Monday, 5 August 2019

Katibu Mkuu Wizara Ya Fedha Awataka Watafiti Na Wadadisi Kuzingatia Viwango Ukusanyaji Wa Takwimu

...
Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amewataka wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa sekta isiyo rasmi nchini kuzingatia viwango vya ubora katika ukusanyaji wa taarifa ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi zenye kubaini mahitaji na changamoto za sekta hiyo nchini.

Akizungumza katika Ufunguzi wa Mafunzo ya Wadadisi na Wasimamizi wa Utafiti wa Sekta isiyo rasmi Nchini  jana Jumapili (Agosti 4, 2019) Jijini Dar es Salaam, Bw. James alisema matokeo ya utafiti huo yataisaidia Serikali kufahamu mchango halisi wa sekta isiyo rasmi katika Pato la taifa ikijumuisha ulipaji kodi.

Aliongeza kuwa ni ukweli ulio dhahiri kuwa sekta isiyo rasmi imekuwa nguzo muhimu katika pato la taifa kwani kulingana na utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi uliofanyika mwaka 2014 ilibainika kuwa, asilimia 21.7 ya watu waliokuwa na ajira walikuwa katika sekta isiyo rasmi, na hivyo kuleta kiashiria kuwa sekta hiyo ina mchango muhimu katika pato la taifa.

Bw.James alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejiwekea malengo mbalimbali katika kuinua uchumi wa wananchi wake ikiwemo kubaini changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta isiyo rasmi ikiwemo hali ya upatikanaji wa masoko, fursa za mikopo, ujuzi unaohitajika pamoja na matumizi ya teknolojia kwa nia ya kuongeza tija kwenye uzalishaji.

“Sina shaka na ubora wa takwimu zitakazokusanywa kwa kuwa mnaendelea kufanya kazi hii kwa karibu sana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Benki ya Dunia (WB), tumieni uzoefu wenu ili na sisi Watanzania tunufaike kuifahamu zaidi sekta hii katika kukuza uchumi wa Tanzania” alisema Bw. James.

Kwa mujibu wa Bw. James alisema utafiti wa kwanza wa kitaifa katika sekta isiyo rasmi ilifanyika nchini mwaka 1991 na kufuatiwa na utafiti kama huo katika Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 1995, hivyo ni kipindi kirefu kimepita na kufanya kuwepo na mahitaji makubwa ya takwimu zinazoakisi hali halisi ya sasa ya sekta hiyo nchini.

Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa alisema hatua ya Serikali ya Awamu ya Tano kufanya utafiti huo ni uthubutu mkubwa kwa Tanzania kwa kuwa ni nchi chache za Bara la Afrika zimeweza kufanya utafiti huo kwa ajili ya kupima sekta yenyewe na upatikanaji wa rasilimali fedha sambamba na kubaini fursa za ajira kwa wananchi wengi wakiwemo wananchi maskini.

“Kama mnayofahamu Serikali kwa sasa inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21 ambao unahitaji takwimu katika ngazi za chini za utekezaji, ili kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa lengo la kufikia lengo la angalau asilimia 40 ya watu wenye ajira ifikapo mwaka 2020” alisema Dkt. Chuwa.

Aidha Dkt. Chuwa alisema Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu na Shirika la Kazi Duniani (ILO) imeshakamilisha maandalizi yote ya kufanyika kwa utafiti huo, unaotarajia kuanzia katika Mkoa wa Dar es Salaam Mwezi Agosti hadi Novemba mwaka huu.

Dkt. Chuwa alisema muundo wa utafiti huo umegawanyika katika ngazi kuu mbili, ikiwemo ngazi ya ukusanyaji wa taarifa katika ngazi ya kaya na ngazi ya pili ni ngazi ya biashara (uchumi), ambapo katika ngazi ya kaya, utafiti huo umejikita katika maeneo ya taarifa za kidemokrasia, elimu, hali ya ulemavu, ajira, ukosefu wa ajira.

Akifafanua zaidi, Dkt. Chuwa alisema sampuli ya utafiti huo katika ngazi ya kaya pia utahusisha maeneo ya kuhesabia yapatayo 200 yaliyo mkoani Dar es Salaam na kaya zilizochaguliwa zaidi ya 2,400 pamoja na ukusanyaji wa taarifa kutoka kwenye biashara zaidi ya 4,000 na matokeo ya utafiti huo yatawezesha upatikanaji wa taarifa za kitakwimu ambazo ni wakilishi katika ngazi za Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam.

MWISHO


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger