Sunday, 17 November 2019

Bodi Ya Rea Yampa Siku 14 Mkandarasi Wa Umeme Mkoani Simiyu Kujirekebisha

...
Na Teresia Mhagama, Simiyu
Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imempa siku 14 mkandarasi wa umeme vijijini mkoani Simiyu kuongeza kasi ya usambazaji umeme katika vijiji alivyopangiwa la sivyo Bodi hiyo haitasita kuchukua hatua mbalimbali za kimkataba ikiwemo ya kusitisha mkataba.

Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Wakili Julius Kalolo  alisema hayo tarehe 16 Novemba, 2019 wilayani Busega mkoani Simiyu mara baada ya kukagua kazi ya usambazaji umeme katika Vijiji mbalimbali vya wilaya ya Bariadi na Busega akiwa amembatana na Mjumbe wa Bodi hiyo, Dkt Andrew Komba na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.

” Bodi haijaridhishwa na kasi ya mkandarasi huyu kwani amepewa kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 152 vya Mkoa wa Simiyu lakini mpaka sasa amesambaza katika vijiji 54 ambayo ni takribani asilimia 30 tu ya kazi anayopaswa kufanya hivyo tumempa siku 14 aonyeshe mabadiliko la sivyo tutachukua hatua.” Alisema

Wakili Kalolo alieleza kuwa, Serikali imetimiza jukumu la kutoa malipo kwa mkandarasi huyo ili kazi ya usambazaji umeme ifanyike kwa kasi hivyo visingizio vya ucheleweshaji wa kazi havikubaliki kwani kwa mujibu wa mkataba wa mkandarasi huyo anapaswa kumaliza kazi mwezi Aprili mwaka 2020.

Aidha, alimwagiza mkandarasi huyo kampuni ya Whitecity Guangdong JV, kuwasilisha mpango kazi wake kwa Bodi hiyo, Mameneja wa TANESCO mkoani Simiyu pamoja Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu ili kuweza kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa kazi anazofanya.

Awali Bodi hiyo ilikutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini ambapo, Mjumbe wa Bodi ya REA, Dkt. Andrew Komba alitoa shukrani kwa viongozi wa mkoa wa Simiyu kwa kufuatilia utekelezaji wa kazi ya usambazaji umeme vijijini.

Aidha, aliomba kasi hiyo iongezeke ili Mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA III) ukamilike kwa wakati.

Alisema kuwa, msukumo wa kuwafuatilia wakandarasi unahitajika ili kutimiza lengo la Serikali  la kupeleka umeme katika vijiji vyote vilivyopo katika mpango  wa REA III mzunguko wa kwanza ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.

Aidha alitoa wito kwa viongozi wa Serikali katika  ngazi mbalimbali za mkoa, kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma ya umeme kwani Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika kuwasambazia umeme wananchi hivyo wanapaswa kuunganisha umeme kwa wingi na kuutumia katika shughuli za kiuchumi na kijamii


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger