. Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bachungwa (aliyenyanyua mkono) akiangalia mashine za kukamua mafuta kwenye kiwanda cha Mt. Meru mjini Singida; kiwanda kinachosadikiwa kuwa kikubwa kuliko vyote Afrika Mashariki na Kati, mbele yake ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Injinia Paskasi Muragili nyuma yake ni Sailesh Patel, Makamo wa Rais wa Kiwanda cha MT Meru-Tanzania
Na John Mapepele, Singida
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bichungwa ameitaka Wizara yake kwa kushirikiana na Mkoa wa Singida ndani ya mwezi moja kufanya mkutano wa kitaifa utakaowashirikisha wadau wote wa zao la Alizeti.
Mkutano huo utakuwa ni wa kujadili mnyororo wa thamani wa zao hili kuanzia kwa mkulima hadi kwa wenye viwanda ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kufuta gharama kubwa ambazo serikali inatumia kuagiza mafuta ya kula toka nje ya nchi.
Bachungwa ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya siku mmoja leo kwenye Mkoa wa Singida kutembelea viwanda vya kukamua Alizeti ambapo alikagua shughuli zinazofanywa na kiwanda kikubwa cha kukamua mafuta Afrika mashariki na Kati cha Mt. Meru na Kiwanda cha Singida Fresh Mill vilivyopo ndani ya Manispaa ya Mji wa Singida.
Alisema lazima kuwepo na mkutano huo haraka wa wadau wote wa zao hilo ili kunusuru fedha nyingi zinatumika na nchi kununua mafuta ya kula kutoka nje ya nchi
Alisema katika kundi la bidhaa la vyakula, mafuta ya kula yanashika nafasi ya pili kuwa kutumia gharama ya asilimia 22.6 ikiongozwa na zao la Ngano linalotumia asilimia 57.3 huku Sukari ikitumia asilimia 16.2 ikifuatiwa na Mahindi ambayo yanatumia gharama ya asilimia 2.6 kulipiwa toka nje ya nchi ambapo aliongeza kuwa Tanzania kama nchi inatumia jumla ya kiasi cha shilingi trioni 1.3 kwa mwaka kuagiza bidhaa zote za vyakula kutoka nje ya nchi.
Bachungwa alisema Tanzania imejaliwa kuwa na maeneo makubwa ya ardhi yenye rutuba ambayo yanaweza kupanda mbegu bora za Alizeti ambazo zinaweza kutosheleza viwanda vya ndani na kuuzwa nje ya nchi, kinachotakiwa ni wadau wote kukaa kama taifa na kujadii namna bora ya kuongeza thamani kwenye mnyororo wa mzima wa thamani wa zao la Alizeti.
Aliwataja baadhi ya wadau muhimu katika kikao hicho kuwa mikoa inayolima zao la Alizeti, wizara inayohusika na kilimo, Mifugo na Uvuvi, Fedha, tasisi za utafiti zinazojiusisha na Alizeti, wajasiliamali na wawekezaji wa viwanda vikubwa vya kukamua mafuta ya Alizeti hapa nchini.
Alisema alichogundua katika ziara hiyo ni kuwa hakuna mfumo mzuri wa kufungamanisha kilimo cha alizeti na viwanda hali inayowafanya wadau washindwe kupata faida na badala yake kuhangaika kutafuta masoko ya bidhaa hizo nje ya nchi na kuwakosesha watanzania ajira na mapato kwa taifa.
“Nimeshangaa viwanda vinahangaika kuuza mashudu nchi jirani na kulalamikia kodi na ushuru unaotozwa na Serikali wakati tunaviwanda vyetu vya kutengeneza vyakula vya kuku vinahangaika usiku na mchana kutafuta mashudu wakati Singida yamejaa” alihoji Bachungwa
Aliutaka Mkoa wa Singida kutumia fursa ya kuwa jirani na Makao Makuu ya Nchi, Dodoma kupanga mipango mizuri kwa kutenga maeneo maalum ya uwekezaji kama ambavyo Mkoa wa Pwani ulivyonufaika kwa kuwa karibu na Jiji la Dar es Salaam kwa kutenga maeneo ambayo sasa maeneo hayo yameendelea kujengwa viwanda vya kisasa hivyo kuendana na kauli ya Serikali ya awamu ya Tano inayosisitiza ujenzi wa viwanda
Aidha aliwataka watendaji Serikalini kote nchini kubadilika na kuondokana na dhana kwamba mapinduzi ya viwanda yataletwa na Wizara ya Viwanda na Biashara na badala yake mikoa iweke mikakati mahususi ya kuwavutia wa wekezaji kuja kuwekeza na baada ya kuwekeza waendelee kuwalea ili waweze kuendelea kuweka mitaji zaidi ktika mikoa husika.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi alimshukuru Waziri Bachungwa kwa kufanya ziara hiyo ambapo alisema tayari mkoa wake umeshafanya vikao vya mara kwa mara na wadau mbalimbali wa zao la alizeti ambapo amesema hata wiki moja iliyopita Mkoa wa kushirikiana na Shirika na Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Viwanda Vidogo Nchini (SIDO) walitoa mafunzo maalum kwa wajasiliamali wa zao hilo ambapo amesema mkutano huu utakuwa na manufaa makubwa kwa kuwa utakuwa katika ngazi ya kitaifa na itashirikisha wadau wengi zaidi.
“Mkoa tunafarijika sana kwa wazo lako ulilotoa la kuwa na mkutano wa kitaifa wa wadau wote wa zao la Alizeti kwa kuwa ni ndoto yetu kuboresha thamani ya zao hili ili kuleta mapinduzi makubwa kwa wadau wote na taifa kwa ujumla, nakuahidi sisi kama Mkoa tutafanya haraka iwezekanavyo kuhakikisha mkutano unafanyika ndani ya mwezi huu” alisisitiza Dkt. Nchimbi
Alisema katika kuratibu mkutano huo mkoa utawashirikisha wadau mbalimbali ambao wataandaa maonyesho maalum ya mnyororo wa zao la Alizeti ili washiriki waweze fursa kuona bidhaa mbalimbali zitokanazo na zao hilo.
Aliongeza kuwa Mkoa umekuwa ukifanya kampeni mbalimbali ikiwa ni pamoja na kampeni ya mbegu hasara na mbegu bora iliyolenga kuwafanya wakulima kuachana na mbegu za asilia ambazo mavuno yake yalikuwa yanazidiwa mara saba zaidi na mbegu bora ya kisasa.
Alizitaja baadhi ya faida ya mbegu bora kuwa ni kuokoa akiba ya ardhi, kuokoa muda, bei ya kuuza kuwa juu ambapo pia aliishukuru benki ya kilimo nchini TADB kwa kutoa mikopo ya zaidi ya bilioni 4 kwa wadau mbalimbali wa zao la alizeti kwenye mkoa wa Singida.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Injinia Paskasi Muragili ameishukuru Serikali kwa kupanga kufanya mkutano huo kwenye Wilaya yake ambapo alisema Wilaya yake ndiyo mzalishaji mkuu wa mbegu bora za Alizeti hivyo mkutano huo utasaidia kuwapa msukumo mpya wadau wote kuboresha thamani ya mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo.
0 comments:
Post a Comment