu la vyama vyote vilivyosajiliwa kubaki hai, siyo jukumu la CCM kuvilea vyama visife, kifo kibaya cha chama huanza mapema.

“Ni kama ugonjwa wa kichwa, huanza taratibu, maumivu ya kichwa huanza polepole, na kifo cha chama huanza polepole kwa kushindwa, kifo cha kisiasa siyo kifo cha watu na katika siasa kuna kufa na kuzaliwa, vipo vilivyokufa, vipo vinachechemea, vingine haviwezi kufa, navijua," alisema.

Dk. Bashiru pia alitolea ufafanuzi madai ya CCM kununua wanachama kutoka vyama vya upinzani, akisema hakuna anayenunuliwa na kwamba wanaotoka upinzani ni 'watamu kweli' na matarajio yao ni kupokea wengine wengi zaidi kipindi hiki.

“Sijawahi kuona mavuno mazuri kama ya mwaka huu na mwaka jana na shughuli inaendelea, kama huo ndiyo mwelekeo wa vyama vya upinzani kufa, vijifunze namna ya kutunza wanachama wao," alitamba.

MCHUJO MKALI CCM
Katika mahojiano hayo, Dk. Bashiru pia alidokeza kuwapo mchujo mkali ndani ya chama kuwapata wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kuweka wazi kuwa mgombea wao wa urais mwaka huu ni Dk. John Magufuli.

Alisema kuna vigezo kadhaa vitakavyozingatiwa ikiwa ni pamoja na kufuatilia nyendo za wanachama wao ambao tayari wameshaanza kupitapita na kupenyeza fedha kwa miamala ya simu ili kupita kwenye kura za maoni.

“Ninawatahadharisha, uteuzi siyo kura za maoni peke yake, ni kura za maoni na mjadala wa jina kwa jina kuhusu sifa za aliyeshinda na kukubalika kwa wananchi, hatutafuti wagombea wa CCM, tunatafuta wagombea wa CCM watakaopigiwa kura na wana CCM na wasiyo wana CCM na mwisho vikao ndivyo vinateua,” alisema.

Dk. Bashiru alisema kila mwana CCM ana haki ya kugombea uongozi, lakini hana haki ya kuteuliwa kwa sababu uamuzi wa kuteua ni wa vikao na hakuna atakayeteuliwa kuwania ubunge na udiwani bila kuangalia rekodi yake ya utendaji na mahudhurio yake kwenye vikao vya Bunge na mabaraza.

“Hakuna uteuzi wa bure, wapo wanaojihangaisha kuzungumza na wapigakura wakidhani wakimalizana nao kwenye kura za maoni, wamepata uteuzi, tutazingatia kura za maoni, na kwenda kwenye kumbukumbu zako ulisema nini, uliahidi nini na umetekeleza nini," alionya.

Dk. Bashiru pia alizungumzia maandalizi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka huu, akisema imejikita katika vipaumbele vitatu ambavyo ni kilimo, maji pamoja na ulinzi na usalama.

UKAWA TISHIO
Mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), pia alikiri kuwa kuungana kwa baadhi ya vyama vya siasa katika kile kilichoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kulikuwa tishio kwa CCM katika uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema hilo lilijidhihirisha kwenye idadi ya kura ambazo CCM ilizipata kwa nafasi ya urais, akibainisha kuwa ilikuwa mara ya kwanza mgombea wao kushinda kwa kura chache.

Mtaalamu huyo wa sayansi ya siasa alisema Ukawa pia ulisababisha CCM kupoteza majimbo mengi zaidi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

“Rais John Magufuli alipata kura ambazo mgombea wa CCM hajawahi kuzipata katika mfumo wa vyama vingi -- asilimia 58 na mgombea wetu (alikuwa) hajawahi kutofikia asilimia 60, Rais mstaafu Jakaya Kikwete wakati anaingia alifikia asilimia 80,” alifafanua.

Dk. Bashiru pia alitoa ufafanuzi kuhusu kauli yake kwamba mchakato wa Katiba Mpya ni kiporo kilichochacha, akisema Ukawa ulioaminiwa na wananchi umesambaratika.

“Ndiyo maana nakiita kiporo kilichochacha, Ukawa iko wapi? Wanaweza kuingia na ajenda hiyo mwaka huu? Wanaweza kuaminika mwaka huu? Walikuwa wanatafuta Katiba Mpya kweli? Haijapatikana wamesambaratika…

"Kumbe ilikuwa ni geresha, ilikuwa ni kuteka mchakato wa Katiba Mpya kutafuta Ikulu, Ikulu haikupatikana, Ukawa imesambaratika. Kuwa na wanasiasa wa namna hiyo wa kuwavuta wananchi kutafuta jambo jema na kuwaacha solemba, nacho ni kiporo kilichochacha.

"Sasa, unataka kuumwa matumbo kula kiporo cha namna hiyo? Hatujamaliza matatizo ya Corona, tuingie kwenye kuumwa matumbo? Rais Magufuli akasema 'hatuwezi kuwa na siasa za kinafiki, watu wanatafuta Ikulu kwa kisingizio cha Katiba Mpya'", alisema.

UPINZANI KUITWA IKULU
Dk. Bashiru pia alimpongeza Rais Magufuli kwa kuendelea kukutana na Watanzania wa makundi mbalimbali Ikulu, akikumbusha kuwa amefanya hivyo kwa wafanyabiashara, wenye ulemavu na makundi mengi ambayo hukutana na wasaidizi wake.

"Ameshatuelekeza tukutane na makundi ya wawakilishi wote, anakutana na mabalozi, hata viongozi wa upinzani wana haki ya kukutana naye Ikulu, ndiye pekee ameifanya Ikulu ionekane ni ya Watanzania.

“Kama hiyo ndiyo inatajwa ni kujenga maridhiano, ni mkakati mzuri lakini siyo ile ya mtazamo wa kisiasa, bali kwa mtazamo wa kitaifa, Ikulu ni ya Watanzania wote na kila mmoja anaweza kukutana na Rais Ikulu,” alisema.

Chanzo: Nipashe


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger