Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limesema zaidi ya watu 100 wameuwawa kwenye miji 21 nchini Iran wakati wa machafuko yaliyozuka wiki iliyopita kupinga kupanda kwa bei ya mafuta.
Katika taarifa iliyochapishwa jana, shirika hilo limesema polisi wa kulenga shabaha walifyetua risasi kuelekea makundi ya waandamanaji kutoka juu ya majengo na katika kisa kimoja kutoka ndani ya helikopta.
Shirika hilo lenye makao yake mjini London limesema taarifa yake ni kutoka duru za kuaminika na vyanzo vingine ikiwemo mashuhuda, kanda za video na maelezo ya watetezi wa haki za raia.
Amnesty imesema vikosi vya polisi na intelejensia havikurudisha miili ya waliuwawa kwa familia zao na vimelazimisha baadhi ya miili kuzikwa haraka bila kufanyiwa uchunguzi wa kitababu.
Taarifa hiyo imefichua jinsi vikosi vya usalama nchini Iran vinavyoendesha mauaji ya raia kinyume na sheria ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu katili na nguvu iliyopindukia.
Raha Behreini, ambaye ni mwanasheria na mtafiti wa Amnesty International amesema "Mamlaka za Iran zina historia ya kutumia ukatili na nguvu kubwa dhidi ya wale wanatimiza haki yao ya kujieleza na kuandamana kwa amani. Hata hivyo inaonekana mara hii, wamezidisha zaidi ukandamizajai kwa sababu hawataki maandamano hayo yawe makubwa"
Iran yenyewe haijatoa taarifa ya idadi ya watu waliokamatwa, kujeruhiwa au kuuliwa wakati wamaandamano hayo yaliyosambaa haraka kwenye karibu majiji na miji 100.
Mamlaka nchini humo zimezima huduma za mtandao wa intaneti tangu siku ya Jumamosi na hali hiyo imeendelea hadi jana jumanne.
Kukosekana kwa upatikanaji taarifa kumevifanya vyombo vya habari vya Iran na maafisa wa nchi hiyo pekee kuwa na uwezo wa kutoa taarifa kuhusu kinachoendelea.
Afisa mmoja nchini Iran amesema maandamano hayo yamepungua nguvu baada ya kikosi cha ulinzi wa mapinduzi cha jeshi la Iran kutishia kuchukua hatua kali iwapo yataendelea.
Credit:DW
Credit:DW
0 comments:
Post a Comment