Sunday, 6 October 2019

Kanuni bora za ufugaji wa kuku wa kienyeji(kuku Asili)....Soma Hapa Uwe Tajiri

...
Ufugaji wa kuku wa asili ni nyenzo muhimu katika kupambana na wimbi la umasikini kwa kuongeza kipato cha kaya. 

Hata hivyo, pamoja na soko la uhakika, bado ufugaji kuku haujaweza kutumika ipasavyo kupambana na umaskini unaowakabili Watanzania wengi.

 Ni mazoea kwa jamii nyingi hapa Tanzania kufuga kuku wa asili kama sehemu ya mila na desturi zao. Kuku wa asili amekuwa akifugwa bila ya kupatiwa huduma muhimu kama makaazi bora, chakula cha ziada, tiba, kinga za magonjwa mbali mbali. 

Muhtasari huu unatoa muongozo wa ufugaji wa kuku wa asili ili uweze kuzalisha na hatimae kukuza kuku kwa wingi.

Usafi wa vyombo na mazingira ya kuku
Uchafu ni mama wa magonjwa, hivyo zingatia haya;
1.  Vyombo vya chakula na maji visafishwe mara kwa mara kwa maji safi na sabuni.

2. Pumba au chakula kilicholowana na kuchanganyika na kinyesi cha kuku kitolowe na kufukiwa.

3.  Choma moto au zika kwenye shimo refu kuku waliokufa kwa ugonjwa.

4.  Usifuge kuku na ndege wa jamii nyingine kwa mfano bata katika banda moja.

5.  Ondoa mbolea mara kwa mara kutoka katika banda la kuku.

6.  Tumia dawa za kuulia vimelea kusafishia banda na upake chokaa angalau mara moja kwa mwaka.

7.Ziba matundu yote yanayoweza kuruhusu panya na wanyama wakali kama vicheche kuingia katika banda la kuku.


Magonjwa na kinga kwa kuku wote

1.Ndui ya kuku
Huathiri sana vifaranga wanaokua na ujitokeza kwa wingi wakati wa mvua za muda mrefu. Husababisha vivimbe katika uso/ kishungi na hata sehemu nyengine zisizo na manyoya.

2.Mdondo/kideri
Mdondo, au kwa majina mengine lufuo, au kideri ni ugonjwa hatari katika magonjwa ya kuku wa asili. Ni ugojwa wa virusi ambao huathiri kuku wa rika zote, huweza kuangamiza kuku wote kijijni.

3.Ukosefu wa vitamini A
Ugonjwa huu husababisha macho kuvimba na kutoa uchafu mziito kama sabuni iliyolowana. Kuku wenye dalili hizi hawaponi na hata kufa. Ugonjwa hujitokeza baada ya kipindi kirefu cha kiangazi kwa ajili ya ukosefu wa majani mabichi.

4.Kosidiosisi
Huathiri kuku wa umri wowote lakini huuwa zaidi vifaranga na kuku wanaokua. Kuku hudhoofika, manyoya huvurugika na kuku huwa kama wamevaa koti. Kuku huarisha damu au kinyesi cha kahawia na huzubaa na kuonekana kama wamevaa koti.

5.Viroboto, chawa na utitiri
Hawa ni wadudu wa nje wanaoshambulia ngozi. Huweza kusababisha ugonjwa kutokana na kunyonya damu. Viroboto hushambulia kichwa na kunata huku wakinyonya damu. Viroboto huuwa vifaranga. Chawa na utitiri hughasi kuku hadi wakashindwa kutaga na kuatamia.

6.Minyoo
Minyoo huweza kudhofisha kuku na kuwafanya waweze kuugua maradhi mengine kirahisi. Muone mtaalaam ukihisi kuku wako wana minyoo.


Chakula cha ziada
1.Wapatie vifaranga nyongeza ya protini kwa kuwachanganyia vumbi la dagaa au vichwa vya dagaa vilivyotwangwa kwenye pumba za mahindi.

2.Changanya kikombe kimoja cha vumbi la dagaa na vikombe vitano vya pumba za mahindi (tumia kikombe kidogo cha chai).

3.Mchwa na wadudu wengine wanaweza kutumika kama nyongeza ya protini.

4.Vuna mchwa kwenye vichuguu au tengeneza mchwa katika njia za mchwa.

5. Kutengeneza mchwa: changanya kinyesi cha ng’ombe na majani makavu, mabua ya mahindi au maranda ya mbao katika chungu au ndoo ya zamani.

6Mwagia maji hadi kila kilichomo kilowane kisha weka katika chombo kama ndoo au chungu. Weka chombo chako katika njia ya mchwa ukikigeuza juu chini na subiri hadi kesho yake asubuhi, kisha beba vyote vilivyomo na uwamwagie kuku mahali walipo.

Utotoleshaji wa vifaranga
Chagua jogoo bora na tetea bora kuzalisha kuku.

Sifa za jogoo bora
1.  Awe na umbo kubwa, awe ukiko mzuri na usioangukia upande mmoja.

2.  Apende kuwa na himaya yake. Ukimpata jogoo mwenye sifa hizi mueke yeye na matetea kumi. Hivyo ukiwa na matetea ishirini jogoo wawili wanatosha.

Sifa za tetea bora
Tetea bora ni yule mwenye umbo kubwa, mwenye uwezo wa kutaga mayai ya kutosha, kuatamia na hatimaye kutotoa vifaranga.

Uhifadhi wa mayai
1.  Weka mayai mahali safi na penye hewa ya kutosha.

2.  Tumia kasha lililokatwa na kujaza mchanga mkavu na safi au kasha la kuhifadhia mayai.

3.  Weka sehemu butu ya yai iwe upande wa juu na ile iliyochongoka itizame chini.

4.  Andika namba au tarehe katika siku lilipotagwa.

5.  Mayai yakishatagwa yatolewe na kuhifadhiwa na moja liachwe kwenye kiota ili kumuita kuku kuja kutaga kesho yake.

Kuatamiza mayai
1.  Kuku awekewe mayai yatakayokuwa na uwezo wa kuyaatamia na kuyatotoa yote.

2.  Mayi 10 hadi 12 yanatosha kuatamia.

3.  Mayai ya kuatamiza yasizidi wiki 2 toka kutagwa.

4.  Yai la mwisho kutagwa liwe la kwanza kuchaguliwa hadi yapatikane mayai 10 mpaka 12, na apewe kuku wa kuyaatamia.

5.  Mayai ya kuatamiza yasafishwe kwa kitambaa kikavu na safi au kilichowekwa spiriti

Kutotolesha vifaranga wengi kwa wakati mmoja
1.  Kama unataka kuku zaidi ya mmoja watamie na kutotoa kwa mpigo fanya yafuatayo;

2.  Kuku wa kwanza akianza kuatamia muwekee mayai yasiyo na mbegu mfano mayai ya kuku wa kisasa au kuku asiye na jogoo.

3.  Rudia zoezi hilo hadi utakapofikisha kuku watano kisha wawekee kuku wote mayai yenye mbegu.

Matunzo ya vifaranga ili kuzuia vifo
Vifaranga wengi hufa kabla ya kufikisha miezi miwili kutokana na magonjwa, baridi na kuliwa na wanyama wengine. Ili kupunguza vifo vya vifaranga wa siku 1 hadi miezi miwili zingatia yafuatayo;

Ulinzi dhidi ya mwewe na wanyama wengine
1.  Weka vifarang kwenye tega na kuwafunika ili wasiende mbali wakati wa mchana. Wape maji na chakula. Hakikisha hawapigwi jua wala kunyeshewa mvua. Wakati wa usiku walale na mama yao.

Chanjo ya mdondo kideri/lufuo
Kama tetea alichanjwa kabla ya kuanza kutaga vifaranga wanaoanguliwa huwa na kinga ya mdondo ya kuwatosha kwa wiki 3 za kwanza za maisha yao. Wachanje vifaranga hao dhidi ya mdondo wafikishapo umri wa siku 18.

Vifaranga ambao historia ya chanjo ya mama haijulikani, wapewe chanjo ya mdondo siku tatu baada ya kuanguliwa, rudia hadi wakifikisha wiki tatu kisha uchanje kila baada ya miezi 3

Kinga dhidi ya kosidiosisi
Kinga ya kosidiosisi kwa vifaranga, itolewe hata kama ugonjwa haujajitokeza.

1.  Wape dawa ya amprolium kwa muda wa siku tatu mfululizo mara wafikishapo siku saba tokea waanguliwe kama kinga ya kosidiosisi.

2.  Dawa inaweza kutolewa hata kama wamevuka umri huo. Fuata maelekezo ya mtaalam juu ya kiasi cha dawa kinachopaswa kuchanganwa katika maji au pumba

3.  Kama vifaranga wadogo wataonesha dalili za kuzubaa kama kuvaa koti wapewe dawa ya amprolium kwenye maji kwa utaratibu ufuatao;

Dawa siku tatu mfululizo: usiwape kwa siku mbili; gawa tena kwa siku tatu

Hitimisho
1.  Hakikisha banda na vyombo vya chakula cha kuku ni visafi kuepusha magonjwa.

2.  Usichanganye kuku na bata katika banda moja

3.  Lisha chakula cha ziada hasa kwa vifaranga.

4.  Kideri, kosidiosisi, ndui na upungufu wa vitamini A ni vyanzo vikuu vya vifo vya kuku wako. Kumbuka kukinga kuku wako dhidi ya magojwa haya.

5.  Kumbuka kuchagua mayai ya kuatamiza kama ilivyoelekezwa ili kuepuka kupata mayai viza.

6.  Vifaranga wadogo hadi wiki nane huhitaji matunzo mazuri, fuata maelezo kuzuia vifo.

7.  Kumbuka ukiuza kuku wengi kwa mpigo utaongeza mapato yako, jitahidi kuzalisha vifaranga kwa wingi ili upate kuku wengi baadae.

8.  Muone mtaalam wa mifugo ulie karibu nae kwa ushauri zaidi.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger