Wednesday, 20 November 2019

MABINTI WA DARASA LA NNE WAUZA POMBE ZA KIENYEJI

...
Shehe wa Kijiji cha Mpwayungu Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Nurdin Mbawala amesema watoto wa kike kuanzia darasa la nne wanatumiwa na wazazi wao kuuza pombe za kienyeji hivyo kuhatarisha usalama wao.


Aidha amesema hali hiyo inawaweka watoto hao katika hatari ya kutumika katika ngono wakiwa kwenye umri mdogo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika mkutano wa majadiliano kwenye mradi wa Sauti Yangu unaotekelezwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Woman Wake Up (Wowap), mradi unaofadhiliwa na Shirika la Child Fund Korea kupitia Jukwaa la Haki za watoto, alisema vitendo vya wazazi kupeleka watoto vilabuni vimekithiripamoja na hatia zinazochukuliwa na serikali ya kijiji.

Alisema mtendaji wa kijiji hicho, Selemani Kibakaya anafanya juhudi kubwa ikiwa ni pamoja na kutembea na fimbo kuwasaka wanaofanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto lakini jambo hilo limekuwa likiendelea.

Alishauri viongozi wa vijiji kuweka mikakati kuhakikisha hakuna mtoto anayekwenda kilabuni kuuza pombe.

“Mtoto mdogo wa kike ndio maziwa yanaanza kutoka tena yuko darasa la nne anashinda kilabuni kuuza pombe, huyo mtoto anajengewa mazingira gani, usalama wake ukoje?” alisema.

Alisema wazazi wamekuwa wakitumia watoto kama mitaji na walevi ndio wanapenda kuhudumiwa na watoto kama hao.

“Huo ni ukatili wa hali ya juu sana, hapo mzazi hawezi kuona shida kumuuza mtoto wake maana kuna watoto walishaulizwa kwa nini wanauza pombe walisema mama zao waliwaambia kama watakataa kufanya biashara hiyo hawataweza kununuliwa sare za shule au madaftari.” Alisema.

Aliitaka jamii kulivalia njuga suala hilo ili kuhakikisha watoto wa kike au hata wa kiume hawafanyi kazi ya kuuza pombe kwenye vilabu.

Mwalimu Sane Nshashi wa shule ya Msingi Nagulo Mwitikila alisema wakati wa kutungwa kwa sheria ndogo ndogo suala la watoto kutumikishwa kwenye vilabu vya pombe za kienyeji liangaliwe na kutungiwa sheria.

Alisema tatizo hilo limekuwa na athari kubwa ka watoto wa kike kwani wanashinda vilabuni hadi usiku wa manane na kukosa muda wa kujisomea na hata kupumzika.

Kwa upande wake Gabriel Hoya amesema matatizo ya watoto yako mengi sio kwenye mimba tu hata suala la watoto kutumikishwa kwenye vilabu vya pombe liangaliwe.

Pia alitaka kuangaliwa suala la wazazi walevi ambao wamekuwa wakishinda na wakati mwingine kulala kwenye vilabu vya pombe na kushindwa kutimiza wajibu wao kenye malezi ya watoto.

“Mzazi anashinda kilabuni, wakati mwingine harudi nyumbani, watoto wanajilea wenyewe wanakwenda shule bila viatu, mavazi yamechanika, hawajala hili ni tatizo kubwa.” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Elimu wa Kata, mwalimu Sunday Mtambo alisema pombe za kienyeji ni chanzo kikubwa cha baadhi ya wazazi kutofanya kazi. /“Kuwe na muda maalumu wa kufungua na kufunga vilabu ili pombe isilete athari kwenye uchumi wa familia,” alisema.

Akijibu hoja hizo mtendaji wa kijiji cha Mpwayungu, Selemani Kibakaya aliwataka wananchi kushirikiana ili kuhakikisha watoto hawatumikishwi kwenye vilabu vya pombe za kienyeji.

Amesema sasa wamekuwa wakikamata watoto wanaotembea usiku, jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa watoto kuwa na woga.

Mratibu wa Wowap, Nasra Suleiman alisema jamii inatakiwa kushirikiana ili kulinda haki na ustawi wa watoto.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger