Thursday, 14 November 2019

KITABU CHA HISTORIA YA MAISHA YA RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA CHAAMSHA UPYA ARI YA KUJISOMEA

...
Keki ya mfano ya Kitabu cha Mhe. Benjamin William Mkapa
Msanii maarufu nchini Muzu Suleimanji akiwa na wadau wakiwa na nakala ya kitabu hicho.
Profesa Saida Othman (kulia) akiwa na wadau wengine na nakala zao
Profesa Semboje akielezea kitabu hicho kwa Bw. Ali Mufuruki na Mkurugenzi Mtendaji wa Standard Chartered Bw. Sanjay Rughan
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akinunua nakala yake.


Na Sultani Kipingo
Ujio wa Kitabu cha historia ya maisha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa kumeelezwa kuwa ni mojawapo ya chachu za ajabu kupata kutokea hivi karibuni katika kuwahamasisha Watanzania kurudia upya hamu ya kujisomea vitabu ambayo inazidi kupotea kutokana na kile klnachoaminika kuwa ni utandawazi.

Uchunguzi uliofanyika mara baada ya uzinduzi wa kitabu hicho Novemba 12, 2019 jijini Dar es salaam umebaini kwamba wengi wanakisaka kitabu hicho kwa udi na uvumba ili kukisoma, kila mtu akiwa na sababu zake.

Wengine wanakitafuta ili kupata kwa undani mwandani wa “Mzee wa Ukweli na Uwazi”, wakati wengine wakitaka kuona endapo kweli “Che Nkapa” kafukua makaburi, wakati wengine wengi Zaidi wakijikuta wana hamu tu ya kumsikiliza kiongozi aliyevutiwa na usemi wa “Mtaji wa Maskini ni Nguvu zake mwenyewe.

“Tulim-miss Mzee wetu ndio maana tuna hamu ya kusoma maandiko yake” anasema Mariam Kindiko, mfanyabishara wa nguo na urembo maeneo ya Kijitonyama. “Wengi tuliobahatika kuwepo na akili zetu wakati wa enzi zake tunamkumbuka kwa jinsi alivyorejesha ghafla heshima ya mtu kufanya kazi”, anaongezea huku akicheka.

Watu wapatao sita hivi katika maeneo mbalimbali wanapita mle mle kwa Bi Mariam, na wengine wanaenda mbali Zaidi kuunga mkono ushauri alioutoa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa kutaka kitabu hicho cha Kiingereza kitafsiliwe kwa lugha ya Kiswahili ili wengi wafaidike nacho.

“Tunajua Che Nkapa alitaka kuwasiliana moja kwa moja na wasomi wenzie lakini sie walalahoi tusiojua Kiinglishi tunamwomba atufikirie kututafsiria kama alivyosema (Rais Magufuli) Ngosha” anasema Twalib Zakaria wa Kigamboni.

Uchunguzi huo umeonekwa kwamba ni kweli kwamba kitabu cha Mzee Mkapa kimezua mijadala kila kona ya nchi, ikiwemo kwa wanasiasa ambao kila lizukapo jambo jipya baadhi yao huwa wa kwanza kudandia treni kwa mbele, lakini si uwongo kwamba ghlafa bin vuuuup watu wamehamasika na kutaka kukisoma hicho kitabu.

“Watanzania wamepata ari ya kusoma vitabu baada ya kukiona kitabu cha Mzee Mkapa na kumaizi kwamba mitandao na magazeti havina ujazo wa kutosha kikidhi kiu yao ya kujua mambo”,anasema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam aliyeomba jina lihifadhiwe.

Mhadhiri huyo anasema kinadharia na kivitendo kiu ya kujua vitu ama mambo hufanya watu wategemee ama wapendelee kilichopo mbele yao (mitandao, magazeti ya kawaida na udaku na soga za kijiweni), jambo ambalo limedhoofisha utamaduni wa kusoma vitabu.

“Kwa sehemu kubwa ni kwamba ukosefu wa vitabu vya kusisimua na vyenye mafundisho kumesababisha kufa ama kufifia kwa utamaduni wa kujisomea na ndio maana nasema kitabu cha Mheshimiwa Mkapa ni mfano hai kwamba kusoma kunaweza kuhamasishwa kwa kuwepo vitabu vyenye maudhui ya kuvutia”, amesema mhadhiri huyo.

Wahojiwa wengi pia wameshukuru kusikia kwamba Rais wa Awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Aamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete nao wako mbioni kuachia vitabu vya historia za maisha yao.

“Mbali na kuandika historia kwa ukamilifu pia hatua ya watu mashuhuri kuandika biography zao kunasaidia kuweka rekodi na kumbukumbu sawa kwani mambo muhimu hayo Watanzania tumeyapa kisogo sana” anasema msanii Nathan Mpangala.

Mwanamuziki mkongwe John Kitime anakubaliana na Mpangala, akiongezea kwamba iko haja kila mtu mashuhuri afanye kuandika historia ya maisha yake na kwa jinsi walivyo wengi utashangaa jinsi kila mtu atakavyopenda kusoma vitabu”, anaongezea.

Akielezea kitabu hicho, Profesa Rwekaza Mukandala anasema Mtoto Benjamin William Mkapa, alifundishwa kupika chakula na mama mzazi Stephania akiwa mdogo. Alipokwenda shule hapo kijijini Lupaso, Ndanda na hatimaye St. Francis Pugu na Makerere, alifundishwa kupika, kufinyanga, kubuni na kuchambua mawazo na kuyaweka sawa kama msomi mbunifu na mwandishi. Kitabu hiki ni zao la mpishi wa mawazo mahiri aliyebobea. 

"Ni kitabu cha kurasa mia tatu na kumi na tisa, katika sura ya kumi na sita. Kuna utangulizi ulioandikwa na Mheshimiwa Joaquim Chissano, Rais mstaafu wa Msumbiji, Pia kuna picha nyinge nzuri, na viambatisho viwili. Mchapaji Mkuki na Nyota wamefanya kazi nzuri sana, sikubaini kosa hata moja", anasema msomi huyo aliyepata kuwa Makama Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Profesa Mukandala anaweka bayana kwamba kitabu hicho kina sehemu kuu tatu. Kwanza tunapewa vionjo vitamu tukielezwa kuzaliwa kwake, kukua na kwenda shule. Hii ilikuwa matayarisho ya kufikia nia au azma yake ya maisha. 

Kisha tunaletewa mlo wenyewe (main course) uliosheheni kumbukumbu na ngano za huyo kijana sasa mtu mzima akiwa kazini, mpaka akaukwaa urais wa Tanzania. Mwisho tunaelezwa kwa ufupi maisha yake baada ya kumaliza ngwe yake ya miaka kumi ya urais.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger