MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara kujisajili na kupata namba ya utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa kuwa inatolewa bure bila malipo yoyote.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya wiki ya elimu kwa Mlipakodi inayoendelea wilayani Kibiti katika mkoa wa Pwani, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Richard Kayombo amesema TRA inawakaribisha wafanyabiashara wote ambao hawajajisajili kufika maeneo maalumu yanayotoa huduma na elimu kwa mlipakodi katika wiki hii ili wasajiliwe na kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi waweze kufanya biashara zao kwa Uhuru na kulipakodi stahiki bila usumbufu.
"Tunafanya wiki ya huduma na elimu kwa lengo la kusogeza huduma karibu na walipakodi na kuwatatulia changamoto zao zinazohusu ulipaji Kodi" amesema Kayombo.
Aidha, Kayombo ameongeza kuwa mbali na kutoa elimu kwa njia ya semina na matamasha maofisa wa TRA wanapita madukani kutoa elimu kwa wafanyabiasha na kuwasajili kupata namba ya utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ili kuongeza idadi ya walipakodi na kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari miongoni mwa watanzania.
Amesisitiza kwamba, TRA imejipanga kufanya wiki ya elimu kwa mikoa miwili miwili kwa mwezi na hivyo amewataka wafanyabiashara wa kutumia fursa hii kujisajili na kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi na kuhakikisha cheti wanatundika katika maduka yao katika sehemu inayoonekana.
Hata hivyo, ameongeza kuwa pamoja na kuwa na wiki ya elimu lakini pia TRA imetenga siku ya Alhamis kila wiki kwa mameneja wa wilaya na mikoa nchini kote kuwasikiliza wafanyabiashara na kutatua changamoto zao ili kuchochea ari ya ulipaji kodi kwa hiari.
Wiki ya elimu kwa mlipakodi inafanyika katika mikoa ya Morogoro na Pwani kuanzia tarehe 11 hadi 17 Novemba, 2019 ambapo wananchi na wafanyabiashara watapata fursa ya kuelimishwa masuala ya ulipaji kodi
Huduma zinazotolewa katika wiki hii ni usajili wa wafanyabiashara na utoaji wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi, Ulipiaji wa kodi ya majengo, elimu ya kodi na kutatua changamoto mbalimbali za walipakodi ili kuongeza ulipaji kodi kwa hiari.
0 comments:
Post a Comment