Thursday, 21 November 2019

Naibu Waziri Mabula Azitaka Halmashauri Nchini Kudhibiti Ujenzi Holela

...
Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka halamashauri nchini kuhakikisha zinadhibiti ujenzi holela kwa kuhakikisha utoaji vibali vya ujenzi ktika maeneo yao unazingatiwa na kusimamiwa ipasavyo.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana katika halmashauri za wilaya za Morogoro, Mvomero pamoja na Manispaa ya Morogoro wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Morogoro.

Alisema, halmashauri nchini zina wajibu wa kudhibiti ujenzi holela katika maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na Watendaji wa Mitaa na kuweka taratibu ambazo hazitamruhusu mtu kufanya ujenzi wowote bila kupata kibali cha ujenzi kutoka halmashauri husika.

‘’ ili kuondokana na ujenzi holela katika halmashauri zenu mwananchi asifanye ujenzi wowote bila kupata kibali cha ujenzi kutoka halmashauri ‘’ alisema Dkt Mabula

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, zoezi la urasimishaji linaloendelea sasa katika maeneo mbalimbali siyo zoezi la kudumu na kulegalega kudhibiti ujenzi holela kutasababisha zoezi hilo kutokuwa na maana kwa kuwa ujenzi holela utakuwa ukiendelea.

Akigeukia suala la utoaji hati za ardhi, Dkt Mabula aliagiza Hati zilizokamilika katika ofisi za Msajili wa Hati wamiliki wake watangaziwe kupitia njia mbalimbali zikiwemo radio  za Kijamii (Local Radio) sambamba na hati hizo kutolewa kwa wamiliki wake katika eneo maalum litakaloandaliwa  karibu na maeneo wanaoishi wamiliki wa hati hizo.

Alisema, njia ya kuwatafuta wananchi ambao hati zao zimekamilika itasaidia kupunguza mlundikano wa Hati za Ardhi zilizokamilika kwenye Ofisi za Msajili wa Hati tofauti na utaratibu wa sasa unaomtaka mwenye hati kuifuata ofisi za ardhi au ile ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi za Kanda kwenda kuchukua.

Awali Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro Patrick Mwakilili alisema halmashauri yake imepanga kupima viwanja 1,000 kwenye  makao makuu ya wilaya Mvuha na viwanja 3,900 katika mji mdogo wa Kisaki ambao ni lango la kuingilia Mradi wa Kufufua Umeme wa Stiglers George na Hifadhi ya Taifa ya Mwl Nyerere zamani Selous.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya wilaya ya Morogoro,  tayari maeneo tisa ya kufanyiwa urasimishaji makazi yameanishwa aliyoyataja kuwa ni Pangawe, Mkambarani, Fulwe, Ngerengere, Mvuha, Kisaki , Mtamba, Mkuyuni na Dhutumi na kubainisha kuwa halmashauri yake imepokea na kuridhia maombi kutoka makampuni manne kwa ajili ya kazi hiyo.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zilizopo katika wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, ujenzi unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Akiwa katika ukaguzi huo, Dkt Mabula mbali na kulipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuisimamia vyema miradi yake ya ujenzi katika maeneo mbalimbali nchini ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Ofisi hizo za TFS hasa baada ya kuelezwa na Msimamizi wa ujenzi huo Mhandisi Grace Musita kuwa hatua iliyofikiwa sasa na Shirika lake katika kujenga ofisi hizo za TFS ilitakiwa kufikiwa tarehe 13 Desemba 2019.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger