Serikali imepanga kuajiri Watumishi 44,800 wa Kada ya Afya kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa watumishi wa kada hiyo na kuboresha huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika wakati akijibu swali la Mhe. Silafu Jumbe Maufi (Viti Maalum) aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuajiri watumishi wa kada ya afya ili kuboresha huduma za afya nchini.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, Serikali ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele cha ajira kwa kada ya afya na imekuwa ikitoa vibali vya ajira kwa kuzingatia ukomo wa bajeti kuu ya mshahara na vipaumbele vya mwajiri husika.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameweka bayana kuwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali ilitoa vibali vya ajira 8,000/= kwa kada ya afya, lakini lengo halikufikiwa kwa sababu ya kuwepo kwa wataalamu wachache wa kada hiyo waliojitokeza kuajiriwa Serikalini.
Ili kukabiliana na upungufu wa Watumishi wa kada ya afya, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewahimiza Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwahamasisha wananchi katika majimbo yao kusoma masomo yatakayowawezesha kuajiriwa katika kada ya afya kwa lengo la kuwahudumia Watanzania.
0 comments:
Post a Comment