Thursday, 14 November 2019

Chama cha National League for Democracy (NLD) Chajitoa Uchaguzi Serikali za Mitaa

...
Chama cha National League for Democracy (NLD) kimetangaza rasmi kujitoa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, huku kikimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ajiuzulu
 
Uamuzi wa chama hicho umeongeza idadi ya vyama vya siasa vya upinzani vilivyofikia uamuzi wa kujitoa kushiriki uchaguzi huo kufikia vinane. Vingine ni ACT-Wazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chauma, NCCR-Mageuzi, UPDP, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Kijamii (CCK).

Kwa mujibu wa taarifa ya NLD iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Oscar Makaidi, kinamtaka Jafo kujiuzulu mara moja kwa madai kuwa ameshindwa kusimamia uchaguzi huo na kulitia taifa hasara.

“NLD hatuna imani naye licha ya kuagiza kuwa wagombea wote walioenguliwa, warudishwe, agizo ambalo hana mamlaka nalo kikanuni wala kisheria," Makaidi alisema.

Katika taarifa yake hiyo, NLD kimeamua kujitoa katika uchaguzi huo kwa kuwa una kasoro kubwa na haziwezi kurekebishika katika muda uliobaki.

Chama hicho kimemwomba Rais John Magufuli kusitisha uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 na mchakato wake wote uanze upya.

“Kwa kuwa Tamisemi imeshindwa kusimamia uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa, tunataka usimamiwe na tume huru ya taifa ya uchaguzi,” alisema.

Makaidi pia alisema NLD haikubaliani na uamuzi wa Jafo kuwa amefuta uamuzi wote uliofanywa na wasimamizi wasaidizi kwa kuwa hana mamlaka hayo kikanuni na kisheria.

“Tunaamini kwamba kuendelea na uchaguzi chini ya usimamizi ule ule ni kuhalalisha upungufu wote uliojitokeza, mwingi ukiwa ni wa makusudi.

"Kuendelea na uchaguzi huu ni kuendelea kutegemea makosa mengine huko mbeleni hasa wakati wa upigaji kura na utangazwaji wa matokeo yake.

“Tumepokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wagombea wetu yanazothibitisha ukiukwaji na ubakwaji wa demokrasia kwa kiwango cha kutisha kiasi cha kuufanya uchaguzi huu kuwa kituko.

“Kwa ujumla, uchaguzi umepoteza sifa ya kuitwa uchaguzi, hivyo tumeazimia kujitoa," Makaidi alieleza zaidi katika taarifa yake hiyo.

Kiongozi huyo wa NLD aliwataka wanachama na wagombea wao wote nchi nzima kuwa watulivu na kutojihusisha kwa lolote kuhusiana na uchaguzi huo mpaka hapo watakapotaarifiwa vinginevyo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger